Riwaya

Pendo (2)

na katika maisha.

Nyota ya amani na upendo; si nyingine ni Ommy John niliekutana wakati natafuta kibarua kule- King Godown kutafuta angalau kibarua maana hata cha kupeta kahawa kingenifaa,.

Hata hivyo, nikumbuka namna karani alivyonijibu na kuniambia nirudi baada ya wiki mbili. Nami nikamuitikia ukizingatia ajira zimekuwa tabu tupu. Hata kwa wasomi, ajira zimekosekana hata hizo za kupeta kahawa sembuse sisi ambao tuliogopa umande; Na ukata ndio huo!

Nikiwa na hali ngumu ya maisha niliendelea kuwa na subira yenye kuvuta heri pamoja na kuwa nilipata vishawishi toka pande zote mbili si wasichana wenzangu, si wavulana. Wengine wakaniambia,

"Wewe mshamba binti mzuri hivyo watu tunakuhitaji hutaki kula maisha. Maisha ndio kama haya tunayokuambia dunia inakwisha hivyo usifikiri huko Ahera kuna kutesa. Wee zidi kukaa hapo unashangaa shangaa."

"Mh! Shoga mbona unakuwa bonge la mshamba namna hiyo, wenzio tunatesa hivyo kwa binti kama wewe hautakiwi kuwa hivyo, wee kalabagao na ubwezi wako," yote hayo sikuona kama yana umuhimu kwangu, nikawajibu

"Kama ushamba wangu, yanini kunifuata niacheni na ukalabagaho na ubwezi niwe nao. Mna thamani gani nyie ambao ni wajanja wenye kujiona limwengu wote ni wenu?"

Sikupenda kabisa niwe na tabia kama ya mabinti wenzangu wa hapa Dar -Es-Salaam, wanayoifanya na kujiuza mithili ya bidhaa ya gengeni au basi eti hata wanadiriki kunadi miili yao kama miili nyumba inayopigiwa mnada baada ya mwenye nyumba kushindwa kurejesha mkopo.

Majuma mawili yalishapita, nilipewa kibarua cha kuchambua kahawa. Nikaanza kazi moja kwa moja bila ya masihara.

Siku hiyo niliiona chungu, nilijuta kuzaliwa katika dunia hii ya Musa yenye masumbufu na kero namna hii maana vibarua wote macho yao waliyaelekeza kwangu .

Kila mmoja likuwa na lake la kusema. Mwenye kusema huyu katokea wapi, alisema. Mwenye kusema kimbwa koko hiki wamekiajiri cha kazi gani, alisema mradi tu, sikufahamu sababu hasa ya yote hayo hata nikadhani labda hali niliyo kuwa nayo ya kutisha na kuchakaa, ndiyo iliyowafanya wanichukie ghafla namna hiyo.

Sikupata jibu mpakajiona labda nina kasoro. Lakini, mawazo yakanijia haraka haraka. Nikajua kila mmoja anasababu yake. Nilijua wapo walioona nimeziba nafasi za ndugu zao, wengine licha ya kuchaa, walijua ingawa ninaonekana nimechakaa, nikioga vizuri na kujipaka mafuta ya dukani kma wanawake wenzangu, labda nitawazidi kete.

Lakini kama ni hivyo, walikuwa wanapotea maana pale sikwenda kufanya mashindano ya urembo. hata hivyo, nilijua dhahiri wale wanaume waliokuwa mstari wa mbele kunifokea huku wakijipitisha pitisha karibu na mimi ili nijue kuwa ndio mabosi, walikuwa na ajenda yao ya siri. hiyo naomba nisikuambie ni ipi.

Basi, mara tukaambiwa muda wa chakula tayari tuondoke tukapate chochote. nilibaki pale pale nikiendelea na shughuli zangu. Ningeenda wapi na hali sina senti hata moja zaidi ya shilingi kumi niliyokuwa nimeifunga kwenye pindo la upande wa kanga niliyojifunga kwa ajili ya nauli ya kunirudisha nyumbani baada ya kazi?

. 'Anti mbona wewe haujaenda kupata chakula?" ' Tumbo linaniuma hata sina hamu ya chakula', nilimjibu kuli mmoja aliyenijia na kuniuliza.

"Pendo! Pendo....! mbona umekaa kimya mpenzi kulikoni" Ommy alinishtua toka kwenye lindo la mawazo, "Aa usiwe na wasiwasi Ommy" Kumbu kumbu ya akili yangu ikahama na kurudi pale tulipokuwa. Tukaendelea kuburudika na baadaye tukaamua kuogelea.

"Njoo huku tuogelee." " Hapana naogopa nitazama." Baada ya kuridhika, tuliondoka kuelekea nyumbani. Safari hii Ommy ndiye aliyeshika usukani tulipofika nyumbani, tuliegesha gari leu na kuingia ndani kila mmoja akiwa chakari hajitambui.

Kisha tulielekea bafuni tukaoga , kila mmoja kwa wakati wake. Baadaye kila mmoja alitafuta usingizi wa kuupumzisha mwili na akili yake. Siku hiyo, sikupata usingizi . Kwa masaa mengi niliendelea kuwaza juu ya maisha magumu nuliyokuwa nayo huku hata wale ndugu, jamaa na marafiki zangu kila mmoja akitumia nafsi na utaalamu wake kunisengenya, na kunisimanga.

Mawazo yangu yakarudi tena kule godown nikamkumbuka kijana huyo ambaye alikuwa ni kuli aliyetoa noti ya shilingi 200/= nikale..

Nakumbuka sasa hata nilivyoipokea huku nikisema ASANTE japo sikwenda kula maana niliona itanisaidia mlo wa jioni

Ni kweli bila Mungu kunitumia kijana huyo kulifanya hilo la maana, basi usiku wa siku hiyo ningelala bila kupata chochote cha kuficha tumboni mwangu.

Nikaendelea kuteseka hivyo hivyo na uchambuzi wa mfuko wa kahawa nikilipwa shilingi 300/= Nilichambua kwa muda wa wiki nzima, mfuko mmoja maana sikuwa mzoefu na pili, kahawa yenyewe ilikuwa chafu kupita kiasi.

hata hivyo, wazoefu waliichambua kwa siku mbili hali iliyonifanya kuugua mafua na kikohozi cha hali ya juu kilichonisababishia madhara makubwa. Ukizingatia sikuwa hata na senti ya kununua dawa na mshahara wenyewe huo, bado, niliona maisha yanazidi kuniniwia magumu.

Ingawa wahenga walisema mvumilivu hula mbivu, mazingira ya kazi niliyokuwa nayo yalinionesha kuwa kadri ninavyovumilia, ndivyo ninavyoelekea kula mbovu.Nikamua kujisalimisha mwenyewe.

Niliacha na kuanza tena kutanga tanga kwenye mashirika na makampuni binafsi ili kutafuta kibarua sehemu nyingine.

sehemu nyingine niliahidiwa kurudi baada ya mwezi na nyingine nikathibitishiwa kuwa, nimelamba galasha kwa kuwa hakuna nafasi ya kazi hata moja.