Michezo

MICHUANO YA GLOBAL AFRICAN FOOTBALL INTERCORPORATION:

FAT yaahidi kufanya maajabu

Na Widimi Elinewinga,

Chama cha Soka nchini FAT, kimesema kuwa kitafanya maandalizi mazuri kwa timu ya taifa, Taifa Starskwa ajili ya michuano ya Global African Football Intercoporation inayotegemewa kufanyika Nairobi kuanzia Oktoba 29 , mwaka huu bila kutegemea msaada kutoka FIFA.

Akiongea mwishoni mwa wiki, Mwenyekiti wa FAT Kanali Idd Kipingu, alisema kuwa, Taifa Stars itapiga kambi mjini Dar-Es-Salaam kwa kipindi cha mwezi mmoja kabla ya kwenda kwenye michuano hiyo.

"Tunataka kufanya vizuri na timu itaandaliwa vyema bila ya msaada kutoka FIFA, na wala FAT haiwezi kuitoa timu ya Taifa katika mashindano hayo kwa sababu ya kutokuwa na msaada wowote kutoka FIFA," alisema Kipingu.

Aliongeza kuwa timu ya Taifa, Taifa Stars itakuwa kambini chini ya mshauri wa ufundi Burkhard Pape ambaye aliletwa na FIFA nchini.

Taifa Stars imealikwa na kampuni ya Global African Football Intercorporation ya Afrika ya Kusini kushiriki michuano iliyoandaliwa na Kampuni hiyo itakayoshirikisha nchi za Ghana, Uganda na Kenya.

Waandaji wa michuano hiyo watagharamia usafiri wa ndege kwenda na kurudi kwa wachezaji 18, viongozi sita, kamisaa mmoja wa Mechi na waamuzi wawili wanaotambuliwa na FIFA.

FIFA imekuwa na msuguano na vyama vya michezo nchini hasa baada ya kuenguliwa madarakani na viongozi wakuu wawili wa FAT, aliyekuwa Mwenyekiti Muhidin Ndolanga na Katibu wake, Ismail Aden Rage.

Sitaichezea Yanga- Manyika

Na Gerald Kamia, Morogoro

MLINDA Mlango wa Yanga Peter Manyika amesema kuwa hataichezea Yanga katika msimu ujao wa Safari Lager.

Akiongea na KIONGOZI, Manyika amesema kuwa mipango yake ya kuhamia timu ya Tusker ya Kenya ambao ni mabingwa wa Afrika Mashariki na Kati, imekwenda vizuri na hivi karibuni atajiunga na timu hiyo.

Manyika ambaye alikuwa tegemeo kubwa kwani ni golikipa namba 1 wa Yanga amesema kuwa matatizo aliyoyapata ndani ya Yanga baada ya kufungwa na Simba yamefanya kujifunza soka ya Tanzania na akadai kuwa hana hamu tena na soka ya Tanzania.

Manyika amesema kitendo alichofanyiwa na baadhi ya wanachama wa Yanga si cha kiungwana kwani jambo la kumsingizia mtu kupokea Mlungula si jambo zuri kwani linamzalilisha mchezaji na kumharibia maisha yake kisoka na kijamii.

Manyika amesema kuwa yeye anaipenda Yanga na alikuwa akiidakia muda wote ila kutokana na imani potofu ya baadhi ya wanachama ndio chanzo cha yeye kuondoka.

Timu zailaumu FAT kwa kuikubali Yanga

Na Mwandishi Wetu, DSJ

BAADHI ya timu nchini zimekuwa zikilalamikia Chama cha Soka nchini (FAT) kuwakubali Yanga licha ya klabu hiyo kuchelewa kuthibitisha ushiriki wao katika kombe la FAT.

Akiongea na gazeti hili mwishoni mwa wiki hii, Katibu Mkuu wa FAT, Amin Barkhroon alisema kuwa wao hawakuipendelea timu ya Yanga isipokuwa, walitoa sababu ambazo FAT waliziafiki.

"Sisi kama Chama cha Soka nchini, hatutakuwa tunavikumbusha vilabu siku ambazo michuano kama hiyo itakuwako ila, ni kuvitaka kufuata katiba ambayo itakuwa ikionyesha kila kitu,"alisema Barkhroon.

Kutokana na hilo Barkhroon aliongeza kuwa viongozi wa vilabu wanatakiwa kufuatilia katiba kama inavyoonesha na alisema kuwa hilo suala la kukumbusha vilabu kuwa na michuano litakuwa mwisho wake ni mwaka huu.

Wakati huo huo: Barkhroon alisema kuwa watakutana na vilabu husika ili kuweza kuzungumzia sheria hizo.

Katibu wa MRFA akanusha kumuonya Mwenyekiti

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

KATIBU Mkuu wa Soka Mkoa wa Morogoro(MRFA) Salum Mwintanga, amekanusha habari kuwa amemuonya Mwenyekiti wake kuacha tabia ya kuzungumza ovyo kwenye vyombo vya habari.

Akiongea na mwandishi wa habari hizi, Mwintanga amesema kuwa habari hizi si za kweli kwani zina nia ya kutaka kumgombanisha yeye na Mwenyekiti wake na akadai kuwa hakuna mgogoro wowote ndani ya(MRFA).

Amesema kuwa habari hizo zimekuja mara baada ya wao kurudishwa madarakani kwani hapo awali walisimamishwa kutokana na baadhi ya viongozi wengine kushindwa katika uchaguzi na wakawa wanatoa maneno ambayo yaliwapelekea wao kusimamishwa.

Katibu huyo amesema kuwa Mwenyekiti wake ndiye msemaji mkuu na yeye ni kama mtendaji tu na akaongeza kuwa, kikatiba, hawezi kumzuia Mwenyekiti wake kuzungumza.

Amesema amefanya kazi na Mwenyekiti wake tangu 1994 na miaka yote hiyo, Komanya ambaye ni Mwenyekiti alikuwa akizungumza na vyombo vya habari bila matatizo.

Amesisitiza kuwa habari hizo ni za kutungwa na wala hazina ukweli wowote kwa kuwa walioandika habari hizo hawakwenda kupata ufafanuzi kutoka kwake.

Kauli hiyo ya Mwintinga imekuja baada ya gazeti moja la michezo litokalo mara moja kwa wiki kuripoti kuwa Katibu huyo amemkaripia Mwenyekiti wake kufuatia madai kuwa Mwenyekiti huyo amekuwa akiongea sana na vyombo vya habari kuhusu (MRFA) pasipo kumshirikisha.

Wachezaji waikimbia Reli ya Morogoro

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

TIMU ya soka ya Reli imekimbiwa na wachezaji wake 3 ambao ni Hazazi Hunter, Yahaya Issa na Abubakari Mohamed ambao wamesajiliwa na timu ya Yanga ya dar-Es-Salaam, kwa ajili ya Ligi Kuu ya Muungano na Safari Lager.

Akithibitisha habari hizi, Mwenyekiti wa muda wa timu ya Yanga, Abbas Tarimba amesema kuwa wachezaji hao ni miongoni mwa wachezaji wengine watatu ambao wamesajiliwa na timu hiyo.

Alisema wachezaji wengine ambao walishasaini fomu za kusajili na Yanga siku ya Jumatano ni Abdulkadiri Jash kutoka timu ya Miembeni Zanzibar, Waziri Mahadhi Costal Union, Fred Mbuna kutoka timu ya Majimaji ya Songea.