Michezo

Nigeria yampigia magoti Kanu

lYataka aende Sydney kwa kuwa ni Mnaigeria

LAGOS, Nigeria

MSHAMBULIAJI wa klabu ya soka ya Arsenal ya England, Nwankwo Kanu, amepigiwa magoti na Chama cha Soka cha Nigeria (NFA), ili abadili msimamo wake wa kutoichezea Nigeria katika mashindano ya Olimpiki Mwaka 2000 huko Sydney Australia.

Katibu Mkuu wa NFA, Tijjani Yusuf, alisema ingawa chama chake kinatambua dhahiri kuwa Kanu ana maisha yake yanayombidi kuyalinda, wamemuandikia kumuomba abadili msimamo wake na hivyo kuichezea Nigeria katika mashindano hayo.

""Ingawa Kanu ana maamuzi yake anayopaswa kuyaheshimu, tumemuandikia tukimuomba abadili msimamo wake na hivyo, aichezee Nigeria katika Olimpiki. Hii ni kwa sababu tunaamini kuwa tunao uhusiano mwema na Timu ya Arsenal," alisema.

Katibu huyo alisema chama chake cha NFA kinathamini uhusiano huo na kwamba tayari kimekwisha iarifu klabu ya soka ya Arsenal namna Nigeria inavyomhitaji Kanu katika michezo hiyo ya Olimpiki mwaka huu.

"Kwanza kabisa, ni lazima wote tukumbuke kuwa Kanu ni Mnigeria," aliongeza Yusuf.

Kanu ambaye amevuma miongoni mwa wasukuma soka bora katika bara la Afrika, hivi karibuni aliomba kuondolewa katika kikosi cha Nigeria kinachojulikana kama "Super Eagle" ili apate fursa ya kujiimarisha zaidi katika timu yake ya Arsenal.

Mjadala mkubwa umezuka kufuatia uamuzi wa Kanu kukataa kwenda Sydney ambapo Kanu anashutumiwa kwa anaikimbia na kuikana nchi yake.

Awali, mshambuliaji huyo alikubali kuichezea nchi hiyo katika mashindano hayo ya Olimpiki.

Miaka minne iliyopita, Kanu alikuwa nahodha wa Nigeria aliyeiongoza kwenye mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika mjini Atlanta, Marekani.

Alikuwa katika kikosi chenye wachezaji 22 watakaoshiriki mashindano hayo ya Olimpiki, akiwa mmoja wa wachezaji watatu wenye umri mkubwa.

BMT yaombwa kuutazama sawa uwanja wa Samora

lWashabiki wasema unaweza kumliza mke wa Marehemu Samora Machel

Na Dalphina Rubyema, Iringa

WAPENZI wa michezo mkoani hapa, wameuomba uongozi wa Baraza la Michezo nchini(BMT,) kuingilia kati ukarabati wa uwanja wa michezo wa Samora unaonekana kuharibika zaid hali inayohatarisha maisha ya watumiaji wa uwanja huo.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi uwanjani hapo hivi karibuni wakazi hao walisema kwa pamoja kuwa, ni jambo la kusikitisha na la aibu kuona serikali kupitia Baraza la Michezo inashindwa kukarabati uwanja huo ambao una jina la Rais wa zamani wa Msumbiji, Hayati Samora Machel.

Walisema kushindwa kukarabati uwanja huo kunaonesha jinsi gani serikali isivyo mjali kiongozi huyo ambaye ameacha kumbukumbu nzuri duniani katika kupigania uhuru na ukombozi wa Msumbiji na Afrika .

Pia walisema halihiyo inaonesha namna seriklai kupitia vyombo vyake, isivyojali suala la michezo katika baadhi ya maeneo nchini.

"Hivi sasa Mama Samora akija Iringa akaoneshwa kuwa huu ndio uwanja wenye jina la marehemu mumewe, anaweza kulia! Ataona mmewe anazalilishwa," alisema Paschal Mwanvika, mkazi wa Tosamaganga aliyekuwa miongoni mwa washabiki hao wa michezo waliokataa majina yao yasindikwe gazetini Bw.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia hali mbaya ya uwanja huo ambao umejaa mashimo.

Hali ya jukwaa pia inatisha kwani misumari na mbao zilizojenga jukwaa hilo, tayari zimekwishalegea na kuwa kama mashimo yanayohitaji umakini wa hali ya juu kwani usipofanya hivyo kuna hatari ya kuanguka hali inayoweza kukusababishia majeraha ama vifo.

Mbali na hilo, viti vilivyokuwa vimewekwa kuzunguka uwanja huo, vyote vimeibiwa na badala yake yamebaki mapengo matupu hali inayosababisha watazamaji wa michezo mbalimbali hususani mpira, kusimama ama kukaa chini.

MAANDALIZI YA LIGI YA MUUNGANO,USAJILI

Wachezaji wa Yanga wakacha mazoezi

lSasa kuingia kambini wiki hii

Na Joseph Kiboga

WACHEZAJI wa Kalabu ya soka ya Yanga waliotakiwa kuwa wameingia kambini katikati ya wiki juma lililopita kwa ajili ya maandalizi ya Ligi ya Muungano na Ligi Kuu, msimu ujao, bado hawajaingia kambini kama ilivyotangazwa na uongozi wa klabu hiyo.

Kocha wa timu hiyo, Roul Shungu alikaririwa mwanzoni mwa wiki akisema kuwa timu hiyo ingeingia kambini Septemba 7, mwaka huu lakini, mwandishi wa habari hizi alipofika klabuni hapo, hakukuta dalili ya kuwepo kwa kitu kama hicho licha ya ubao wa matangazo kuandikwa kuwa mazoezi ya timu hiyo yangeanza Alhamisi.

Shungu alipoulizwa juu ya hali hiyo alisema hata yeye hajui kwanini timu haijaingia kambini ila, alidai anadhani kuwa, ni kutokana na ushiriki wa wachezaji hao katika mechi za mchangani.

"Nafikiri wamekwenda kucheza huko mitaani lakini nina uhakika kuwa mazoezi yataanza rasmi Jumatatu ya wiki ijayo," alisema Shungu.

Alifafanua kuwa ni kawaida kwa timu za nchini kuchelewa kuingia kambini na mara baada ya mazoezi kuanza na akasema atapata fursa ya kuchuja wachezaji lakini alikanusha kuwapo kundi la wachezaji ambao atawasajili kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.

Tuna matatizo katika safu ya ulinzi hivyo tutakachofanya ni kuziba mapengo machache katika safu hiyo na wala si vingine," alisema.

Alisema kuwa kuna wachazaji wengi wa vilabu vya daraja la kwanza wanaofanya mazoezi katika uwanja wa Kaunda ambao walikuwa na timu hiyo lakini, si kwa misingi kuwa wanataka kusajiliwa na Yanga.

"Wapo hata wa Prison ambao walikuwepo hapa leo lakini si kwamba wanataka usajili Yanga," alisema na kuongeza kuwa kuna wachezaji wengi wanaocheza klabu za mikoani ambao walianzia Yanga.

Shungu alieleza kuwa kutokana na hali hiyo wachezaji hao wanapokuwa likizo vijijini hufanya mazoezi yao Jangwani.Ufafanuzi huo umefuatia kuonekana kwa wachezaji Omary Mahadhi wa Coastal Union ya Tanga, Lagu Shija wa CDA Dodoma, Said Msasu wa Bandari Mtwara na kipa wa Prison na Taifa Stars Aman Simba katika mchezo wa Yanga dhidi ya Kombaini ya Ilala.

Viwanja vitatu kuwaka moto Jumamosi

Na Mwandishi Wetu

WAKATI Ligi Soka Daraja la Tatu inatarajiwa kuanza Jumamosi hii katika manispaa ya Temeke, tayari homa ya ligi imekwisha anza kuyatia moto matumbo ya baadhi ya timu zinazoshiriki ligi hiyo.

Hali hiyo imeanza kudhihirika ndani ya klabu ya Politan ya Tandika Magorofani ambayo imepania kufanya mazoezi ya nguvu, na ili kuthibitisha homa hiyo, klabu hiyo imewakemea kwa nguvu zake zote wachezaji watakao puuzia kuripoti kwenye mazoezi na kwamba wachezaji wa namna hiyo, watakiona cha mtemakuni kwa mujibu wa sheria walizojiwekea.

Mwenyekiti wa klabu hiyo Bw. Juma Mkinga, amekaririwa akisema kuwa, wachezaji wote wa klabu yake waliosajiliwa, watatakiwa kuripoti na kuanza mapema mazoezi. Alisema mwisho wa kuripoti kwenye mazoezi ni Jumapili hii.

Wakati huo huo: Ligi hiyo katika Manispaa ya Temeke, inaanza Jumamosi hii kwa viwanja vitatu kuwaka moto katika mapambano tofauti.

Klabu za soka zitakazoumana katika viwanja hivyo ni Mvinyo Sports Club na Jamaica Sports Club zitakazoumana katika uwanja wa Tandika Mabatini.

Katika uwanja wa shule ya msingi Kigamboni, Bafanabafana itamenyana na SIFA Mtoni Sports Club, wakati timu ya Sakramento itapambana vikali na timu ya soka ya Evarist Sports Club.

Ligi hiyo itashirikisha jumla ya timu 35 zitakazopangwa katika makundi manne tofauti.