Make your own free website on Tripod.com

Michezo

Simba kukutana kujadili migogoro

Na Widimi Elinewinga

KIKAO cha Kamati ya Utendaji Klabu ya Simba leo kinatarajia kukutana ili kujadili migogoro inayoisibu klabu hiyo jijini Dar-Es-Salaam.

Akiongea ofisini kwake mwishoni mwa juma, Mwenyekiti Msaidizi wa Klabu hiyo, Juma Salum alisema kuwa baada ya kukaa Jumamosi hii, siku inayofuata atatangaza rasmi tarehe ya Mkutano Mkuu.

"Tumeamka na maazimio kwamba mara tu baada ya kurudi Kagera tumekuta kuna vurugu kubwa tu kwamba wanachama wanataka mkutano lakini kwa bahati nzuri, sisi tulikuwa na mikakati hiyo mapema," alisema Salum.

Baadhi ya wanachama wa Simba wanataka Mkutano huo ufanyike mapema ili waweze kuondoa tofauti zilizopo kati ya Mweka Hazina Msaidizi, Mohamed Mwinyi na Katibu Mkuu wa Simba, Kassim Dewji.

Mgogoro huo ulimpelekea Mwinyi kusimamishwa.

Mkorofi mwingine 'kuumana' na Tyson Oktoba

NEWYORK, Marekani

MABONDIA wawili wenye sifa lukuku za kutumia mbinu mbaya za kupigana wawapo ulingoni, Mike Tyson na bondia wa Poland, Andrew Golota, wanatazamiwa kupanda ulingoni kuchapana makonde mwezi ujao.

Pambano hilo linalosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa ndondi ili kumjua bingwa wa kucheza "rafu" na kukiuka kanuni za ndodi, linatarajiwa kufanyika tarehe ya 20 ya mwezi huo wa Oktoba, mwaka huu katika ukumbi wa Detroit Piton, wa Chama cha Mpira wa Kikapu (NBA).

Kwa Mike Tyson, hilo litakuwa ni pambano la kwanza kulifanyia nchini Marekani baada ya pambano lake na Orlin Norris lililokuwa sio la kuwania mkanda wowote lililomalizika kwa utata.

Katika jumla ya mapambano yake 48, Mike Tyson alishinda 42 kwa Knock out na kushindwa matatu tu.

Tyson atakuwa anapigana nchini Marekani baada ya kushinda mapambano mawili nchini Uingereza Juni 24, alipomtoa kwa Knocout, Lou Saverese kwa raundi ya kwanza kunako sekunde ya 38.

Miezi mitano iliyopita, Mwanamasumbwi Julius Francis, alionja joto ya jiwe toka kwa Mike Tyson baada ya kutolewa kwa KO kunako raundi ya pili katika pambano lililofanyika Manchester na kushuhudiwa na mashabiki takribani 22,000.

Tyson ambaye ni bingwa wa zamani wa ngumi za uzito wa juu duniani, hivi karibuni alipigwa faini ya Dola za Kimarekani 187,500 na Bodi ya Nidhamu ya Ngumi ya Uingereza, baada ya kumsukuma mwamuzi, John Coyle ambaye alikuwa tayari amesimamisha pambano kati yake na Saverese.

Wanandondi hao wote, Mike Tyson na Andrew Golota, wote waliwahi kufutiwa mapambano kwa kosa la kutumia mbinu mbovu za kimichezo wawapo ulingoni.

Tyson alifungiwa baada ya kumng’ata sikioni mara mbili, mpinzani wake, Evander Holyfield katika pambano lililofanyika mwaka 1997.

Alinyang’anywa leseni yake na Tume ya Ngumi ya Nevada, ilimpiga faini ya Dola za Kimarekani milioni tatu.

Golota alishapigana mapambano 36 na kushindwa manne. Mapambano 29, alishinda kwa Knockout. Alifungiwa kucheza ndodi baada ya kumpiga ngumi ya chini ya mkanda mpinzani wake, Riddick Bowe katika pambano lao la mwaka 1996.

Pia, bondia huyo aliwahi kufungiwa kwa kumpiga begani bondia, Samson Po’hua, mwaka 1995 na mwaka 1996, alimsukuma kwa kichwa, bondia Dannell Nicholson. Hata hivyo, Golota alishinda mapambano hayo.

LIGI DARAJA LA NNE TEMEKE;

Alwatan yaipeleka mputamputa Mzimu

Na Mariam Kossey

TIMU ya Soka ya Alwatan imeitoa jasho timu ya Mzimu baada ya kuifunga mabao 3-0 katika mpambano wa Ligi Daraja la Nne wilaya ya Temeke, uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Kigamboni jijini Dar-Es-Salaam.

Katika mchezo huo uliochezwa juzi, bao la kwanza la Alwatan liliingia kimiani kunako dakika ya 11 ya mchezo baada ya piga nipige iliyotawala uwanja katika lango la Mzimu na kumpa nafasi Omary Mohamed kupiga shuti kali lililo mweka pembeni kipa wa Mzimu, Michael Kambangwa na kutinga golini na mnamo dakika ya 30, Omary Mohamed, alipata nafasi nyingine na kufunga bao la pili.

Nafasi pekee ya timu ya Mzimu ilikuwa katika dakika ya 34 wakati Fadhili Juma, alipopiga shuti la mita 25 hivi, lililoishia mikononi mwa kipa wa Alwatan, Charles Ngalya.

Goli la la salama lililofungwa na Juma Kibanda, liliingia dakika ya 59 baada ya Kibanda kugombea mpira na Omary Mohamed.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho kati ya Mzizima na KKK.

Askofu ahimiza vijana kushiriki michezo

Na Lazaro Blassius, Tanga

ASKOFU wa Jimbo Katoliki la Tanga, Mhashamu Anthony Banzi, amewataka vijana nchini kufanya kazi kujielimisha na kushiriki michezo badala ya kujingiza katika vitendo viovu.

Mhashamu Banzi alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akihutubia mamia ya vijana walioshiriki katika kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu kilichofanyika kwenye ukumbi wa Kanisa Kuu la jimbo hilo eneo la Chumbageni.

Alisema kwa kuwa michezo hujenga afya na kuimarisha urafiki baina ya jamii, vijana hawana budi kuishiriki na hivyo kuepuka vitendo viovu kama uasherati, imani potofu, utoaji mimba, madawa ya kulevya na mapenzi haramu.

Katika mawaidha yake yaliyochukuwa zaidi ya saa moja, Askofu Banzi amewataka vijana kuheshimu utu na uhai wa wengine kwa kuwa waaminifu na wavumilivu,, pamoja na kutimiza wajibu wao kwa wazazi, Kanisa na Taifa.

Katika kilele cha maadhimisho hayo, pia ulizinduliwa Umoja wa Vijana Wakatoliki jimboni humo (UVIKATA).

Alisema ingawa jimbo hilo limechelewa kuunda umoja huo, bado anayo matumaini kuwa utakuwa ni chombo cha kuwaunganisha vijana wote.

Kilele cha maadhimisho hayo kulitanguliwa na ibada ya hija iliyoanza kwa maandamano kutoka Kanisa la Mtakatifu Theresia, Ngamiani huku vijana wakiwa wamebeba mabango yanayolaani matendo maovu, mmomonyoko wa maadili na ukosefu wa ajira.

"Pamoja na kuweka mabango yanayotangaza matumizi ya kondomu kila barabara, pamoja na kugawa mipira hiyo hata kwa wanafunzi, ukimwi bado unaendelea kuua vijana. Jiepusheni na mafundisho hayo. Kuweni watii kwa Neno la Mungu. Leo hata dawa ya Ukimwi ikipatikana; Amri ya Sita USIZINI itabaki pale pale," alisema Askofu Banzi akikemea uasherati kwa kujidanganya kutumia kondomu dhidi ya ukimwi.

Katika sherehe hizo Mkurugenzi wa Idara ya Walei Jimbo, Bw. Sylvesta Mgoma na Katekesi Sr.Valleria Morasa walishiriki pamoja na Mlezi wa Vijana Jimbo Padre Titus Mdoe ambaye pia ni Mkurugenzi wa Miito.

FAT yaomba Msajili aongeze muda wa marekekebisho

Na Pelagia Gasper

KAMATI ya Utendaji wa Chama cha soka nchini(FAT), imemuomba Msajili wa vyama vya michezo na klabu nchini kuiongezea muda wa kufanya marekebisho ya Katiba ya chama hicho.

Mwenyekiti wa FAT Kanali Idd Kipingu, aliliambia gazeti hili kuwa ombi hilo lilifikiwa kwenye kikao cha kamati hiyo kilichofanyika Jumapili iliyopita yalipo Makao Makuu ya chama hicho jijini Dar-Es-Salaam.

Kipingu alisema kuwa, kamati yake ilifikia uamuzi huo kwa vile ilibaini kuwa kazi ya kurekebisha Katiba hiyo inahitaji utafiti wa kina wa kuimarisha mahitaji ya kitaalamu ambayo yanakosekana kwenye Katiba ya sasa.

"Na kazi hiyo inahitaji kuwashirikisha wataalam wengine kutoka nje ya kamati yetu hivyo nao hatujui watahitaji muda gani kufanikisha kazi hii," alisema.

Hivi karibuni Msajili aliyakataa marekebisho ya Katiba ya chama hicho yaliyofanywa mjini Morogoro, ambapo aliruhusu Uchaguzi Mkuu wa chama hicho kufanyika kwa masharti kuwa, uongozi mpya ufanye marekebisho hayo katika muda usiozidi siku 90 tangu kuingia madarakani. Uongozi mpya ulichaguliwa Agosti 6, mwaka huu mjini Dodoma.

Aidha, Kipingu alisema kikao hicho kiliunda kamati ndogondogo sita ili kuisaidia katika utendaji wa shughuli za FAT.

Alizitaja kamati hizo kuwa ni kamati ya Fedha na Mipango, Kamati ya Ufundi, Kamati ya Nidhamu na Rufaa, Kamati ya Waamuzi, Kamati ya Tiba na Kamati ya Wanawake na watoto.

Kuhusu usimamizi wa Ligi Kuu ya Bara. Kipingu alisema Kamati hiyo iliamua kuwa Chama cha Soka Mkoa wa Dar-Es-Salaam(DRFA), kisimamie mechi za Dar-Es-Salaam kama ilivyo kwa vyama vya mikoa mingine.

Zamani DRFA ilikuwa ikibanwa na FAT katika suala hilo.

Pia Kipingu alisema kikao hicho kilikemea vikali fujo zinazotokea kwenye mechi za ligi kuu ya bara iliyokwisha hivi karibuni.

Ngorongoro Warrious ilifungwa kwa kuwa iliibiwa Msumbiji-Mokake

Na Widimi Elinewinga

TIMU ya Taifa Ngorongoro Warrious imewasili nchini ikitokea Maputo Msumbiji ilikoenda kucheza mchezo wa marudiano na timu ya vijana ya nchi hiyo na Kocha wake, Mokake amesema moja ya sababu za kufungwa kwao, ni kuibibiwa vifaa.

Akiongea katika ofisi za Chama cha Soka nchini,(FAT), Kocha Mkuu wa timu hiyo, Ernest Mokake, alisema kuwa wachezaji wa Ngorongoro Warrious, walicheza kwa nguvu zote lakini siku hiyo ilikuwa si siku yao ya kuendelea na michuano hiyo.

Baada ya kurejea nchini juzi Mokake amesema kubwa lililowaathiri wachezaji wake ni pamoja na kupotelewa na vifaa vyao ambavyo imesemekana kuwa vilipotea katika uwanja wa ndege wa Malavix katika mazingira yenye utata.

Timu ya Ngorongoro ilifika tamati yao katika uwanja wa Machari wa nchini Msumbiji kwa kutolewa kwa penalti nne kwa mbili.

Kufungwa huko kuliamsha hisia kwa mashabiki wa soka hapa nchini katika kufahamu endapo timu hiyo itavunjwa kama ilivyo ada kwa viongozi wengine wa FAT waliotangulia.

Wakati huo huo: Mwenyekiti wa Chama cha kusakata kabumbu nchini Luteni Kanali Idd Kipingu, amesema kuwa timu zote za vijana hazitavunjwa, bali zitaimarishwa na kupewa mechi nyingine za kujiandaa na michuano ya kimataifa.

Kwa upande wa Ngorongoro Warrious, Kipingu alisema kuwa timu hiyo itakuwa inakutana kwa nyakati tofauti kambini ili kuweza kufanya mazoezi ya pamoja.

"Na timu nyingine ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 17 Kilimanjaro Boys, wao wataunganishwa katika michuano kama ya Kombe la Nyerere ili waweze kupata uzoefu wa michezo mikubwa," alisema Kipingu.