Make your own free website on Tripod.com

Michezo

KINYANG’ANYIRO CHA LIGI KUU YA MUUNGANO:

Mtibwa yatamba kuinyuka Yanga, kutwaa Ubingwa

Na Gerald Kamia

TIMU ya Mtibwa Sugar ya mjini Morogoro, imetamba kuwa itatwaa ubingwa wa Muungano kupitia mgongoni mwa timu ya Yanga.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini Dar-Es-Salaam, Kocha Mkuu wa timu ya Mtibwa John Simkoko, amesema kuwa haoni pingamizi lolote la kuizuia timu yake kutwaa ubingwa wa Muungano.

Simkoko amesema kuwa, timu yake haihofii timu yoyote katika ligi hiyo na kudai kuwa, watafanya kama walivyofanya katika Ligi Kuu ya Safari Lager iliyomalizika na kwmba, itaifunga tena timu ya Yanga na kutangaza ubingwa.

"Timu yangu safari hii inataka kuonesha maajabu katika soka la Tanzania ambalo limejaa usimba na uyanga. Tunataka tutwae vikombe vyote ili tukomeshe tabia hiyo ya usimba na uyanga ambayo inarudisha nyuma maendeleo ya soka hapa nchini," alitamba Simkoko.

Akizungumzia kuboronga kwa timu yake katika mechi za kwanza, kocha huyo alisema kuwa, hiyo ndio kawaida ya timu yake kufanya vibaya katika mechi za mwanzo kwani hata kwenye Ligi Kuu ya Safari Lager, timu hiyo ilianza hivyo na hatimaye, ikatwaa ubingwa.

Hatumtimui Shungu ng'o - Yanga

Na Gerald Kamia

KLABU ya Soka ya Yanga ya jijini Dar-Es-Salaam, imesema haina mpango wowote wa kumtimua Kocha wake Mkuu, Roul Shungu kama inanavyodaiwa na baadhi ya wanachama wa timu hiyo.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi wiki iliyopita jijini Dar-Es-Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Timu hiyo Isack Shekiondo, alisema kuwa, kwa sasa uongozi wa klabu hiyo haufikirii jambo kama hilo kwa kuwa hawaoni sababu za msingi za kumtimua kocha huyo.

Alisema hizo ni chuki binafsi zinazofanywa na baadhi ya wanachama wa klabu hiyo ya soka. wanaotumiwa na baadhi ya watu kwa manufaa yao na kuwataka wanachama hao kuwa makini katika kutoa madai yao.

‘Mwaka jana timu yetu imemaliza ligi ikiwa imeshika nafasi ya pili baada ya kuukosa ubingwa katika hatua za mwisho na sasa timu yetu, ndiyo inayoongoza Ligi Kuu ya Muungano, ikiwa ndio timu pekee ambayo haijafungwa na timu pekee ambayo imetikisa nyavu za timu pinzani mara nyingi. Sasa hao wanataka mafanikio gani?" alisema Shekiondo.

Makamu Mwenyekiti huyo amewataka wana Yanga kuelewa kuwa, hata kama uongozi wa klabu hiyo utachukua hatua za kumtimua kocha huyo wajue kwamba hakuna kocha yeyote wa Kitanzania atakayeiletea mafanikio kama wanayoyataka wanachama hao.

Alidai kuwa baadhi ya makocha maarufu nchini, walishaifundisha klabu hiyo lakini, hakuna aliyeiletea mafanikio yeyote kati ya yale wanayoyataka wao katika timu hiyo.

Kauli ya Shekiondo imekuja kufuatia baadhi ya wanachama wa timu hiyo kutoa shinikizo kwa uongozi wa klabu hiyo kumtimua Kocha Mkuu wa timu hiyo kwa madai kuwa, kiwango chake cha ufundishaji kimeshuka.

Ligi Kanda ya Dar sasa kufanyika Novemba

Na Widimi Elinewinga

Ligi ya Kanda ya Dar es Salaam imepangwa tena kufanyika mwanzoni mwa mwezi Novemba mwaka huu

Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Soka mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) Athuman Nyamlani Athumani alisema wiki hii kuwa kusogezwa mbele kwa ligi hiyo kumesababishwa na kuchelewa kumalizika kwa ligi za wilaya ambazo mpaka hivi sasa bado zinaendelea.

Awali ligi hiyo ilikuwa imepangwa kuanza rasmi Oktoba 22 mwaka huu, lakini vyama vya soka vya Temeke (TEFA) na Kinondoni (KIFA) bado zinaendeleza Ligi ya Daraja la Tatu na Nne.

Katibu huyo aliongeza kuwa ligi itachezwa kwa mfumo mpya ambao hakuutaja isipokuwa alisema itamalizika kabla ya mwaka 2001 kwani michezo itachezwa katika viwanja vingi.

Akifafanua kuhusa suala la madai ya kutoa msaada kwa ajili ya kuchangia kuendeleza ligi hizo za wilaya alisema hilo ni jukumu la chama cha wilaya husika kuwalipa waamuzi

MASHINDANO YA UMITAVUTA

Kanda ya Mashariki wawanyuka Kusini 2-1

Na Wiliam Kapawaga, Morogoro

TIMU ya soka ya Kanda ya Mashariki, Jumatano iliyopita iliinyuka timu ya Kanda ya Kusini kwa bao 1-0 katika moja ya michezo ya kitaifa ya UMITAVUTA uliofanyika katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Kigurunyembe katika manispaa ya Morogoro.

Bao hilo la pekee katika mchezo huo, lilipatikana katika dakika ya sita ya kipindi cha kwanza baada ya mchezaji Leatus Magoda, kupata pasi safi kutoka kwa Joseph Mwakibibi na kuiunganisha kimiani kiustadi.

Katika pambano hilo la kusisimua, Kanda ya Kusini uliumiliki mpira kwa muda mwingi lakini safu yao ya ushambuliaji ilimimina mabao mengi nje ya lango.

Kabla ya pambano hilo, kulikuwa na pambano lingine la soka kati ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Kanda ya Kati ambapo timu zote zilitoka sare ya 2-2.