Michezo

SUALA LA UTEUZI WA MAKOCHA WA TIMU YA TAIFA:

Uamuzi wetu ni wa mwisho - FAT

Na Modest Msangi

CHAMA cha Soka nchini(FAT), kimesema kina uamuzi wa mwisho katika uteuzi wa makocha wa timu ya Taifa.

Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa FAT, Amin Bakhroun ambapo amesema kuwa FAT imezingatia sifa za makocha pamoja na viwango vyao vya ufundishaji.

Kauli hiyo imekuja siku chache baada ya taarifa iliyotolewa na Meneja wa Timu ya Kajumulo ,Juma Simba, aliyekuwa akidai uteuzi wa makocha wa timu ya Taifa Tanzania Bara, Abdallah Kibadeni (King Puta) na Msaidizi wake Sunday Kayuni, haukufuata taratibu za uteuzi wa makocha wa Timu ya Taifa.

Katika taarifa yake, Simba alidai kuwa kuteuliwa kwa makocha hao kumeonesha dhahiri upendeleo.

Alisema ingawa waliteuliwa, makocha hao hawana uwezo wa kufundisha timu ya taifa kwa kile alichokieleza kuwa kufanya vibaya kwa timu walizokuwa wakifundisha awali kabla ya uteuzi huo.

Alitoa mfano wa makocha ambao labda ndio wangestahili kuteuliwa kuwa ni pamoja John Simkoko wa Mtibwa Sugar ya Morogoro ambaye timu yake ni bingwa wa Ligi Kuu ya Safari Lager kwa kipindi cha miaka 2 mfulululizo.

Mwingine ni Jamhuri Kiwelu wa timu ya Kajumulo World soccer. Alisema hao ni baadhi ya makocha ambao timu zao ni nzuri na zilifanya vizuri katika Ligi Kuu ya Safari Lager, Tanzania Bara.

Kaimu Katibu Mkuu huyo wa FAT, Bakhroun alisema FAT haiwezi kuchagua kocha kwa kutumia vigezo vya timu anayofundisha.

"Kama ni hivyo FAT itakuwa na makocha wapya kila mwaka kwa maana mwaka huu Mtibwa, mwaka kesho Tukuyu atakuwa bingwa, hivyo atachukuliwa kwa sababu wamekuwa mabingwa, hawateuliwi namna hiyo"alisema.

Aliongeza kuwa FAT inafuata taratibu zake na vigezo mbalimbali ikiwa ni pamoja na uwezo wa kufundisha na elimu ya makocha.

Aliwataja Abdalla Kibadeni na Sunday Kayuni kuwa ni miongoni mwa makocha wazuri walioteuliwa na FAT kufundisha Timu ya Taifa ya Tanzania Bara.

Alisema makocha hao wana uwezo wa kufundisha na akawataka mashabiki wa soka nchini, wasubiri kuona watakachokifanya makocha hao wa timu ya taifa katika Mashindano ya Challenge yatakayofanyika baadaye mwaka huu.

Makocha hao Abdalla na Sunday, waliteuliwa hivi karibuni na FAT kuwanoa wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania Bara ambapo watashirikiana na makocha wa Zanzibar katika kuteua timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

LIGI DARAJA LA TATU

Bogoyo yainyuka Kambarage 1-0

lNew Kids nayo yanyukwa na Blue Eangle

Na Widimi Elinewinga

Timu ya soka ya Bogoyo mwishoni mwa wiki hii ilifanikiwa kuichabanga timu ya

Kambarage jumla ya goli 1-0 katika mechi za ligi daraja la tatu zinaendelea jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo uliofanyika katika uwanja wa CCM Msasani, goli hilo la pekee kwa

timu ya Bogoyo lilipatikana katika dakika ya 74 kipindi cha pili.

Goli hilo liliingizwa kimiani baada ya timu hiyo kufanya mabadiliko ya kuutawala mpira ambapo mchezaji James Masimu baada ya kupata pasi toka kwa mchezaji Ruben Julius na kuachia shuti kali hadi golini.

Katika kipindi cha kwanza Kambarage walionyesha kuumiliki mpira lakini hawakufanikiwa kuzitoboa nyavu za wapinzani wao na hivyo kuwafanya kukosa mabao mengi.

Wakati huohuo, timu ya Blue Eagle nayo iliichabanga timu ya New Kids jumla ya mabao 2-1 mchezo uliofanyika katika uwanja wa Karume katika mfululizo wa ligi daraja la nne Maniospaa ya Ilala.

Blue Eagle walipata bao lao la kwanza mnamo dakika ya 32 kupitia mchezaji wao Mwinyi Hasan baada ya kupiga shuti kali lililokwenda moja kwa moja na kujaa wavuni.

Bao hilo la Blue Eagle lilitawala hadi mwisho wa kipindi cha kwanza na katika kipindi cha pili dakika ya 88 mchezaji Nico Mdifwa aliipatia New Kids bao la kusawazisha.

Bao hilo la kusawazisha liliamsha makali ya Blue Eagle na kuifanya kuchachamaa ambapo katika dakika ya 90 mchezaji Evans Mdwela aliipatia timu yake bao la ushindi na timu hiyo kuondoka kiwanjani hapo ikiwa kifua mbele.

MAONESHO YA BIDHAA ZA WAWATA

Dar Es Salaam yanyakua kombe la ushindi

Na Dalphina Rubyema

JIMBO Kuuu Katoliki la Dar-Es-Salaam limejinyakulia kombe la ushindi katika maonesho ya bidhaa za Wanawake Wakatoliki Tanzania (WAWATA) yaliyomalizika mwanzoni mwa wiki katika nyumba ya makumbusho Jijini.

Akikabidhi kombe hilo kwa washindi,Waziri wa Jamii, Wanawake na Watoto,Bibi Mary Nagu, alisema kuwa bidhaa mbalimbali zilizooneshwa katika maonesho hayo kutoka majimbo mbalimbali ya Kanisa Katoliki nchini kwa kutumia rasilimali asilia zinaonesha jinsi gani Wanawake wanaweza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambavyo ni vizuri na imara kuliko vile vya kutoka nje ya nchi.

"Yaani bidhaa zenu ni nzuri mno, swali linabaki kujiuliza, kwanini tutumie chupa ya chai wakati tuna vibuyu vilevyotengenezwa kwa umahiri kabisa na wanawake wa hapa hapa Tanzania?' alihoji Bibi Nagu.

Katika maonesho hayo,Jimbo Kuu la Dar-Es- Salaam pamoja na kunyakua kombe la ushindi,lakini vile vile walijinyakulia kitita cha shilingi 50,000.

Jimbo lililoshika nafasi ya pili katika maonesho hayo ni Jimbo Katoliki la Arusha ambalo lilipewa zawadi ya sh. 100,000 wakati Jimbo Katoliki la Bukoba lijinyakulia kitita cha shilingi 80,000 kwa kushika nafasi ya tatu.

Wakati Jimbo Katoliki la Moshi lilizawadi sh.60,000 kwa kushika nafasi ya nne,Jimbo Katoliki la Njombe lililoshika nafasi ya tano lilijizolea kitita cha sh.40,000.

Waziri Nagu vile vile aliyakabidhi sh.10,000 majimbo mengine yaliyoshiriki maonesho hayo .

TPBS wakutana kumjadili Katibu Mkuu

Na Mwandishi Wetu, Moshi

KAMISHENI ya ngumi za kulipwa nchini (TPBC) inakutana leo Jumamosi hii katika ukumbi wa hoteli ya Friends Corner jijini Dar-Es-Salaam, kumjadili Katibu Mkuu wa Kamisheni hiyo Bw. Fidelis Haines ambaye anatuhumiwa kwa rushwa.

Rais wa Kamisheni hiyo Onesmo Ngowi, amesema TPBC itakutana kujadili pamoja na mambo mengine, mgogoro uliojitokeza katika Kamisheni hiyo kati ya mabondia na Katibu Mkuu wao ambapo mabondia walikuwa wakidai kwamba alikuwa akiwaomba hongo ili awapangie mapambano.

Ngowi alisema kuwa binafsi amesikitishwa na hatua hiyo ya utendaji katika Kamisheni hiyo iliyojitokeza hivi karibuni.

Alisema yeye binafsi kwa kipindi kirefu amekuwa mjini Moshi kwa shughuli zake binafsi ambapo nafasi yake ilikaimiwa na Bw. Meky Mapee ambaye ni mjumbe wa kamati ya TPBC.

Amesema taarifa alizopokea ni kwamba, Katibu Mkuu Fidelis hakufungiwa nje ya ofisi bali kilichofanyika ni kubadilisha vitasa vya ofisi hiyo iliyopo jengo CRDB tawi la Azikiwe.

Alidai kuwa baada ya kugundua kuna baadhi ya watu wenye funguo za ofisi hiyo ambao si viongozi, waliamua kubadilisha vitasa na kumkabidhi funguo mpya Dk. Mapee.

Viongozi waliohusika na ofisi hiyo walitakiwa kuchukua funguo hizo kwake na sio kama ilivyotangazwa kwamba Katibu Mkuu huyo alifungiwa nje.

Amesema Mkunato huu wa Jumamosi unaofanyika saa 8 mchana, utatoa nafasi kwa mabondia kutoa dukuduku juu ya Katibu Mkuu.

Bw. Onesmo Ngowi ambaye pia ni Raii wa IBF Afrika, alikataa kusema hatua ambayo itachukuliwa endapo itabainika kuwa Katibu Mkuu huyo alikuwa akiomba hongo kwa mabondia.

"Tusubiri Jumapili mara baada ya mkutano huo, tutaeleza wazi yote yatakayoamriwa maana mkutano huo utawashirikisha wanachama wote pamoja na mabondia," alisema.

Alipoulizwa kuhusu swala la tuhuma za Katibu Mkuu alikata simu.