Michezo

ROBO FAINALI YA KOMBE LA FAT

Nani kutamba Jumapili, Simba au Yanga?

l Shungu asema wataamua tena mnyama

Na Gerald Kamia

HATIMAYE ule mpambano wa kukatana shoka kati ya mahasimu wawili wa soka hapa nchini Yanga na Simba, kugombea kombe la FAT umepangwa kufanyika Jumapili hii kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, mjini Arusha.

Mchezo huu ni muhimu kwa timu zote mbili kwani kila timu inawania kuingia kwenye nusu fainali ya kombe la FAT ambapo mshindi katika kombe hilo, ataiwakilisha nchi katika kombe la washindi barani Afrika.

Hata hivyo, mchezo wa kesho utakuwa mgumu na wakuvuta nikuvute ukichukulia kuwa kila timu imeahidi kutoka na ushindi mnono.

Awali, mchezo huo ulipangwa kufanyika Novemba 1, mwaka huu katika uwanja wa Taifa na kuahirishwa kutokana na tarehe hiyo kutarajiwa kutumika kumuapisha katika uwanja huo wa Taifa.

Simba, kesho itashuka dimbani huku ikikumbuka kipigo ambacho ilikipata baada ya kufungwa na Yanga kwa magoli 2-0, katika mchezo wa Ligi Kuu ya Safari Lager ambayo imemalizika hivi karibuni.

Klabu hiyo ya Simba, sasa inataka kulipiza kisasi kwa vijana hao wa mtaa wa Jangwani jijini Dar-Es-Salaam.

Kocha Mkuu wa Timu ya Yanga, Mkongo, Roul Shungu, amesema kuwa kesho atashusha dimbani kikosi cha mauaji chenye mchanganyiko wa damu changa na wazoefu aliowataja kuwa ni Edibili Lunyamila, Idd Moshi, Mohamed Hussen ambao watashirikiana na Fred Mbuna, Azizi Hunter na Abdukadri Tash, ambao Shungu ametamba kuwa, wataisambarataisha vibaya Simba.

Naye Kocha Mkuu wa timu ya Simba, King Kibadeni Mputa, ametamba kuwa timu yake haitokubali tena kufungwa na vijana hao wa Jangwani na akazidi kudai kuwa, timu yake itatumia kikosi kipya kabisa cha wachezaji.

Amewataja wachezaji baadhi atakaowatumia kesho kuwa, ni John Thomasi, Masamaki, Said Maulid, Shauri Idd na Steven Mapunda Garincha ambao ametamba kuwa wana kiu kubwa ya kuifunga Yanga.

....Tarimba apania kuwanyuka Simba kuifurahisha Mobitel

Na Dalphina Rubyema

MABINGWA wa Ligi ya Muungano, Klabu ya soka ya Yanga ya jijini Dar-Es-Salaam, wameahidi kunyakua ushindi katika mechi ya kuwania kombe la FAT katika mchezo ambao utachezwa Jumapili hii mjini Arusha ambapo Yanga itapambana na watani wake wa jadi Simba.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga, Tarimba Abbas, wakati timu yake ilipokuwa ikikabidhiwa zawadi ya ushindi wa Kombe la Ligi ya Muungano kutoka kwa wadhamini wake, Kampuni ya Simu za Mkononi ya Mobitel.

Katika makabidhiano hayo, yaliyofanyika jijini Dar-Es-Salaam, Tarimba alisema kuwa, timu yake itacheza kwa ustadi mkubwa kuhakikisha inanyakua tena ubingwa wa kombe la FAT.

Tarimba alisema lengo kubwa la kupania ushindi huo, kuendelea kuwatia moyo wadhamini wao wa Mobitel.

Katika hafla hiyo, Meneja wa Mobitel nchini, Jim Bell, alitoa "kadi poa" yenye thamani ya dola 50(sawa na shilingi 40,000) kwa kila mchezaji wa timu ya Yanga.

Meneja huyo pia alitoa zawadi ya simu ya mtandao mpya wa Buzz GSM kwa mchezaji bora wa Ligi ya Muungano, Edibily Lunyamila, ambaye alipata nafasi hiyo baada ya kupigiwa kura na wachezaji wenzake wa timu hiyo ya Yanga.

Bill alisema kuwa, kampuni yake itaendelea kuidhamini timu hiyo ya Yanga kwani kiwango chake cha uchezaj kinaridhisha.

"Kiwango chenu cha uchezaji kinaridhisha mbali na kunyakuwa ushindi wa Ligi ya Muungano, mna uwezo pia wa kuchukua ubingwa wa Afrika ingawa FIFA imeifungia Tanzania," alisema Bill.

Simba yakana kuchuja wachezaji

l Yasema ni baada ya Kombe la FAT

Na Mwandishi Wetu

Klabu ya soka ya Yanga imesema kuwa kwa sasa haijamuacha mchezaji yeyote kwa kuwa zoezi hilo litafanyika mara baada ya kumalizika kwa kombe la FAT.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi yalipo Makao Makuu ya Klabu hiyo, Jangwani, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Fred Felix Minziro, amesema kuwa ameshangazwa na baadhi ya wachezaji ambao hawafiki mazoezini eti kwa madai kuwa wamesikia kwenye vyombo vya habari kuwa wameachwa.

Kocha huyo amewataka wachezaji wote wa timu hiyo kufika mazoezini kwani timu hiyo haijamuacha mchezaji yeyote kwa kuwa zoezi la kuchagua wachezaji halijafanyika na badala yake, litafanyika mara baada ya kumalizika kwa kombe la FAT.

Alidai kuwa, asiyefika mazoezini ndiye atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye timu hiyo.

Aidha, Minziro ameongeza kusema kuwa, timu yake kwa msimu huu, haitosajili wachezaji wengi kwani kusajili wachezaji wengi ni kuipa mzigo klabu hiyo.

"Tutakachoangalia msimu huu ni mchezaji bora. Ni bora tubaki na wachezaji kumi na tano ambao wanajituma, kuliko kukaa na idadi kubwa ya wachezaji ambao wataipa mzigo timu," alisema Minziro.

DSJ kumenyana na DSA leo

Na Widimi Elinewinga

TIMU ya mpira wa miguu ya Chuo cha Uandishi wa Habari cha Dar-Es-Salaam (DSJ) leo inamenyana na watani wao wa jadi timu ya Chuo cha Uhasibu (DSA) katika uwanja wa nyumbani DSA jijini Dar-Es-Salaam.

Akizungumza na gazeti hili Kapteni wa DSJ ambaye pia ni Rais wa Chuo hicho, Renatus Mgongo, amesema kwamba ataupa umuhimu mchezo huo na atatumia mbinu zote kuhakikisha timu yake inaibuka na ushindi.

"Nitawatumia wachezaji wangu walewale ambao waliisambaratisha DSA katika mchezo wa awali," alisema Mgongo.

Katika mechi ya awali iliyofanyika katika kiwanja cha DSA, timu ya DSJ iliibugiza DSA jumla ya magoli 2-1.

Mchezo huu wa leo utakuwa ni mfululizo wa mechi za kirafiki za kuendeleza michezo na kudumisha ushirikiano biana ya chuo na chuo.

USAJILI WA WACHEZAJI MSIMU UJAO:

Hatutambui wachezaji wetu kusajiliwa Simba- Mtibwa

Na Gerald Kamia

KLABU ya soka ya Mtibwa imesema kuwa haitambui kusajiliwa kwa wachezaji wake wawili na klabu ya Simba ya jijini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini wiki iliyopita, Mratibu wa timu ya Mtibwa, Jamal Bayesel, amesema kuwa Mtibwa sio kwamba inawang’ang’ania wachezaji hao, bali inachotakiwa kufanya Simba, ni kufuata taratibu zinazotakiwa.

Bayser amesema kuwa, Mtibwa ni timu kubwa ambayo inaweza kuondokewa na wachezaji wake maarufu na ikasajili wengine wazuri kuliko hao walioondoka ila inachotakiwa kufanya kwa timu zinazowataka wachezaji hao, ni kufuata taratibu za uhamisho zinazotakiwa.

Mratibu huyo amesema kuwa kwa sasa timu yake imemruhusu mchezaji mmoja tu, ambaye taratibu za kuhama timu zimefuatwa na timu inayomhitaji mchezaji huyo aliyemtaja kuwa ni Yusufu Macho ambaye amesajiliwa na timu ya Moro United.

Kauli ya Mratibu huyo inafuatia kauli ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa Timu ya Simba, Kassim Dewji kudai kuwa timu ya Simba imekamilisha taratibu zote za usajili wa wachezaji akina Dua Said na Kassim Issa.

Alidai kuwa, wanandinga hao watasukuma ndinga katika timu ya Simba kwa msimu ujao wa ligi.