Michezo

SAKATA LA USAJILI WA WACHEZAJI MSIMU UJAO:

Simba yalipiza kisasi kwa Mtibwa

Na Gerald Kamia

KLABU ya soka ya Simba ya jijini Dar-Es-Salaam, imetimiza nia yake ya kulipiza kisasi kwa timu ya Mtibwa baada ya kufanikiwa kuwanyakua wanandinga wawili kutoka klabu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi jijini wiki hii, katibu Mkuu wa Simba, Kassim Dewji, amesema kuwa lengo lao ni kuwaonesha viongozi wa klabu hiyo ya Mtibwa kuwa simba si timu ya kuchezea hata kidogo

Katibu huyo amewataja wachezaji hao walionyakuliwa na timu yake kuwa ni mchezaji wa zamani wa timu hiyo, Dua Said, pamoja na beki wa pembeni wa Mtibwa na Taifa Stars, Kassim Issa ambaye amedai kuwa usajili wa Dua umekamilika na kuhusu Kassim wanamalizia taratibu za mwisho zitakazomwezesha mchezaji huyo kusakata ndinga kwenye klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi.

Dewji pia amewataja wachezaji wengine ambao tayari wameshasajiliwa na timu ya Simba kuwa ni John Masamaki kutoka(Reli), Hemed Mrisho(Prison) Joseph Kaniki (Kagera Stars) na wengine ambao amesema wanatoka katika timu za Nazareti, AFC ya Arusha.

Aidha, Katibu huyo amesema kuwa wamemruhusu mchezaji Patrick Betwel, kujiunga na timu ya Mtibwa kwa kuwa mchezaji huyo hakuwa na faida yeyote katika klabu hiyo ya Msimbazi na kuhusu mchezaji mwingine aliyeripotiwa kujisajili na timu za Mtibwa ni kiungo Willcef Cetto.

Dewji amesema kuwa mchezaji huyo ataichezea timu hiyo ya Mtibwa, ikiwa atavunja mkataba na timu ya Simba wa miaka miwili ikiwa ni pamoja na kurudisha kiasi fulani cha fedha za mkataba.

Wakati huo huo: Katibu huyo wa Simba amewataka wachezaji wote wa timu hiyo kuripoti mazoezini tayari kwa kujiandaa na mpambano wao wa kukata na shoka baina ya timu hiyo na mahasimu wao wakubwa, timu ya Yanga katika mchezo utakaofanyika Novemba, mwaka huu katika uwanja wa Taifa jijini.

Ubingwa bila kuifunga Simba haunogi-Shungu

Na Mwandishi Wetu

BAADA ya kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Muungano msimu huu, klabu ya soka ya Yanga ya jijini DAR-Es-Salaam, imetamba kuwa watawaadhibu vibaya watani zake wa jadi, timu ya Simba katika mchezo wa kugombea kombe la FAT ambao umepangwa kufanyika Novemba, mwaka huu katika uwanja wa Taifa jijini.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi wiki hii jijini Dar-Es-Salaam, mara baada ya kutawazwa rasmi kuwa mabingwa wa Muungano, Kocha Mkuu wa Timu ya Yanga ,Roul Shungu amesema kuwa ubingwa bila kuwafunga Simba haunogi kwa hiyo ubingwa utakuwa mzuri zaidi mara baada ya kutoa kipigo kwa Simba.

Kocha huyo mwenye asili ya Jamhuri ya Watu wa Kongo, amesema kuwa kwa sasa timu yake ni moto wa kuotea mbali kwani imesheheni kila idara na kuwatahadharisha Simba kuwa, lazima wafanya usajili wa kutosha kabla ya mpambano huo.

Shungu amesema kuwa kwa sasa usajili uliofanyika kwa timu hiyo ya Jangwani unamuumiza kichwa kwani wachezaji wote waliosajiliwa na timu hiyo, ni wazuri na ndio maana anapata tabu kuamua mchezaji yupi acheze na yupi asicheze.

Aidha, Shungu ameongeza kusema kuwa kwa kudhihirisha hilo, timu yake katika mchezo huo wa kombe la FAT, itawatumia wachezaji ambao hawakucheza kwenye kombe la Ligi Kuu ya Muungano ambao amedai wataisambaratisha Simba kuwa ni Azizi Hunter, Abdukadri Tash na wengine ambao wamesajiliwa na timu hiyo.

Wakati huo huo: kocha huyo amesema kuwa timu yake itaanza kumtumia mchezaji wake mpya aliyesajiliwa na timu hiyo kutoka katika timu ya Kajumulo, Salvatory Edward katika mpambano dhidi ya Mahasimu wao wakubwa, timu ya Simba ambao utafanyika Novemba , mwaka huu.

Shungu amkingia kifua Sauko

Na Widimi Elinewinga

KOCHA Mkuu wa klabu ya Yanga ya jijini Dar-Es Salaam, Raoul Shungu, amesema kuwa Katibu Mipango wa Klabu hiyo, Abdul Sauko, anafanya kazi nzuri katika klabu hiyo tofauti na baadhi ya wapenzi wanavyodhani.

Akizungumza na waandishi wa habari mwanzoni mwa wiki, Shungu alisema kuwa, Sauko amekuwa mstari wa mbele kuiletea klabu hiyo maendeleo.

Aliongeza kuwa wapenzi wa Yanga wanaomshutumu Sauko wakidai anaingilia upangaji wa timu hiyo wanamwonea.

Kocha huyo ambaye ni raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo(DRC), alisema Soka la Tanzania haliwezi kuendelea iwapo wapenzi na wanachama wataendelea kulumbana.

Aliwataka wapenzi wa timu wasitishe kulumbana na badala yake, wafikirie maendeleo ya Klabu hiyo ikiwa ni pamoja na ubingwa wa Ligi ya Muungano.

Kwa upande wake Sauko alisema hajawahi kumchukia mchezaji yeyote katika timu hiyo.

"Kama ningekuwa ninamchukia mchezaji wa timu, nisingefanya juhudi za kuwasajili," alisema Sauko na kuongeza,

"Nimchukie mchezaji halafu itakuaje mimi kama kiongozi mwingine wa klabu nimekuwa mstari wa mbele kuhakikisha tunasajili timu nzuri."

Sauko alikuwa akishutumiwa na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kwa madai anamwingilia Shungu katika upangaji wa timu.

TASWA kuchagua marubani wengine Desemba 31

Na Mwandishi Wetu

CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Nchini(TASWA),kimepanga kufanya Uchaguzi Mkuu wa viongozi Desemba 31, mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari katika mgahawa wa Food World jijini Dar-Es-Salaam mwanzoni mwa wiki, Katibu Mkuu wa TASWA, Mwina Kaduguda, alisema kuwa muda wa viongozi wa zamani wa miaka mitatu umefika tamati na hivyo TASWA hawana budi kupata marubani wengine.

Alisema, "Fomu za kugombea zitaanza kutolewa Novemba 24, mwaka huu na Oktoba 23 hadi Novemba 23 itakuwa ni siku za kuchukua fomu kwa ajili ya kujiandikisha uanachama kwa waandishi wanaotaka kujiunga na TASWA," alisema Kaduguda.

Aliongeza kuwa, gharama ya mtu atakayechukua fomu kwa ajili ya uanachama atalipa shilingi 2000 na ada ya uanachama kwa mwaka ni shilingi 3000.

Akielezea mafanikio ya TASWA katika kipindi cha miaka mitatu, alisema kuwa chama kiliweza kufanya mahusiano mazuri na makampuni na akatoa mfano wa kampuni ya Bia nchini TBL ambayo iliweza kuisaidia shilingi milioni 5.

Hivi sasa chama hicho kimeweza kupata ofisi ambayo kwa muda mrefu wamekuwa hawana na hivi karibuni, kutakuwa na sherehe kwa ajili ya ufunguzi wa ofisi hiyo.

Mtibwa yazidi kumlilia Keto

Na Wiliam Kapawaga, Morogoro

TIMU ya soka ya Mtibwa Sugar ya Morogoro bado inamuota kiungo wa kutumainiwa wa klabu ya Simba ya Dar-Es-Salaam, Wilcliff Keto na kudai kuwa, mchezaji huyo lazima atue kwenye kikosi cha timu ya Mtibwa kwa ajili ya Ligi Kuu ya Safari Lager Msimu ujao.

Mratibu wa klabu ya Mtibwa Sugar, Bw. Jamal Baisa, ameliambia KIONGOZI kuwa, timu hiyo bado inafanya mikakati mizito ili kuhakikisha kuwa Keto anasajiliwa na klabu ya Mtibwa.

Baisa amesema kuwa mpaka sasa mazungumzo baina ya Mtibwa na mchezaji huyo bado yanaendelea na akabainisha kuwa yamefikia hatua nzuri.

Amesema kuwa uwezekano wa mchezaji huyo kujiunga na Mtibwa ni mkubwa sana, kwa kuwa baadhi ya taratibu muhimu za kumsajili kiungo huyo zimekwisha kamilika.