Michezo

Ligi Kuu Bara yakumbwa na balaa

lTimu zatishia kwenda kortini

lRage asema hizo ni ngonjera tu

Na Mwandishi Wetu

LIGI Kuu ya Tanzania Bara Safari Lager Primier League imekumbwa na balaa kufuatia uamuzi wa timu zilizoshika dira kuahidi kwenda kortini.

Ligi hiyo ya mfumo mpya mwaka huu iinakaribia ukingoni na tayari timu za Reli ya Morogoro na Majimaji ya Songea zimeshuka daraja.

Wakiongea kwa nyakati tofauti mapema wiki hii viongozi wa timu za Reli na Majimaji walisema, kamwe hawatakubali kushuka daraja mwakani kwa madai kuwa ligi hiyo haina kibali cha Halmashauri Kuu ya FAT na imekuwa ikiendeshwa kwa Mizengwe.

‘Kwa ujumla ligi ilikuwa na mizengwe mingi hata FAT wenyewe wanakiri kuna waamuzi walioboronga. Kwa vigezo hivyo hatushuki daraja kamwe. Tutakataa rufaa hadi Mahakama Kuu ya Tanzania" alisema mmoja wa viongozi wa Reli juzi mara baada ya mechi dhidi ya Kajumulo World Soccer.

Kauli hyo inafuatia ile ya uongozi wa klabu ya Majimaji ya Songea mwishoni mwa wiki kukata rufaa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kupinga kushuka daraja.

Akijibu kitisho cha kwenda Kortini, Katibu Mkuu wa FAT Ismail Aden Rage alisema jijini kuwa viongozi hao wanaimba ngojera tu ili kufurahisha midomo yao lakini la msingi ni kwamba mwakani, watakuwa daraja la kwanza na si ligi Kuu.

Hadi sasa timu za Simba, Yanga na Kajumulo zote za jijini Dar Es Salaam, zimefanikisha kuingia katika timu nane bora, ligi ambayo itaanza mapema Juni mwaka huu.

Timu zingine zilizovuka hatua ya makundi ni Mtibwa ya Morogoro na hatma ya Coastal Union ya Tanga na AFC ya Arusha itajulikana kesho.

Yanga yashtukia utapeli wa Kajumulo

Na Mwandishi Wetu

TIMU ya Soka ya Yanga ya jijini imesema kuwa imeshtukia utapeli wa timu ya soka ya Kajumulo World Soccer ya jijini wa kudai kuwa haitapeleka timu uwanjani Jumapili.

Makamu Mwenyekiti wa Yanga Bw. Izack Shekiondo aliliambia gazeti hili kuwa wamegundua janja ya timu hiyo ya Kajumlo kuwa ni kutumia mbinu ya kusema kuwa haitapeleka timu uwanjani ilikuilaghai na kuifanya Yanga ibweteke na hivyo kutokufanya maandalizi.

Alisema yeye pamoja na wenzake wamebaini mbinu hiyo na kwamba watajiandaa vya kutosha ili Jumapili, washushe ‘Kossovo’ kwa klabu ya Kajumulo bila huruma.

Alisema hata kama Kajumulo itagoma, atapeleka kikosi cha pili na wao maangamizi yao yatakuwa ni yale yale.

Kauli ya Shekiondo inafuatia madai ya kocha Mkuu wa tumu ya Kajumulo, Jamhuri Kiwelu, kuwa wako tayari kulipa fani ya 500,000 kuwa FAT na kupatia Yanga pointi zote tatu kuwa hazina faida kwao.

Jamuhuri alisema uamuzi huo hauna maana ya kwamba wanaiogopa Yanga lakini wanataka kwenda Nairobi, Kenya na Lusaka Zambia kwa ajili ya mazoezi ya kujiandaa na ligi ya timu nane bora.

Kajumulo na Yanga zote zimeshaanza kucheza Ligi Kuu ya Nane Bora, baada ya kushika nafasi mbili za juu katika kundi la Mashariki.

'Maaskofu' wawanyuka 'Wamama Wakuu'

Na Christopher Kidanka, Morogoro.

Timu ya soka ya masista ya Mkude ya wanafunzi wa shule ya Sekondari ya Masista ya Bigwa mjini hapa imeichapa timu ya Tai ya shuleni hapo 1-0 katika pambano kambambe la kirafiki kusherekea mahafali ya kidato cha sita.

Katika mpambano huo uliosisimua hivi karibuni, timu ya Mkude inayoundwa na masista ilikuwa ikiigiza kama Maaskofu Katoliki wakati Tai, inayoundwa pia na masista iliigiza katika mchezo huo kama Mama Wakuu wa Mashirika ya kitawa.

Baada ya timu zote mbili kukaguliwa na mgeni rasmi, Askofu wa Jimbo Katoliki la Morogoro, Mhashamu Telesphor Mkude, mechi ilianza kwa kasi huku pande zote zikionesha umahiri mkubwa katika ulimwengu wa soka.

Katika mchezo huo wa kusisimua uliochekesha na kuwavutia mashabiki wa soka, Tai walionekana kushangiliwa kwa nguvu na masista ambapo Mkude ilikuwa ikishabikiwa na Mhashamu Askofu Askofu Telesphor Mkude pamoja na wageni waalikwa.

Bendi ya Matarumbeta ya Masista iliyokuwa ikitumbuiza ilifanya hali uwanjani hapo kusisimua kama ile ya Uwanja wa Jamhuri mjini hapa siku Mtibwa ilipocheza na Cotton Sports ya Cameroun.Mtibwa ilifungwa 1-0.

Mkude ambao walitawala mchezo, walicheza kwa kasi kwa muda wote waliokuwa uwanjani na walifanya mashambulizi mengi langoni mwa adui wao kiasi cha kumfanya mlingo wa Tai, Sr. Martha Joseph kufanya kazi ya ziada kuokoa majalo yaliyoelekezwa langoni kwake. Hadi mapumziko timu zote zilikuwa hazijafungana.

Wakati wa mapumziko bendi ya matarumbeta ilipita uwanjani kutumbuiza watazamaji waliokuwa wakiongozwa na Askofu Mkude.

Katika kipindi cha pili timu zote zilionekana kuwa na uchu wa magoli ambapo kila moja ilizi kufanya mashambulizi makali.

Hata hivyo, kasi hiyo ya wachezaji ilionekana kuwachosha haraka.

NI katika dakika ya 18 kipindi cha pili ndipo kosa la mchezaji wa Tai Sr. Anatolia Joseph la kuunawa mpira katika eneo la hatari liliwaliza Tai ambapo Sr. Blasia Bayege, baada ya kumhadaa kipa wa Tai, Sr. Martha, alipachika bao.

Hadi kipenga cha mwisho, timu ya soka ya wanawake ya Mkude (Maaskofu) ilitoka kifua mbele ikitamba baada ya kuwa imeifunga Tai (Mama Wakuu) kwa bao 1-0.