Michezo

WAKATI KLABU YA YANGA IMETANGAZA RATIBA YA UCHAGUZI

Simba yasema wapinzani wao pekee ni Prisons sio Yanga

Na Mwandishi Wetu

HUKU klabu ya Soka ya Yanga ikijiimarisha kwa kutangaza kufanya Uchaguzi Mkuu mwezi ujao, watani wao wa jadi Simba, wamewabeza na kudai sasa wapinzani wao wakuu ni Prisons, na sio Yanga tena

Wakiongea na gazeti hili jijini mwishoni mwa juma, wachezaji wa Simba walisema kuwa klabu ya Prisons ya Mbeya ndiyo pekee inayowapa shida hivi sasa wanapokutana nayo kutokana na uwezo wao wa kisoka na siyo Yanga tena.

"Tuliwabana sana katika mechi ya awali huko Mbeya, lakini walipokuja huku Dar, walibadilika na kucheza soka tofauti na tulivyowadhania" alikiri mmoja wa wachezaji hao kwa sharti la kutotajwa jina lake gazetini.

Mwaka jana klabu ya Simba , ilifungwa na Prisons katika Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, "Safari Lager."

Simba na Prisons, zote zimefanikiwa kuvuka katika hatua ya makundi ya Ligi Kuu, baada ya kushika nafasi mbili za juu, Simba ikiwa ya pili na Prisons ikiwa ya kwanza na zimeshiriki katika hatua ya pili yenye jumla ya timu nane tu.

Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Abassi Tarimba, "aliyebatizwa" jina la Yeltsin baada ya kufanikiwa kuiongoza Yanga katika mageuzi yaliyokuwa yameshindikana kwa muda mrefu, amesema Yanga itafanya Uchaguzi Mkuu mwezi Juni mwaka huu.

Amesema ametangaza tarehe ya uchaguzi huo baada ya Msajili wa Vyama kuyakubali mabadiliko ndani ya klabu yake yaliyoipelekea kuwa kampuni hali ambayo sasa itaiwezesha kuingia katika soko la hisa.

Aliwataka wana Yanga kutokuwa na hofu ya kuibuka kwa mgogoro mwingine katika klabu hiyo kama wa mwanzo aliosema ulikuwa ukichochewa na wanachama wachache.

Katika taarifa hiyo, Tarimba alisema kuwa Kamati ya Utendaji ya Yanga imekubali kwa kauli moja kuwa uchaguzi huo wa kuwapata viongozi wa kuchaguliwa ufanyike mwezi ujao.

Alisema pia kuwa kamati hiyo imepitia barua ya kuomba msamaha ya mchezaji, Saidi Mwamba Kizota ambaye alifungiwa kwa kosa la utovu wa nidhamu ambapo inadaiwa alikuwa akiwashawishi wenzake wagome mazoezi na sasa, amesamehewa rasmi na klabu hiyo.

Tarimba amesema Kizota amesamehewa na yupo huru kurudi uwanjani baada ya yeye mwenyewe kukiri makosa yake na kuomba radhi.

Madrid yachekelea ushindi

Madrid HISPANIA

KILABU ya Real Madrid ya Hispania imeelezea furaha yake ya ajabu baada ya kuwafunga Mabingwa watetezi wa Klabu bingwa ya Ulaya Manchester United, na mshindi wa pili Bayern Munich.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari vya Hispania, Mkurugenzi Mkuu wa Real Madrid Bw. Julio Senn alisema ni wazi kuwa ulimwengu wa soka sasa unaifahamu Bayenn na wao ndio bora zaidi duniani.

'Najua kwamba tumesalia na mita chache tu kufikia ubingwa lakini hilo si kubwa kwetu suala la kujivunia ni kuibuka kutoka katika hali mbaya na kufikia hali bora zaidi' alisema Mkurugenzi huyo.

Real inapambana na majirani zao Valencia pia ya Hispania katika fainali ya kombe hilo huko Paris Ufaransa mai 24 mwaka huu.

Hata hivyo Senn ameshatabiri kuwa pambano hilo litakuwa kali lakini watashinda na kuzidi kung'arisha nyota yao katika michuano hiyo ambayo ndiyo mikubwa katika ngazi ya vilabu kwa bara la Ulaya.

Hadi kufikia fainali Real Madrid imezitoa Manchester United na Bayern Munich baada ya kudorora kwenye raundi za awali.

Vilencia imefika fainali baada ya kuzifunga Lazio ya Italia na Barcelona ya Hispania ambayo ilikuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa kombe hilo.

 

Manchester yahaha kusaka wachezaji

MANCHESTER, Uingereza

BAADA ya kujeruhiwa mara mbili, Mabingwa wa Zamani wa Ulaya Manchester United wametangaza rasmi kuwa wanasaka wachezaji wapya wa kuiongeza nguvu safu ya ushambuliaji.

Kocha Mkuu wa timu hiyo Sir Alex Furgason alikaririwa na shirika la utangazaji la Uingereza B.B.C akisema kuwa tayari amepewa ruhusa na uongozi wa Klabu hiyo kuwa asake wachezaji watatu wakiwa ni washambuliaji wawili na mlinzi mmoja.

Hata hivyo Furgason hakusema ni wachezaji gani ambao watajaza nafasi hizo ili wasaidiane na vinara wa safu hiyo, Dwrigh York na Andy Cole.

Lakini Mashabiki wa Manchester wameshamtaja Mu-Argentina Gabriel Batistuta na Mnigeria Austen J.J. Okocha anayechezea soka Ufaransa.

Wachunguzi wa soka wamesema kuwa hatua ya Manchester kutangaza kusaka wachezaji inatokana na vipigo viwili mfululozo, kile cha Brazili mwishoni mwa mwaka jana katika mashindano ya klabu bingwa ya Dunia na kile cha juzi dhidi ya Real katika Klabu bingwa ya Ulaya.