Michezo

SUALA LA KLABU YA YANGA KUWA KAMPUNI

Moshi waanza kufuka Jangwani

lWanachama waomba kampuni isisajiliwe

Moshi wa hatari umeanza kufuka katika klabu ya Yanga yenye makao yake mtaa wa Jangwani Kariakoo jijini Dar Es Salaam, baada ya wanachama kuapa kuwa watazuia mageuzi ya klabu hiyo kuwa kampuni.

Akiongea na Gazeti hili mwishoni mwa juma, kiongozi wa kundi la wanachama wa Yanga waliokwenda ofisi ya msajili wa vyama vya michezo kupinga Yanga isiandikishwe kama kampuni, Othumani Hamis, alisema zaidi ya nusu ya wanachana wa Yanga hawaafiki mageuzi hayo.

Alisema mkutano uliopitisha mabadiliko hayo ulijaa hila na uliitishwa na watu wasio kuwa na haki ya kisheria kufanya hiyo.

"kwanza mkutanao wenyewe ni batili kwani Katiba ya Yanga inatamka wazi kuwa ni viongozi wa kuchaguliwa pekee yao, ndio wenye mamlaka ya kuitisha na kusimamia mkutano wa marekebisho ya katiba," alisema Hamisi huku akiungwa mkono na kundi la wenzake.

Akifafanua madai ya kuwapo kwa hila katika mkutano huo, mwanachama huyo alisema, idadi ya wanachama hao waliohudhuria ni ndogo mno na wengi wao ni "feki" ambao alidai kuwa waliorodheshwa na viongozi hao wa muda tu.

Mbali ya kupinga Yanga kuwa kampuni, wanachana hao walisema kuwa hawaridhishwi na mwenendo wa klabu yao. "Kwanza tunashagaa kwanini viongozi wanamng’ang’ania huyu kocha, Roul Shungu toka Kongo ambaye hakuna lolote la maana alilofanya," alisema mwanachana mwingine.

Wakizungumzia uongozi wa sasa, walisema hawana ugomvi nao lakini waitishe uchaguzi ili wagombee na kushinda kihalali badala ya kusubiri kuwekwa na wanachana kwa mizengwe.

Klabu ya Yanga ambayo ni moja ya klabu kongwe nchini iliitisha mkutano wa wanachama mwanzoni mwa mwaka huu wa kujadili katiba ambapo ulikubali kubadili klabu ya Yanga kuwa kampuni.

Hata hiyo hadi sasa kampuni hivyo bado haijasajiliwa ili iweze kufanya kazi kwa mujibu wa sheria za makampuni nchini.

Leo, Yanga inatarajiwa kupambana na Kariakoo ya Lindi mjini Lindi katika moja ya michezo ya ligi kuu ya soka Tanzania Bara Safari Lager.

Wakati huo huo: Chama cha Mpira wa Miguu Wilaya ya Temeke (TEFA) kimepata viongozi wapya watakaongoza jahazi kwa kipindi cha muda wa miaka mitatu katika uchaguzi uliofanyika Mgulani jijini wilayani hapo hivi karibuni.

Mwenyekiti wa uchaguzi huo Bi. Elizabeth Nyambibo, aliwataja walichaguliwa kuwa ni Mwenyekiti, Bw. Hussen Jumanne Kibwana aliyeshinda kwa kura (224) Mzee Abdallah Kipukuzwa aliyepata kura (88).

Nafasi ya Mwenyekiti msaidizi ilichukuliwa na Bw. Abushiri Kilungo, Katibu Mkuu Bw. Abdallah Kitumbi, Katibu Msaidizi ni Mzee Hassan Mpanjila

Bi. Nyambibo alizitaja nafasi nyingine kuwa ni Mweka Hazina Bw. Mahidi Battashi, wakati nafasi ya Mjumbe wa Mkoa ilinyakuliwa na Bw. Ramadhan Chenga.

Wajumbe wa Kamati ya Utendaji ni Bw. Hassan Ally Msumary, Bw. John Mwangakala na Bw. Obby Stellec Anaripoti Lecardia Moswery.

 

Annelka 'afufua ndoa' yake na Real Madrid

lAlipigiwa kura ili kupangwa

Mshambuliaji wa kimataifa wa Ufaransa, Nicolal Annelka amefufua matumaini ya "ndoa" yake na klabu ya Real Madred ya Hispania ambayo imekuwa ikilegalega.

Akihojiwa na Televisheni ya Uingereza (BBC) juzi usiku, Annelka ambaye aliwahi kuichezea Arsenal,alisema kuwa anafurahi kuwa "ndoa" yake na Real iliyokumbwa na matatizo mengi sasa inaanza kupata uhai.

Annelka alisema kuwa aliingia uwanjani katika pambano dhidi ya Braern Munchi ya Ujerumani katika nusu fainali ya klabu bingwa ya Ulaya akiwa na uhakika wa kubaki Real Madrid na hiyo ilimtia nguvu zaidi.

"Nilipata uhakika huo baada ya mashabiki wa klabu hiyo kupiga kura ya kutoa maoni yao kuamua kama nipangwe katika mechi hiyo au la, na nilishinda kwa asilimia 90,"alisema Annelka.

Kabla ya pambano la juzi kati ya Real Madrid na Bayern Munch, washabiki wa Hispania walipiga kura ya maoni kuamua kama Annelka apangwe katika pambano hilo au la, na mashabiki walimpa kura za diyo kwa asilimia 90 dhidi ya 10 ilizotaka asipangwe.

Hatua ya mashabiki kumpa ushindi Annelka, ilikuja katika kipindi ambacho mshambuliaji huyo alikuwa kwenye hati hati ya kutemwa.

Tafauti ya Annelka aliyenunuliwa na Real Madrid kwa thamani ya shilingi bilioni 28 na kuwa mchezaji ghali kuliko yeyote katika klabu hiyo, ilikuja mwezi mmoja uliopita baada ya kutofika kwenye mazoezi na kupewa adhabu ya kufungiwa kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Pamoja na kufungiwa, Annelka pia alipigwa faini ya Sh. Milioni 200, lakini akasamehewa baada ya kuomba hadharani.

Hata hivyo, Anelka aliyafuta yote hayo baada kuingizwa uwanjani na kufunga bao la kuongoza katika dakika ya tatu ya pambano hilo.

Hata Bayern wenyewe imekiri kuwa bao la Annelka ndilo lililowatia balaa na hata wakajifunga wenyewe bao la pili.

Timu hizo mbili zitarudiana wiki ijayo katika uwanja wa Olmpic mjini Munich ambapo Bayern watapaswa kushinda zaidi ya mbao ili kuingia fainali.