Michezo

Polisi 40,000 wenye silaha kudhibiti fujo michuano ya Ulaya

lUingereza yaruhusu mashabiki wake wafungwe

Uholanzi

JUMLA ya polisi 40,000 tayari wamesambazwa kwenye viwanja mbalimbali vya soka nchini Uholanzi na Ubeligiji wakiwa na silaha kali kwa ajili ya kuwadhibiti mashabiki wenye ghasia katika fainali za Michuano ya Mataifa ya Ulaya (EURO 2000) inayoanza leo inayotarajiwa kushuhudiwa na mashabiki zaidi ya milioni 1.2.

Polisi hao ambao baadhi yao wameazimwa toka mataifa mengine ya Ulaya, mbali na wenyeji wa michuano hiyo, wanapewa silaha kali yakiwamo mabomu ya kutoa gesi ya machozi, mbwa na bunduki za rashasha.

Kwa mujibu wa taarifa ya waandaaji wa michuano hiyo iliyosomwa juzi kwa waandishi wa habari na kukaririwa na Televisheni ya Uingereza Sky, Polisi hao pamoja na kulinda amani, watapaswa pia kufanya upelelezi wa kina ili kuwazuia mashabiki wa Uingereza wenye historia mbaya ya kufanya fujo.

Taarifa hiyo imesema kuwa mashabiki wa kutoka nchi za Uturuki na Uingereza watapaswa kupekuliwa mwili mzima ili kuona kuwa hawapiti na silaha yoyote hata nyembe.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uingereza Bw. Jack Stral, amekaririwa akisema kuwa nchi yake imetoa kibali kwa nchi yoyote ya Ulaya kuwashitaki na hata kuwahukumu mashabiki wake ambao watafanya fujo katika fainali za "Euro 2000."

Waziri huyo ameonya kuwa mashabiki wake wenye ghasia watahukumiwa hata kwa sheria za Kiislamu iwapo hawatajizuia kufanya ghasia katika mataifa hayo.

Hata hivyo kamati hiyo ya maandalizi imetoa kipaumbele katika mechi za Ujerumani na Uingereza ambayo itachezwa Juni 17 mwaka huu, kutokana na nchi hizo kuwa wapinzani wa jadi.

Upinzani wa Uingereza wa Ujerumani si wa soka tu bali ni hata kwenye siasa kwani zilipigana katika Vita Kuu vya Pili ya Dunia.

Michuano ya Ulaya inafunguliwa leo huko Ubeligiji ambapo wenyeji wataikaribisha Sweden, wakati kesho kutakuwa na mechi tatu ambazo ni mabingwa wa dunia, Ufaransa, Uturuki na Italia na Uholanzi na Jamhuri ya Czech.

Mapambano hayo ya Jumapili hii, yanapewa umuhimu wa pekee kwani zipo timu tatu zinazopewa nafasi ya kutwaa ubingwa ambazo ni Denmark, Uholanzi na Ufaransa ambazo tayari zimetamba kuwa hakuna timu yenye ubavu wa kuwapokonya ubingwa huo.

Mmoja wa washambuliaji hatari wa Ufaransa Nicolaus Annelka, aliyepewa jezi namba tisa, alisema juzi kuwa wao ni mabingwa wa dunia hivyo endapo watakosa ubingwa wa Ulaya ambao una hadhi ya tatu kiulimwengu, litakuwa ni doa kubwa kwa ubingwa wao.

Michuano hiyo itaendelea Juni 12 kati ya Ujerumani na Romania ambapo pia Uingereza itapambana na Ureno.

Juni 13, Hispania itajitupa uwanjani kuumana na Norway na mechi ya pili siku hiyo, itakuwa kati ya Yugoslavia na Slovenia.Juni 14 kutakuwa na pambano moja pekee, kati ya Italia na wenyeji Ubelgiji wakati Juni 15, Sweden itapambana na Uturuki. Juni 16, Czech itakwaana na Ufaransa na Denmark itambapamba na Uholanzi.

Uingereza itajitupa tena uwanjani Juni 17 kupambana na Ujerumani wakati Ureno ikipambana na Romania huku Slovenia nayo ikipambana na Hispania Juni 18, sambamba na Norway na Yugoslavia.Uturuki na Ubelgiji, zitapambana Juni 19. Juni 20 ni Uingereza na Romania wakati Juni 21, Denmark itaikwaa Jamhuri Czech na Yugoslavia itaikabili Hispania.

Michuano hiyo itaingia hatua ya robo fainali Juni 24 na 25 ambapo mechi zote nne zitachezwa na kupatikana wababe wanne ambao watacheza nusu fainali hapo junu 28 na 29.

Fainali ya michezo hiyo itakuwa Julai 2 mwaka huu, ambapo mbabe wa bara zima la Ulaya atapatikana.

Shekiondo kugombea tena Yanga

Na Pelagia Gasper

MAKAMU Mwenyekiti wa Klabu ya Yanga Joseph Shekiondo anatarajia kutetea kiti chake katika Uchaguzo Mkuu wa klabu hiyo unaotarajiwa kufanyika Julai 1, mwaka huu.

Shekiondo ametoa kauli hiyo jijini kutaka kuwahakikishia wanachama wa Klabu hiyo kuwa bado ni kiongozi mwenye mapenzi mema na klabu ya Yanga.

Alikanusha habari ambazo zimekuwa zikienea hivi karibuni kuwa amejiuzuru nafasi hiyo na kwamba amekuwa akishirikiana na baadahi ya wanachama kutaka kuung’oa madarakani uongozi uliopo.

"Mimi bado ni Makamu Mwenyekiti wa Yanga na ninatarajia tena kugombea nafasi hiyo katika uchaguzi ujao", alisema.

Hata hivyo klabu hiyo ya Yanga, imeishaifanyia marekebisho Katiba na kwamba hakutakuwa na nafasi ya Mwenyekiti wala Makamu wake, bali kutakuwa na Rais na makamu Rais.

Chini ya viongozi hao litakuwepo Baraza la Seneti ambalo litakuwa na jukumu la kutoa ushauri juu ya uendeshaji wa klabu hiyo.

Katiba hiyo ilifanyiwa marekebisho na kupitishwa na wanachama wa klabu hiyo Januari mwaka huu na kwamba itaendeshwa kwa mfumo wa kampuni jambo linalipigwa na baadhi ya wanachama.

Wanachama wanaopinga klabu hiyo kuendeshwa kwa mfumo wa kampuni walimtaja Shekiondo kuwa miongoni mwa wanachama wanaopinga Yanga kuwa kampuni

BMT kukutana Jumamosi kujadili rufani

Na Agatha Rupepo DSJ

KAMATI ya Utendaji ya Baraza la Michezo Tanzania (BMT) wanakutana Jumamosi hii katika ofisi ya Baraza hilo kujadili rufaa mbalimbali.

Katika kikao hicho zitajadiliwa rufaa mbalimbali ikiwemo ya timu ya Majimaji ya Songea kupinga kushushwa daraja na pia kujadili rufaa nyingine ya wagombea walioshindwa katika Uchaguzi Mkuu wa Chama cha Soka cha Ligi ya Makundi uliotumiwa msimu huu.

Aidha, Kamati ya BMT itajadili rufaa ya Chama cha Soka cha Wilaya ya Ilala (IDFA) inayolalamikiwa na wagombea 11 waliopinga uchaguzi huo wakisema kuwa uchaguzi huo haukufuata taratibu na kanuni za Katiba na Uchaguzi.

Wagombea hao waliamua kukata rufaa yao kwa Afisa Utamaduni, Joel Mkude ambaye alikataa rufaa yao kwa madai ya kutolipa ada ya rufaa kwa kipindi kinachohitajika pamoja na kutoambatanisha vielelezo vya rufaa hiyo.Kutupwa kwa rufaa hiyo kulipelekea wagombea hao kupeleka rufaa yao BMT ambapo Katibu wa BMT Mohamed Lutta, aliiagiza Kamati ya Uchaguzi ya Wilaya ya Ilala kukaa tena na kuiangalia rufaa hiyo.Kutokana na kamati hiyo kushindwa kutoa maelezo kwa BMT, Baraza hilo liliiandikia tena Kamati ya Utendaji ya Uchaguzi wa Ilala kusimamisha uchaguzi wa mkoa wa DRFA na kuitaka kuhudhuria mkutano ili kutoa maelezo.

Baraza hilo limetaka kamati hiyo kupeleka nakala ya katiba iliyotumika siku ya uchaguzi, muhtasari wa Mkutano Mkuu wa Uchaguzi wa IDFA na nakala za fomu za maombi ya uchaguzi na vithibitisho vya elimu.