Michezo

Kibarua cha Shungu sasa mashakani

lYadaiwa hakubaliki kwa akina Matunda

Na Mwandishi Wetu

KUREJEA madarakani kwa uongozi wa kuchaguliwa ndani ya Klabu ya Soka ya Yanga jijini, chini ya Rashid Ngozona Matunda na wenzake, kumeelezwa kuwa ndio mwisho wa ajira ya kocha kutoka Jamhuri ya Kongo ,Roul Shungu.

Hayo yamesemwa jana na mmoja wa wanakamati Kuu ya Yanga, ambaye alidai kuwa kocha huyo tayari alisimamishwa kazi na kamati hivyo muda mchache kabla ya kupinduliwa.

"Sikia bwana, hilo halihitaji hata kumpata Mwenyekiti lipo wazi kuwa huyu Shungu si kocha si maana ana majungu tu na kamati yetu wala haina haja ya kumjadili" alisema mjumbe huyo ambaye aliomba asitajwe jina.

Akifafanua hoja hiyo, alisema kuwa Shungu mwenyewe anajua wazi kwamba chini ya uongozi wa Matunda, hana ofisi kwa kuwa alihusika hata kuchochea mgogoro ambao ulisababisha mapinduzi yaliyoigharimu Yanga kwa kiasi kikubwa.

Mjumbe huyo alisema tangu Shungu aingie Yanga, hajaleta lolote zuri mbali na Kombe la Afrika Mashariki na Kati ambalo ni sawa na Kombe la kimkoa tu.

Aidha, alisema kuwa Yanga inaweza kumchukuwa kocha Tauzany Nzuisaba mwenye asili ya Burundi ambaye ametemwa na Simba.

"Nzuisaba alishawahi kufundisha Yanga na kupata mafanikio makubwa tu, na kilichomhamisha ilikuwa ni deni tu ambalo Yanga sasa inaweza kuzungumza naye.

Nzuisaba alishawahi kufundisha Yanga akiwa kama kocha Msaidizi chini ya Mzee Tambwe Leya ambaye pia ana asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Kongo.

Yanga ilirejeshwa chini ya Uongozi wa akina Matunda na wenzake mwanzoni mwa wiki iliypitana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni.

Nina hamu ya kuitwa Mahakamani - Kipukuswa

Na Pelagia Gasper

MAKAMU Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba, Abdallah Kipukuswa, amesema kuwa anasubiri kwa hamu, barua ya kuitwa mahakamani ili ajibu tuhuma zinazomkabili juu ya matumizi ya sh. Milioni 2.5 za klabu hiyo.

"Mimi nashangaa sana huu uongozi mpya, nasoma tu kwenye magazeti ‘Kipukuswa kupelekwa mahakamani’ lakini hawajanifuata.

"Mimi nimejiandaa kikamilifu kwa ajili ya kwenda mahakamani kujibu tuhuma hizo lakini nashangaa sipati barua" alisema Kipukuswa kupinga madai kuwa alitumia isivyo halali sh. Milioni 2.5 zilizotolewa na wadhamini wa michuano ya Ligi Kuu ya Safari Lager, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa ajili ya usafiri wa wachezaji.

Kipukuswa wakati huo, alikuwa Kaimu Mwenyekiti wa Klabu hiyo baada ya mwenyekiti wake, Yusufu Hazali na Katibu Mkuu Halfan Matumla, kufungiwa na msajili wa vyama na klabu za michezo Tanzania, Leonard Thadeo kwa kukiuka katiba ya klabu hiyo.

Alisema anashangaa kuona uongozi mpya unaongea na magazeti kwamba watampeleka mahakamani lakini mpaka saa hajapelekewa karatasi yeyote ya kumuita mahakamani.

Wakati wa makabidhiano ya ofisi na nyaraka mbalimbali za klabu hiyo, Machi mwaka huu, Kipukuswa alieleza kuwa fedha za klabu hiyo ziko benki lakini baada ya uongozi mpya wa Mwenyekiti Juma Salum kwenda benki, hakupata fedha zozote.

Wakati huo huo: Katibu Mkuu wa Simba Kassim Dewji, amesema klabu yake itaanzisha gazeti litakaloruhusu wana Simba litakalokuwa likitoka mara mbili kwa mwezi.

Alisema gazeti hilo litaanza wakati wa raundi ya pili ya ligi kuu itakayoshirikisha timu nane bora. Mhariri wake atakuwa Katibu Mwenezi wa Simba, Juma Nkamia

Uholanzi, Hispania zategemewa kufanya maajabu

MICHUANO ya Fainali za Klabu Bingwa ya Ulaya maarufau kwa EURO 2000 inatia nanga mwishoni mwa wiki ijayo huku tayari timu za Uholanzi na Hispania zikihofiwa na wapinzani.

Katika fainali hizo ambazo kwa mara ya kwanza zinafanyika kwenye Mataifa mawili, zitaanza rasmi Juni 10 mwaka huu.

Tayari karibu timu zote zimetaja vikosi vyake na kutoa sura halisi ya nani anapewa nafasi ya kutwaa Ubingwa.

Kwa mujibu wa Mahojiano ya wataalamu wa soka barani Ulaya, yaliyofanywa na televisheni ya India DD News, timu za Uholanzi na Hispania zinapewa nafasi kubwa ya kufanya maajabu.

DD News ilimkariri Rais wa Shirikisho la Ulaya, Laurent Johnson akisema kuwa itakuwa ni makosa kwa timu yoyote kati ya washiriki kudharau kwani karibu zote ni nzuri na soka yaUlaya imebadilika sana.

Aidha, Johnson alisema yeye binafsi na si kama Rais wa Jumuiya hiyo, anaipa nafasi kubwa timu ya Uholanzi.Kauli hiyo pia iliungwa mkono na mwanasoka wa dunia wa zamani, Diego Maradona, ambaye alisema kuwa Uholanzi ndiyo timu anayoiona kuwa ni bora kuliko zote za Ulaya kwa sasa.

Hata hivyo alisema watu wengi waubadili mtizamo wao na kuiangalia kwa makinii timu ya Hispania ambayo imejaa wachezaji wa Real Madrid iliyotwaa ubingwa wa Ulaya hivi karibuni."Hispania tayari ilishatoa onyo kwa timu pinzani baada ya kufanikiwa kungiza timu zake tatu kwenye nusu fainali ya Klabu Bingwa ya Ulaya, mwezi uliopita.

Denmark si tishio sana lakini kipa wake Peter Schumiche,l aliye kuwa akiichezea Manchester United ni hatari sana na inaweza kuleta madhara" alionya Maradona.

Hata hivyo wapo watu barani Ulaya wanaoamini kuwa timu ya Uingereza iliyoitandika Ukreni 2-0 juzi kwenye mechi ya majaribio, nayo inaweza kuwa ni tishio pia.Lakini kocha wake mwenye makeke mengi Kevin Keegan, tayari alishasema kuwa katika kundi lake anaihofia timu moja tu ambayo ni Ujerumani.

"Kama tukiifunga Ujerumani, basi tutakuwa na uhakika wa kuvuka hatua ya makundi na kuingia robo fainali.Uingereza na Ujerumani zina historia ya kuwa wapinzani wa jadi kutokana na kupigana katika vita vya pili vya Dunia.Michuano hiyo itaonyeshwa moja kwa moja kwa ushirikiano wa vituo vya televisheni vya DTV na ITV vya jijini.