Michezo

BAADA YA KUMPATA MALIMA, SIMBA WASEMA:

Ubingwa sasa ni wetu

lNdoto zote za Yanga sasa ni kwa Kajumulo

Na Mwandishi Wetu

BAADA ya kumtia mikononi beki wa kimataifa, Bakari Malima, klabu ya soka ya Simba ya jijini, imesema kuwa sasa ubingwa wa soka wa ligi ya Jamhuri ya Muungano Mwaka huu, ni mali yao.

Kocha mkuu wa klabu hiyo ya Simba, Abdallah King Kibaden, alisema juzi kuwa timu yake ilikuwa na pengo kwenye safu ya ulinzi na sasa limezibwa na kwamba sasa hali hiyo ya uwepo wa Malima katika timu yake, inawahakikishia ushindi kwa kuwa pengo hilo limezibika ipasavyo.

Alisema kuwa beki huyo mwenye nguvu maarufu kwa jina la "Jembe Ulaya", walimhitaji mno huko Msimbazi ili kutia moyo safu ya ulinzi iliyopo chini ya wachezaji vijana ambao hujituma kwa moyo wa dhati.

Malima, hatimaye ametua Msimbazi baada ya kugombaniwa kwa karibu wiki mbili kati ya klabu ya Simba na Kajumulo World Soccer, pia ya jijini.

"Tunakwenda kwenye Super League, tukiwa imara, lengo letu ni kuirudishia klabu yetu ya Simba hadhi yake ya miaka ya 93-94.

Sasa tunaweza kutwaa vikombe vyote viwili vilivyopo mbele yetu; ubingwa wa Bara na ule wa Muungano, ni lazima." Alitamba kocha huyo mwenye historia nzuri na klabu ya Simba.

Hata hivyo, tofauti na zamani ambapo mpinzani mkuu wa Simba alikuwa Yanga, mwaka huu sasa mpinzani wake ni Prisons ya Mbeya, wakati mpinzani mkuu na ndoto tupu wa Yanga ni Kajumulo.

Timu zote hizo zimetoka sare kwenye makundi yao katika mechi zote mbili.

Simba iliongoza kundi la Nyanda za Juu Kusini na Kajumulo kundi la Mashariki. Super League, inatarajiwa kung’oa nanga Juni 17, mwaka huu.

Hata hivyo, hali itategemea maamuzi ya ngazi za juu za soka nchini juu ya mfumo wa timu za Majimaji ya Songea na Reli ya Morogoro, zinazopinga kushuka daraja.

Simba na Yanga zitakumbana Julai 24, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini.

PAMOJA NA KUTWAA UBINGWA WA UINGEREZA

Furgason akiri kushindwa

lAahidi kujiunda upya

LONDON, Uingereza

PAMOJA na kutwaa ubingwa wa ligi Kuu ya Uingereza, ‘Priemier League,’ mapema hata kabla ya ligi kumalizika, Kocha Mkuu wa Manchester United, Alex Furgason, amekiri kuwa ameshindwa kutimiza ahadi aliyowapa mashabiki wa timu hiyo.

Akihojiwa na watangazaji wa kipindi cha michezo cha televisheni binafsi ya Sky News ya Uingereza mapema wiki hii, Furgason ambaye amejijengea heshima kubwa Uingereza alikiri kuwa pamoja na kutwaa ubingwa, bado ameshindwa kukidhi matakwa ya mashabiki wake.

"Ndiyo ni kweli nimeshindwa kufikia idadi ya mabao 100 niliyokuwa nimeahidi kuyaweka nyavuni mwa wapinzani wangu msimu huu" alisema kocha huyo.

Alisema kuwa pamoja na kushindwa katika hilo, pia timu yake imetolewa mapema na Real Madrid ya Hispania katika michuano ya Klabu ya Ulaya kinyume cha matarajio yake.

Real ndio mabingwa wa sasa wa klabu bingwa ya Ulaya, baada ya kushinda katika fainali yenye kuvunja historia ya Miaka 45 ya mashindano hayo ya kukutanisha timu mbili za taifa Moja.

Furgason alisema kuwa kutokana na kushindwa kwao, ataisuka upya Manchester na kuwa mwakani itakuwa bora zaidi ya sasa, na atahakikisha kuwa hauzwi mchezaji hata mmoja kwenye kikosi chake bali anachofanya, ni kununua wachezaji wapya tu.

Madrid na Valencia zahofia vurugu za mashabiki

PARIS, Ufaransa

SHIRIKISHO la Soka la Ulaya limekumbwa na wasiwasi mkubwa juu ya hali ya usalama katika mshindano ya Shirikisho hilo mwaka huu "EURO 2000", yatakayofanyika Ubelijiji na Uholanzi.

Maofisa wa shirikisho hilo waliokuwa mjini Paris, Ufaransa kusimamia fainali za klabu bingwa ya Ulaya, kati ya Real Madrid ya Hispania na Valencia, walisema kuwa wanahofia sana mashabiki wa London na wale wa Instanmbul katika michuano hiyo.

Rais wa Shirikisho la Soka la Ulaya, Laurent Johnson, alisema uhasama uliojitokeza kati ya mashabiki hao katika mashindano ya Shirikisho hilo mapema mwezi huu na kusababisha vifo vya watu, unatia shaka.

Johnson alisema shirikisho lake linachunguza kwa makini hali itakavyokuwa na ikibidi hatua zaidi za kiusalama zichukuliwe.

Alidokeza hatua hizo kuwa ni pamoja na kuomba msaada wa polisi maalum katika nchi mbalimbali za Jumuiya ya Ulaya, ikiwepo Uingereza yenyewe na Uturuki.

Alizitaja hatua nyingine kuwa ni pamoja na kuzuia mashabiki wa London kwenda nchi yanapofanyika mashindano hayo.

Hata hivyo, alisema hatua hiyo itakuwa ya mwisho baada ya nyingine zote kufanyika kwa kuwa inavujna haki ya msingi ya binadamu.

Rais huyo wa Shirikisho la Ulaya aliionya Uingereza kuwa tabia ya mashabiki wake inaweza kuwanyima nafasi ya kuandaa michuano ya kombe la dunia mwaka 2006 ambayo imekuwa ikiiwania kwa nguvu.