Make your own free website on Tripod.com

Michezo

Simba kuigomea Yanga

lFAT yaipiga mkwala, yasema ole wao

Na Pelagia Gasper

TIMU ya Soka ya Simba imesema kwamba haitatii marekebisho ya ratiba ya Ligi Kuu yaliyotolewa na FAT ambayo yameipanga mechi kati yake na watani wake wa jadi Yanga Agosti 5 mwaka huu.

Katibu Mwenezi wa Klabu hiyo Juma Nkamia alisema kwamba hatua hiyo ya kuisusia mechi hiyo imefikiwa na kikao cha kamati ya utendaji wa klabu hiyo iliyokutana juzi usiku.

Alisema Simba ilikuwa imeshapanga ratiba yake ya mwaka mzima na inajua mchezo wa marudiano kati yake ya mwaka mzima na inajua kuwa inacheza mechi ya marudia kati yake na Yanga itafanyika Agosti 19, mwaka huu.

"Sisi msimamo wetu uko palepale, bora tupoteze pointi, lakini Agosti 5, hatupeleki timu uwanjani", alisema.

Hata hivyo, kaimu Katibu Mkuu wa FAT, Amin Bakhresa, ametishia kuwa iwapo wanamsimbazi hao wataingia mitini kwa kisingizio cha kubadilishwa ratiba, basi rungu la FAT litaiangukia Simba kichwani.

Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa juma katika ofisi za chama hicho cha soka nchini, Kaimu Katibu Mkuu huyo ambaye sasa ni takribani majuma mawili yamepita tangu ashike usukani huo, alisema wanachama wa Simba watajutia kitendo alichokiita cha kihuni cha viongozi wao.

Alisema uamuzi wa kubadili katiba umefanya na kamati ya utendaji ya FAT kwa mujibu wa sheria,

Hivyo,ni dhahiri kuwa Simba watapatwa na pigo la kulipishwa faini ya shilingi laki tano na kupoteza mchezo huo kwa kuwa chama hicho sasa hakina blaa blaa.

Katika mchezo huo Yanga ndio mwenyeji, jambo linaloonesha kwamba endapo Simba itashikilia msimamo wake, Yanga itaingia hasara ya mamilioni ya shilingi.Nkamia amesema pia kwamba Simba haipo tayari kuchezeshwa na mwamuzi Nassor Hamduni wa Kigoma na kusisitiza kwamba mwamuzi aliyepangwa awali ndiye anayestahili. Hakumtaja mwamuzi huyo.

"Sisi tunajua mechi hiyo imepangwa ili ifanyike kabla ya Uchaguzi Mkuu wa FAT ili wapate fedha na hiyo sisi kamwe hatukubali," alisema.

Wakati huo huo: Waamuzi Jaisi Makanjira wa Iringa na Issack Shirikisho wa Tanga, wameondolewa katika orodha iliyopangwa mwanzoni mwa mwezi kwa madai ya kutokuwa na sifa za kuchezesha ligi Kuu.Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya FAT, Abdallah Bulembo, amesema jijini kuwa

uamuzi huo umefikiwa na Kikao cha Kamati ya Utendaji, kinachoendelea, kilichozingatia ushauri wa kitaalamu uliotolewa na Chama cha Waamuzi wa Soka Tanzania(FRAT).

Makanjira ni mdogo wa aliyekuwa mjumbe wa kamati ya utendaji wa FAT, Bakari Makanjira aliyeondolewa katika nafasi hiyo kwenye Mkutano Mkuu wa chama hicho uliofanyika wiki iliyopita mjini Morogoro.

KAMPENI ZA UCHAGUZI MKUU UJAO:

TOT kupata upinzani toka TLP

Na Josephs Sabinus

KIKUNDI cha Sanaa cha Tanzania One Theatre (TOT), safari hii huenda kikapata wakati mgumu kukipigia kampeni Chama Cha Mapinduzi katika Uchaguzi Mkuu ujao kutokana na Chama cha TLP na chenyewe kuunda kikundi kitakachowapia kampeni.

Kwa mujibu wa Mwana TLP aliyejitambulisha kama Katibu Mwenezi wa Vijana wa TLP mkoani Morogoro, Bw.Fidelis Lubuva, amesema jijini wiki iliyopita kuwa chini ya ushirikiano na vijana wenzake wa TLP, atahakikisha kuwa TOT inapata wakati mgumu na hivyo kukoma kuwaponda wasanii na viongozi wa vyama vya upinzani kwa njia ya usanii.

Lubuva ambaye ni msanii chipukizi mwenye kipaji cha kutunga na kuimba, mwenye shahada ya Chuo cha Sanaa cha Bagamoyo, anasema, "Nimeamua kujitokeza kula sahani moja na Komba katika majukwaa wakati wa kampeni zijazo baada ya kukerwa na kauli zake za kuwaponda wasanii wengine na viongozi wa vyama vingine vya siasa kwa kutumia usanii ambao hata mimi ninao."

Alisema Kapteni John Komba ambaye ni Mkurugenzi wa TOT, amekuwa akidai kuwa wapinzani na wasanii wengine si lolote wala chochote na akaongeza kuwa kitendo cha Komba kusema atavichukua hata vikundi vingine vya usanii ili visichukuliwe na vyama vya upinzani kikiwamo TLP, ili kupigia debe CCM, hakikumfurahisha kama msanii na mwanachama wa chama cha upinzani.

Lubuva ambaye kikundi chake kinaitwa TLP THEATRE GROUP kikiwa na makao yake katani Mazimbu katika mkoa wa Morogoro, anasema kikundi chake kitahakikisha kinapiga kampeni hadi TLP kinajizolea viti vingi vya udiwani, ubunge na kumpa mgombea wake Bw. Augostine Mrema, kiti cha urais bila ugomvi wala kashfa bali kwa kuburudisha na kuelezea sera za chama.

Licha ya kusema kuwa kikundi hicho kinatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni na Mwenyekiti wa TLP taifa, Bw. Mrema, Lubuva pia alimsifia Komba huku akisema,

"Wakati Komba akiwa JWTZ, alikuwa msanii mzuri aliyeunufaisha umma wa Watanzani bila kujali itikadi, lakini sasa amebweteka mno CCM."

Manyika asikitiishwa na tuhuma dhidi ya Yanga

Gerald Kamia na Christina Mbezi,DSJ

MLINDA mlango wa kutumainiwa wa klabu ya Yanga, Peter Manyika amesikitishwa na madai ya wanachama wa Klabu hiyo ya kumtuhumu kuwa aliihujumu timu hiyo ili ifungwe na wapinzani wao Simba.

Akizungumza na KIONGOZI mara baada ya kuwasili nchini na timu ya Taifa ,Kipa huyo amesema kama mchezaji wa Yanga, asingeweza kufanya kitendo kama hicho.

"Napenda niwahakikishie siwezi kuhujumu timu yangu kwani naipenda na imenitoa mbali. Iweje leo niihujumu, mimi bado ni mpenzi waYanga na kufungwa ilikuwa bahati mbaya tu" alisema.

Baadhi ya wanachama wa Klabu hiyo, mwishoni mwa wiki wameuandikia barua uongozi wa klabu wakitaka umsimamishe mlinda mlango huyo kwa madai kuwa alipokea hongo ili timu hiyo ifungwe na Simba.Timu hizo zilipambana mwezi uliopita na Simba iliibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Yanga.

wanachama wa klabu hiyo walianza kuwatuhumu baadhi ya wachezaji wa Yanga kuwa waliihujumu. Wachezaji waliotuhumiwa sambamba na Manyika ni, Sekilojo Chambua na Muhamed Hussein.