Michezo

Bara la Afrika lagubikwa na huzuni

lTelevisheni zashikwa na vigugumizi

lBaadhi wadai ukoloni umerejea Afrika

ZURICH, Uswis

BARA zima la Afrika Alhamisi iliyopita, liligubikwa na simanzi baada ya Afrika Kusini kukosa uenyeji katika fainali za Kombe la Dunia Mwaka 2006 katika dakika za mwisho.

Tukio la kupigwa kura za kuamua nani aandae fainali hizo, lilioneshwa na karibu televisheni zote duniniani ambazo zilikatiza matangazo yao ya kawawida na kujiunga na Televisheni ya Uswis, majira ya saa tisa mchana kwa saa za Afrika Mashariki.

Inaaminiwa kuwa, Afrika Kusini imeshindwa kwa hila za Wazungu kwani ilikuwa imefungana na Ujerumani kwa kupata kura 11 kila moja lakini baadae, FIFA ikatangaza kuwa Ujerumani imeshinda kwa kupata kura 12 na Afrika Kusini imepata kura 11 kwa kile walichodai kuwa mjumbe mmoja hakupiga kura.

Jumla ya wapiga kura wanaoamua nani aandaye fainali za Kombe la Dunia, ni wajumbe 24 wa Kamati ya Utendaji ya FIFA kutoka katika mabara yote ya dunia.

Katika hatua za awali, Morocco ilikuwa ya kwanza kutupwa nje baada ya kuambulia kura 3 tu.

Uingereza nayo iliachia ngazi kwenye hatua ya pili ambayo ilifananishwa na nusu fainali.

Baada ya Ujerumani kutangazwa kushinda, Bara la Afrika lilishikwa na huzuni na baadhi ya Televisheni za Afrika ikiwepo ya Afrika Kusini, ziliduwaa kwa takribani dakika tatu huku watangazaji wake wakionekana kushindwa kujizuia kuonesha uchungu walionao.

Awali TV hiyo ilikatiza matangazo yake ya kawaida na kipindi maarufu cha "Education" na kupiga muziki na kukatiza mara kwa mara ikionesha maandalizi ya Afrika ya Kusini isubiri kutangazwa kushinda.

Rais wa zamani wa Afrika ya Kusini Nelson Mandela, alifanya kampeni hadi usiku wa manane hali iliyoashiria huenda Bara la Afrika, lingepata nafasi hiyo kwa mara ya kwanza.

Baadhi ya wananchi wa Afrika Kusini waliohojiwa walisema kuwa kitendo hicho ni sawa na kurejea tena kwa ukoloni barani Afrika.

MABADILIKO YA UONGOZI FAT MASHABIKI WASEMA:

Ni matokeo ya Kapuya kufurumshwa kwa chupa

Na Mwandishi Wetu

BAADHI ya Mashabiki wa soka nchini, wamekitambia kitendo cha kumrushia chupa Waziri wa Elimu na Utamaduni, Profesa Juma Kapuya wakati wa mechi kati ya Timu ya Taifa(Taifa Stars) na Mauritius kuwa ndicho kilichosababisha mabadiliko ya uongozi katika Baraza la Michezo Nchini(BMT).

Wakizungumza na gazeti hili juzi katika Uwanja wa Karume, Ilala Jijini, Mashabiki hao walitamba kuwa mabadiliko hayo yote ni matunda ya ghasia zao walizozifanya muda mfupi baada ya kumalizika pambano hilo na kwamba aliyerushiwa chupa si Kapuya tu, bali hata watu kadhaa wakiwemo viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu nchini (FAT) walikurupushwa kwa mawe.

"Tumeukomboa mfumo wa michezo nchini kwa gharama ya jasho, na hii ndiyo dawa ambayo inaweza kufanya kazi," alisema shabiki mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Juma.Alisema ghasia walizofanya mashabiki wa soka baada ya timu ya taifa (Taifa Stars) kufungwa, zinaashiria kuwa Watanzania wamechoka na ubababishaji na kwamba ilikuwa ni lazima mabadiliko ya haraka yafanyike.Katika mabadiliko hayo aliyoyafanya Waziri Kapuya baada ya kufanyiwa hayo Uwanja wa Taifa, aliahidi kutoa tamko la serikali ambapo alitangaza kulivunja Baraza la Michezo na kuliunda upya.

Maamuzi hayo yalienda sambamba na kufikishwa mahakamani kwa viongozi wa juu wa FAT kwa tuhuma za kutafuna mamilioni ya fedha za chama hicho.

Baraza jipya la michezo lipo chini ya Mwenyekiti wa Kampuni ya Habari Corporation, Jenerali Ulimwengu, ambaye aliongoza tume ya kuchunguza watuhumiwa wa tuhuma hizo.

Kitendo cha Waziri na viongozi wa juu wa FAT kurushiwa mawe kimelaaniwa na washabiki wa michezo na watanzania kwa ujumla kwa kuwa kinahatarisha amani ya nchi.

Mmoja wa watu waliolaani kitendo hicho, ni Katibu Mkuu wa FAT Ismail Aden Rage ambaye alidai kuwa mashabiki hao walikodiwa ili kuihujumu FAT.

KMMD yatupilia mbali rufaa

Na Pelagia Gasper

KAMATI ya Michezo Mkoa wa Dar es Salaam, (KMMD) kupitia kitengo chake cha nidhamu na usuluhisho, imesisitiza kuwa imetupilia mbali rufaa ya warufani 15 waliokuwa wanapinga matokeo ya uchaguzi wa chama cha soka cha Manispaa ya Ilala (IDFA).

Kwa mujibu wa barua iliyotolewa na mwishoni mwa juma na Mwenyekiti wa KMMD, Bw. Wilfred Ngirwa ambaye aliyoionesha kwa gazeti, kamati hiyo ilipewa madaraka ya maamuzi hayo chini ya kanuni GNN 442 kifungu 6(e), (a) na (I) ambapo ilikaa Juni 19, mwaka huu.

"Kamati ilipitia kwa makini madai yote 15 pamoja na vielelezo vyote lakini iliona madai na vielelezo hivyo havitoshi na vimekosa ushahidi hivyo tuliamua kutupa rufaa yao," alisema Ngirwa ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa wa dar-Es-Salaam.

Barua hiyo iliyotumwa kwa warufani wote 15 na nakala kutumwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo Taifa(BMT),na Katibu Mkuu wa FAT, imewakumbusha warufani hao kutumia haki yao kukata rufaa ngazi za juu iwapo hawataridhika na uamuzi uliotolewa na kamati hiyo.

Hata hivyo mmoja wa warufani hao, Hamisi Ambari, hivi karibuni alikaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa endapo rufaa yao BMT itatupwa, wataenda kwa Waziri wa Elimu na Utamaduni na hatimaye ikibidi, watatinga mahakamani kama Waziri naye atatupilia mbali madai yao.

Warufani hao ni James Mwalamele, Kafuru Ramadhani, Jacob Mwakisu, Selemani Mpuluko, Abdala Kondo, Omary Mkama, Ramadhani Mwanamsoka na Wengine na wanaodai uchaguzi wa IDFA ulipofanyika Aprili 16 mwaka huu, ulikuwa na kasoro na hivyo wao wakaamua kukata rufaa.

Baadhi ya madai yao ni kuwa Katiba iliyotumika katika uchaguzi huo, ni ile ya mwaka 1971 badala ya mpya baadhi ya walioshinda uchaguzi huo kuwa na elimu duni tofauti na Katiba inavyotaka na mmoja wa viongozi aliyeshinda uchaguzi huo, aliwahi kufungiwa maisha kujishughulisha na masuala ya soka (Hamisi Kisiwa).

Ufafanuzi wa KMMD juu ya kutupilia mbali rufaa hiyo, umekuja siku moja baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa KMMD imetengua matokeo ya uchaguzi wa IDFA kuanzia Juni 20, mwaka huu.