FAINALI ZA EURO 2000

Ufaransa yaonywa, Italia wana kundi la waganga

ARMSTARDAM, Uholanzi

TIMU ya Taifa ya Ufaransa ambayo kesho inapambana na Italia katika kinyang’anyiro cha kuwania Kombe la Dhababu la Ubingwa wa Ulaya, imeonywa kuwa wapinzani wao wanatumia ushirikina katika mchezo.

Onyo hilo limetolewa na wachezaji wa Uholanzi muda mfupi baada ya kumalizika kwa pambano la nusu fainali kati yao na Wataliano ambao walifungwa kwa penati.

Wakihojiwa na Televisheni ya India (DD NEWS), wachezaji hao walisema kabla ya kuanza kwa pambano walikuwa hawaamini kwamba kuna uchawi katika soka lakini, baadaye walikubaliana na kauli ya wengi kuwa Italia walikwenda kwenye mashindano hayo pamoja na waganga wengi."Romania walituambia kuwa walikwenda Italia kufuata waganga na wakaajiri mmoja lakini, Italia walikuwa na waganga zaidi ya saba", alikaririwa mchezaji mmoja akisema.

Alisema hata walipokuwa uwanjani walishindwa kuamini kwani mpira uligoma kabisa kupenya kwenye lango la Italia na hilo litabaki kuwa kumbukumbu kwao hadi milele.

Katika pambano hilo, Italia pamoja na kuzidiwa sana kimchezo, iliweza kuhimili vishindo vya Uholanzi na kufikia dakika za penati ambapo kipa wao alidaka tatu kati ya tano zilizopigwa.Hata katika dakika za mchezo, Uholanzi walipata penati mbili lakini, zote walikosa.

Hali hiyo ya Uholanzi kukosa kabisa penalti ilishangaza wataalamu wa soka dunia nzima kwani chama cha soka cha nchi hiyo kiliajiri bingwa wa soka kufanya utafiti wa jinsi ya kupiga penati na ripoti yake ikatumika kuwaandaa.

Katika ripoti hiyo iliyokusanywa kwa zaidi ya miaka saba ikijumuisha mashindano mbalil mbali duniani, mtaalamu huyo alisema kuwa mpigaji wa penati atakayepiga kwenye kona ya juu ya goli, ana asilimia 80 ya kufunga bao na atakaye piga chini, ana asilimia 40 tu, ya kufunga.Hata hiyo elimu hiyo juzi haikufua dafu kwani mchezaji Jep Stam ambaye alipiga penati yake juu alipaisha mpira.

Dennis Bekerms ambaye alipiga mbili za chini zilidakwa, huku mshambuliaji hatari dunianai, Partik Kuluvet alifunga moja na moja iligonga mwamba.

Hata hivyo, kwa mahesabu ya haraka, Italia inapewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kwa kuwa haijapoteza mechi hata moja, lakini, Ufaransa ambao ni mabingwa wa dunia, tayari walisha fungwa na Uholanzi.

Mechi hiyo ya fainali ya mashindano ya Ulaya ambayo yanaelezwa kuwa na msisimko kuliko mengine yoyote yaliyopita, itachezwa kwenye Uwanja wa Mfame nchini Uholanzi.

Wabunge wawafundisha ‘siasa’ mapadre

lWawanyuka mabao 4-1

Dalphina Rubyema na Christopher Kidanka, Dodoma

WABUNGE wamewachezea "siasa" mapadre baada ya wengi wao kukacha mechi ya kirafiki iliyopangwa kuchezwa kati yao na mapadre wa Kanisa Katoliki mjini hapa na wanne tu kuonekana uwanjani na kuwachezesha, "majeshi ya kukodi"

Wapenzi wa soka mjini hapa ambao hivi karibuni waliwaona Wabunge wa Tanzania wakimenyana na Wenzao wa Kenya, walikatishwa tamaa baada ya kuona timu ya wabunge iliyopangwa kucheza na mapadre ikiwa na wabunge wanne tu, na wengine wakiwa wachezaji wasio wabunge.

Habari zilizopatikana toka katika Uwanja wa Jamhuri wa mjini hapa zimesema kuwa wabunge wengi hawakuwepo mjini hapa na hivyo kuilazimu timu yao kuwatafuta wachezaji wasio na nyadhifa za ubunge wakiwamo madereva na wengine.

Mapadre Wakatoliki waliomba kucheza mechi ya kirafiki baina yao na wabunge wa Tanzania katika kusheherekea Maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi lililoandaliwa na Kanisa na kufanyika kitaifa jimboni Dodoma, Juni 25, mwaka huu.

Wabunge waliocheza na majimbo wanayotoka kwenye mabano ni, Salim Mohamed Salim (Konde), Rashid Khalid Salim (Wingwi), Mzee Ngwali Zubeir (Nungwa) na Ali Sheha Musa (Mkwajuni).

Waziri Mkuu Fredrick Sumaye, Spika wa Bunge Bw. Pius Msekwa, mawaziri na Maaskofu ambao walitarajia kuwaona waheshimiwa wabunge uwanjani walilazimika kuwaangalia vijana wazoefu katika medani ya soka kama vile Peter Matiku, Sulemani Miraji Suleiman na Matthew Gonzalves, ambao wamechezea timu kubwa wakiwatoa jasho mapadre.

Timu hiyo iliyotarajiwa kuwa ya waheshimiwa Wabunge iliwabugiza mapadre mabao 4-1.

Katika dakika ya 28 ya kipindi cha kwanza, Suleimani Miraji aliiandikia timu yake bao la kwanza na kuipeleka mapumziko ikiwa kifua mbele.

Katika kipindi cha pili Matthew Gonzalves, alitikisa wavu wa mapadre katika dakika ya 7.

Hata hivyo Padre David Kijaji, aliwainua vitini mashabiki wa timu yake katika dakika ya 15 ya kipindi hicho kwa kuifungia timu yake bao la pekee.

Wakati bado bao hilo linashangiliwa Paul China, alizima kelele hizo na kuzihamishia timu ya Wabunge kwa kufunga bao la tatu dakika hiyo hiyo.

Kunako dakika ya 50, Matthew Gonzaleves aliwaongezea Wabunge bao la nne.

Hii ni mara ya kwanza kwa mapadre Wakatoliki kuomba kucheza mechi ya kirafiki na Wabunge.

Hadi mwisho wa mchezo, timu ya Wabunge ilikuwa ikiwatambia Mapadre kwa mabao 4-1.

Mapato ya Simba ,Yanga kukatwa

lNi kufidia hasara ya uvunjaji vioo Uwanja wa Taifa

Na Mwandishi Wetu

MENEJA wa Uwanja wa Taifa, Abraham Thawe, amesema watakata mapato yaliyopatikana hivi majuzi katika mechi ya Ligi Kuu ya Safari Lager (Nane bora) kati ya timu ya Simba na Yanga za jijini ili kufidia hasara iliyojitokeza baada ya mashabiki wa timu zote mbili kuvunja vibaya vioo vya uwanja huo.

Akizungumza na KIONGOZI mara baada ya mechi hiyo kumalizika Thawe alisema lengo ni kupunguza ama kutokomeza kabisa vitendo vya uharibifu wa uwanja vinavyofanywa na mashabiki.

Mbali na kukata mapato hayo, pia alisema itabidi hali ya ulinzi iimarishwe kwa kuwashirikisha wahusika wote wakiwemo mashabiki wa timu husika wapewe darasa la nguvu kuhusu sheria 17 za soka.

Alisema hali ya uharibifu na vurugu zikiendelea kudumishwa na baadhi ya mashabiki, upo uwezekano mkubwa wa kupata mapato kidogo kwani watu wasiohusika hawatahudhuria kwa wingi kama kawaida.

Vurugu hizo kubwa ambazo zilipelekea kuzusha sakata la kuvunja vioo vya uwanja huo mbele ya mwamuzi Charles Manyama kwenye mechi kati ya timu ya Simba na Yanga, ziliibuka baada ya mwamuzi huyo kutoka Tabora kutaka kukataa goli la pili la Simba lililowekwa kimiani na Steven Mapunda kwa madai kuwa mfungaji alikuwa amezidi.

Katika mchezo huo wa Ligi Kuu ya Safari Lager (Nane Bora) ulichezeshwa na mwamuzi Manyama na wasaidizi wake Leslie Liundi (Dar) na Isihake Shirikisho wa Tanga ambapo walishutumiwa kwa kuchezesha vibaya.

Katika mechi hiyo Simba waliibuka washindi kwa kuwabamiza wapinzani wao bao 2-1.

Mboma aongeza muda wa kustaafu michezo jeshini

Na Pelagia Gasper

MKUU wa Majeshi nchini Jenerali Robert Mboma, amesema kuanzia sasa umri wa kustaafu ushiriki wa shughuli za michezo jeshini utakuwa miaka 40 badala ya 35 ya hapo awali.

Jenerali Mboma aliyasema hayo wakati akiwavisha vyeo askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ), waliofanya vizuri katika michezo mbalimbali wakati wa hafla iliyofanyika katika ukumbi wa maafisa wa jeshi Upanga jijini.

Wanamichezo hao watumishi wa JWTZ, waliopandishwa vyeo mwanzoni mwa juma, ni pamoja na bondia, Nassoro Michael na mwanariadha Restuta Joseph ambaye zamani alikuwa "Private" na sasa amekuwa koplo.

Bondia Nassoro Michael, alipandishwa cheo kutoka, "Warrant Officer II" hadi "Warrant Officer I."

Wanamichezo hao wamepandishwa vyeo kutokana na kufanya kwao vizuri katika mashindano mbalimbali ya kimataifa na kitaifa na kujinyakulia medali za dhahabu hivyo,kuliletea Taifa sifa kubwa.

Akizungumzia umuhimu wa michezo jeshini na hasa kwa manufaa ya wanajeshi wenyewe, Jenerali Mboma amesema michezo hujenga mwili, kuuchangamsha na kuimarisha urafiki.

Pia alisema, kwa askarianayefanya mazoezi na kushiriki michezo mbalimbali, humuwia rahisi kutekeleza kazi zake za jeshini.

"Napenda kuwambia wanamichezo kuwa ukiwa na afya njema unaweza kutekeleza vyema kazi zako jeshini kuliko mtu ambaye hafanyi mazoezi au kushiriki michezo ya aina yeyote ile kwa sababu usipofanya mazoezi una hatari ya kupata maradhi mengi kama vile kisukari, ugonjwa wa moyo na kadhalika," amesema Mboma.

Aliongeza kuwa kutokana na Jeshi kuona umuhimu wa mazoezi, ameamua kuongeza umri wa kustaafu shughuli za michezo jeshini kutoka miaka 35 hadi 40 ili kuwawezesha wanajeshi kujenga vyema miili yao na kufanya shughuli za kijeshi vizuri zaidi.