Michezo

Simba yakanusha madai ya rushwa

Na Pelagia Gasper

KLABU ya soka ya Simba ya jijini Dar-Es-Salaam, imekana kuhusika na tuhuma zinazotolewa dhidi yake za kujihusisha na vitendo vya rushwa ili ishinde katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Safari Lager,(Nane Bora) inayoelekea kumalizika.

Mwenyekiti wa Klabu ya hiyo ya Simba, Juma Salum amekanusha vikali madai ya tuhuma za utoaji rushwa yanayoelekezwa katika timu yake, ni dhana potofu za baadhi ya watu binafsi wasioipenda timu hiyo na hivyo kuzusha maneno hayo ili kuiharibia maendeleo yake kisoka.

"Sisi tunacheza mpira tu, wala hatutoi rushwa kama inavyoelezwa na baadhi ya watu kwani siku zote kwenye soka hakuna timu inayoridhika kufungwa na hao ndio wanaozusha hayo’, alisema.

Salum ambaye alionekana kushtushwa na tuhuma hizo alihoji kuwa ni kwa nini wasitoe rushwa kwa timu ambazo hazina uwezo wa kutosha badala yake wakimbilie katika timu zenye uwezo kama Yanga na Kajumulo.

Sakata la madai ya tuhuma za utoaji rushwa dhidi ya Simba kwa timu nyingine limezua sokomoko na kusababisha gorikipa wa Yanga, Peter Manyika na kipa Issa Managu wa Kajumulo, kuingia matatani wakituhumiwa kupokea rushwa kutoka Simba.

Aidha tuhuma za utoaji rushwa zimepelekea Chama cha Soka nchini (FAT), hivi karibuni kudai kuwa kitaanza kuchunguza madai hayo kwa baadhi ya wachezaji wa timu zinazoshiriki katika Ligi Kuu ya Mwaka huu ambayo inanukia nukia rushwa.

Baadhi ya hatua ambazo FAT imedai itazichukua kama itabainika kuwepo kwa rushwa katika madai hayo, ni pamoja na timu kufutwa, wachezaji watakaobainika kufungiwa kucheza soka maisha, wahusika kufunguliwa mashitaka mahakamani na matokeo ya mechi zinazohusika yatafutwa.

Hata hivyo katika mfululizo wa ligi kuu ya Safari Lager (nane bora) inayokaribia kufikia ukingoni , timu ya Simba iliwahi kufungwa na watani wao Yanga jumla ya mabao 2-0 katika uwanja wa Taifa.

Mbali na mchezo huo timu hiyo iliwahi kupoteza mchezo wake mwingine kwa kufungwa goli moja na Singida United katika mchezo wa kwanza uliochezwa katika uwanja huo huo.

Anzisheni klabu za kulipwa-Wito

Na Widimi Elinewinga, Morogoro

SERIKALI imesisitiza haja ya kuwapo vilabu na michezo mbalimbali ya kulipwa ili kuwaendeleza wachezaji pamoja na kuboresha viwango vya michezo nchini.

Afisa Mtendaji wa Michezo katika Idara ya Maendeleo ya Michezo ya Wizara ya Elimu na Utamaduni, Frank Macha, wakati akitoa mada juu ya sera ya Taifa ya maendeleo ya michezo katika semina ya siku mbili ya waandishi wa habari za michezo Tanzania (TASWA) iliyofanyika katika chuo cha Tanesco, Morogoro hivi karibuni.

Alisema kwa kuanzisha vilabu na michezo ya namna hiyo, wapenzi wa michezo watakaokuwa wamejitokeza kufanya hivyo, watakuwa wamewachangia kuboresha michezo nchini kwa kuwafanya wachezaji kufaidika na hivyo kujenga ari ya michezo kwa ufanisi.

"Serikali iko tayari kusimamia vyombo husika ili kuhakikisha haki inatendeka kwa wachezaji watakaoingia kwenye mikataba ya kulipwa", alisema Macha.

Macha alitoa changamoto kwa TASWA kuwa na timu ya netiboli mbali na ile ya mpira wa miguu na kuitaka kuanzisha michezo mingine mbali na hiyo.

Watanzania wanne waenda kushiriki Olimpiki Australia

Na Mariam Kossey, DSJ

JUMLA ya wanariadha wanne wa Tanzania pamoja na viongozi wao watatu, mwishoni mwa wiki iliyopita wamepanda ndege ya Shirika la Gulf Air kuelekea Sydney, nchini Australia kushiriki mashindano ya Olimpiki.

Akizungumza jijini Dar-Es-Salam kabla ya kuondoka nchini, Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania, Erasto Zambi, aliwataja wachezaji hao kuwa ni Angelo Simon, Wilbroad Focus, Zebedayo Bayo na Restituta John.

Viongozi walioambatana na wanariadha hao ni pamoja na Dk. Mwamkema, Suleiman Nyambui na Katibu Erasto Zambi.

"Mwanariadha Lwiza John ambaye tulimuengua kwenda kushiriki mashindano haya anatakiwa kuheshimu kamati ya Olimpiki ambayo ilikaa na kumjadili yeye," alisema Zambi.

Lwiza baada ya kuenguliwa huko, amesema kuwa atakwenda kupiga hodi katika ofisi ya Waziri wa Elimu na Utamaduni, Profesa Juma Kapuya kumwelezea yaliyomsibu.

Michezo hiyo ya Olimpiki imepangwa kuanza rasmi Septemba 15.

Michezo ya walemavu kufanyika Dar Septemba

Na Widimi Elinewinga,Morogoro

MICHEZO kwa walemavu nchini imepangwa kufanyika katika uwanja wa Taifa Dar-Es-Salaam, Septemba 10 mwaka huu.

Kwa mujibu wa Afisa wa Michezo katika Idara ya Maendeleo ya Michezo ya Wizara ya Ellimu na Utamaduni, Frank Macha, walemavu watashiriki mchezo wa mpira wa mikono, wavu, kukimbia na baiskeli.

"Kufanyika kwa michezo hiyo hapa nchini ni moja ya utekelezaji wa sera ya maendeleo ya michezo iliyotungwa tangu mwaka 1995 ambayo imesisitiza kuwepo kwa makundi maalum ya walemavu," alisema Macha.

Aliwataka wazazi wenye watoto walemavu kuwapa mwanya wakushiriki katika mashindano hayo ili kuleta msisimko.

Mashindano hayo kwa walemavu yameandaliwa na kampuni ya Roots and Shoots ya Marekani ambayo ina tawi lake nchini hapa

1500 waomba uanachama Yanga

lWengine waomba gharama ipunguzwe

lWaamuzi wataka wapewe uhuru , wasiingiliwe na FAT

Na Mwandishi Wetu

ZOEZI la Uchukuaji wa fomu za kampuni ya Yanga, umekuwa ukiendelea vizuri ambapo zaidi ya wanachama 1,500 wamejitokeza kuomba uanachama mpya.

Mweka Hazina wa kampuni ya Yanga Pastory Kyombya aliliambia gazeti hili kuwa zoezi hilo linakwenda kasi ikilinganishwa na miaka iliyopita.

Amesema, fomu hizo huuzwa kwa bei ya sh. 500/=.

Hata hivyo wapenzi wengi wa kampuni hiyo wameutaka uongozi unaohusika, kujaribu kupunguza gharama ya kujiunga kuomba wanachama.

"Licha ya wanachama wetu kujitokeza kuchukua fomu, lakini bado wanalalamikia ada hiyo ya uchukuaji wa fomu," alieleza Kyombya.

Zoezi la kuandikisha wanachama wapya kwa kampuni hiyo lilianza Julai 5, mwaka huu.

Wakati huo huo: Chama cha Waamuzi Tanzania (FRAT), kimetaka kisiingiliwe kazi zake na kipewe madaraka zaidi ya maamuzi ili waamuzi wake waweze kuchezesha michezo bila matatizo.

Mwenyekiti wa FRAT Taifa, Kassim Chona alisema kuwa FRAT ipo mstari wa mbele kuwanasa waamuzi juu ya maadili lakini hali iliyopo hivi sasa ya waamuzi kuboronga katika michezo kadhaa, inatokana na chama cha soka nchini FAT kuchukua madaraka ya FRAT.

"Sisi tunaamini ya kwamba tuna waamuzi wazuri wanaostahili kuchezesha michezo bila matatizo endapo kazi hiyo itafanywa na FRAT bila kuingiliwa," alisema Chona.