Michezo

LIGI KUU YA SAFARI LAGER

Yanga kujihakikishia Ubingwa?

Na Gerald Kamia

Timu ya Yanga baada ya kutoa vipigo mfululizo kwa timu za Simba na Coastal Union ya Tanga Jumamosi hii inaingia uwanjani kwa lengo la kutafuta uwezekano wa kutwaa pointi tatu dhidi ya timu ya Singida United mchezo utakaofanyika kwenye Uwanja wa Umoja mkoani Singida.

Ikiwa Yanga itashinda mchezo huu, basi itakuwa imejihakikishia nafasi ya kutwaa ubingwa wa ligi Kuu ya Safari Lager inayoshirikisha jumla ya timu nane zilizofuzu kucheza ligi hiyo.

Timu zote leo (Jumamosi), zitaingia uwanjani huku zikiwa na rekodi ya kushinda mechi zake zilizopita.

Wakati Yanga iliibwaga Coast Union ya Tanga kwa magoli 2-1, Singida United nayo iliibugiza Simba kwa goli 1-0.Katika mchezo wa kwanza uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, timu ya Yanga ilifanikiwa kuwafunga Singida United kwa jumla ya magoli 2-1.Mchezo mwingine utakuwa ni kati ya vibonde wa ligi hiyo; timu ya Kagera watakapo wakaribisha timu ya Kajumulo ya jijini mchezo ambao utafanyika katika uwanja wa Kaitaba mkoani Bukoba.

Mchezo huo ni muhimu kwa timu ya Kajumulo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupata moja kati ya nafsi tatu za juu.

Ligi hiyo itaendelea tena kesho (Jumapili hii) kwa pambano kati ya timu ya Simba na Coast Union ya Tanga mchezo ambao utafanyika katika Uwanja wa Taifa jijini.

Timu zote mbili zitaingia uwanjani kesho huku zikiwa na majeraha ya kufungwa mechi zake zilizopita Wakati Simba imepoteza matumaini ya kutwaa ubingwa kwa kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Yanga na Singida United, Coastal Union nayo imepoteza mchezo dhidi ya Yanga katika mchezo uliofanyika Jumatano iliyopita.

Kibadeni atakiwa kujiuzulu

Na Gerald Kamia

BAADA ya kupokea vipigo viwili mfulululizo kutoka kwa timu za Yanga na Singida United, washabiki na wapenzi wa klabu ya soka ya Simba wamesema kuwa, hawamtaki Kocha Mkuu wa timu hiyo, Abdalla Kibadeni na kwamba hana budi kuachia ngazi.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwenye Uwanja wa Karume jijini, mashabiki hao wamesema hawana imani na kocha huyo na kwamba wanachotaka wao ni yeye Kibadeni kujiuzulu.

"Ni bora aachie ngazi mwenyewe aende akafundishe Kajumulo kabla hajapatwa na matatizo makubwa kuliko kutuharibia timu yetu ambayo tunaijua inawachezaji wazuri," alisema Issa Maulid mkazi wa Temeke

"Kila mwaka sisi tunakuwa wasindikizaji sijui tutachukua ubingwa lini. Mwaka jana tulianza vizuri lakini mwishoni, timu ikaanza kuboronga na mwaka huu vilevile; sijui kuna nini." alisema Bw. Abbas Mohamed na kuungwa mkono na Mustapha Mruta.

Wapenzi hao wa soka wameendelea kusema kuwa wanamwomba kocha huyo na viongozi wasiofaa kuachia ngazi mapema na kuiacha Simba ili ichague viongozi na makocha wanaofaa kuliko kukaa na wababaishaji.

Klabu ya Simba imekumbwa na mgogoro mkubwa kufuatia kufungwa na watani wao wa jadi, Yanga kwa jumla ya magoli 2-0 katika mchezo uliofanyika Jumamosi iliyopita jambo lililowafanya baadhi ya viongozi wa Simba kuwatuhumu baadhi ya wachezaji wa timu hiyo kuwa walihusika na kipigo hicho.

Wachezaji waliotuhumiwa ni pamoja na golikipa, Doi Moke, Wiliam Fanibulleh, Bakari Malima na Patrick Betweel.

Klabu za simba na Yanga zimekuwa zikukumbwa na migogoro kufuatia timu moja kuibuka na ushindi dhidi ya nyingine.

Ikumbukwe kuwa mgogoro kama huu, uliikumba Yanga katika raundi ya kwanza mara baada ya kufungwa na Simba na sasa ni zamu ya klabu ya Simba.

Juhudi za kuwasiliana na Kocha huyo Mkuu wa Simba, Abdalla Kibaden ili kuzungumzia suala la kutakiwa kwake kujiuzulu, mwishoni mwa juma hazikuzaa matunda kwa kuwa kila alipopigiwa simu yake ya mkononi, ilikuwa imefungwa

Mokake atamba Ngorongoro Warrious kuwakomesha Msumbiji

Na Widimi Elinewinga na Gerald Kamia

KOCHA wa Timu ya Taifa ya Vijana chini ya miaka 20 Ngorongoro Warrious, Ernest Mokake amesema kuwa timu yake kwa sasa ipo "fit" kukabiliana na Timu ya Vijana ya Msumbiji.

Akizungumza jijini mwishoni mwa wiki katika ofisi za chama cha Kabumbu nchini, (FAT), Mokake alisema kuwa wamejiandaa vyema na mchezo wa leo.

Aidha alisema kuwa timu ya Ngorongoro inamajeruhi takribani sita na alipotakiwa kuwataja majeruhi hao hakutaka kuweka bayana akihofu Wanamsumbiji hao wasije wakayafanyia kazi majina hayo katika mchezo wa leo lakini akasisitiza kuwa licha ya kuwa na majeruhi hao anamatumaini makubwa ya kuibuka na ushindi.

Timu ya soka ya Msumbuji iliwasili jijini juzi ikitokea nchini Maputo Msumbuji tayari kwa mchezo wao wa leo.

Akiongea muda mfupi bada ya timu hiyo kuwasili katika uwanja wa ndege, Kocha Mkuu wa timu hiyo Joachim Joao, alisema kuwa wao wamekuja nchini wakijua kuwa timu ya Tanzania ni ngumu kwa kuwa iliitoa timu ya Namibia raundi ya kwanza.

Timu hiyo iliwasili na kikosi cha watu 25 wakiwemo wachezaji pamoja na viongozi.

Mashindano ya Lawn Tennis kuanza Agosti 14

Na Widimi Elinewinga

MASHINDANO ya "Lawn Tennis" ya Afrika Mashariki na Kati kwa umri chini ya miaka 14, yataanza kuchezwa rasmi Agosti 17 katika Viwanja vya Gymkhan jijini Dar-Es-Salaam.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mchezo huo nchini, Richard Rugimbaria alisema kuwa Tanzania ambayo ndiyo mwenyeji wa michuano hiyo itashirikisha wachezaji nane.

Aidha Rugimbaria aliongeza kuwa kambi ya mazoezi ya timu hizo itaanza rasmi Agosti 14 mpaka 17 ambapo mchezo wa kwanza kuanza utachezwa Agosti 17 mpaka 21.

Michuano hiyo itashirikisha nchi nane na Tanzania ni ya Tisa. Timu hizo ni Shelisheli, Kenya, Djibout na Rwanda.Nchi nyingine ni Burundi, Ethiopia na Sudan.

Mashindano haya ya Lawn Tennis yanafanyika kila mwaka.