Michezo

LIGI KUU YA SAFARI LAGER

Nani kutamba leo; Simba au Yanga?

lShungu asema ama zao ama zetu ushindi ni lazima

Na Gerald Kamia DSJ

HATIMAYE mashabiki na wapenzi wa soka nchini leo watapata jibu la nani zaidi baada ya kumalizika kwa mpambano mkali kati ya timu ya Simba na Yanga ,pambano ambalo litafanyika katika Uwanja wa Taifa jijini.

Wababe hawa mechi watakayo cheza leo itakuwa niya raundi ya pili ya ligi ya Safari Lager inayoshirikisha timu nane zilizofuzu katika hatua hiyo .

Katika mchezo wa leo kila Timu imeahidi kutoka na ushindi dhidi ya mpinzani wake jambo ambalo linaufanya mchezo kuwa wa vuta ni kuvute kwa pande zote mbili.

Katika mchezo wa raundi ya kwanza Timu ya Simba ilifanikiwa kuwalaza wapinzani wake bao 2-1 jambo ambalo Yanga imeahidi kuwa haitarudia kosa.

Kocha Mkuu wa Timu ya Yanga ,Mkongo Raul Shungu amesema kuwa mchezo wa leo ni muhimu timu yake ishinde ili ijiweke katika mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa. "leo ndio leo ama zao ama zetu ushindi ni lazima kwa timu yangu" alisema Shungu.

Naye Kocha Mkuu wa Timu ya Simba Abdalla Kibadeni amesema kuwa ushindi kwa timu yake ni lazima ‘wembe ni ule ule tulioutumia mara ya kwanza kwa sasa tunabadilisha upande wa pili" alitamba Kibadeni.

Katika mchezo wa leo timu zote zitaingia uwanjani zikiwa na wachezaji wake muhimu.

Upande wa Simba utawategemea zaidi washambuliaji wake Steven Mapunda, ‘Garincha’, Ally Yusufu ‘Tigana’ pamoja na Said Maulid huku ngome yao ikilindwa na Bakari Malima, Musa Msangi, Patric Betwel na nyanda wao Doe Moki.

Kwa upande wa Yanga wao watajivunia zaidi wachezaji wake wazoefu akina Edibili Lunyamila, Mohamed Husen ‘Mmachinga’ Shaban Ramadhani na Sekilojo Chambua.

Upande wa mabeki utakuwa na mkongwe Said Mwamba Kizota, Ally Mayay, Banza Chikala pamoja na Mlinda mlango Chachala Muya.

BMT yapongezwa kufanya uteuzi mzuri wa uongozi wa FAT

Na Gerald Kamia, DSJ

WAPENZI wa soka nchini wameupongeza uongozi wa Baraza la Michezo nchini (BMT) kwa uteuzi wa viongozi wa chama cha soka nchini (FAT) ambao umezingatia zaidi utendaji wa viongozi na wala sio majina.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari hizi wiki hii kwenye uwanja wa Karume Jijini mara baada ya kutangaza majina ya waliopitishwa kugombea uongozi wa FAT, wapenzi hao wamesema kuwa matunda ya majina ya viongozi walioteuliwa yanaonekana siyo ubabaishaji.

"Baraza la michezo linastahili kupongezwa kwa kuweza kuchagua viongozi ambao ni watendaji wazuri na matunda yao yanaonekana"alisema Hamisi Shaban mkazi wa Ilala.

"Kwa mfano kwenye nafasi ya mwenyekiti kwa kweli wamemchagua mtu ambaye ana uchungu na maendeleo ya soka hapa nchini sote tunaelewa ndugu Kipingu mchango anaoutoa kwa taifa hili nafikiri sasa FAT ya mwaka huu itakuwa na viongozi wanaojua utendaji wa kazi sio wababaishaji kama tulivyo zoea" alisema bwana Shaban Mtupa kauli ilioungwa mkono na Abdala Issa.

Wapenzi hao waliendelea kusema kuwa ‘sasa viongozi waliochaguliwa ni sura mpya na ni watu wenye uchungu na taifa hili tunategemea kuwa Tanzania haitakuwa kichwa cha mwendawazimu tena katika soka".

Hivi karibuni Baraza la Michezo la Taifa (BMT) lilitangaza majina ya waliopitishwa kugombea uongozi katika Chama cha Soka nchini (FAT)ambapo katika uteuzi huo nafasi ya Mwenyekiti imeenda kwa Mlezi wa Timu ya Taifa ya Vijana, Kanali Kipingu jambo ambalo limeungwa mkono na wapenzi wa soka hapa nchini.

Ligi ya Mpira wa kikapu Dar kuanza leo

Na Widimi Elinewinga,DSJ

LIGI ya Mpira wa Kikapu kwa mkoa wa Dar-Es-Salaam,inayojulikana kama RBA KILI LEAGUE kwa msimu wa mwaka 2000 itaanza kuchezwa rasmi leo katika viwanja mbalimbali jijini

Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake katikati ya wiki,Katibu Mkuu Msaidizi wa Chama cha Mpira wa Kikapu mkoani Dar es Saalam (DARBA), Martha Kente , alisema ligi hii itashirikisha timu 14 za wanaume na inatarajia kuwa na timu 6 za wanawake.

Alisema timu hizo za wanawake zitapatikana baada ya kucheza ligi ya mtoano ambayo inaendelea.

Aidha Kente alisema ligi ya msimu huu imegawanyika katika makundi matatu ambapo ambayo aliyataja kuwa ni pamoja na lile la Wilaya ya Kinondoni ambalo litashirikisha timu za Pazi, Mbezi Waves, Oilers, UDSM, Magnet na Srelio

timu za Kundi la pili ni timu za wilaya ya Ilala ambazo ni Savio , Vijana, Magone na Jogoo ambapo kundi la mwisho ni lile la timu za wilaya ya Temeke ambazo ni ABC , JKT , Cargo na Chang’ombe Boys.

Timu za kundi la kwanza zitakazo fungua dimba ni UDSM itakayopambana na timu ya SRELIO mchezo utakaofanyika katika uwanja wa TANESCO

Ambapo timu ya Pazi itapambana na timu ya Mbezi Waves katika kiwanja cha Drive In.

Katika kundi la pili leo timu ya Savio itakwaana na timu ya Jogooo katika kiwanja cha Don Bosco na katika kundi la mwisho timu ya JKT itapambana na timu ya Cargo katika kiwanja cha JKT kilichopo Mgulani .