MAZISHI YA PADRE KIJA
Mamia
ya watu wamzika Padre Kija
Na
Charles Hililla, Shinyanga
MAMIA ya watu kutoka
ndani na nje ya nchi wamejitokeza kwa wingi kumzika aliyekuwa Katibu Mtendaji
wa Idara ya Mawasiliano katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania,Padre
Norbet Kija aliyefariki dunia Septemba 19 na kuzika Septemba 22 mwaka huu
Jimboni kwake Shinyanga.
Akizungumza katika kwenye misa ya
mazishi ya Padre huyo,Askofu wa Jimbo la Shinyanga,Askofu Aloysius Balina
alisema kuwa Binadamu siku zote anatakiwa kuishi maisha yanayompendeza Mungu
ili kuleta heshima na maana ya uwepo wake hapa
duniani kwani hajui siku wala saa atakayoitwa kwa Mungu
"Uwepo wa binadamu hapa duniani ni
pamoja na kumjua Mungu na kufanya mambo yanayoendana na mapenzi yake na siyo kuishi kwa vile
ulijikuta upo duniani"alionya Askofu Balina.
Askofu Balina alimtaja marehemu padre
Kija kuwa alikuwa na tabia ya upole na unyenyekevu tabia ambayo alisema ni
mfano wa kuigwa na jamii.
Aliendelea kusema kuwa moyo wa marehemu
wa kuwafikiria zaidi na kujitoa kwa
ajili ya wengine kuliko kujifikiria mwenyewe ni moja ya sifa zilizompa
mafanikio katika shughuli zake mahali pote alipofanya kazi au kuhudumia.
Misa hiyo ya kumuombea marehemu padre
Kija ilitanguliwa na ibada fupi ya kupokea mwili huo iliyofanyika nje ya mlango
wa Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki la Shinyanga ambapo iliongozwa na padre Norbert
Ngussa.
Baada ya ibada hiyo jeneza lililokuwa
limewekwa mwili wa marehemu liliingizwa kanisani kwa ajili ya watu mbalimbali
kutoa heshima zao za mwisho.
Marehemu Padre Kija amezikwa kwenye
makaburi ya mapadri yaliyopo nyuma ya Kanisa Kuu Jimbo Katoliki la Shinyanga.