Tuutukuze Msalaba kwa kudumisha amani, upendo

TUNAELEKEA mwisho wa mwaka huu wa 2000, ambao umekuwa ni mwanzo wa milenia ya tatu.

kwa Wakristo, tumeuita ni Mwaka Mtakatifu na pia, Mwaka wa Jubilei Kuu. Katika mwaka huu, kumekuwa na mambo mengi ambayo yamefanyika kitaifa, kijimbo, kiparokia na hata katika jumuiya ndogondogo za Kikristo.

Kwa jumla, tunaweza kusema kuwa katika mwaka huu wa 2000, kumekuwa na mambo mengi ambayo yametendeka katika kuuadhimisha.

Katika Kanisa Katoliki la nchini Tanzania, licha ya kufanyika kwa ibada mbalimbali pamoja na mikesha, mafungo na kupokea Sakramenti, pia kumekuwa na kuutembeza Msalaba wa Jubilei katika maparokia na jumuia mbalimbali za Kikristu.

Maajabu mengi yametendeka katika ibada mbalimbali za Msalaba. Waamini wameubeba, wamekesha nao hata wamekuwa wakifanya Ibada Takatifu mbele yake.

Wenye matatizo mbalimbali kutokana na imani yao kwa Msalaba huo, wamesaidiwa kwa namna moja au nyingine. Kwa kifupi, tunaweza kusema kwamba kwa njia ya Msalaba waamini na wasio waamini wameamshwa imani yao katika chombo hiki cha ukombozi wa wanadamu.

Jubilei hii Kuu, inatukumbusha hasa tendo la Ukombozi alilolifanya Bwana Wetu Yesu Kristu kwa kutufilia Msalabani ili aweze kutupatanisha tena na Baba wa Milele tuliyekuwa tumemwasi kwa kutenda dhambi.

Kwa upande wetu sisi waamini Wakristo, Msalaba unatufundisha mambo mengi yakiwamo matendo mema kama vile huruma, upendo na uvumilivu wa Bwana wetu Yesu Kristu.

Msalaba ni ishara wazi kwetu sisi Wakristo unaonesha kwamba tumekombolewa kwa njia hiyo na hivyo, tunapaswa kuuenzi na kuutukuza bila kuuonea aibu wala kuwa na woga wo wote.

Ni dhahiri kabisa kuwa tunao wapinzani wengi wa chombo hicho cha Ukombozi hapa na pale. Lakini, tunatumaini kuwa heshima ambayo tumeupatia Msalaba mwaka huu, itazidi kuongezeka katika jamii yetu.

Tumesema kuwa jambo kubwa katika kuutukuza Msalaba ni kutambua hasa kuwa ni kitu gani tunafundishwa kutokana nao.

Jambo muhimu na kubwa tunalofundishwa nao, uvumilivu na kusameheana. Uvumilivu ni fadhila kubwa sana tunayohitaji katika maisha yetu.

Katika jamii, tunaishi na binadamu wenzetu ambao wanye tabia tofauti na za aina mbalimbali.

Ni kwa maana hiyo, hatuna budi kutumia upendo, heshima, utu na kuvumiliana kwa hali ya juu kwa kuwa kwa namna yoyote iwayo, hatuwezi kukwepa kabisa maudhi na kutokuelewana miongoni mwa jamii.

Ni kwa maana na nafasi hiyo, tunapaswa kuukumbuka Msalaba ambao kwa njia yake Kristo anatufundisha kuvumilia.

Tunapaswa kuvumiliana katika familia zetu, katika jumuiya zetu na mahali po pote pale ambapo tunaishi na kushirikiana na wenzetu.

Waamini wote ambao wanashiriki katika kuubeba Msalaba, kuutolea heshima na kuufanyia ibada, wanapaswa kuwa wamebadilika kabisa katika tabia.

Hivi sasa katika taifa letu tunajiandaa kwa Uchaguzi Mkuu wa rais, wabunge na madiwani. Kampeini zinafanyika hapa na pale kwa maneno pengine yasiyopendeza masikioni mwa wengi.

Tunapaswa kuvumiliana na hivyo kuchukuliana tabia hizo zilizo tofauti kwa jinsi zilivyo.

Litakuwa ni jambo lisilo sawa sawa ikiwa raia Wakristu ambao wameshiriki kikamilifu katika ibada ya Msalaba, watakuwa katika mstari muovu wa kuleta fujo na kuvunja amani katika nchi yetu.

Ikiwa Wakristo ambao wameubeba na kukesha na Msalaba watakuwa na uvumilivu kati yao, hapo tutaonja mapato na matunda yake kwa kuiletea amani nchi yetu.

Kwa maneno mengine, tunaweza kusema kuwa kwa njia ya Ibada Takatifu ya Msalaba, waamini Wakristo watazidi kuwa chumvi na mwanga katika jamii yetu ya Tanzania.

Ni kwa njia hizo za ibada kwa Msalaba, wataleta utamu katika nchi yetu, yaani watawapatanisha wananchi wenye kufarakana kwa sababu za kisiasa au kidini.

Tunafundishwa kwamba Kristo kwa kuwambwa kwake pale Msalabani, aliwakusanya wafuasi wake wote na wale ambao siyo wafuasi wake.

Tumeshuhudia kwamba katika Mwaka huu wa Jubilei wakati wa kuutembeza Msalaba, siyo waamini Wakristo pekee yao walioshiriki katika ibada hizo, bali na hata wale wasio waamini Wakristo.

Jambo hilo limetufundisha kwamba kwa njia ya Msalaba, tunapaswa kuwa kitu kimoja hasa katika taifa letu. Tunaweza kuhitilafiana katika mawazo yetu, lakini kutoka na mawazo tofauti tusifarakane wala kugombana, bali tuyabadili mafarakano na kuwa patano ilanalojenga zaidi umoja, upendo na manani baina yetu.

Tunapenda kuwapongeza viongozi wetu wa Kanisa, maaskofu walitoa uamuzi wa kuutukuza Msalaba kwa namna ya pekee katika Mwaka huu wa Jubilei.

Tunapofanya tathmini ya maadhimisho ya Jubilei Kuu, Ibada ya Msalaba husimama mahali pa pekee kabisa.

Wengi wametambua umuhimu na maana ya Msalaba katika kumfuata Kristo. Msalaba kama tulivyosema, ni alama wazi kabisa ya ukombozi wetu kwani hakuna Ukombozi bila Msalaba.

Kwa miaka hiyo yote 2000 ya Ukristo wetu Msalaba umekuwa ni kitambulisho thabiti cha ufuasi wetu.

Pia, Msalaba huo umekuwa kiunganishi chetu waamini, sisi kwa sisi na pia sisi na wenzetu wasio waamini Wakristu.

Tunazidi kutoa rai kwa waamini wenzetu Wakristu kwamba tuendelee kuuenzi Msalaba ambao ni chombo cha Ukombozi wetu.

Kwa njia ya kuuangalia Msalaba tunapaswa kujifunza kuvumiliana na kuchukuliana kama Kristo mwenyewe alivyofanya katika kazi hiyo ya kutukomboa kwa Msalaba na kifo chake.

Tuzidi kuwa na imani zaidi katika Msalaba na hivyo tuutangaze kwa kuuishi tukivumiliana na kusameheana daima tunapokoseana iwe ni katika familia, katika jumuiya zetu na hasa katika taifa letu kwa ujumla.

Itakuwa aibu na fedheha na hata kuudhalilisha Ukristo sambamba na Mwaka huu Mtakatifu wa 2000, kama atajitokeza atakayeisliti nafsi na imani yake, akawa kichocheo cha vurugu katika jamii.

Uchafuzi wa mazingira Kibakwe ni mradi wa maendeleo ya Afisa Misitu

Ndugu Mhariri,

Naomba unipe nafasi katika gazeti hili ili nitoe dukuduku langu kuhusu uharibifu wa mazingira katika tarafa yetu ya Kibakwe.

Kibakwe kwa asili ni tarafa iliyokuwa na mazingira mazuri sana. Hivi sasa, Kibakwe imepoteza umaarufu wake kwani imekuwa makorongo matupu yaliyo sababishwa na ukataji miti ovyo.

uharibifu huo unafanyika mbele ya macho ya Afisa Misitu wa Tarafa Bw. Clemence Msigala. Cha kushangaza, amekuwa anafumbia macho.

Watu wanaendelea kukata ovyo miti ya asili. Wanavamia milimani na jambo la hatari zaidi ni kwamba, miti imefyekwa mpaka kwenye vyanzo vya maji huku IDIRI.

Halitakuwa jambo la kushangaza chemichemi hizo zikikauka kwa yeyote anayetaka kuthibitisha hili atembelee Kibakwe na afuate njia ya miguu kwenda Wotta atakwenda kushuhudia vioja vinavyotendeka katika milima ya kwenda IDIRI.

Nchi yote imekuwa tupu kabisa. Miti iliyokuwa inaifunika milima hiyo imekatwa yote bila woga wala huruma.

Bwana miti yupo Uongozi wa Tarafa upo, uongozi wa kata upo, serikali ya kijiji ipo.

Inasikitisha sana kuona serikali inawalipa watu mishahara mikubwa lakini kazi wanayofianya ni kuyahujumu mazingira ya nchi yetu.

Inashangaza sana utamkuta Afisa misitu huyo tangu Januari hadi Desemba, tangu asubuhi mpaka jioni, tangu tarehe 1-31 ya kila mwenzi ni mtu wa kunywa (kulewa) pombe tu, mbaya zaidi ni kwamba uzembe huu sio wa siri kwani Katibu Tarafa anatambua juu ya hujuma hizi na hata DC anajua ukiachilia mbali viongozi wa Idara ya misitu.

Inaelekea kuna sababu inayowafanya wamfumbie macho mtumishi mzembe.

Hata hivyo, ukweli ambao hautageuka kuwa uwongo ni kwamba uharibifu huu wa mazingira na hasa ukataji ovyo wa miti unaofanywa bila hatua kuchukuliwa ni mradi unaomletea mapato Afisa misitu huyu pamoja na wenzake. Hiyo si siri.

Naushauri uongozi wa Serikali ufanye marekebisho ya haraka ili kuyanusuru mazingira ya Kibakwe ambayo sasa asilimia zaidi ya 75 ni jangwa.

Bwana miti: Raha unazozipata ni mauti yetu sisi na vizazi vyetu. Hivyo, ni dhambi na sijui utajaungama vipi ili upate maondoleo, JIREKEBISHE.

Wote mnaoshiriki kwa namna moja au nyingine kukata miti hovyo, nawaambia miti hiyo itakuwa ndizo kumi za kuwaunguzeni huko Jehanamu. Shime wana Kibakwe tutunze mazingira yetu.

Romanus Mwakalolo

C/O S.L.P 114

MPWAPWA