Ni kweli wagonjwa wa Ukimwi wanatibiwa bure?

SUALA la uchangiaji wa huduma muhimu za kijamii katika nchi yoyote, ni muhimu. Hii pia inahusisha uchangiaji usio wa moja kwa moja kwa njia za kodi na ushuru mbalimbali ambao pia huchangia kuinua na kukuza pato la taifa.

Tunasema uchangiaji wa namna hiyo ni muhimu kwa kuwa kuiachia kazi ya utoaji huduma zote kwa serikali, ni kuipa mzigo serikali ambao haiwezi kuubeba hasa kwa taifa changa kama hili la Tanzania ambalo linahitaji ushirikiano baina yake na watu wake.

Hata hivyo, katika jamii yoyote, wapo watu ambao kwa sababu moja ama nyingine, ni watu wanaostahili kusamehewa kufanya kazi na hao ni kama vilema, watoto na wazee.

Ni kwa kujali hali zao na umuhimu wao kwa taifa, ndio maana wanapata ruhusa za namna hiyo.

Pia, wapo watu wengine ambao pia hali zao, zinahitaji huruma, upendo na utu wa wenzao ili waishi katika jamii huku wakipata huduma na mahitaji muhimu ya kijamii kama chakula, mavazi, elimu na huduma za afya.

Suala la afya ni suala muhimu kwa kila mwanadamu au kiumbe yeyote mwenye uhai.

Ni kwa kujua umuhimu wake, ndio maana hata imekuwapo haja ya jamii kuchangia huduma za afya ili zitolewe kwa ubora unaokaribia kuridhisha kama sio kuridhisha kabisa.

Hata hivyo, licha ya kujulikana umuhimu wa kuisaidia serikali katika suala la uchangiaji wa huduma hiyo ya afya na matibabu, tayari serikali yenyewe ilishatoa msamaha kwa baadhi ya watu ambao imefanya tafiti mbalimbali na kukiri kwa kinywa chake kwamba hawawezi kumudu gharama za matibabu na huduma za afya.

Miongoni mwa watu hao, ni watoto wadogo ambao wameruhusiwa kupata huduma hiyo ya afya bure.

Wengine, ni kundi la waathirika wa magonjwa mbalimbali wakiwamo wakoma, wenye TB, na wagonjwa wa UKIMWI.

Kinachotushangaza na hata kutufanya tujiulize masuala mengi juu ya serikali yetu tukufu ni kwamba, je, watu hao hususani wagonjwa wa UKIMWI ambao ni miongoni mwa wagonjwa wanaoruhusiwa kupata huduma ya afya bure, wanapata huduma hiyo bure kama inavyotajwa?

Inasikitisha sana na pia hali iliyo wazi kwa kila mtu kwamba unapokwenda hospitali, hutakosa kuwakuta wagonjwa ambao ingawa hali zao si mbaya kiasi cha kukaribia kifo, lakini ni mbaya; wakiwa wamepangishwa foleni wakisubiri kumuona daktari na huku wengine wakihaha na kuhofia kukosa matibabu kwa kuwa hawana pesa.

Tunasema hivyo tukiamini kuwa ni mara nyingi wameonekana hata wakathibitishwa kuwa ni waathirika wa UKIMWI lakini, swali linakuja kuwa, ni kwanini wanalipishwa michango ya tiba kama watu wengine?

Ni mara ngapi wamekuwa wakionekana kushikilia vyeti mikononi huku wakiwa hawana muelekeo baada ya kuambiwa gharama za madawa katika madirisha ya hospitali nyingi zikiwamo za serikali ambazo ndilo kimbilio la watu?

Inashangaza mno kuona kuwa wakati mashirika yasiyo ya kiserikali yana mpango wa kueleweka wa kutoa huduma za tiba bure kwa wagonjwa wa UKIMWI, lakini bado ni kitendawili kigumu kwa hospitali za serikali kuonekana kama zisizo na mpango unaoeleweka na wazi wazi juu ya wagonjwa hao.

Ni dhahiri kuwa wagonjwa wa UKIMWI wanapofika katika hospitali hizo za serikali, huchukuliwa sawa na wagonjwa wengine na kuambiwa hakuna dawa na hivyo, waende wakajinunulie wajuako.

Serikali ina maana gani ina posema wagonjwa hao watapata huduma ya tiba bure kama wanapokwenda hawapati hiyo dawa na badala yake wanaelekezwa pa kununua?

Kama serikali ilijua hawana uwezo wa kumudu kuchangia gharama za tiba na ikaondoa madai ya mchango dhidi yao, serikali hiyo hiyo ina mpango gani inapokuwa haina dawa na huku ikijua kuna watu wanaitegemea kwa matibabu ya bure?

Je, dawa zinapokosekana huwa kuna mpango wowote wa kuwasadia kuzipata toka mahali pengine wakati hospitali hizo za serikali zikishughulikia upatikanaji wake?

Tunadhani umefika wakati serikali ikaacha kuwadanganya watu kuwa inawatibu bure wagonjwa wa UKIMWI wakati wanasimama madirishani sawa na wengine kisha kuambulia kuambiwa hakuna dawa.

Huu ni unafiki na ni dhambi kwa Mungu kuwadanganya wagonjwa kama hao kuwa unawatibu bure huku unawaambia hakuna dawa waende wakajitafutie, sasa watafute wapi, na nani awalipie?

Hivi dawa zao zinapokosekana hospitali, hao waliothibitishwa kuwa na UKIMWI, huwa wanapewa walau senti kidogo ili ziwasaidie kutafutia dawa katika hospitali za kibinafsi, au huwa wakiambiwa hakuna dawa unakuwa mwisho wa maneno?

Serikali inaposema inabeba jukumu fulani, ilibebe kweli na sio kusema imebeba kwa maneno na hali kwa vitendo haimo.

Ili kuboresha hali hii hasa kwa wagonjwa wa UKIMWI, ushirikiano baina ya serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs), hauna budi kuboreshwa kwani kwa sasa haujakuzwa vizuri.

Mfano, Kumekuwapo na madai kuwa kunaendeshwa utafiti katika hospitali ya Lugalo kuhusu dawa ya UKIMWI, lakini mashirika mengi kama Vile PASADA, hayajahusishwa kwa njia moja ama nyingine wakati ni dhahiri kuwa mashirika hayo ndiyo yanayojihusisha na utoaji huduma kiroho na kimwili kwa waathirika wengi wa UKIMWI.

Inabidi serikali kupitia watendaji na vyombo vyake, ijiulize kama kweli ushirikiano baina ya mashirika hayo yasiyo ya kiserikali na serikali yenyewe unaridhisha na kisha ijiulize kuwa NI KWELI WAGONJWA WA UKIMWI WANATIBIWA BURE?

Kutompa mfanyakazi mshahara sahihi ni dhambi

Ndugu Mhariri,

Nimekisikia kipindi chenye jina hapo juu kutoka Radio Tumaini (Jumamosi 5/08/2000 saa sabasaba hivi za mchana) kwa ufupi, kijana Mtangazaji wa kipindi hicho alijitahidi sana kuelezea kuhusu ajira - waajiri , waajiriwa na hasa mabaa na vilabu vya pombe vinapotumika kama vyanzo vya ajira kwa vijana hususani wasichana.

Mwisho wa kipindi chake, kijana huyo alishauri kuwa wenye mabaa na vilabu vya pombe wasitoe mshahara mdogo, tena bila mkataba rasmi kwa hao.

Uhaba wa mshahara na maisha magumu ndivyo vinavyopelekea wasichana hao wakubali kufanya mambo yasiyofaa ukiwamo ukahaba(kuuza miili).

Kufanya hivyo ni kinyume cha maadili ya Kitanzania na pia ni hatari sana hasa siku hizi kutokana na ugonjwa hatari uliopo sasa wa Ukimwi.

Mimi ninaongeza na kushauri kuwa,

i. Wanaomiliki mabaa na vilabu vya pombe (waajiri) wajue kuwa moja ya dhambi zinazoleta hasara ya Mungu papo kwa papo ni hii ya "Kutompa mfanyakazi wako mshahara wa haki" Kwa dhambi hii, Mungu hachelewi; anamuadhibu tena kwa ukali kila anayevunja amri hii!

ii. Ni dhambi kubwa kwa mtu (Mkristo) kujiweka katika hatari ya kutenda dhambi/kufa bila sababu kubwa! Kwenye mabaa kwenye disko kwenye Dogoli,kwenye ngoma zinazokesha usiku, kwenye taarabu n.k. mikusanyiko hiyo mahali kama humo wakati kama huo ni vyepesi zaidi kuvutwa kufanya dhambi kwa hiyo yafaa vijana wasiende huko wala wasifanye kazi kama hizo!

(zamani watoto /wasichana wa Kikristo (Wakatoliki)ilikuwa taabu sana kuwakuta kwenye sehemu kama hizo nilizozitaja).

iii. Mwisho kabisa vijana msiuze miili/ msizini sababu sio tu kuogopa kupata ukimwi ila hasa ni kwamba Mungu amekataza jambo hilo na kwamba anayefanya hayo anafanya dhambi na kama mtu huyo hatatubu na kuacha uzinifu, basi atatupwa motoni.

 

Asante sana

Mwalimu Mkatoliki,

Innocent M. Mongo,

S.L. P 1288

MOROGORO.

Barabara mbona zinakwanguliwa tu, kila mwaka?

Ndugu Mhariri,

HUWA sipendi kusemasema kwenye vyombo vya habari lakini kwa hili, naomba uninyofolee nafasi kidogo nitolee dukuduku langu kwenye gazeti lako.

Ninakerwa na kushangazwa na adha za kuona na kutimuliwa vumbi kila mwaka katika barabara za Manisapaa hii ya Temeke kwa madai ya matengenezo.

Kila mwaka watu wa Temeke hasa Mtoni, ni lazima tuone barabara zikikwanguliwa kwa hisia kuwa zinatengenezwa.

Kinachoshangaza ni kwamba, kila baada ya matengenezo hayo kinachofuatia ni vumbi kutimka mithili ya unga kwenye mashine na mvua ikinyeesha tu, hata ya dakika tano, barabara hizo hugeuka na kuwa mto au bwawa la tope.

Sasa, serikali katika manisapaa hii haioni kwa inapoteza muda na fedha huku ikiongeza adha na kero kwa watu wake kwa kukwangua barabara kila mwaka badala ya kutafuta mara moja ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la barabara?

Ninadhani matengenezo hayo huwa yanalenga kuwanufaisha wachache vinginevyo, tatizo hili lingekwisha toweka.

Ni vipi kila mwaka kazi ifanyike hiyo hiyo na kurudiwa mwaka unaofuata na mara nyingine hata mwaka hauishi watengenezaji wanakuja tena kujineemesha.

Ninashauri serikali ikusanye nguvu kwanza ili ikianza kazi, ifanye kazi iliyo bora kuliko kufanya kazi ya danganya toto.

Pia, iwatafute makandarasi wenye uzoefu na moyo wa kufanya kazi bora bila tamaa

Maana jamii inataka kazi bora, na sio bora kazi.

James Mbogo,

Mtoni kwa Aziz Ali,

SLP

DAR-ES-ALAAM.

Magazeti ya dini yasipige vita dini nyingine

Ndugu Mharairi,

Naomba kutoa yangu machache kwenye gazeti hili la KIONGOZI ambalo ni miongoni mwa magazeti yanayomilikiwa na taasisi au madhehebu ya kidini ambalo mpaka sasa bado lina sifa ya kutoingilia uhuru na heshima dhidi ya dini nyingine.

Ingawa kwa kiasi kikubwa kwenye magazeti ya dini jamii hutarajia kupata masuala ya kiroho na hata ya kijamii kwa kiasi fulani kutegemea sera za gazeti au chombo husika cha habari, hatutarajii kupata habari za kashfa, uchochezi na matusi dhidi ya vikundi vingine vya dini.

Ninasema hivyo kwa kuwa moja ya magazeti ya namna niliyoitaja hapo juu, limekuwa na tabia ya kuandika huku likiegemea upande mmoja tu wao wenyewe na ukiona kikundi kingine kimeandikwa, kwenye gazeti hilo, ujue ni tusi au kashfa dhidi ya kikundi hicho.

Sasa, mimi nadhani sio vema wala ustaarabu kuishia kubomoa dini za wenzio tu kwani kwa kufanya hivyo ni kuingilia uhuru wa kuabudu.

Pia kupigana vita watumishi wa Mungu ni unafiki kwa kuwa huwezi kujidai unampenda Mungu wakati unampiga vita mwenzio.

Ninaomba niishie hapo ila watu wa namna hiyo wajifunze kupitia gazeti hili ambalo hata tangu nikiwa kijana, nimelikuta likiandika na bado linaandika mambo kwa misingi ya imani za Kimungu na sio vita baridi dhidi ya wengine.

Kwa hilo napenda kukupa hongera na timu yako nzima kwa kazi mnayoifanya.

Joyce Mathias,

SLP 30005,

Dar-Es-Salaam.