Misaada ya wafadhili itumike kwa malengo sahihi

WATANZANIA tumebahatika kuwa na wafadhili au wahisani wengi hasa kutoka huko ng’ambo- Ulaya na Marekani. Serikali nyingi na watu binafsi wamekuwa wakitoa misaada mbalimbali ya maendeleo katika sekta nyingi hapa nchini.

Ama kwa hakika tuna lazima kabisa ya kutoa shukrani kwa mioyo hiyo ya ukarimu.

Wamekuwa wakitoa misaada ya hali na mali katika sekta ya kilimo, afya, na elimu.

Wako wafadhili wanaotoa misaada kwa ajili ya sekta ya usafiri na uchukuzi, wakitupatia hela kwa ajili ya ujenzi wa barabara nchini.

Hivyo tunaweza kusema kuwa nchi yetu imepata baraka kubwa kupewa misaada toka kwa ndugu zetu, na tunawashukuru sana.

Jambo la kusikitisha ni kwamba, tunapoangalia kwa makini, tunatambua kuwa misaada mingi ambayo imetolewa na wahisani, imeshindwa kukidhi malengo yake na hivyo kutokamilika kwa miradi hiyo.

Kwa mfano tunaona barabara kadhaa ambazo hazijakamilika, na kama zimekamilika basi siyo imara na huharibika mapema sana.

Pengine wahisani wamewahi kutusaidia katika mambo ya afya, yaani kutupatia hela kwa ajili ya majengo ya zahanati au hospitali. Inashangaza kuona hayo majengo hayakamiliki na hivyo kuwa nusu nusu tu. Tunajiuliza ni kwa nini mambo yamekuwa vile.

Jibu tunaloweza kutoa kwa haraka ni kukosekana UADILIFU.

Kuna ukosefu mkubwa sana wa uadilifu katika taifa letu na hakuna uaminifu kwa wale ambao wanakabidhiwa misaada na wafadhili wetu.

Wengi husema kama misaada tupatayo kutoka kwa wafadhili ingetumika ipasavyo mambo yasingekuwa kama yalivyo.

Kwa mfano, mara moja nilisimuliwa na rafiki yangu kulikuwa na jamaa ambaye alikuwa amekabidhiwa misaada na wafadhili wa huko Ulaya. Kumbe wale jamaa waliamua kuja hapa nchini na kumtembelea.

Walishangaa kuona ana nyumba nzuri, na magari manne yameegeshwa nje. Lakini kwa bahati mbaya walipoikagua miradi wakaona haijakamilika kabisa, licha ya yeye kuishi katika ufahari mkubwa.Hivi karibuni nimekuwa nikisikiliza Radio One kipindi kinachohusu kero katika taifa letu.

Moja ya kero zilizozungumzwa ni kuhusu suala la misaada kutokutumika sawasawa.

Walisema bayana kabisa kwamba wakubwa wengi hasa wale wenye kukabidhiwa misaada hiyo huitumia kwanza kwa manufaa yao wenyewe na kiasi kidogo, hutumika kwa malengo yaliyotarajiwa.

Ama kwa hakika hilo ni jambo la kusikitisha na tena ni la aibu sana.

Sote tunatambua kuwa nchi yetu ni maskini na hata viongozi wetu wengi ni maskini na hivyo, wakati wapatapo nafasi ya kusimamia misaada hiyo hujitahidi kujaza kwanza mifuko yao.

Tunasema kuwa huo ni ubinafsi mkubwa na ni tabia inayoturudisha nyuma kimaendeleo licha ya kupata misaada mingi kutoka kwa wafadhili wetu.

Siyo misaada ya pesa tu, bali pia kumekuwa na wafadhili wanaokuwa tayari kutoa misaada ya vitu kama vile nguo, na vifaa mbalimbali kama vile dawa na hata vyombo vya hospitalini.

Wafadhili wametoa nguo, chakula madawa na vitu vingine kwa ajili ya wasiojiweza, wagonjwa na walemavu au watu waliopatwa na maafa fulani, lakini la kushangaza ni kuona vitu hivyo havikuwafikia hao walengwa.

Wengi hutumia ule msemo wa kufa kufaana, yaani kufaidika kutokana na maafa ya watu wengine.

Kwa sababu ya ukosefu wa uadilifu na uaminifu, kuna wafadhili wengine ambao wanaona afadhali wailete misaada yao kwa njia ya Kanisa, kwani hapo wanakuwa na hakika kuwa misaada hiyo itawafikia walengwa kwani bado wanaamini kuwa kuna bado uaminifu kwa upande wa Kanisa.

Ni jambo lililo dhahiri kuwa kuna uadilifu mkubwa kwa upande wa mashirika ya kidini, licha ya mapungufu ya kiasi fulani. Tunapenda kuyapongeza mashirika ya kidini kwa uadilifu na uaminifu katika kuitumia misaada ya wafadhili wetu.

Tunayaomba mashirika yasiyo ya kidini na watu binafsi wanaopewa misaada kutoka wafadhili wetu waige mfano wa mashirika ya kidini katika kuwa waadilifu na waaminifu.

Ni kweli kuwa siyo viongozi wote wanaokosa uaminifu na uadilifu katika kutumia misaada kutoka kwa wafadhili wapo viongozi waadilifu na waminifu. tunawapa hongera sana.

Wanaofanya mambo vibaya tunawashutumu na kuwaagiza wabadilishe tabia hizo mbaya za kuwakosea wananchi haki ya misaada wapewayo na wahisani. Ni jambo la aibu kuona wafadhili kwa sababu ya ukosefu wa uadilifu, wanaamua kufika na kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.

Ni aibu kubwa kuwa na viongozi waliojaa ubinafsi na wasio waaminifu katika utendaji wao. Tunajua kuwa wasomi wetu wengi ni watu wastaarabu. na waandishi Lakini mambo yanapojionesha kinyume, basi tunashangazwa na kusikitika sana.

Wako viongozi wengi ambao dhamiri zao zimekufa kabisa kuhusu mali ya umma na hivyo hawaoni vibaya kutumia mali ya umma kwa manufaa yao binafsi. Huo tunasema siyo uungwana na wala siyo ustaarabu.

Kwa nini Askofu Kilaini aitwe Msaidizi?

Mhariri wa KIONGOZI,

Naomba nitoe kiherehere changu katika gazeti lako angalau niuelimishe umma wa Wakatoliki kuhusu matumizi fasaha ya neno "msaidizi" pale linapotumiwa sambamba na cheo cha Mhashamu Askofu Method Kilaini.

Sisi wote tunajua kwamba Mhashamu Askofu Kilaini ni asilimia mia kwa mia Askofu kamili.

Kwa maana hiyo, haileti mantiki kumwita Askofu Msaidizi (Assistant Bishop) kama ambavyo inasikika makanisani hapa Dar-Es-Salaam.

Upungufu huu nionavyo mimi unatokana na utovu uliokubuhu wa kutozingatia Kiswahili fasaha. Kwa nini tusimwite Mhashamu Askofu Kilaini, Msaidizi wa Kardinali au Vicar General wa jimbo Kuu" badala ya kusema, "Mhashamu Askofu Msaidizi Method Kilaini."

Tulitumie neno "msaidizi" kuelezea na kukuza (qualify) kazi ya Askofu huyo na siyo uaskofu wake.

STEPHEN WAUPONERA

BOX 2444,

DAR-ES-SALAAM.

 

Jibu la hoja hiyo ya ASKOFU MSAIDIZI

Ndugu Stephen

Tunashukuru kwa maoni yako juu ya neno msaidizi kuhusiana na cheo cha Askofu Method Kilaini ambayo tumeyachapisha kama yalivyo bila kubadili neno lolote.

Ni kweli Askofu Kilaini kama askofu yeyote duniani, ni asilimia mia kwa mia, askofu.

Tofauti ni kwamba yeye hana mamlaka ya kutawala jimbo. Pili, hadhi yake ni "Askofu Msaidizi wa Jimbo la Dar-Es-Salaam"(Auxiliary Bishop), na siyo Msaidizi wa Kardinali.

Tuseme Mwadhama Kardinali anaacha uongozi na akawekwa mwingine ambaye si Kardinali, Askofu Method Kilaini bado anakuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo la Dar-Es-Salaam.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Dar-Es-Salaam, ndiye aliyeomba jimbo lipatiwe Askofu Msaidizi(Auxiliary Bishop) na siyo Msaidizi wa Askofu(Assistant Bishop) kama ulivyomuita kwa Kiingereza maana, wasaidizi wa askofu ni wengi. Ni waamini wote wa Jimbo.

Zaidi ya kuwa Askofu wa Dar-Es-Salaam, Mhashamu Kilaini ameteuliwa na Askofu wa Jimbo la Dar-Es-Salaam kuwa Naibu/Makamu wake(Vicar General).

Aidha, Askofu Method Kilaini, ni Msaidizi wa Jimbo la Dar-Es-Salaam na si Msaidizi wa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam.

Jimbo Kuu la Dar-Es-Salaam, ni pamoja na Zanzibar, Morogoro, Tanga, Mahenge na Dodoma.

Yeye (Askofu Kilaini),hahusiki na majimbo hayo. Askofu Mkuu aliyepo (kwa sasa ni Kardinali Pengo), ndiye anayehusika nayo.

Hivyo jina sahihi ni"Askofu Method Kilaini, Askofu Msaidizi wa Jimbo la Dar-Es-Salaam kama hati ya Papa ilivyoagiza.

Hapo awali hapa Tanzania tulikuwa na Askofu Msaidizi, Elias Mchonde aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Askofu Mkuu Edgar Maranta, wa Dar es Salaam (1956 -1964) na baadaye alikuwa Askofu wa Mahenge (1964-1969).

Aidha, Askofu Yakobo Komba aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Askofu Abate Eberhard Spiess wa Peramiho (1962-1969) na baadaye alikuwa Askofu wa Songea 20 Mei 1969 hadi 1987 na halafu Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Songea ( 23 Novemba 1987 -1992). Wengine walikuwa Maaskofu wasaidizi Gervasius Nkalanga na Christopher Mwoleka.

Isitoshe, Maaskofu Wasaidizi ni wengi duniani.

-MHARIRI

BUDEGE! Mbona bado takataka zinarundikana ovyo Keko machungwa?

Ndugu Mhariri,

Naomba walau mistari miwili kwenye ukurasa huu wa gazeti lako ili niwaambie mawili tu kama sio matatu, hawa wazoaji takataka wa Kampuni ya BUDEGE ambayo kwa sasa ndio mkandarasi wa uzoaji taka eneo la Keko-Machungwa katika Manispaa ya Temeke.

Siku za nyuma, mlianza shughuli hiyo kwa kasi ambayo ilitutisha ingawa ilianza kutoa matumaini kuwa huenda hali ya usafi katika eneo hilo itapendeza na kuvutia.

Baada ya muda si mrefu wa huduma yenu, hatujui kilichotokea, kimya kikatawala na sisi wakazi wa eneo hili kila mmoja akajua lake.

Mwenye kuchimbia takataka akachimbia, mwenye kujificha na kutupa barabarani usiku, akafanya hivyo mradi tu, aliondoa hapa takataka na kuzihamishia hapa bila mpango.

Ni majuzi tu, tumefarijika baada ya kuona mmeanza tena kutoa huduma hiyo katika eneo letu tunawakaribisha sana na kuwashukuru kwa kutukumbuka tena.

Hata hivyo, licha ya kuanza vizuri, bado tunashangaa na hatuelewi ratiba yenu ikoje kwa sababu inashangaza tunapolipa pesa kwa ajili ya kuondoa takataka katika maeneo yetu, lakini bado takataka zinakaa katika marundo na madampo ya muda mrefu, mpaka siku tatu, nne.

Hii inatufanya tusione maana ya kulipia na kibaya zaidi, mrundikano kama huo unahatarisha afya na maisha ya wakazi na kingine kibaya zaidi, yanatia kero hata kwa kutazama na harufu mbaya inayojitokeza.

Mimi ninajua utaalamu wa kuzoa takataka mnao na mnajituma sana kwa kuwa mnafanya kazi mpaka hata masaa ya jioni sana.

Lakini, ninadhani mmechukua eneo kubwa au maeneo mengi kuliko uwezo wenu kiasi kwamba mnapofanya mizunguko hadi mrudi mlipoanzia, muda unakuwa umepita sana na dosari hizo zilizotajwa zinakuwa zimekithiri na kuhatarisa afya za wateja wenu.

Mimi ninawashauri kuwa, kwa kuwa mnalipwa kwa ajili ya kazi hiyo, basi ongezeni vitendea kazi hasa magari ya kuzolea takataka na wafanyakazi ili kila wakati, maeneo mnayohudumia, myahudumie kweli kwa wakati muafaka kama inavyotegemewa badala ya ubabaishaji unaoonekana sasa.

Naomba mjue kuwa hayo mamia ya pesa mnayopokea halafu mnabana matumizi, yanatafutwa kwa jasho na msoto wa hali ya juu. Kibaya zaidi mjue kuwa mnapopokea pesa hizo mjue siku hiyo kuna mahitaji muhimu yatakosekana katika familia.

Hivyo mtu akikupa pesa yake, na wewe walau mhudumie aridhike ndiyo maana upo na ndiyo maana unalipwa

Mmoja wa wakazi,

KekoMachungwa,

Dar-Es-salaam.