MKAPA: Kama tunamuenzi Nyerere 'SODA' za nini wodi ya wazazi, polisi?

KWA mara nyingine rasmi, Oktoba 14 mwaka huu, Watanzania waligubikwa na wingu kubwa la majonzi wakati wakiadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kifo cha Muasisi wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Siku hiyo ya Jumamosi iliyopita, kila Mtanzania mwenye mapenzi mema kwa Taifa, alikuwa na mtindo wake wa kuadhimisha kumbukumbu hii.

Wengine wengi waliadhimisha kwa sala na ibada mbalimbali. Wengine waliimba, wengine kusikiliza hotuba zake na wengine kusoma makala zenye wasifu wa kiongozi huyo Mtanzania, aliyewaacha Watanzania wenzake mithili ya mti uliokatwa ghafla huku bado ndege wengi wakiutumainia katika maisha yao baada ya kifo chake tarehe kama hiyo ya mwaka jana huko Uingereza kutokana na ugonjwa wa saratani ya damu.

Wapo Watanzania na hata wananchi wa mataifa mengine walioadhimisha siku hii kwa kukumbuka maneno na matendo yake katika kutetea uhuru, haki na amani kwa wanyonge kote duniani na hata kuimarisha amani na umoja wa kitaifa kwa Watanzania.

Hakuna kiongozi hata mmoja wa Watanzania mwenye akili timamu, au mwananchi asiye mnafiki, ambaye baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere, nafsi yake haikuguswa kwa namna ya pekee.

Hii inatokana na matendo ya Hayati Nyerere yalivyoonesha kuwa yalikuwa ya kishujaa na yaliyojaa upendo kwetu Watanzania wenzake, na bara la Afrika kwa jumla.

Kila mmoja anajua dhahiri kuwa amani tunayojivunia Watanzania hata kuwafanya watu wa mataifa mengine kutuonea gele, imetokana na Mwalimu Nyerere.

Mshikamano na umoja wa kitaifa uliopo miongoni mwetu, ni matunda mema ya juhudi za Mwalimu na hata elimu waliyonayo wasomi wengi wa Tanzania kama sio wote, ni mazao bora ya kazi na busara za Mwalimu.

Sisi tunaamini kuwa kilio cha Watanzania wote kumpoteza kiongozi shupavu, mwenye busara na mpenda haki kwa wote, Mwalimu Nyerere, kilikuwa kilio "cha kutoka tumboni" na kwamba hakuna aliyetoa "kilio cha mdomoni" ambacho ni cha kinafiki.

Tunaamini kuwa hakuna aliyelazimishwa kulia na kutoa ahadi mbalimbali kama ile ya kusema tutamuenzi Baba wa Taifa kwa kufuata nyayo zake, kumbe moyoni anajua dhahiri kuwa ndiye atakayeongoza jahazi linaovuta kamba ya kupinga juhudi za Mwalimu.

Kinachotushangaza na kutusikitisha, ni kushuhudia maneno TUTAMUENZI BABA WA TAIFA, yanakuwa wimbo wa kutafutia umaarufu wakati matendo yanakuwa kinyume.

Inashangaza kuona kuwa hata baadhi ya viongozi wa vyama, mashirika na taasisi mbalimbali za kiserikali na za kibinafsi, nao wako mstari wa mbele kuimba nyimbo hizo huku ndio wa kwanza kuchelewa, kutoroka kazini na kujilimbikizia mali kinyume na kipato chao halali na hata kufanya ubadhirifu.

Inashangaza pia kuwaona wengine ndio wanajipenyeza kuwa chemichemi ya vurugu na uharibifu wa amani iliyodumu nchini mwetu kwa muda mrefu.

Ikumbukwe kuwa unapomuenzi mtu, daima unakuwa unaiga na kuyaendeleza yale yote aliyofanya. Unapinga na kukemea yale yote aliyopinga.

Sasa je, Watanzania, ni kweli tunamuenzi Baba wa Taifa au tunapiga porojo za mdomoni na majukwaani.

Baba wa Taifa alikuwa akikemea tabia ya kutoa na kupokea rushwa, hata katika hotuba zake nyingi, zinaeleza. Alijua dhahiri rushwa ni adui wa haki katika ulimwengu wowote unaopaswa kuwa.

Ni dhahiri alijua kuwa, kwa ugonjwa wa rushwa, wanaokufa na kuibua vilio vya samaki visivyo na machozi, ni wanyonge na wenye vipato duni.

Ni hao watakaokosa huduma za msingi katika jamii kama elimu, haki za kisheria na nyinginezo nyingi.

Zaidi ya yote ni hao hao watakaokufa kwa kukosa huduma za afya.

Sasa kama ndivyo, inakuwaje sehemu nyingi zikiwamo polisi na mahakama wanaotarajiwa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya rushwa, bado wanaendelea navyo? Je, ni kweli kwamba wakubwa wa taasisi hizo na vituo vyake hawajui kuwa wananchi wanaombwa maelfu kadhaa ya pesa kwa kununulia karatasi za mahakama?

Je, serikali kupitia vitengo vyake husika, haijui kuwa hata polisi wanapokwenda kumkamata mharifu, huomba nauli ya mkononi, na kudai chai toka kwa mlalamikiwa? Hiyo ni nauli au chai gani?

Tukiacha hivyo vyombo vya dola, kwa nini serikali kupitia Wizara ya Afya na vitengo vyake kwa kushirikia na Taasisi ya Kuzuia Rushwa(PCB), wasifanye mitego ya mara kwa mara katika mahospitali hasa wodi za wazazi ambako rushwa inanuka na imeanikwa juani kwa sura ya SODA?

Inashangaza, inakera na inasikitisha kuona taasisis inayoapa kumuenzi Mwalimu nyerere ndiyo watumishi wake wanawalazimisha akina mama wajawazito wanaojifungulia kwao wawanunulie "soda" eti kwa kuwa wamewahudumia hadi wakajifungulia pale.

Kama sio rushwa, ni soda gani anayolazimishwa mgonjwa (mjamzito au mama aliyejifungua), kumnunulia nesi badala ya nesi huyo anayelipwa mshahara unaotokana na wavuja jasho kwa ajili ya shughuli hiyo, kumpa pole mgonjwa huyo?

Na kwanza ingawa "soda" hiyo "wanaipaka rangi" ya zawadi, ni zawadi gani anayolazimishwa mtu kuitoa baada au kabla ya kuhudumiwa, tena kwa ukali wa namna hiyo na kupangiwa kiasi maalumu kinachoambatana na lawama dhidi ya kidogo kilichotolewa?

Tunadhani umefika wakati ambao kila mmoja anayesema anamuenzi Baba wa Taifa, amuenzi kweli kwa matendo na sio kwa unafiki.

Maeneo hayo ya rushwa hayana budi kumulikwa ili akinamama wajawazito wajifungue kwa amani bila hofu ya kudaiwa malipo yasiyo rasmi.

Kwa kuwa hivi sasa Baba wa familia ya Watanzania ni Rais Benjamini Mkapa, sisi tunauliza KAMA TUNAMUENZI NYERERE, "SODA" WADI YA WAZAZI NA POLISI, NI ZA NINI?

Barua za Mkufu

Maana:

BARUA ya mkufu ni ile ambayo mtu anaiandika na kumpelekea mwingine akimwagiza naye aandike barua kadhaa awapelekee watu wengine.

Tendo hilo la kuziandika barua hizo linasukumwa au na tamaa ya bahati ya kupata kitu kikubwa au hofu ya kupata janga kubwa barua hizo zisipoandikwa katika muda maalum toka mtu anapoipokea hiyo barua. Mfano mmoja wa aina ya barua ya mkufu ya Mt. Yuda Tadei. Mtakatifu wa yasiyowezekana. barua za namna hiyo zimezusha mashtaka katika dhamiri za watu.

Uchunguzi wa Barua.

Barua ya mkufu inamtumainisha mtu kupata bahati kama atasambaza barua ile, mfano wa barua nilioleta hapo juu unaweza kuelezea vizuri barua za mkufu zilivyo kwa jumla, barua hiyo ina sentensi moja isemayo 'You will receive luck within four days of receiving this letter, provided you in turn send it on' (Utapata bahati katika siku nne baada ya kupokea barua hii kwa sharti kwamba wewe unaipitisha kwa mwingine). Barua hiyo hiyo inayosentensi hii katika herufi kubwa: 'Please Circulate 20 copies of this letter and see what happens in just 4 days' (tafadhali tawanya nakala 20 za barua hii na uone kitakachotokea katika siku 4 tu).

Kwa kweli barua ya mkufu si tu inamtumainisha bali pia inamtisha mtu kwa kuleta mifano ya watu mbalimbali waliopata bahati baada ya kutekeleza masharti na waliopata majaga baada ya kutoijali hiyo barua kwa kuitupa au kutotekeleza madai yake.

Mazuri ya Barua.

Barua ya mkufu ina baadhi ya mambo mazuri kweli ya msingi ya dini ya kikristo. Ni ukweli kwamba kwa mapenzi yake Mt. Yuda Tadei amewasaidia watu wengi waliokuwa katika hali hii ngumu ya kukatisha tamaa (the Saint of the impossible - Mtakatifu asiyewezekana)

Barua ya Mt. Yuda inaanza na sentensi 'With love all things are possible' (kwa upendo vitu vyote vinawezekana). huu ni ukweli tuliofunuliwa. Kama Mungu ni Upendo (1Yoh. 4:16) na ndivyo alivyo, tunahusianisha sentensi hiyo na maneno ya Bwana Yesu; ' Kwa Mungu mambo yote huwezekana' (Mt. 19:26) Tuna imani katika Mungu mwenye nguvu yote.

Kwa kumweleza Mt. Yuda kama 'Mtakatifu wa yasiyowezekana' tunakiri uwezo wa Mungu ndani yake na barua inahimiza imani katika mtakatifu huyu kwa kuleta mifano ya watu waliopata bahati mbalimbali katika maisha yao.

Mapungufu.

Kitu chochote hakitakosa kasoro Barua ya mkufu kama ile ya Mtakatifu Yuda inamjenga mtu dhana kuwa Mtakatifu Yuda ndiye anayeleta bahati. Hilo si kweli, Mungu ndiye asili ya kila kitu chema na zawadi zote (taz. Yak 1:17) anamtumia Mt. Yuda au Mtakatifu mwingine kupitisha fadhili zake kwa binadamu Bila Mungu binadamu hawezi kufanya kitu cho chote chema (taz Yn. 15:5).

Kasoro mojawapo kubwa ya barua za mkufu ni kumfanya Mungu mdeni wetu. Mtu anafikiri kwamba kwa vile ameandika barua zinazotakiwa na kuzipeleka kwa wengine katika muda uliopangwa lazima apate bahati; asipoipata anakata tamaa na anakata uhusiano na Mungu ambaye anaonekana kuwa amevunja 'mkataba'. Hilo si kosa upande wa Mungu ila upande wa Binadamu mwenyewe ambaye hana mawazo sahihi juu ya Mungu. Tukipata fadhili yoyote ni sababu ya wema wa Mungu, si sababu ya hali au matendo yetu mema (taz Lk 17:9 - 10: Rum 3:28;11:35).

Kasoro nyingine ya barua za mkufu ni ile ya kumwingizia mtu woga kiasi kwamba anatekeleza masharti ya barua kutokana na hofu (woga) ya kupata janga. Neno la Mungu linasema 'hamkupokea tena roho ya utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana ambayo kwa hiyo twalia Aba, yaani Baba' (Rum. 8:15;taz. pia 2Tim. 1:7). Hofu huteteresha na hata huharibu uhuru wa mtu ambao huvuta tuzo ikiwa mtu ametenda jema na adhabu ikiwa ametenda mabaya.

Hatima

Pamoja na mazuri yaliyopo katika barua za mkufu, kasoro katika barua hizo ni kubwa sana. kutokana na kasoro hizo barua hizo zisimjengee mtu dhamiri mbaya ni vema kutozishughulikia na kuzitia kapuni

Bruno Ngonyani

Askofu wa Lindi.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi isicheleweshe matokeo

Mhariri,

Napenda kutoa maoni yangu kupitia kona ya safu hii ya barua za Wasomaji.

Toka nchi yetu hii ya amani na utulivu ikubali kuwa katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mnamo mwaka 1992.

kumekuwepo na tatizo moja kubwa lakini linaloonekana dogo hasa pale serikali inapoamua kupuuza ingawa sina hakika kama inalipuuzia kwa kutokulijua au inalilijua lakini inasubiri kuona matokeo yake.

Suala la Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuchelewesha majibu pale unapofanyika uchaguzi katika majimbo, ni suala baya ambalo likiendelea kupuuzwa, ipo siku litatuletea balaa na moto wake hautazimika kiurahisi.

Ningependa kutumia nafasi hii kuiuliza serikali ni kikwazo gani kinachoifanya Tume ishindwe kutoa matokeo kwa muda muafaka kwa vile idadi ya watu waliopiga kura hutolewa kila kituo na kusimamiwa kikamilifu na watendaji wa serikali kila manispaa.

Kitendo cha kuchelewesha matokeo siyo tu kwamba kinaonesha udhaifu mkubwa kwa serikali, bali kinaweza kusababisha kutokea kwa vurugu zitakazoathiri nchi nzima kutokana na mwamko wa hali ya kisiasa nchini.

Kwa vile serikali iliutangazia umma kuwa Tume iliyoundwa ni ya haki na haitapendelea chama chochote, iwajibike kuwatendea haki Watanzania wanaokuwa na kiu ya kutangaziwa matokeo juu ya chama na wagombea walioshinda.

Kukwama kwa chama fulani kusiifanye Tume ishindwe kutoa matokeo kwa muda uliokusudiwa kwa vile hapa ndipo kutakapokuwepo na mvutano na kusababisha vurugu kutokana na Tume kukumbatia upande mmoja.

Mwananchi mpenda haki

Willbord Edwad

Charambe - Dar es Salaam