Tumkumbuke, kumuombea na kumuenzi Baba wa Taifa

JUMAMOSI hii Taifa linafanya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Sasa ni mwaka mmoja tokea Baba yetu na kipenzi chetu ametutoka hapa duniani kwenda kwenye makao ya milele ya Mwenyezi Mungu.

Watanzania bado wanamkumbuka Baba wa Taifa katika akili na mioyo yao.

Kipindi cha "wosia wa Baba" cha Radio Tanzania, kimekuwa kikiwakumbusha Watanzania kazi na jitihada alizozifanya Baba wa Taifa katika uhai wake kupigania haki za wanyonge Tanzania na duniani kote.

Mwalimu Nyerere alitufanyia Watanzania mambo mengi mazuri achia mbali aliyoyafanya nje ya nchi yetu, hasa katika kupigania haki na uhuru katika mataifa mbalimbali ya Kiafrika.

Hakuna binadamu mwenye akili na utu ambaye ataweza kumsahau hayati Baba wa Taifa kirahisi.

Litakuwa jambo la aibu akitokea Mtanzania anayethubutu kumsema vibaya Hayati Nyerere.

Tunavyofahamu, hakuna ruksa kuwasema vibaya waliotutangulia. Lakini, kwa Mwalimu, jambo linalotufanya tusiseme vibaya juu yake ni kazi alizozifanya kwa ajili ya Watanzania.

Ni kweli kuwa duniani hakuna binadamu mkamilifu. Lakini, aliyejitahidi kwa juhudi zake zote kufanya mambo mema kwa kadiri ya uwezo na nia zake njema, hatuna budi kumpongeza na kuzidi kumwombea kwa Baba wa milele.

Ndivyo inavyotupasa Watanzania kumfanyia Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere. Inatupasa kujiuliza pamoja na yule Mtunga Zaburi ya 116, anaposema: "Nimrudishie nini Bwana kwa ukarimu wote alionitendea?"

Nasi Watanzania tungeweza kujiuliza, "Tumrudishie nini Bwana kwa ukarimu wote aliotutendea kwa zawadi tuliyopewa katika mtumishi Nyerere."

Ni ukweli usiofichika kuwa Tanzania isingekuwa na sura iliyo nayo kama siyo kutokana na huyo Baba wa Taifa. Watanzania tusingekuwa na heshima katika ulimwengu kama siyo kwa ujasili wa Nyerere.

Umoja tulio nao katika taifa letu usingekuweko kama siyo kutokana na juhudi zake.

Kuna baadhi ya wananchi wanaodiriki kusema kuwa amani na utulivu tulio nao katika Taifa letu havikutokana na Mwalimu.

Watu wa namna hiyo tunasema wanakosa shukrani na pia upeo wao wa kuona na kuhukumu mambo, ni mdogo mno.

Kwetu Watanzania wengi, tunatambua mchango mkubwa alioutoa marehemu Nyerere katika kulijenga taifa hili.

Anayefuatilia vizuri hotuba mbalimbali zinatolewa na Radio Tanzania, ataona ni jinsi gani Baba wa Taifa alivyokuwa na upendo, huruma na uchugu juu ya Taifa hili na watu wake.

Kutokea kifo chake, viongozi wetu na hata watu binafsi wamekuwa wakitoa ahadi kuhusu kumuenzi na kumkumbuka.

Wengi wameahidi kuyatunza yote aliyoanzisha na kuyaishi Mwalimu yakiwemo maisha yanayolenga kudumisha amani, upendo, udugu na mshikamano wa kitaifa.

Tunaweza kusema kwa jumla kwamba sisi Watanzania tumejitahidi sana kuyaishi maelekezo ya Baba wa taifa.

Lakini tunapojiandaa kwa Uchaguzi wa kwanza bila Mwalimu, kumejitokeza watu wanaotaka kufanya mambo kinyume cha maelekezo ya Hayati Baba wa Taifa.

Tunasema kuwa watu hao ni wenye ubinafsi na uroho na wasiolitakia taifa letu kudumu katika ule urithi aliotuachia Baba yetu mpenzi, Mwalimu Nyerere, urithi wa amani na upendo.

Kati ya mambo mazuri aliyotuachia Mwalimu Nyerere, tabia ya kuheshimiana na kuvumiliana.

Kwa jumla, Watanzania hatuna utamaduni wa kudharauliana wala kukashifiana po pote pale. Daima ni watu wa kushauriana kwa uvumilivu na heshima, na huo umekuwa hasa ni urithi kutoka kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

Kwa sababu hiyo nchi yetu imekuwa katika amani na mshikamano mkubwa hadi leo hii. Lakini tunapoanza kudharauliana, kukashfiana na kuanikana kasoro zetu kwenye majukwaa ya siasa, tunapoteza urithi wetu kutoka kwa Baba wa Taifa.

Leo tunapofanya kumbukumbu ya mwaka mmoja tokea tumempoteza Baba wa Taifa, hatuna budi kujiuliza ni kwa jinsi gani kila mmoja amemuenzi Baba wa taifa katika kuyaishi yale aliyokuwa akifundisha kwa maneno na matendo ya maisha yake mwenyewe.

Je, tumekuwa kweli vyombo vya amani, umoja na mshikamano kama alivyokuwa huyo Baba yetu wa Taifa? Je, tumekuwa kweli wajenzi wa taifa letu tukifanya kazi kwa ushirikiano kama alivyotufundisha huyo Baba wa Taifa ama sivyo?

Kwa kifupi siku ya leo ni siku hasa ya kufanya tathmini kuhusu kumuenzi na kumkumbuka Baba.

Tunapenda kutoa rai kwa Watanzania wote kwamba siku hii ya Oktoba 14, na siku zijazo ziwe ni kwa ajili ya kufanya tafakari kuhusu mambo mema aliyoyafanya Baba wa Taifa katika uhai wake.

Tunapofanya tafakari hiyo, ni wajibu wetu kuahidi kwamba tutayafuata mambo yanayodumisha umoja wetu, mshikamano wetu na hasa Utanzania wetu.

Hayati Mwalimu alitujengea heshima kubwa nje ya nchi yetu hivyo, nasi inatupasa kuendeleza utaifa huo popote tunapokwenda na kujishughulisha. Tunazidi kuomba:

RAHA YA MILELE UMPE EE BWANA, NA APUMZIKE KWA AMANI. AMINA. Serikali itueleze madeni inayolipa ilikopeshwa lini?

Serikali itueleze madeni inayolipa ilikopeshwa lini?

Ndugu Mhariri,

Kupitia gazeti lako hili, napenda nitoe dukuduku langu linalonitatiza kwa muda mrefu kwa faida ya Taifa zima na watu wenye tatizo kama mimi.

Kwa muda mrefu jamii ya Watanzania imekuwa ikishangilia na kupiga makofi kutokana na taarifa zinazotolewa na serikali kwamba Watanzania tumepewa msaada wa kitita cha dola hali inayotufanya tuanze kusahau matatizo tuliyonayo.

Hata hivyo, furaha hiyo huwa inabadilika na kuwa kiini macho pale tunapoambiwa kwamba kila kichwa cha Mtanzania hata kama kazaliwa leo, anadaiwa.

Nina imani kwamba wapo watu wengi kama mimi wasiofahamu kwamba wamehusishwa vipi na madeni hayo. Hivyo, serikali iwajibike kutufahamisha mzigo huo wa madeni unaotukabili tulikopeshwa lini kwa vile haijawahi kutokea tukaelezwa kwamba Tanzania imekopeshwa bali tunasikia nchi imepewa msaada wa mapesa.

Kuna suala lingine linalonitatiza ambalo pia serikali inastahili kulitolea ufumbuzi.

Huu msaada tunaoelezwa tumepewa, huwa unaisaidiaje nchi yetu au labda huwa siyo msaada ndiyo mkopo wenyewe? Kama ni mkopo, iweje ukaitwa msaada au hakuna lugha nyingine ya kutumia zaidi ya kuuita msaada?

Kama suala hili linaeleweka hivi, napenda nitumie nafasi hii kuishauri serikali iache mara moja kuwaadaa wananchi wake juu ya misaada, bali itangaze bayana kwa lugha inayoeleweka kwamba kilichotolewa kwa wananchi siyo msaada ila ni mkopo na kwamba kila Mtanzania atatakiwa kuurejesha tena kwa riba.

Nina imani kwa kutumia nafasi hii, Serikali yetu tukufu itatafuta lugha nzuri ya kutumia badala ya kuuita mkopo kuwa ni msaada na kama ni msaada ni toka lini ukampa mtu msaada kisha ukamdai.

Labda tuelezwe bayana kwamba upo wakati serikali inaomba mkopo lakini hilo huwa halitangazwi kwa wananachi na ndiyo maana wanadai madeni hayo bila kujua kwamba Mtanzania alikopeshwa lini.

Ndugu Mhariri nimeamua kuliweka jambo hili bayana kwa vile hakuna hata siku moja niliyowahi kusikia kuwa Tanzania imekopeshwa, bali inasikika kwamba tumepewa msaada wa mabilioni ila tunashangaa msaada huo unazidi kuwa mzigo kutokana na kuendelea kukamuliwa kodi sisi wakulima kukopwa mazao yetu kana kwamba huo msaada ni hewa maana badala ya kwenda mbele kwa msaada tunarudi nyuma kwa kulipa madeni.

Mpenda haki

Wilbroad Bandihai

Box 413

BABATI

Mwaka wa Jubilei Kuu wa 2000, utukumbushe yaliyopita

Tunaelekea mwisho wa mwaka 2000, Mwaka Mtakatifu wa Jubilei Kuu, tukiendelea kuuadhimisha kadri ya Kalenda ya Kanisa Katoliki inavyoonesha.

Hata hivyo, katika Jimbo letu la Njombe, bado tunayo kumbukumbu kubwa ya Mwaka 1999, uliokuwa mwaka wa mwisho kufanya maandalizi ya kuingia mwaka 2000 na mwaka wa furaha kwa taifa la Mungu sababu ya kuongezeka kwao.

Wakati huo huo, ulikuwa mwaka wa uchungu kwa sababu ya misiba iliyotokea ikigusa jamii kubwa ya watu, ndani na nje ya jimbo letu.

Mwaka 1999 ulianza vizuri na kama ilivyo kawaida yetu, kila mwanzo wa mwaka, tunatakiana "Heri ya Mwaka Mpya." Tulishuhudia mwaka huo ukindelea vema japo maeneo mengine hayakupata mvua ya kutosha na kusababisha njaa.

Hayo si mageni kwetu kwani hata miaka ya nyumba yamewahi kutokea.

Katika mwaka 1999, mwezi wa sita, Jimbo la Njombe ulikuwa na furaha kubwa kupata mapadre wapya watano.

Wakati huo huo, ulikuwa na waseminari wawili katika mwaka wa Kichungaji ambao walipewa Ushemasi mwezi Desemba.

Hayo yalikuwa ni matukio ya furaha kwa wanajimbo na taifa la Mungu kwa jumla.

Katika nyumba ya Imiliwaha, hali kadhalika Mungu alishusha neema zake. Mwezi Oktoba kulikuwa na maadhimisho ya kufunga Nadhiri na pia kwa wengine kutimiza Jubilei za miaka 25 na 50. Hayo yote bado yalikuwa ni matukio ya furaha.

Katika kipindi hicho, Wakristo wengi walirekebisha maisha yao kwa kuondoa vizuizi vya kupokea Sakramenti, vilivyowatenga na huduma ya Kanisa. Wengi walirudi katika Kanisa na kupokea Sakramenti ya Upatanisho na Ndoa nyingi zilifungwa.

Watoto wengi walibatizwa na jitihada ya kila muamini iliongezeka akijitayarisha kuiendea milenia ya tatu kwa kuwa karibu zaidi na Mungu.

Mipango kamambe ya kaadhimisha Jubilei Kuu iliandaliwa. Yote hayo kwa wanajimbo yaliashiria furaha inayowaingiza kitika milenia ya tatu.

Furaha ilianza kupungua baada ya jimbo zima kujulishwa kwamba hali ya afya ya Baba Askofu si nzuri.

Aprili 1999 baada ya Pasaka, Mhashamu Baba Askofu alienda Ulaya kwa ajili ya matibabu. Tukio hili lilitushtua kwa kuwa hatukujua atakuwa huko Ulaya hadi lini? Tutaishije bila Askofu Jimboni?

Muda wote Baba Askofu akiwa katika matibabu, wanajimbo wote tulisali kumwombea afya njema huku tukisubiri kujulishwa maendeleo ya afya yake.

Kwa bahati nzuri taarifa zilitufikia mara kwa mara kueleza maendeleo yake kwamba ni mazuri. Mwezi Julai Askofu alirejea nyumbani. Wanajimbo tunaamini, Mungu mwema alisikiliza sala zetu.

Furaha ya kurejea kwa Askofu ilikuwa imetanguliwa na majonzi mazito.

Tukio lililoleta majonzi hayo ni ajali ya boti iliyotokea tarehe 28.06.1999 katika Ziwa Nyasa.

Mapadre watatu, sista mmoja na watu wengine 18 walipoteza maisha yao. Safari yao ya hapa duniani ikawa imefikia hatima kwa njia hiyo ambayo kila mmoja aliyesikia habari hiyo aliguswa; watu wa dini mbalimbali hali kadhalika viongozi wa Serikali.

Kitulizo kimoja cha mwanadamu ni kumzika mwenzi wake. Kumbe Mungu akazuia jambo hilo kufanyika kwa wengi wa waliopatwa na ajali hiyo. Padre mmoja na sista pamoja na watu kadhaa, kaburi lao lilikuwa ni ziwa lenyewe kwani maiti(miili) yao, hazikuonekana kabisa.

Katika tatizo hili zima, wengi kutoka majimbo jirani kama Mbeya, Songea, Iringa Mbinga walitupatia msaada wa kila hali. Serikali kupitia polisi na wataalamu wa Shirika la Reli, ilitusaidia sana kutafuta maiti na kutufariji. Kwao wote tunasema Asante Sana.

Viongozi mbalimbali: Maaskofu, Mapadre, Watawa, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma na viongozi wengine wa Serikali, walikuwa nasi katika msiba huo; kwao tunasema Asante Sana. Mshikamano kati ya kanisa na Serikali uendelee.

Tarehe 23.11.1999 zikiwa zimebaki siku 38 tu, kuingia mwaka 2000, Padre Sales Mabena akiwa amemaliza kozi ya kichungaji alipoteza maisha yake katika ajali ya gari huko Johanesburg, Afrika ya Kusini.

Alikuwa pamoja na mapadre wawili wamisionari Wakonsolata na mlei mmoja ambao pia walipoteza maisha yao katika ajali hiyo.

Mwili wa marehemu Padre Sales Mabena ulirudishwa Tanzania hadi kuja kuzikwa jimboni kwake. hakika hapo ulionekana upendo mkubwa sana. Shukrani zetu ziwaendee wote waliohusika na kazi hiyo. Shukrani za pekee ziwaendee Wamisionari Wakonsolata, wanajimbo la Iringa na wote walioshiriki kupokea maiti huko Dar Es Salaam yaani wananchi wakazi wa Dar-Es-Salaam wazaliwa wa Jimbo la Njombe na wote wenye mapenzi mema ambao pia walikesha na maiti katika nyumba ya Betania. aidha kufikisha maiti ya padre Sales hadi jimboni kwake Njombe kwa ajili ya mazishi kule Matola. (Tunawashukuru sana).

Tunatambua ujirani mwema ulioneshwa na ukanda wa majimbo Katoliki ya kusini; jimbo Kuu la Songea, jimbo la Mbinga, Mbeya na Iringa. TUNAWASHUKURUNI SANA. Wote walikuwa pamoja nasi katika misiba yote ilipotokea.

Kuwataja mmoja mmoja kwa waliohusika si rahisi, tunawashukuru wote waliotufariji, vikundi mbalimbali vya watu vilijionesha kwa namna ya pekee ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania na vikundi vingine, kwao wote tunasema ushirikiano wenu wa hali na mali kwetu wanajimbo la Njombe vimetufariji kwa vikubwa sana nasi tumejisikia kuwa tunao ndugu wenye moyo wa sadaka moyo wa kusaidiana katika dhiki.

Shukrani kwa wote waliofika Jimboni Njombe wakashiriki pamoja nasi masikitiko yaliyotusibu. Wengi bila kujali nafasi zao kwa moyo wa upendo walifika na kutufariji, wanajimbo tunasema Asante Sana.

 

WAAMINI

JIMBO KATOLIKI LA NJOMBE