Wazanzibar, igeni Wabara tumshukuru Mungu

JUMAPILI iliyopita Watanzania Bara walihitimisha zoezi la upigaji kura kumchagua Rais, Wabunge na Madiwani. Mambo yalivyo, hadi sasa tunasikia namna waangalizi wa kimataifa wanavyosema hasa kwa upanda huu wa Tanzania Bara.

Watanzania wa bara wana kila sababu ya kujivuna kuwa wameiva au kukomaa kidemokrasia kwa kuwa walifanya zoezi la upigaji kura kwa utulivu, haki na amani.

Ripoti mbalimbali kutoka huko mikoani, zinatuambia kwamba uchaguzi pia ulikwenda vizuri, kwa haki na amani.

Lakini, mambo yaliyotokea huko Visiwani, ni ya kutisha, kuabisha na hata kuwakatisha tamaa Watanzania na walimwengu wengine wenye mapenzi mema na taifa hili.

Kwa mtazamo wa kidini na wa kumcha Mungu, tunasema kuwa kumeingiliwa na shetani. Kwa maadili ya kawaida tunasema huko Zanzibar kumekosekana uadilifu na uaminifu. Kwa maneno mengine, tunasema kuwa kuna ukosefu wa ustaarabu. Mtu mstaarabu, hufanya mambo kwa uadilifu bila ubinafsi, upendeleo wala hila za kichinichini.

Tunasema kuwa kutofanikisha upigaji kura kule Visiwani, kidini na hata kimaadili ya jamii, ni ukosefu wa ucha Mungu. Utovu huo wa nidhamu uliowasumbua watnzania waliojiandaa muda wote kisha kuharibiwa dakika za mwisho, ni matunda ya wasio waadilifu ndani ya jamii kutokumuogopa Mungu na badaa yake kufanya mambo kwa kumtii shetani na tamaa zake.

Tunavyojua tamaa za madaraka, tamaa za mali, ugomvi na vita, ubinafsi na fujo na matunda ya jasho la shetani na hivyo, wale waliosababisha kwa namna moja ama nyingine au kushiriki au kuchangia kwa njia kadhaa kuvuruga uchaguzi na kuleta fujo huko Visiwani, ni wale wafuasi na wanaoshirikiana na shetani katika himaya zake na hivyo kuletea aibu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Taifa limeingia katika gharama kubwa kuandaa marudio ya uchaguzi kutokana na fujo hizo za kishetani. Kwa hakika kabisa tunalaani kweli kweli kitendo hicho.

Tunasema serikali husika haina sababu ya kukwepa kuhusika moja kwa moja na lawama hizo kwa kuwa ndiyo iliyowakabidhi majukumu aidha watu inaojua kuwa sio waadilifu wala watendaji bora, au iliwakabidhi watu wa kuokota mitaani bila kujua wanakula na kulala wapi.

Tunasema hivyo kwa sababu mtu mungwana na mstaarabu, aliyeiva kimaadili ndani ya jamii, chama na serikali, kamwe hawezi akasababisha kuvurugika kwa kitu au zoezi la taifa ndiyo maana tunasema baadhi ya watendaji wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, ni wale waliozolewa kusikojulikana.

Sisi tunalaani kabisa vitendo hivyo vinavyoturudisha nyuma kimaendeleo.

Tunatambua dhahiri kuwa wapo ambao hawakutimiza wajibu wao ipasavyo na hao, jamii imekodoa macho ikisubiri kuona kama hawajiwajibishi wenyewe, basi wanawajibishwa na serikali kupitia vyombo vyake kwa uwazi na ukweli bila kufichana, kufumbiana macho wala kulindana huku wanachi wengine wakidanganywa kwa mazingaombwe na viini macho.

Tuna haja hiyo kwa kuwa sasa tumezinduka na kubaini kuwa kumbe tunaishi na watu wasio na uchungu wala huruma kwa Taifa letu.

Hakuna siyejua namna nchi yetu ilivyo maskini. Hivyo, ni dhahiri kuwa, katika kurudia uchaguzi, ni kutaka kukimaliza kile kidogo tulicho nacho na huo ni ukatili mkubwa wa aina yake kwa Watanzania.

Licha ya hayo, wapo viongozi kadhaa wa vyama, waliokwenda kwenye vituo vya uchaguzi na hata katika kampeni zao, wakiwa na matumaini makubwa kupita kiasi kushinda, na kuingia ikulu, nao mchango wao katika kututia hasara na kutuvurugia uchaguzi, ni mkubwa.

Walisahau kuwa waamuzi wakuu ni wapiga kura ambao ndio wana uhuru wa "kufanya vitu vyao" bila kuingiliwa wakati wakipiga kura.

Kwa bahati mbaya viongozi hao nao waliathirika sana na "mob-pschology" sambamba na wafuasi wao. Hao mara kadhaa walipiga ovyo makelele na kuwasha moto wa vurugu katika maeneo kadhaa.

Inaonekana hao walipanga matokeo hata kabla ya uchaguzi na yanapofika matokeo rasmi baada yauchaguzi, wanashangaa na kuhaha wakisema kuwa kumetokea shida na kumbe shida ni wao wenyewe.

Ni jambo la kusitikisha sana na kuonesha kutokomaa kisiasa, kuona mgombea uliyemtaka ameshindwa, ukaanza kudai ucghaguzi haukuenda vizuri.

Kwa mfano wagombea wakitofautiana kwa zaidi ya kura 20,000, kisha mtu aanze kugoma kupokea matokeo hayo, basi hapo kuna kasoro kwa mtu huyu. Tunaambiwa kwamba asiyekubali kushindwa siyo mshindani.

Kuna wagombea wengine ambao hawakufanya utafiti wa kina na hivyo wakadanganyika na kujiaminisha kuwa wataweza kufaulu katika uchaguzi kumbe sivyo.

Ukitaka kujua ukweli juu yako, waulize wapinzani wako, watakuambia wazi wazi lakini marafiki, mara nyingi hawaelezi ukweli kama ukweli ulivyo.

Wapo waliowaonea aibu wagombea wa namna hiyo lakini sasa, kura hazina aibu zimewaambia ukweli. Wagombea hao tunaomba wakubali maamuzi ya kura na hivyo kukubali matokeo; ndiyo maamna ya ushindani na kukomaa kidemokrasia.

Hao hawana budi kujua kuwa sauti ya wengi, ni sauti ya Mungu, na tunapaswa kuitii kwa kuwa ndivyo alivyopanga na kuongoza.

Tunatoa mwito kwa Watanzania wote kukubali matokeo hayo kwa moyo wa kidini, tukimwogopa Mungu ambaye tulimwomba na tunazidi kumwomba.

Tunaamini kuwa ni kwa sababu ya maongozi yake katika nchi hii tumefanikiwa kuwa na uchaguzi wa amani, haki na upendo, hasa katika Tanzania Bara.

Tunamwomba Mwenyezi Mungu azidi kutudumisha katika amani hiyo ili tuweze kuliletea Taifa letu maendeleo ya kweli. Kwa upande wa wale wenzetu wa Visiwani, tunazidi kumwomba pia Mwenyezi Mungu awajalie uchaguzi wa amani na haki hapo kesho.

Afukuze kila pepo mchafu na wafuasi wake wote wenye kumsaidia katika kutuchafulia hewa yetu hapa Tanzania ili Watanzania wa Visiwani na Serikali husika wafike mahala wajitambue kuwa sasa wao si watoto wachanga bali ni watu waliokomaa kisiasa na kimaadili.

Mungu ibariki Tanzania Bara, Ibariki Tanzania Visiwani, Dumisha uhuru, umoja, amani na mshikamano wetu wa kitaifa. Amina.

Mnaokataa matokeo wanatukera

Ndugu Mhariri,

Mimi ni miongoni mwa wananchi ambao wanakerwa sana na baadhi ya wagombea uongozi wanaokataa matokeo baada ya kutangwa kuwa wameshindwa.

Bila aibu mimi ninasema watu hao hawalifai taifa letu kwa kuwa kwa mtindo huo, ninaamini kuna kitu wanachokifukuzia ndani ya ngazi za uongozi walizogombea.

Pia ninashawishika kusema kuwa hao ndio wale wagombea ambao walikuwa wakiwalaghai wananchi kwa zawadi za pilau, kipande cha sabuni, kanga na kiberiti.

Ninadhani baada ya matokeo kuonesha kuwa wameshindwa, sasa wanahaha kwa kuwa hawajui namna watakavyofidia gharama walizotumia wakati wakiwadanganya wananchi ili wawaone kuwa ni wakarimu kumbe wanajitengenea mapito ili baadaye wawanyonye kama kupe anavyong’ang’ania ngozi ya ngombe hata kama ng’ombe amekufa na hata ngozi imekwisha chunwa.

Ninapenda kuwaambia wazi kuwa inabidi wajijue kuwa kama kura zimesema wameshindwa, basi ni kweli wananchi hatuwataki hao. Hivi kwanini watung’ng’nize kuwa viongozi wetu na sisi hatupendi tuongozwe nao?

Kama wanataka kufidia kanga, na vibriti vyao, wajue walitoa kafara isiyo na jibu kwa sababu hakuna aliye waomba.

Pia, kama kweli ni wanasiasa safi, wajue kuwa wanapong’ang’ania wanataka kutuletea yaliyokuwa kwenye uchaguzi Mkuu uliopita ambapo kila mgombea aliyeshinda, alifungua kesi ya kupinga na kutaka kutengua matokeo.

Hao wa nmna hiyo ni wanafiki wakubwa kwanini wasubiri baada ya matokeo ndipo waanze kulalama, kama ni njama hawakuwa wakiziona mwanzoni.

Imefikia hatua wagombea wasitake kumalizia njaa njaa zao kwa kutusumbua wananchi badala ya kufanya kazi nyingine, tunakalia kazi moja ya kuchagua na kushiriki mikutano ya kampeni kila wiki.

Tunasema tumechoka kwa kuwa wanatusumbua na kutukera na pia wanalifanya taifa lipoteza pesa nyingi ambazo zingesaidia kuboresha huduma za jamii na kuletea maendeleo.

Dismas Mwita,

Mtoni Kijichi

SLP 4586

Dar-Es-Salaam.

 

Polisi wawaangalie wasio na kosa

Ndugu Mhariri,

Kufuatana na namna ambavyo nimekuwa nikiona kwenye televisheni juu ya matumizi ya askari wa jeshi la Polisi katika kutuliza vurugu wakati wa uchaguzi,nina wasiwasi na ninasikitika kusema kuwa wengine wanafanya kwa kujifaurahisha, kwa jazba au wanafanya bila kuzingatia mafunzo na maagizo waliyo pewa.

Hivi hawa Askari hawajui kumuona na kumfahamu mtu asiye katika vurugu kiasi kwamba wakianza kupiga, wanawapiga hata vikongwe wa kike wasio jua hili wala lile ili mradi wamepita jirani nao?

Inabidi ploisi wajenge utamaduni wa kutotaka kuogopwa bali wawe karibu na wananchi ili hata yule mwenye fununu juu ya uhalifu fulani unaotaka kutendeka, basi awe jasiri na anayejiamini kufanya hivyo.

Ninasema hivyo kwa kuwa ninajua kwa hakli ya sasa, upo uwezekano mkubwa mtu akawa na suala fulani, wakati anamulekea polisi ili amdokezee,akaambulia kupigwa virungu.

Tunaamini enzi za polisi kupenda kuogopwa na wananchi zilikwisha enzi za ukoloni na hivyo, ili kudumisha usalama wa raia na mali zao, ndani na nje ya mipaka ya nchi, ushirikiano baina ya wananchi na majeshi ni muhimu kuimarishwa katika misingi ya kupendana na sio kartoka misingi ya kuogopana na kuumizana.

Hata hivyo, katika kutuliza fujo mbalimbali, ni vema majeshi yakawa yako stendibai yakisubiri dakika rasmi ya machafuko badala ya kuanza kurandaranda mitaani na silaha za kutisha kwani hali hiyo inaupokonya uhuru wa wananchi kufanya shughuli zao za kujitafutia riziki na kulijenga taifa.

Ninashauri askari kanzu watumike zaidi kuwasaka wahalifu na kuwaficha kistaarabu badala ya hali inayoonekana sasa.

Hivi jeshi la Polisi mnataka vizazi vyetu vilitambue vipi jeshi letu, kama marafiki au maadui?

MWANANCHI MPENDA HAKI NA AMANI

DAR-ES-SALAAM