Busara za Watanzania zionekane sasa

MARA baada ya Uchaguzi Mkuu wa Kwanza kuvishirikisha vyama vingi vya siasa katika mfumo wa kidemokrasia mwaka 1995, jamii ya Watanzania ilianza mikakati kwa ajili ya Uchaguzi mwingine unaoufuatia. Ndio huu unaofanyika Jumapili hii ya Oktoba 29.

Watanzania tunalo jukumu kubwa kuuthibitishia ulimwengu kuwa busara, amani, upendo na mshikamano tulivyo navyo, hatukuvipata kwa bahati mbaya; bali ulikuwa ni mpango sahihi wa Mungu kutufanikishia kuwa nayo.

Watanzania wote Bara na Visiwani kama ndugu moja, wote wanasongwa na jukumu hilo kubwa la kutumia busara na hekima kuwapata viongozi safi na waadilifu; watakaoliongoza Taifa la Tanzania kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Kwa kujua umuhimu wa zoezi hili, Watanzania wa Bara wanajitokeza kwa wingi Jumapili hii kuwachagua madiwani, wabunge na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nao Watanzania wa Visiwani, wanakabiliwa na jukumu la kuwachagua viongozi hao waliotajwa, na nyongeza ya Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, pamoja na Wawakilishi wa Baraza la Wawakilishi.

Siku hii ni muhimu katika historia ya Watanzania kwa kuwa kwanza, ni siku ya Uchaguzi katika mfumo wa vyama vingi ambao ni wa kwanza nchini kwa uzoefu kwa kuwa wa kwanza ambao labda tuuite wa majaribio, ulikuwa ule wa mwaka 1995.

Tunasema hivi tukiamini kabisa kuwa makosa kadhaa hata ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi imekiri kuwa yalijitokeza, kwa kiasi kikubwa yalitokana na jamii nzima wakiwamo wagombea, vyama na wafuasi wao pamoja na Tume yenyewe, kutokuwa na uzoefu katika Uchaguzi wa katika mfumo wa kidemokrasia wa vyama vingi kwa kuwa ulikuwa mtindo mgeni.

Tunajua dhahiri kuwa yapo baadhi ya mataifa machache yaliyokodoa macho ya uchu yakisubiri kushangilia na kupenyeza mizizi ya ukoloni ndani ya nchi yetu yatakapoona eti Watanzania tumekumbwa na pepo wabaya wa machafuko.

Mataifa hayo yanasubiri kwa hamu kushangilia watakapoona Watanzania tunamwaga damu kwa makusudi kutokana na tofauti za kisisasa na zoezi zima la uchaguzi na uroho wa madaraka.

Kubwa zaidi, mataifa hayo yasiyoitakia mema Tanzania, yanasubiri yaitumie nchi kama mfano wa mtu mpumbavu anayejua kuwa yeye ni mshindani, lakini hataki kushindwa.

Katika siku hii ya Uchaguzi Mkuu wa Pili (Jumapili Oktoba 29, 2000), Busara za kila Mtanzania zitaonekana bayana pale kila aliyejiandikisha kupiga kura, atakapoamka na kwenda mapema kwenye kituo chake cha kura na kumchagua kiongozi anayemtaka kwa kuwa ni haki na siri yake.

Busara za Watanzania zitadhihirika endapo kila aliyeanzia kanisani, atauombea uchaguzi huu uanze kwa amani na kumalizika kwa amani na utulivu kisha yeye mwenye akaenda kupiga kura yake halali.

Busara za kila Mtanzania zitaonekana endapo hakuna atakayefanya kosa la kutaka kupiga kura zaidi ya mara moja kwa kuwa ni kinyume kabisa cha sheria na taratibu za uchaguzi.

Busara za kila Mtanzania zitabainika endapo hakuna mpiga kura atakayempigia kura mgombea yeyote aliyetumia lugha za vitisho, ulaghai na kumshawishi kwa rushwa ili amchague kwa kuwa huyo si kiongozi bora.

Busara za kila Mtanzania zitaonekana kama kila Mtanzania atalikana kabisa jaribio lolote la kumtaka kuuza au kununua shahada ya kupigia kura.

Kwa kuwa Watanzania tangu zamani tumerithi hekima za amani, utulivu, udugu, mshikamano na umoja wa kitaifa ambao unayafanya hata mataifa mengine makubwa yatuonee gele na kutuita KISIWA CHA AMANI,busara za Watanzania zionekanae pale tu, kila mmoja atakatumia uwezo wake wote kukana na kukemea kila hoja na jaribio la kuvuruga uchaguzi au kuanzisha vurugu zinazoweza kuhatarisha amani na usalama.

Hatuna shaka kuwa kila Mtanzania anajua kuwa Tanzania ni Tanzania kama ilivyobatizwa kwa jina la KISIWA CHA AMANI na hivyo, hatungependa Tanzania ibatizwe kwa mara mnyingine na kuitwa BURUNDI, KONGO, KOSOVO na kwingineko kwenye utovu wa nidhamu na amani kwa kuwa hata kwenye Maandiko Matakatifu, hakuna yanapomtaka mtu abatizwe mara mbili. Jina la KISIWA CHA AMANI LINATOSHA.

Tunachosema sisi ni kwamba, kila mtu kwa nafasi yake awajibike kulinda amani na utulivu, awajibike kufuata taratibu na kumchagua kiongozi anayefaa.

Kila mgombea azingatie ukweli kwamba asiye kubali kushindwa, si mshindani. Hivyo akubali matokeo halali.

Suala la kung’ng’ania madaraka ni la kishamba na limekuwa chanzo cha matatizo katika nchi nyingi na hata kusababisha mauaji kwa kiasi cha kutisha mno.

Suala hilo ni la kizamani na limepitwa na wakati. Na kibaya zaidi mtu anayeng’ang’ania madaraka, ajue dhahiri kuwa kwamba hawapendi Watanzania na kadhalika Watanzania nao hawampendi na hivyo, hatufai.

Tungependa kutoa wito kwa vyombo husika vya usalama kuona kuwa hakuna anayepewa mwanya wa kuchezea amani na roho za Watanzania kutokana na ushabiki wa kishamba na uchu wa madaraka.

Ushabiki au namna ya kampeni aidha kwa mavazi, mabango nyimbo na mikutano, siku ya kampeni vidhibitiwe kwa maana halisi ya udhibiti.

Endapo tutaichezea tunu hii ya amani aliyopewa Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere atuletee toka kwa Mungu, tukiipoteza tutamlipa nini Mwalimu Nyerere ili aikabidhi kwa Mungu ambaye alituandalia?

Shime Watanzania tutumie busara kuwachagua viongozi wetu, tutumie busara, tukubali matokeo kwa njia ya amani, tutumie busara tuilinde amani ya nchi.

Tusipozingatia hayo yale tunayoyaona kwenye televisheni, katika nchi nyingine tutayashudia kwetu wenyewe.

Hivi ikiwa hivyo, watoto wetu tutawaacha wapi, tutawarithisha nini na tutajibu nini kwa Mungu endapo Watanzania wenyewe tutakuwa vyanzo vya machafuko na mauaji ya Watanzania wenyewe?

MUNGU UBARIKI UCHAGUZI MKUU, MUNGU IBARIKI TANZANIA.

Hongera Kanisa kwa kuanzisha Radio Ukweli

Ndugu Mhariri,

Kwanza kabisa ningependa kutoa shukrani zangu za dhati kwa uongozi mzima wa Jimbo Katoliki la Morogoro kwa kuweza kufanikisha kutoa hudua za Radio Ukweli.

Hiini faraja kubwa kwa wakazi wa Mkoa wa Morogoro na maeneo jirani ambao kwa pamoja wanafaidika na matangazo ambayo yanarushwa na kituo hicho cha Radio.

Ni matumaini yangu kuwa, kuanzishwa kwa kituo hicho cha radio kutaleta changamoto kubwa kwa wakazi wa Mkoa huo ambao kwa muda mrefu hawakuweza kupata huduma za matangazo moja kwa moja na badala yake kupata huduma hizo za matangazo ya radio kupitia mikoa mingine.

Vile vile napenda kutoa pongezi kwa viongozi na watangazaji wote wa Radio Ukweli kwa juhudi zao wanazozifanya ili kuweza kufanikisha zoezi zima la kuwapatia wakazi wa Mkoa wa Morogoro burudani maridadi.

Mwisho ningependa kuwaomba wakazi wa Mkoa wa Morogoro washirikiane bega kwa bega na Uongozi na watangazaji wa radio hii ili kuweza kuboresha kituo hicho badala ya kukaa na kufanya majungu yasiyo faa!

Magabe Changwe,

C/O Box 640

KIGURUNYEMBE

MOROGORO.

Mbona hatupati taarifa za waliotelekeza maiti ya mjamzito Tarime?

 

Ndugu Mhariri,

Kupitia safu hii, ninapenda kuuliza kuwa, mbona gazeti lako la KIONGOZI sasa halijaandika lolote tena kuhusu suala la Hospitali yetu hii ya serikali hapa Tarime.

Ninakumbuka mwaka jana Mwezi wa Nane, kuna mwanamke alifia hapa hospitalini, alikuwa amekwenda kujifungua.

Lakini, hakuna aliyemhudumia hapo hospitali eti kwa kuwa hakuwa na hela mpaka hata manesi wakawa wanamuomba hela hata akaweka vitu rehani ikiwamo redio yake.

Tena cha ajabu, alipofariki tu, usiku huo huo kama saa tano, maiti yake ikaondolewa hospitali na kurudishwa nyumbani halafu baada ya ndugu zake kufuatilia mpaka polisi, ndipo mganga mmoja kutoka hapo hospitali akatumwa kwenda kumpasualia maiti nyumbani ili kutoa mtoto kwenye mimba ya huyo marehemu.

ugomvi wangu ni kwamba, mbona hospitali hiyo haijatoa ufafanuzi kuhusu waliosababisha maskini mjamzito wa watu akafa kama sio mtu namna hiyo?

Au mbona hata serikali haijazungumzia lolote si wilaya wala mkoa?

Tunaomba gazeti hili kwa kuwa ndilo lililoandika habari hizo kwa kina na kutoa hata picha za ushahidi, wafuatilie kwa karibu na kutupa habari hizi.

Hivi sasa gazeti hili kwa kweli limetokea kuwa maarufu hapa tarime na tunaomba mjitahidi kuandika habari za huku pia na kuleta magazeti

Sisi wakazi wa tarime bado tuna kumbuka na tunahamu ya kujua serikali imechukua hatua gani kuhusu marehemu.

Tunaomba kukujulisha wewe na serikali kwa jumla kuwa endapo hamtafuatilia,hawa watu wa huku hawawezi kutoa taarifa hata siku moja maana wanalindana.

Kinachotushangaza mimi na wengine ambao tumeandika barua hii ni kwamba, najua watasingizia mambo ya uchunguzi lakini mbona huko dar-Es-Salaam tuli si kitu kama hicho lakini baada ya siku mbili, tatu tu tayari Mkuu wa Mkoa akaumda tume aikachunguza na kutoa majibu?

NI WAKAZI WAPENDA HAKI

KIJIJI CHA BUHEMBA

TARIME MJINI

Tabata tutakufa kwa kukosa maji

Ndugu Mhariri

Naomba uniweke kwenye kona japo ndogo tu, ya gazeti lako ili nipate wasaa wa kutoa maoni yangu machache kuhusu sisi wakazi wa Tabata.

Kwa kweli sisi wananchi wa eneo hili kwa muda mrefu sana tumekuwa tukisumbuliwa na tatizo la maji.

Cha ajabu ni kwamba, kila kiongozi anayefika maeneo ya Tabata kutaka kura kitu cha kwanza kukitamka, ni kuhusu tatizo la maji.

Wanasema kwamba endapo atachaguliwa, watahakikisha kuwa tatizo hilo linaondoshwa lakini cha ajabu, tatizo hilo linaendelea kuwapo tu.

Sasa, kwa kipindi hiki, sisi wakazi wa Tabata inatulazimu hata kulala kisimani tukisubiri maji .

Tunaomba serikali ijue kuwa, hali ambayo inaashiria hatari kwa kuwa ni majuzi tu, akina mama walidamka saa 6:00 usiku ambapo walifukuzwa na watu wanaosadikiwa kuwa ni wanga.

Mimi ninaomba serikali yetu isikie kilio chetu na hivyo, kujitoa kutusaidia kwa kuwa maji ni muhimu mno katika maisha ya binadamu.

Ingawa ninatoa hili kama ombi lakini ninauliza inakuwaje hata serikali itusahau namna hii katika suala la maji ambalo ni kitu muhimu katika uhai wa viumbe.

Hata hivyo, naomba kupongeza kwa kuwa mwanzoni, tatizo pia lilikuwa barabara lakini, hivi sasa tatizo hilo linaelekea kuisha.

Kwa hilo natoa pongezi na kuomba juhudi hizo ziongezwe.

MAGRETI JOACHIM,

TABATA

DAR-ES-SALAAM