Ipi ni mipaka kati ya Dini na Siasa

HIVI sasa tunapojiandaa kwa Uchaguzi Mkuu katika Taifa letu kuna mambo ambayo yanapaswa kuwekwa sawa ili yaweze kueleweka vizuri kwa wananchi wote. Suala mojawapo ambalo lina utata kwa kiasi fulani ni lile la kufahamu mipaka iliyopo kati ya wale wanaoshughulika na kuhubiri dini kwenye mimbari na wale ambao wanahu siasa kwenye majukwaa ya siasa.Mara kwa mara tunasikia kuwa haifai kuchanganya dini na siasa au siasa na dini. Maneno hayo yana ukweli ndani yake na inatupasa tuyazingatie lakini pia kuna mambo ambayo ni lazima yawekwe wazi zaidi.

Kwa upande wa dini kuna malalamiko ambayo wanasiasa wanayatoa kuwa watu wa dini wanahubiri siasa ndani ya makanisa yao badala ya kuhubiri dini. Lakini hapo tunapaswa kujiuliza, je, dini kama dini inashughulika na nani juu ya nini? Serikali na wanasiasa wanawahimiza viongozi wa dini kwamba inawapasa kukemea maovu yanayozagaa katika taifa letu. Kwa mfano viongozi hao wanaagiza kuwa viongozi wa dini yawapasa kukemea mambo ya rushwa, wizi ubadhirifu wa mali ya umma, uganganyifu, uzembe, wongo, nk.

Pia serikali inawaangiza wahubiri wa dini wahubiri na kukemea kuhusu maadili yanayoporomika katika taifa letu hapa na pale. Licha ya kuagiza kuhusu mahubiri, pia serikali inawaomba viongozi wa kanisa pamoja na waumini wote kwa ujumla kwamba wasaidie katika kujenga mashule, mahospitali, na shughuli nyingine za maendeleo. Hivyo kuna mambo mengi sana ambayo serikali inataka ushirikiano katika utendaji na uongozi wa kidini kwa kuwa una uwezo na pia nia ya kuliokoa na kuliletea maendeleo taifa letu.

Tatizo linalopo kwa sasa hivi ni kule kalauminiwa kwa watu wa dini kwamba wanangilia mambo ya siasa. Manung’uniko hutokea hasa pale ambapo viongozi wa dini wanapowakosoa viongozi wa siasa na hata wa serikali. Kwa kuwa jukumu la dini ni kusema ukweli na hivyo kuwa tayari kukosoa pale ambapo pana uharibifu, basi mara nyingi ni rahisi kabisa kueleweka vibaya. Kwa mfano kwa hivi sasa taifa letu linapojiandaa kwa uchaguzi, viongozi wa dini wanatoa miongozo kuhusu uchaguzi. Wanajaribu kutoa sifa zitakiwazo kwa mtu kuwa kiongozi sawasawa. Viongozi wa dini hawasemi nani awe kiongozi, bali hutoa sifa zifaazo kwa mtu kuwa kiongozi anayefaa. Papo hapo hutamka wazi kwamba wale watu wasio na sifa hizo wasichaguliwe maana hawataweza kuwa watumishi na viongozi bora kwa taifa. Katika kufanya hivyo siyo maana yake dini inaingilia mambo ya siasa.

Ukweli ni kwamba dini inasaidia sana ili mambo ya siasa yaende vizuri bila kudanganyana. Sote tunafahamu ni kwa jinsi gani wanasiasa wengi wanavyodanganya wananchi hasa nyakati za uchaguzi.

Kwa kuwa dini inawahudumia binadamu kiroho na kimwili, siyo rahisi kabisa kusema kwamba ishughulike tu na mambo ya kiroho, bila kushughulikia yale ya kimwili kwani binadamu ni mtu mzima mwenye roho na mwili. Roho ya binadamu hukaa ndani ya mwili wa binadamu na kumfanya awe ni mtu mzima.

Yale mambo mabya anayotendewa binadamu kimwili au kisiasa humletea faraja na athari kiroho pia. Kwa hiyo hayo yote huenda pamoja, yaani ni lazima binadamu ashughulikiwe kikamilifu kiroho na kimwili.

Mara nyingi sana hutokea kwamba kwa sababu ya kutofahamu mambo sawasawa, wanasiasa wetu wanapokosolewa hujitetea kwamba viongozi wa dini wanchanganya dini na siasa kumbe jambo linaloumiza kwa wanasiasa wengi ni kukosolewa na viongozi wa dini.

Viongozi wa dini hawafanyi hivyo kwa sababu ya kuwakomoa viongozi wa serikali au wanasiasa, bali ni kutoa mwelekeo unaofaa kulingana na maadili yanayotakiwa. Tunafahamu kuwa ukweli unauma na hivyo wengi wanapoambiwa ukweli huwa wanapenda kujitetea kwa kuwatupia lawama viongozi wa dini.

Tumeambiwa tukemee maovu katika jamii, na siyo tu maovu ya wananchi wa kawaida tu, bali hata ya viongozi ikiwa wanayo. Tumeambiwa tukemee hali mbaya ya kimaadili katika jamii, hapo hakuna kujali ni nani anayeharibu maadili hayo. Yeyote anayefanya hivyo sharti akimewe bila kujali ni nani kafanya hivyo, mradi shughuli hiyo inafanyika katika njia zinazofaa. Katika Maandiko Matakatifu tunasoma jinsi Yohane Mbatizaji alivyoweza hata kumkemea Herode kwa kuwa alifanya mambo kinyume cha maadili.

Na hivyo na viongozi wa dini siku hizi wanakuwa tayari kukemea matendo maovu ya viongozi wetu wa serikali na siasa ili kuleta maadili sawasawa katika jamii yetu. Hapo siyo maana yake kwamba viongozi wa dini wako katika kutafuta kasoro za viongozi wa serikali au siasa, bali pale wanapoona kuwa kuna kasoro hataaacha mambo yaharibike.

Huo ni wajibu wao ambao wamepewa toka kwa Mwenyezi Mungu na pia kutoka kwenye uongozi halali wa taifa.

Tunapenda kutoa shukrani kwa serikali yetu ambayo inathamini sana mchango wa dini kimaendeleo na hasa katika kudumisha maadili mema pamoja na amani na mshikamano wa kweli. Tunapenda kuona uchaguzi ujao unakuwa katika hali ya amani, utulivu na uelewano ili tuweze kupata viongozi wenye hali nzuri na hasa walio tayari kulitumikia taifa letu. Mungu abariki taifa letu, Mungu abariki uchaguzi wetu wa mwaka huu 2000!!