Watanzania tutastaarabika lini?

KUNA mambo mengi sana yanayotakiwa kuzingatia ili binadamu aweze kupata maendeleo ya kweli. Moja kati ya mambo ya kuzingatiwa sana nalo ni lile la kutunza vifaa mbalimbali vinavyotumika na kuhitajika katika miradi tofauti tofauti.Lakini jinsi mambo yanavyokuwa ni vigumu sana kuelewa kama kweli sisi Watanzania tutafanikiwa katika kuiletea nchi yetu maendeleo. Jambo linalosikitisha sana ni lile la uharibifu wa mali za umma.

Hivi karibuni kumesikika kuwa wananchi wamekuwa wakiiba au kukata nyaya za umeme kule Mkoani Tanga. Pia tumepata habari kutoka kule Wilayani Kisarawe kuwa kuna watu walifukua mambo ya maji na kwenda kuyauza Jijini na hivyo wananchi kukosa huduma ya maji.

Hiyo ni mifano michache kati ya mingi inayotokea katika nchi yetu. Tunao watu waharibifu sana na wenye ubinafsi katika taifa letu. Kutokana na ubinafsi huo watu wako tayari kutumia mali ya umma kwa manufaa yao binafsi bila kujali kabisa madhara yake kwa watu wengine.

Kuna wananchi wengi ambao wako tayari kubomoa vibanda vya kuwahifadhi wasafiri na jua kali au mvua. Kutokana na ubinafsi wao huo, huondoa mabati ya vibanda hivyo na kuyatumia kwa shughuli zao binafsi. Wako wananchi wengine ambao huondoa mabomba ambayo ni kinga katika madaraja yetu na hivyo kuhatarisha wale waendeshao magari.

Kumekuwa na uharibifu hasa katika sehemu za burudani, kwani kuna wananchi ambao wana tabia ya kufanya vitendo hivyo vya uharibifu bila hata aibu.

Tabia ya uharibifu na ubinafsi imezagaa mno katika nchi yetu. Inashangaza sana kuona vitu na mahali huharibiwa bila aibu. Pamoja na tabia ya uharibifu ambayo Watanzania wengi wanayo, pia kuna ile tabia ya kutofanya matengenezo pale ambao pameharibika. Inasikitisha sana kuona mahali pameharibika lakini wahusika hawafanyi lo lote.

Hutokea kwamba taa za barabarani hazifanyi kazi, lakini wale wahusika hawafanyi lo lote. Ni jambo la aibu sana kuona sehemu zina kasoro na uharibifu lakini wahusika hawastuki kabisa na kuwa na kuendelea kuwa na raha.

Na hivyo sisi tunatoa mwito kwa wananchi wote kwamba tuzingatie mambo mawili hayo makubwa . Jambo la kwanza ni kuangalia na kutunza mali ya umma. Uharibifu wa mali ya umma ni tabia mbaya sana na siyo ustaarabu. Mtu mstaarabu ni yule ambaye anatunza mali yake na ya umma vizuri. Lakini tabia ya kuwa waharibifu kwa mali zetu binafsi na hasa zile za umma ni ukosefu wa ustaarabu.

Na hivyo tunalaani vile vitendo vya uharibifu vilivyofanyika kule Chuo Kikuu Mlimani, kule Sekondari ya Mdabulo Mkoani Iringa na penginepo.

Tunalaani kabisa vitendo vya uharibu katika maofisi, katika sehemu za burudani na katika sehemu mbalimbali za huduma.

Na jambo la pili tunapaswa kujenga ile tabia ya kufanya matengenezo ya daima pale ambapo pameharibika. Tuone aibu kabisa kuona mahali na vitu vimeharibika na hatuvifanyii matengenezo. Ule msemo usemao kitunze kitudmu unapaswa kuwa katika mioyo yetu sisi wananchi wote.

Tunapozunguzia jambo la matengenezo hapo tunaangalia mambo mengi sana kwa upana kwani kila kitu ambacho ni kipya baada ya muda huharibika na hivyo huhitaji matengenezo na marekebisho. Mtu yule ambaye hafanyi matengenezo kwa vitu vile ambavyo vimeharibika mwishowe huingia katika gharama kubwa sana.

Tukivifanyia matengenezo vyombo na vitu vyetu mbalimbali kila vinapoharibika tutaweza kusalimisha kiasi kikubwa sana cha pesa. Waswahili wanatuambia kwamba tusipoziba ufa tutakuja kujenga ukuta wote. Hivyo tabia ya utunzaji wa mali za umma na hata mali za mtu binafsi huwafanya wananchi waweze kufanya mambo mengi mazuri bila kutumia pesa nyingi.

Barua ya wazi kwa Mhe. John Malecela

Tafadhali niweke popote katika gazeti lako hili niseme linalotukera sisi wakazi wa jimbo la Kibakwe.

Ndugu Malecela umeanza tena kutusaliti bila haya wakazi wa Jimbo letu? wakati ukifungua ukumbi wa Vijana wa CCM hapa Kibakwe tarehe 8 Aprili, 2000, ulishauri vijana wakirudi makwao wapige debe kuhakikisha MBUNGE na DIWANI wa sasa wanapita tena katika uchaguzi huu wa 2000.

Nakuonea huruma na napenda kukuambia wazi kuwa vijana wa CCM uliowafundisha hivyo hawakubaliani na wewe. Matokeo yake wametoa siri ya kambi, tena wametoa kwa kambi ya upinzani wakidai kuwa kuburuzwa hawataki tena! Huyo Diwani hata kijijini kwake hawamtaki ndiyo maana wamemng'atua katika uenyekiti. Na huyo Mbunge hatufai kwani hajawahi kusema wala kufanya chochote cha manufaa kwa jimbo lake, zaidi ya kuhimiza wastaafu waelimishwe jinsi ya kutumia mafao yao.

Kwa hiyo ndugu Malecela, suala la kuchagua viongozi tuachie sisi waongozwa na si wewe kutuchagulia. ' Tunakuasa , jimbo hili uliache usije ukabeba lawama hata mbele ya Mungu".

Hizi ni zama za ukweli na uwazi, tumechoshwa na tabia yako hiyo ya kutuombea mabaya; Ukitaka kupiga debe pigia CCM na wala si viongozi.

Hotuba yako jukwaani haikuwa na lolote la maana zaidi ya kumsema Mrema na kumsema Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mjini kupitia tiketi ya NNCR -Mageuzi ndugu Felix Kayaula. Napenda kukukumbusha tu kuwa waliomchagua Felix ni wana CCM walio wengi wanaotaka mabadiliko ya Uongozi, NCCR wapo 22 tu kwa mtaa wote. Jiulize kwa nini alichaguliwa?.

Haturudi kula matapishi asilani. Mwaka 1995 ulituomba turuke majivu, tukakubali bila kufikiri kuwa ukiruka majivu unayakanyaga moto! Sasa cha moto tumekiona Kumbuka ndugu 'CHIGWIYEMISI' usia wa Marehemu Mwalimu Nyerere aliosema kwamba "kuwa kiongozi ni kuwa mtumishi wa wananchi na si kuwa mtumikiwa na wananchi" Kiongozi ni yule anayetujali, na hilo unalifahamu.

Damasus G. Mtalaze,

c/o S.L.P 114 Kibakwe

MPWAPWA

CPT Isije kuwa mnafanya ‘kazi ya ukwe’

Ndugu Mhariri

Waswahili wana msemo wa kuthamini tendo ama kazi fulani kuwa na ‘Ya ukwe’.Husema hivyo kwa kumaanisha kazi haina malipo, haina faida, kazi bure.

Natoa pongezi nyingi kwa kanisa Katoliki (Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania TEC) kwa kushirikiana na chama cha wanataaluma wakatoliki (CPT) kwa kutoa kitabu kitabu chenye muongozo wa kuhamasisha Watanzani juu ‘Uchaguzi wa kisiasa, kwa nini tujali’ msimamo wa kanisa kuhusu uchaguzi mkuu ujao.

Kitabu na maelezo yake vimenuiwa kuwafikia wananchi.Lakini kwa kadiri ya maelezo ya mratibu wa CPT, Mariamu Kessy, ni kwamba kila jambo nchini limepelekwa nakala 30 za kitabu hicho.Majimbo hayo yawe ya uchaguzi ama ya kikanisa ama ya kimkoa ya tawala za kiserikali, inamaanisha kwamba vitabu hivyo mpaka sasa ni vichache mno kuweza kuwafikia Watanzania kwa mapana.

Haya yanaweza kuwa nje ya uwezo wa TEC na CPT. Lakini hata hivyo mimi nina jingine zaidi ya uhaba wa vitabu vitakavyouzwa ama kusambazwa. Nalo ni lile la ‘kufanya kazi ya ukwe’. Kwa vipi?

Ingawa mpaka sasa hakujajitokeza mtu binafsi , taasisi ama chama cha kisiasa ambacho kimeisha lalamikia ukweli uliomo katika kitabu hicho, ukweli ambao kila siku huwa unauma kwa asiyeupendelea, lakini ni dhahiri kwamba wapo watu ambao vitawakera. Vitawakera kutokana na mwito wa kuwataka wananchi wawachague viongozi wao kwa makini.Siyo kwa ahadi hewa, hongo na vinginevyo, mwenendo ambao nao katika kila aina ya chaguzi katika nchi hii iliyopangwa jina la ‘Bongoland’.

Bongoland hii ina watu wenye uwezo na ujanja ; ujanja ambao nina hakika umeisha tokea ama utatokea kuvifanya vitabu hivi vya uhamasishaji wa Tanzania kuhusu uchaguzi kuwa ‘kazi ukwe’. Kwa vipi?

Nimekwisha shuhudia, mara kadha, ambapo gazeti fulani lilitokea kuandika juu ya habari ambazo zilifichua mambo kuhusu ‘wakubwa’wakubwa wamekuwa wakipita katika kila kituo cha mauzo kukusanya nakala za magazeti hayo, tena kwa kununua,na kukatisha usambazaji wa ujumbe wasioutaka wakubwa hao utangazwe.

Tukio kama hilo, kwa mwenye gazeti ambalo litakuwa limenunuliwa kwa wingi (nakala zote) huona fahari hata akija gundua kwamba magazeti yake siku hiyo yalikuwa yamevamiwa kununuliwa wakala wa wakubwa walionekna waliokerwa na aliyoyaandika.

Pamoja na kwamba atasikitika yalikuwamo gazetini mwake, ya kufichua mabaya ya mkubwa fulani, hayakusambaa alivyotaka, lakini hataona kwamba amefanya ‘kazi ya ukwe’.

Nafikiri mpaka hapo nimeeleweka. Kwamba, maadamu kuna watu watakaokerwa na busara katika chaguzi zijazo, vitabu hivi vitatotowekwa vinamouzwa kama yanavyotoweka magazeti yanayotoa habari za kuwaumbua vigogo.

Naomba maoni yangu yatiliwe maanani na jitihada zichukuliwe ili vitabu hivi visambazwe kwa mapana.

Zaidi na kuwafikia walengwa wote, epukeni kuzingatia maulizo

 

Maurus John Sichalwe