Lazima tuthamini kazi

TAREHE Mosi Mei kila mwaka ulimwenguni kote huadhimisha siku ya Wafanyakazi.

Katika siku hiyo sherehe hufanyika zenye kuwakupongeza wafanyakazi kwa kazi zao mbalimbali walizozifanya katika siku za nyuma.

Lakini pia katika siku hiyo viongozi mbalimbali huwahimiza wafanyakazi waongeze bidii yao katika utendaji wa kazi zao.

Tukisoma katika vitabu Vitakatifu na vinginevyo tunajulishwa kuhusu umuhimu wa kufanya kazi. Biblia takatifu inatueleza kwamba Mwenyezi Mungu alikuwa ametoa amria kwa wazazi wetu wa kwanza baada ya lile kosa lao kwamba watapata chakula chao na mahitaji mengine kwa njia ya jasho, yaani kwa kufanya kazi. Hivyo maisha ya binadamu yamezungukwa na utendaji wa kazi. Na kitendo kinacholaumiwa sana ni kile cha kutokufanya kazi, yaani kupiga uvivu.

Maneno ya Mtakatifu Paulo katika Waraka wake kwa Watesalonike hutueleza wazi wazi kuhusu kufanya kazi.

Mtume anasema hivi: "Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakul kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote.

Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi kuwa kielelezo kweu, mtufuate. Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine.

Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe." (1Watesalonike 3:7-12).

Hayo ni maneno mazito na yenye maana sana kwa binadamu. Ni jambo la kweli kwamba katika nchi yetu kuna watu wengi na hasa vijana ambao wanapoteza muda wao katika mambo ya upuuzi na hivyo hawafanyi kazi.

Kutokea tumejipatia uhuru wetu, viongozi wetu wa chama na serikali wamekuwa wakiwahimiza wananchi kuhusu kufanya kazi kwa bidii. Kulikuwa na maneno yenye kutukumbusha daima kuhusu utendaji wa kazi kama vile: Uhuru na Kazi, au Uhuru ni Kazi, au Kazi ni Uhai nk.

Viongozi wetu wamekuwa wakipitapita huko na huko kuwahimiza wananchi katika kufanya kazi za maendeleo. Kama wananchi wengi wangekuwa wakiwaitikia viongozi katika mwito huo wa kufanya kazi, nchi yetu isingekuwa katika hali tunayoishuhudia siku ya leo.

Ni jambo la kusikitisha sana kuona jinsi Watanzania wengi walivyo wavivu sana. Kama alivyosema Mkuu wa Mkoa wa Dar Es Salaam, Luteni Yusufu Makamba wakati wa sherehe za Pasaka katika Kanisa la Menonite, Upanga kwamba jambo linalotakiwa ni kufanya kazi.

Na tunaposema kazi, ni kila aina ya kazi. Hakuna kuchagua kazi, bali ni kufanya kila aina ya kazi inayoweza kuwa mbele yako. Kuna wananchi wengi wanashinda wanatafuta kazi, na kumbe kuna kazi nyingi mbele ya macho yao.

Ni jambo kausikitisha sana kuwaona watu wanasafiri na kwenda mijini ili kutafuta kazi. Lakini kumbe kazi za kujipatia riziki zetu kwa kweli ziko kila mahali. Kama alivyosema Luteni Makamba, tunaposema juu ya kazi ni kila shughuli ambayo humletea mwananchi riziki yake ya kuishi na kuyamudu maisha yake.

Katika nafasi ya sherehe za Mei Mosi kwa kawaida huwa kunatolewa zawadi kwa wale wafanyakazi hodari na wazalishaji bora. Tunalopenda kusema ni kwamba licha ya kufanya kazi tunapaswa kufanya kazi kwa ufanisi, yaani kufanya kazi kwa bidii tukitumia juhudi na maarifa.

Kuna baadhi ya wananchi ambao wanafanya kazi kwa kulipualipua na hivyo kutokuleta mapato yanayotamaniwa. Tunapoamua kufanya kazi, tufanye kazi kweli kwa kutazamia mapato mazuri. Kwa mfano wale wahudumu katika mahoteli na hata katika mabaa, wakifanya kazi yao vizuri watawavutia watu na hivyo kuongeza mapato ya hoteli au baa na papo hapo na wenyewe wataongezewa mshahara.

Lakini ikiwa mambo yanakuwa kama yalivyo katika mahoteli na mabaa mengi, wahudumu hawachangamkii wateja, basi hapo tena wateja hupungua na mapato pia hupungua kwa hasara ya mwenye hoteli na pia wahudumu.

Mambo ndivyo yanavyokuwa katika sehemu mbalimbali za kazi. Ikiwa kila mfanyakazi hafanyi kazi kwa juhudi na maarifa, kila mmoja mwenye kuhusika na shughuli hiyo huathirika. Kwa hiyo tunahimizwa kufanya kazi kwa bidii na kuiona kazi hiyo ni mali yetu.

Kuna wakati ambapo wafanya kazi wanapaswa kujiuliza kuhusu malipo au mishahara yao kama kweli wanazalisha kiasi cha kutosha na hivyo kudai malipo zaidi.

Wafanyakazi wakifanya kazi kwa bidii, na waajiri wakiwa waaminifu kwa wafanya kazi wao, hapo tunaweza kutegemea kuwa na hali bora zaidi. Kwa hiyo tunapaswa kuwa na bidii zaidi, ili tuweze kuwa na maisha bora.

Tunapoadhimisha Sikukuu ya Wafanyakazi ulimwenguni, tunapaswa kuiga mifano ya wenzetu ulimwenguni ambao wamefanya kazi kwa bidii na kujituma. Kwa kufanya hivyo wameweza kubadilisha hali za maisha ya nchi zao na pia maisha yao binafsi. Hakuna njia nyingine ya kujiletea maendeleo ya kweli bila kufanya kazi. Kazi ndiyo msingi wa maendeleo, kazi ni sehemu ya uhai wetu.

Mwenyezi Mungu alifanya kazi na anaendelea kufanya kazi, na hivyo sisi binadamu hatuna budi kufanya kazi daima kwani Muumba wetu ni mtendaji daima.

Hongera Rais kwa kuzuia kuuzwa mali za Ushirika

Ndugu Mhariri,

NAPENDA nikupongeze Mtukufu Rais William Benjamini Mkapa, pamoja na viongozi wako kwa kazi nzuri mliyoifanya ya kusitisha kuuzwa mali za vyama vya ushirika.

Hatua hiyo ilikuwa ni wokovu mkubwa kwa wana kanda ya Ziwa na kwingine katika Tanzania hasa kwa wakulima wa mazao ya biashara wanaouza mazao yao kupitia vyama vya msingi na kulipwa kwa wakati muafaka. Nasema hivyo kwa sababu kuuzwa kwa mali za Ushirika pamoja na kwamba kulikuwa na madeni yasiyolipika kungeathiri vibaya wakulima na kukwamisha mahitaji yao ya lazima kama kusomesha watoto wao, kununua chakula mara palipoonekana kuna upungufu huo n.k. wakati wao hawana hatia.

Ni kweli kwamba Uongozi uliokuwepo na wengi waliopita uliweza kufuja pesa za wakulima kwa kuwaibia katika upimaji wa mizani na kuweza kujirundikia mali nyingi ambazo mali hizo ni pesa za wakulima.

Uliweza kukuta karani ambaye ni mpokeaji wa mazao ya wakulima anavyo vitu vingi ambavyo mfanyakazi wa ngazi ya juu katika serikali au mashirika ya umma usingelikuwa na vitu vya namna hiyo.

Pia ukija kwenye ngazi ya juu ya uongozi wa chama cha ushirika hawa ndio utakuta hata Rais mwenyewe hawezi kulingana nao kwa mali walizokuwa nazo.

Matokeo ya hayo yote yamewafanya wakulima wakopwe mazao yao na vyama vya msingi jambo ambalo huwakatisha tamaa wakulima na kuwafanya kuamua kuuza mazao yao kwa wafanyabishara binafsi ambao wanaweza kuwapatia pesa za hapo kwa hapo.

Pamoja na madhambi yote hayo ya viongozi, tunakupongeza Mheshimiwa Rais, kwa kujali zaidi maslahi ya wanyonge na hivyo kuzuia mali za vyama vya msingi n zisiuzwe.

Mh. Kinyondo, Mbunge wa Bukoba Vijijini alidiriki kuwaeleza waandishi wa habari na kuandika katika magazeti kusema kuwa viongozi waliopo Ikulu wanampotosha Rais katika suala hilo la ushirika.

Wananchi walio wengi waliposoma magazeti hayo walishindwa kuelewa kuwa huyu Mheshimiwa Kinyondo pamoja na kwenda kwake shule. Hakutegemea Mheshimiwa hiyo kukutana na waandishi wa habari na kuwakandia viongozi wa Ikulu kuwa wanampotosha Rais.

Ishengoma Katabazi

P.O. Box 10

Kijiji cha Katoma

BUKOBA.