Maaskofu ni Makuhani Wakuu

SIKU ya leo ni siku ya pekee katika Jimbo Kuu la Dar Es Salaam, kwani kunafanyika Sherehe kubwa sana ya kuwekwa wakfu, Mh. Padre Method Kilaini kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam. Tunatoa paongezi nyingi sana kwa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam kwa kumpata Askofu Msaidizi.

Tunasema hongereni sana Wanajimbo Kuu!

Je, Askofu ni nani na anafanya kazi gani katika Kanisa? Majibu ya maswali hayo tunayapata katika Kitabu cha Sheria za Kanisa katika Nambari 375 - 411. Kwa kifupi tunaelezwa kuwa kwa utaratibu uliowekwa wa kimungu, Maaskofu ni mahalifa wa Mitume kwa njia ya Roho Mtakatifu wanayempata. Wao huwekwa kuwa Wachungaji wakuu katika Kanisa, kuwa walimu wa mafundisho ya imani, kuwa makasisi wa ibada na wahudumu wa utawala.

Kwa njia ya kuwekwa wakfu kwao , Maaskofu hupokea pamoja na kazi ya kutakatifuza, pia kazi za kufundisha na kutawala, ambazo, walakini, kwa hali yao zinaweza kutekelezwa tu katika ushirikiano wa kihiearkia na kiongozi aliye kichwa cha Kanisa pamoja na washirki wake.

Kwa hiyo Askofu ndiye mchungaji mkuu wa Kanisa la Jimbo. Yeye ndiye mamlaka yote katika Jimbo, na hivyo hakuna anayeweza kumwingilia katika mamlaka hayo, bali huwajibika mbele ya Baba Mtakatifu ambaye ni halifa wa Petro na ndiye kiongozi halali wa Kanisa Katoliki ulimwenguni.

Askofu ndiye mwalimu mkuu wa mafundisho ya imani katika Jimbo, yeye ndiye kasisi mkuu ambaye amepewa utimilifu wa ukuhani. Yeye ndiye mwenye nguvu za utakatifuzo katika Jimbo, yaani huwapatia watu upadre wakiwa ni vyombo vya kumsaidia katika kuwatakatifuza waumini wakiwagawia Sakramenti mbalimbali.

Kwa hiyo basi, Askofu anapaswa kupewa utii na heshima kutoka kwa Wanajimbo wake, wakiwemo Mapadre, watawa na waumini wote kwa ujumla.

Hakuna chgo chote kinachoweza kufanyika katika Jimbo chenye kuhusu utaratibu wa imani bila idhini ya Askofu.

Tunaweza kusema kwa maneno mengine kuwa Askofu ndiye msimamizi wa mambo yote katika Jimbo. Kwa kuwa hawezi kuwa kila mahali, basi kila Askofu anao wasaidizi wa karibu kabisa ambao ni Mapadre. Hao hufanya kazi kwa niaba yake na chini yake. Hawawezi kufanya kitu ambacho ni kinyume cha Askofu na utawala wake.

Kwa kuwa Askofu ni kiongozi na mtawala katika Jimbo, yeye ni pia Baba katika Jimbo na hivyo anao wajibu wa kuwatunza, kuwalinda na kuwapenda waumini wake waliomo katika Jimbo lake.

Tumezoea sana kuwaita Maaskofu wetu "BABA ASKOFU" kwa maana hiyo ya huduma mbalimbali wanazozitoa kulingana na mamlaka na pia cheo chao.

Waumini wakitambua hali zao za kujiweka chini ya mamlaka wa Maaskofu wanapasika kutoa heshima kubwa kwa hao Wachungaji wakuu. Lakini hasa, hasa hudaiwa utii kwa Maaskofu ambao ni viongozi wa juu katika Kanisa mahalia, Kanisa la Kijimbo. Waumini hudaiwa kuwa na utii kama vile wa watoto kwa wazazi wao, na pia hudaiwa heshima ya juu kabisa.

Utii na heshima ambayo waumini wanapasika kuwatolea Maaskofu hutokana hasa na kuelewa cheo cha kiaskofu na umuhimu wake katika Kanisa.

Ni jambo la kusikitisha sana kuona kuna baadhi wa waumini ambao hawataki kujiweka chini ya Maaskofu na hivyo kuamua kutenda wanavyotaka.

Kuna baadhi ya waumini ambao wanafanya ukaidi "mweupe" kabisa na hivyo kuanzisha mambo ambayo hupingana na hao Maaskofu.

Wako waamini wanaoamua kujitoa katika Makanisa na kwenda kwenye makanisa mengine. Mwumini anapoamua kuacha dhehebu lake na kuingia katika dhehebu jingine, tungeweza kusema kuwa anafanya ukaidi kwa Askofu wake na hivyo kuyavunja yale maagano aliyoyafanya wakati alipobatizwa.

Hivyo pia inapotokea Padre ambaye alikuwa ame ahidi kuwa mtii na kujiweka chini ya Askofu, anaamua kumkaidi Askofu wake, hufanya kinyume cha maagano yake.

Vile vile ikiwa mwumini au Padre ataamua kujifanyia anavyotaka katika Parokia aliyokabidhiwa na Askofu, hufanya mambo kinyume kabisa cha wito wake, huleta fujo katika Kanisa la Mungu.

Tumesema kuwa hivi leo hapa Dar Es Salaam kuna sherehe za kuwekwa wakfu Mh.Padre Method Kilaini kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam. Tunapenda kumtakia heri na pongezi nyingi sana Askofu Method Kilaini.

Pia tunamwombea mbele ya Mwenyezi Mungu ili aifanye kazi hiyo vizuri kwa sifa na utukufu wa kanisa letu la Tanzania na hata la ulimwengu wote.

Tunatambua kuwa kazi hiyo ni nzito, lakini papo hapo tunasema kwa msaada na neema zake Mwenyezi Mungu ataifanikisha tu.

Kwa upande mwingine tunawaomba waumini wa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam kumpatia misaada ya hali na mali Askofu Kilaini. Tunatambua kuwa Jimbo hili ni Kuu na hivyo kazi zake ni nyingi na nzito, lakini kwa ushirikiano na waumini , watawa na mapadre, mambo yatakwenda vizuri tu. Tunawapongeza pia waumini wa Jimbo Kuu la Dar kwa kumpata Mchungaji Mkuu mwingine, mwenye nguvu, mwenye hekima, mwenye elimu na maarifa ya kimungu na kidunia.

Tunatumaini kuwa waumini wa Jimbo Kuu na hata Watanzania wengine kwa ujumla watafaidika kwa vikubwa kwa karama alizojaliwa Askofu Method Kilaini. Tunaweza kusema kuwa hiyo ni zawadi nyingine kwa Jimbo Kuu la Dar Es Salaam pamoja na ile ya kuwa ya Mwadhama, Polykarp Kardinal Pengo. Ama kwa hakika waumini wote tunajivunia zawadi hiyo kwa Kanisa letu la Tanzania na tunaendelea kumshukuru Mwenyezi Mungu.

Mhasibu Jitegemee Sekondari usiharibu jina la shule

Ndugu Mhariri,

SI kawaida yangu kuandika barua magazetini. Lakini jambo moja leo kwa niaba ya wengine, limenisikitisha hadi kuamua kulikemea kupita gazeti kwani likiendelea, huenda likachafua jina zuri la shule yetu ya Jitegemee.

Hapa Shuleni kumekuwa na tabia ya makusudi ya kuwanyanyasa walimu hasa linapokuja suala la malipo yao mbalimbali halali.

Unyanyasaji huu unafanywa na ofisi ya msarifu wa shule kinyume na matarajio ya Mkuu wa Shule pamoja na makamu wake ambao wamekuwa na bidiii katika kuhakikisha kuwa 'memo' zote za walimu za madai mbalimbali zinasainiwa na kuagiza malipo yafanywe haraka.

Cha ajabu ni kwamba msarifu wa shule hataki na hapendi kushughulikia madai au malipo ya walimu haraka kama anavyoagizwa na bosi wake. Anaweza kuchelewesha malipo bila sababu za msingi na pengine hutoa visingizio vya kitoto kama vile 'hamna hela'.

Shule hii ni kubwa na kila siku inakusanya kiasi kikubwa cha pesa, inakuaje mwalimu anaidhinishiwa malipo yake na Mkuu wa shule halafu yeye Msarifu anaikalia 'memo' na ukimfuata anajibu kwa mkato na dharau.

Si mara chache msarifu amesababisha baadhi ya walimu kukosa fedha za matibabu au kushindwa kusafiri kwa sababu ya kutojali shida za walimu hao ambao ndio watendaji wakuu.

Madai haya si majungu kwani walimu wengi sana wamekuwa wakisirshwa na huduma za ofisi ya fedha ambayo inafanya kazi kwa kiburi jeuri na dharau. Tunaomba msafiri awe na ubinadamu kwani sisi hatukuomba kupata shida hizi.

Kwa niaba ya wafanyakazi waathirika wote na kwa manufaa ya shule, tungependa kumuomba msarifu huyo asiharibu jina la shule.

Mkuu wa Shule na makamu wake ni viongozi ambao tayari walishatengeneza jina la shule hii na sasa inasifika kote nchini ,. iweje tangu alipofika tu aanze kwa matatizo namna hiyo?

 

Mwalimu Muathirika,

Kwa niaba ya wengine,

Shule ya Sekondari, Jitegemee

Dar es Salaam.

Mkapa ni urithi wetu kwa Nyerere

Ndugu Mhariri,

 

RAIS Benjamin Mkapa aliridhiwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa chaguo la Watanzania wote.

Ni kiongozi anayefaa ambaye Baba wa Taifa alimpendekeza awe kiongozi, nasi tukampokea, tukamkubali na kumchagua kwa moyo mmoja. Kuanzia tulipomchagua ametuongoza vizuri bila wasiwasi mpaka sasa. Tanzania inaendelea vizuri, tumekwishamuelewa kuwa ni kiongozi mshupavu, maarufu na hana wasiwasi. Linalosikitisha ni kuwa Watanzania wanayumbishwa na baadhi ya wanasiasa ambao hatujauona uwezo wao. Wanataka watu wenye uchu wa madaraka watuvuruge.

Mimi naelewa kwamba mtu anayesifu kitu alichokiona anaweza kuaminika zaidi kuliko yule ambaye ana maneno ya kuambiwa tu.Naomba Watanzania tusiyumbishwe; Chama cha Mapinduzi ndio silaha yetu ya Umoja na Amani. Kimetutoa mbali kikiongozwa na Hayati Baba wa Taifa ambaye hatutamsahau, (Mungu amuweke Mahali Pema Peponi) na sasa kiko mikononi mwa mrithi wake Rais Mkapa. Wanaovuruga nchi hii wanatutia uchungu, lakini Mungu hatapenda waivuruge.

Rais Mkapa ni kumbukumbu tuliyoachiwa na Baba wa Taifa pamoja na kazi nyingine alizozofanya Baba wa Taifa.

Mimi napendekeza ikiwezekana katika Uchaguzi mkuu ujao apite bila kupingwa.

Ahsante,

Wenu katika kujenga Taifa,

Mzee W. Mhando.

Umba River Tours,

P.O. Box 16286,

Dar es Salaam.