Waumini wageuzwe kwa mfungo wa Kwaresma

WIKI hii Waumini wa madhehebu wa Kikristo wameanza Mfungo wao wa kila mwaka wa Kwaresima. Ni kawaida kwa kila mwamuni wa kila dini kuwa na muda fulani ambapo hufanya toba kwa kusali, kufunga, kujinyima na kufanya matendo mema mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia maskini na wale wote ambao wako katika matatizo mbalimbali ya maisha ya hapa duniani.

Mfungo wa waumini Wakristo siyo tofauti sana na ule ambao Ndugu zetu Waislam na madhehebu mengine hufanya. Wote wakitambua hali yao ya dhambi mbele ya Mwenyezi Mungu hutumia wakati huo katika kutubu, kuungama na kukiri makosa yao mbele ya Mwenyezi Mungu. Toba hiyo hufanyika kwa njia mbalimbali. Licha ya kufanya hiyo toba, pia wanashauriwa kusali zaidi wakati huo wa toba. Tunavyofahamu sala ni mahusiano ya karibu sana ya binadamu na Muumba wake. Hapo hutoa sala za kushukuru, sala za kuabudu, sala za kumsifu Mwenyezi Mungu, sala za kumtukuza, sala za kuomba msamaha kwa dhambi mbalimbali tulizomkosea Mwenyezi Mungu na pia zile ambazo tumewakosea binadamu wenzetu.

Tunasema kuwa wakati wa Mfungo mtakatifu, ni pia wakati wa Upatanisho. Binadamu anapokuwa ametenda dhambi huwa amejifarakanisha na Muumba wake, na hivyo huhitaji upatanisho. Siyo hayo tu, pia huyo binadamu huwa amejitenga na binadamu wenzake anayeishi na kushirikiana naye. Kwa hiyo jambo la tatu analopaswa kulifanya mtu yule mwenye kufanya toba ni kufanya matendo mema, yaani kutoa sadaka kwa ajili ya maskini na wale ambao ni wanyonge katika jamii yetu.

Kwa hiyo tunapenda sana kuwapongeza Wakristo wote kwa kuanza Mfungo huu mtukufu. Ni matumaini yetu kuwa Mfungo huu wa Kwaresima utakuwa ni wenye manufaa kabisa kwa Waumini wenyewe binafsi, lakini pia kwa ndugu na marafiki wote. Mfungo huu mtukufu ukiwa unafanyika hasa katika Mwaka huu Mtakatifu, tunaamini kwamba utakuwa ni wa pekee ukizaa matunda ya pekee kwa Taifa la Mungu. Kwa upande mwingine tunasema kuwa ni matumaini yetu kuwa Kanisa kwa ujumla litafaidiaka sana kwa Mfungo huu wa Kwaresima.

Waumini sharti watambue kuwa kuna madhambi mengi katika taifa letu ambayo hayana budi kuondolewa hasa kwa njia ya Mfungo mtukufu. Tunalia sana kuhusu mumong’onyoko wa maadili katika taifa letu. Pia tunahangaika sana na hali ya vijana wetu wanavyoishi na kuleta shida katika taifa letu. Tunahangaishwa na magonjwa mbalimbali katika taifa letu. Hasira ya Mungu itatulizwa tu ikiwa waumini tunafunga na kujinyima mambo mbalimbali. Taifa letu vile vile linakabiliwa na matatizo ya uchumi na hali ya mabadiliko katika siasa. Kwa ufupi tuna matatizo mengi sana hasa katika kubadilisha tabia na mienendo yetu. Tunakabiliwa pia na hali mbaya ya hewa, na shida nyingi sana. Kwa nguvu zetu sisi wenyewe hatuwezi kamwe kuyashinda hayo yote . Tukiwa na imani tunasadiki kuwa kwa mfungo huo wa waumini wakristo utasaidia kabisa kwa kutuletea neema.

Jambo jingine ambalo Waumini Wakristo wanapaswa kulizingatia ni kwamba imewapasawa kutoa sadaka zao kwa moyo wa ukarimu. Wakati huu wa Mfungo ni wakati hasa wa kutenda matendo mema na kuacha uchoyo na ubinafsi. Waumini wanapaswa kuwa wema zaidi, na kuwa wakarimu zaidi. Hivyo ndivyo inavyowapasa wale wote ambao wameamua kufunga na kumrudia Mwenyezi Mungu.

Jambo kubwa sana kwa hao Ndugu Wakristo ni kwamba imewapasa kuwa kweli waaminifu katika Mfungo wao huo. Mara nyingi sana hutokea kuwa Wafungaji wa Mfungo huwa hawashiki utaratibu ule wa Mfungo, yaani hawatimizi ahadi zao kwa visingizio mbalimbali. Wasifunge kwa namna ya kujionyesha, bali hasa inatakiwa kufanya mageuzi ya ndani. Baada ya mfungo, wale wanaofunga inawapasa kubadilika kabisa kutoka ndani ya mioyo yao. Tunaweza kusema kuwa lengo la Mfungo ni kumbadilisha binadamu, ni kufanya mageuzi ya ndani. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa Mfungo mtukufu ni kipindi cha kubadilika kutoka ndani na kuwa binadamu aliye mwema na mkarimu zaidi.

Tunatumaini kuwa ikiwa kweli Waumini Wakristo watafunga kweli kweli basi tunataraji kuona matunda yake katika jamii yetu. Tunaamini kuwa huo Mfungo utaleta baraka katika taifa letu, na hivyo kubadilisha hali ya wafungaji wenyewe binafsi na pia kwa ya taifa letu ili kuleta furaha zaidi katika kanisa na katika taifa kwa ujumla. Tunaamini kuwa kila mfungaji atajiwekea malengo yake binafsi ili kuzidi kuboresha maisha yake binafsi na pia kuwa kweli mwenye faida zaidi katika jumuia yake. Tunafahamu kuwa hakuna mtu aliye kisiwa katika taifa, bali anaishi katika jumuia. Wakati akiishi maisha adili, hapo huleta nafuu pia kwa wale anaoishi nayo. Kinyume chake lakini, binadamu anapoishi katika hali mbaya, basi hapo huleta shida kwa wengine.

Tunazidi kuwaomba Ndugu Wakristo washiriki kikamilifu katika Mfungo huo mtukufu. Wanapaswa kweli kutubu makosa yao mbele ya Mwenyezi Mungu, wanapaswa kujinyima mambo fulani ambayo siyo ya lazima kwa maisha yao kama vile vileo, burudani, chakula na mambo mengineyo. Mfungaji anapaswa kujinyima na kufunga kitu kile ambacho kidogo huumiza ikiwa kama ni sadaka kwa dhambi zake na za wenzake. Wafungaji wanapswa kusali zaidi na kutumia wakati mwingi katika kujihoji na kuyatafakari maisha yao. Mara nyingi binadamu huzama mno katika shughuli za nje, na hivyo muda huu wa Mfungo ni wakati mzuri sana kwa kuzama na kuangalia hali ya ndani ilivyo na kuziona kasoro zake na kuweza kujirekebisha. Na jambo jingine katika mfungo huo wafungaji wanatakiwa kuonyesha upendo wao kwa maskini. Mambo hayo aliyafanya Kristo mwenyewe, na pia mababu na watakatifu mbalimbali waliyafanya. Na hivyo waumini wanaomfuata wanapaswa kuyafanya.

Tunazidi kuwatakiwa Waumini Wakristo wote Mfungo mtukufu wenye neema na baraka tele na hivyo kukomaza ukristo katika taifa letu. Basi tunaomba kwa njia hii ya Mfungo mtukufu waumini wazidi kujipatanisha na Muumba wao, na pia wajenge mahusiano mema na ndugu zao wanaoishi nao. Kwaresima ni mabadiliko, Kwaresima ni mageuzi, Kwaresima ni kuwa na upendo zaidi wenye ukarimu zaidi. Kwaresima ni kuahidi kuacha mabaya na kuzingatia mema na hivyo Kwaresima ni kuwa watu wapya waliojaa huruma na upendo kwa Mungu na jirani.

Gazeti limepotosha ukweli wa mambo

Ndugu Mhariri,

Barua ya Bwana Magnus J. Tebe wa s.l.p 1142 Dar es Salaam katika toleo la Nipashe No: 01821 Jumatatu February 14; haiwezi kupita bila kujadiliwa kwa kina.Zipo sababu kuu muhimu mbili ambazo zimenifanya niijibu barua hii.

1. Ni kweli uliomo ndani yake

2. Au kashfa dhidi ya Kanisa Katoliki.

Mimi ni mkufunzi wa Komisheni ya Haki na Amani ya kanisa Katoliki, (The justice and peace commission) katika ngazi ya Jimbo.

Moja ya jukumu tunayofundisha watu ni kuhakikisha kwamba kanisa na dunia kwa pamoja vinadumisha amani na haki kama yalivyo mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

Yalivyoelezwa na kuitangazia dunia juu ya msamaha wa kodi kwa taasisi za kidini, na kutolewa mfano dhidhi ya kanisa Katoliki, ni mambo mazito, yenye kuhitaji uchunguzi wa kina na vyombo vya dola ili kuujua ukweli wenyewe.

Hapa baada ya uchunguzi kanisa likipatikana na hatia basi litawajibika kwa makosa yake, kwani ni hivi karibuni tu wito umetolewa na viongozi wetu kwamba Mkatoliki anayekwepa kulipa Kodi aungame ili afanye kitubio.

Kutokulipa kodi kwa mujibu wa mafundisho ya kanisa katoliki (CATHOLIC DOCTRINE) ni dhambi inayohitaji toba kwani mkatoliki anakuwa hakutimiza wajubu.

Vile vile uchunguzi ukibaini kwamba maneno na taarifa za Bwana Magnus si za kweli, tunaviachia vyombo vya dola, vijue ni nini kifanyike kwa sababu kanisa kama kanisa hatuna hukumu ya kufanya dhidi ya wale wanaotukosea zaidi ya kuwasamehe.

Unapoichambua kwa kina barua hii, na shutuma zake hususan ju ya ujenzi wa seminari ya Wasalvatori na Augustino Morogoro (Salvatorian Institute) utapata hisia tofauti utapata hisia tofauti.

Kwa faida ya uma na Watanzania kwa ujumla naomba niwaelimishe wale ambao sio Wakatoliki kwamba Salvatorian ni shirika la kimissionari, ambalo lina Kiongozi na ufadhili wake.

Kwa mujibu wa utawala wa kanisa Katoliki mahali lilipo linafanya kazi chini ya mmalaka ya Askofu Mahalia. Katika suala hilo Mhashamu Baba Askofu Tresphory Mkude wa Jimbo la Morogoro ndiye muhusika.

Sasa basi unapohusisha suala la Mjenzi wa Taasisi hiyo na kanisa maana yake umemuhusisha na Askofu Mahalila, katika kashfa (SCANDAL) hiyo kwani anapaswa kufahamu kila kitu kinachoendelea Jimboni kwake.

Kwa sababu Bw. Magnus Tebe, anaonekana kufahamu vizuri juu ya Costal Steel ya Dar es Salaam dhidi ya ujenzi wa chuo hicho, tunaomba awasaidie polisi katika upelelezi kwani anazo Takwimu na vithibitisho vya mali iliyoingizwa nchini bila kulipiwa ushuru, na kampuni imejinufaisha kupitia mgongo wa kanisa, ambalo ni waumini, kumbuka kwamba kanisa katoliki halina uhusiano wowote wa kibiashara na Costal Steel kwani kampuni hiyo ni ya ujenzi yenye uwezo wa kufanya kazi na Taasisi yeyote likiwemo kanisa katoliki.

Kama walikwepa kodi kutumia mgongo wa kanisa vyombo vya dola tunaomba vifanye uchunguzi wa kina na Costal Steel ikigundulika pamoja na wafanyakazi wa kanisa ambao siyo waaminifu wachukuliwe hatua za kisheria kwa mujibu wa kanuni za sheria za nchi na kanisa lenyewe.

Kama tuhuma za Bwana Magnus hazina ukweli nakutahadhalisha kwamba Costal Steel hawatakuacha au kukusamehe kama kanisa litakavyokusamehe.

kuhusu sualala shule za kanisa kutoza Ada ya juu sana kuliko Tasisi zingine hapa nchini; naomba nikuelimishe kwamba Elimu ni Nyenzo muhimu sana kwa mwanadamu yeyote.

Kanisa Katoliki halipo tayari kuudangaya umma kwa kutoa makapi ya Elimu, Elimu inayotolewa ni elimu bora yenye utambuzi wa kina, Tafadhali angalia matokeo ya kila mwaka ya shule za msingi, sekondari na vyuo vinayomilikiwa nalo.

Kwa mantiki hiyo, wanahitajika waalimu wazuri, wenyekulipwa vizuri, na vitabu vingi vizuri vya ziada na kiada, jambo ambalo limekuwa likifanyika miaka nenda miaka rudi.

Kwa gharama hii, unadhani nani atachangia? kanisa limeingia milenia ya tatu; Sinodi ya Afrika imeshazinduliwa. maana ya SINODI ni kutembea pamoja na zaidi sasa ni kanisa la kila mahali hapa Tanzania na Afrika lijitegemee kwa kila jambo.

Hapa inaonekana Magnus bado yupo katika usingizi mzito wa ufadhili wa kimishionari kama mwaka 1800 wakati injili ilipokuwa ikienezwa.

Hivi sasa hakuna ufadhili tena kwani hao waliyokuwa wakitufadhili baada ya miaka mia kupita, wanaona kwamba tumeshakuwa watu wazima wenye uwezo wa kuamua na kutenda mambo yote kwa mujibu wa Hekima na utashi. Hao pia wanamatatizo ya na misaada mingi wanaielekeza kwa wengine wenye kuhitaji baada ya matatizo ya vita kama: Serbia, Bosnia, N.K.

Wafadhili hao hawana visima vya fedha kama unavyodhani wanajichangisha kama vile tunavyochanga sadaka kanisani. Ni pale wewe na mimi tusichangie kitu muhimu kama Elimu. (If you think Education is expensive try Ignorance).

Kuhusu magari na mitambo vinavyoingizwa vyote ni mali ya kanisa kwa mfumo wa utawala wa kanisa Katoliki mali na mitambo viko chini ya Askofu wa mahalia . kwa suala unalolalamikia nenda kapate taarifa sahihi kutoka kwa askofu wa jimbo la Morogoro na atakueleza hivyo vitu unavyodai vilipo badala ya kupika majungu katika Gazeti.

Kama yupo aliyejinufaisha pia kupitia mgongo wa kanisa taarifa zako zitasaidia katika uchunguzi wa kanisa na serikai il sheria ichukue mkondo wake na ulimwengu ufahamu ukweli dhidi ya shutuma zako.

Mwisho kanisa Katoliki halijawahi kupokea Makandarasi kutoka nje, hao unaowaona wakifanya kazi za ujenzi siyo watumishi wa kuajiriwa. wengi wao ni wasamaria wema, yani walei waamini wenye kumcha Mungu na walioamua kuishi maisha ya kumtumikia Mungu bila uroho wa fedha kama ulivyo wewe na kama wameingiza mali.

Basi ni kwa ajili ya matumizi kusudiwa na wakiondoka mali hizo hubaki chini ya Askofu wa jimbo husika kwa ajili ya matumizi ya kanisa.

Wakatoliki sasa tumechoshwa na shutuma nyingi za kijinga kila wakati.

Tunaviomba vyombo vya dola vifanye uchunguzi wa kina juu ya malalamiko ya Bw. Magnus ili ukweli uwekwe peupe.

Hata msamaha wa kodi kama utaendelea kutotolewa ruksa, Tukisha lifahamu hilo kwa kina tutaona nani muathirika.

Waumini wetu tutawaeleza na Bahati nzuri ni wepesi wa kufahamu.

Watakaza mikanda na mali zote za kanisa katiliki tutazikomboa Bandarini na kulipa ushuru hata kama ni asili mia mia moja (100%).

Tupo t ayari nchi nzima kulipia hata Ekaristi tunazopokea kanisani katika ibada zetu, kwa sababu ni sehemu ya Imani yetu kwani tunaona hiyo misamaha dhidi ya kanisa Katoliki inawaumizeni Roho.

Tumsifu Yesu Kristu,

P.J.Bella

Mkufunzi- JPC

JIMBO KATOLIKI LA IRINGA