Tunapaswa kuzingatia Usafi

DALILI ya mtu mstaarabu ni usafi wake binafsi na wa mazingira anamoishi. Tunasema kwa ujumla kuwa wenzetu wazungu ni wastaarabu, yaani ni wasafi, licha ya kuwa watu waaminifu na waadilifu. Mtu ambaye ni mchafu, siyo mwadilifu ni pia siyo mstaarabu.

Viongozi wetu wa kitaifa kwa miaka mingi sana wamekuwa wakiwahimiza wananchi kuhusu mambo ya usafi, licha ya kufanya kazi kwa bidii na ufanisi.

Ni jambo la kusikitisha sana kuona wananchi wengi bado kabisa ni wachafu, wanaishi katika mazingira ya uchafu, wanalala mahali pachafu na kusema kweli tumezungukwa kabisa na uchafu.

Wako wananchi ambao wanaridhika sana kuwa wachafu na kuishi katika mazingira hayo machafu. Mtu yuko tayari hata kupita au kukaa na wenzake akiwa katika hali chafu sana, na hivyo kuona fahari akiwa mchafu kati ya wasafi.

Mara moja niliambiwa na mstaarabu moja kuwa choo ni kioo cha nyumba au mahali watu wanapoishi. Hakuna kitu kunachosikitisha kama binadamu kutokuwa na mahali pazuri pakujisaidia.

Viongozi wetu licha ya kuwahimiza wananchi katika shughuli mbalimbali za maendeleo, wamakuwa wakiwahimiza wananchi kuhusu usafi wa mazingira na uchimbaji wa vyoo ili kuepukana na milipuko ya magonjwa mbalimbali kama vile kipindupindu. Lakini kwa bahati mbaya neno hilo halijazingatiwa kikamilifu.

Mahali pale ambapo binadamu anajisaidia ni lazima pawe pa heshima, yaani pawe mahali penye usafi.

Ni jambo la kusikitisha sana mtu akipita huko vijijini na hata huko mitaani na kuona jinsi hali ya vyoo ilivyo mbaya sana. Jambo linalotakiwa ni kwamba sawa kama vile tunavyoheshimu mahali pa kulia chakula, vivyo hivyo inatupasa tuheshimu mahali pale ambapo tunajisaidia, yaani huko chooni. Na ndivyo ilivyo kwa wenzetu tunaowaita wastaarabu.

Wenzetu kwa sababu ya kuwa wasafi wanadiriki hata kusema kuwa chooni, ni mahali pa kujipumzisha licha ya kutimiza haja walizo nazo. Lakini ni kwa bahati mbaya wananchi wengi wanaona kuwa mahali kama chooni siyo mahali pa kustaarehe, bali ni mahali pa kukimbiwa mara moja mtu akishamaliza haja yake.

Vyoo vyetu ni vichafu mno hata mtu hawezi kustahimili kabisa kubakia pale na kusoma gazeti au kitabu kama wafanyavyo wenzetu waliostaarabika. Ni jambo la kusikitisha pia kuona jinsi watu wanavyokuwa na tabia mbaya ya kutokujali hali ya usafi hasa katika vyoo vile vinavyotumiwa na watu wengi. Mtu anajisaidia atakavyo na hivyo kuwafanya watu wengine waone kinyaa kabisa kuingia sehemu hizo na kujisaidia. Dalili mojawapo ya mtu mstaarabu ni kwamba anawajali wenzake. Hapendi kamwe kufanya jambo ambalo litamchukiza mwenzake, na hivyo mtu hawezi kabisa kuacha mahali alipojisaidia katika hali ya uchafu.

Wananchi wengi hawana aibu hasa wanaume kujisaidia haja ndogo kila mahali. Mapato yake ni kwamba kuna sehemu na kona nyingi sana za mijini ambazo zinanuka sana harufu ya mikojo. Inashangaza kabisa mtu mzima anakojoa popote pale bila aibu. Nimeshuhudia mwenyewe sehemu zile zinazouza vinywaji kama vile bia, soda na hata pombe za kienyeji, hazina vyoo. Mapato yake watu wanajisaidia po pote pale hasa nyakati za giza.

Hivyo tunasema watu wamezungukwa kabisa na uchafu, wanakunywa katika uchafu na pia kuvuta hewa ya uchafu. Huo kwa kweli siyo ustaarabu!

Ni vigumu sana kuweka sheria zinazohusu usafi na wahali kuwaadhibu. Jambo haliwezi kusaidia sana, kwani kinachotakiwa ni elimu ya usafi.

Tunaambiwa kuwa usafi ni tabia. Sawa kama vile kuna wenye tabia ya ukarimu na wema, vile tunawapata watu wenye tabia ya usafi.

Kwa vile ni tabia, basi tunahitaji kuwalea watu wawe na tabia hiyo ya usafi. Tabia kama tabia hulelewa kutoka utoto na siyo ukubwani. Kama wasemavyo wenye hekima kuwa samaki umkunje angali mbichi, hivyo pia tabia ya mtu. Tunapaswa kuwafunza watoto wetu tabia ya kupenda na kuwa wasafi. Wako vijana na hata watu wazima ambao hawana tabia hiyo ya usafi kwa vile hawakulelewa katika hali ya usafi.

Usafi licha ya kuwa ni tabia, pia ni kitu cha kuiga kwa wenzetu. Tunahimizwa katika maisha yetu kuiga mambo mazuri kutoka kwa wenzetu. Yaani yule mtu ambaye kwa bahati mbaya hakuweza kufundishwa usafi nyumbani kwa wazazi wake anapaswa kufundishwa na jamii.

Ni kwa bahati mbaya kwamba sisi wananchi tunaoneana aibu katika mambo hayo ya usafi. Tunashindwa kuwakemea wale ambao ni wachafu.

Kwa mfano hatusemi lolote tukiwaona wenzetu wanajisaidia po pote pale au hata wakichafua mahali kwa vikonyo vya sigara. Tunawaonea aibu wale ambao wanatematema mate ovyo ovyo, hatuwaambii lo lote kumbe hao ndio wanaoeneza magonjwa mbalimbali.

Wakati umefika sasa wa kutoonea aibu watu wachafu, bali tunapaswa kuwakemea na hivyo kujenga tabia ya usafi. Ni jambo la aibu kabisa kuishi katika mazingira machafu, kuvaa nguo chafu, kuwa na vyombo vichafu, kutokuwa na vyoo safi kwa ajili ya kujisaidia.

Pia tuone fahari kama tu wasafi, lakini kamwe tusijione wenye fahari mbele ya wenzetu tukiwa wachafu. Usafi ni ustaarabu, na uchafu ni kinyume cha ustaarabu. Tukitaka kuishi katika uchafu, tusitokee kwa wale wapendao usafi kwani siyo gharama kubwa sana ya kuwa msafi, lakini kuna gharama kubwa mno mtu akiwa mchafu. Magonjwa mengi yenye kuleta vifo hutokana hasa na uchafu, na kinyume chake afya njema kwa kawaida hutokana na usafi!

Mashaka Uchaguzi ujao

Ndugu Mhariri,

Vuguvugu la Katiba ya Tanzania (Tanganyika - Zanzibar) tusichukulie lelemama, kuna ajenda ngumu na ya siri ndani ya uchaguzi ujao.

Chama cha Mapinduzi kina hofu gani? Kubadili Katiba na hata kuacha mambo muhimu yaliyopendekezwa na Tume ya Jaji Kisanga ya White paper, yote yanamaanisha moja kwa moja ya kuwa wao ndio watakaopita katika uchaguzi ujao.

Siamini kama wangekuwa na mashaka mashaka kuwa Cheyo au Mrema huenda wakapita wangeweza wakajitungia mabadiliko hayo na kuyakimbiza harakaharaka ili kukidhi maslahi yao ya kichama, bila kujali maoni ya wananchi.

Mungu ibariki Tanganyika Mungu ibariki Zanzibari

Wenu,

Mzee S. M.Ngunga.

Merry Water Ltd,

S.L.P 7472

Dar es Salaam

 

Kushiriki ibada kwa mama Esta ni makosa?

Ndugu Mhariri,

Yupo mama aitwaye Estahapa Dar es Salaam. Yeye huendesha ibada za kuwaombea wagonjwa na wenye matatizo hasa ya uzazi Idadi kubwa ni wanawake nao hupendelea kuvaa rozari kama wanamaombi yeye ananyumba yake hapa Mikocheni A na ndipo anapofanyia ibada haitozi chochote, bali anapokea asante.

nimefahamu Esta toka 99 (lakini sijamwona).

Nimewauliza washiriki kwa kutaka uhalali wa Mkatoliki kushiriki . Nikawauliza viongozi wa jumuiya ndogo ndogo lakini sikupata jibu la kuridhisha nikabaini baadhi ya viongozi hushiriki.

Ilitokea semina katika Kanisa fulani(siku nyingi kidogo) kipindi cha maswali nikakumbika swala hilo.padre Muhusika akaniambia yeye hajui hivyo akamwagiza kiongozi wa kanisa hilo (mwenyekiti) afanye utafiti. Ilikuwa mwaka jana nilipoona kimya kwa muda wa miezi nikaamua kuandika barua kwa padre fulani nilimuliza hivi je kushiriki ibada kwa Esta ni halali? toka nimetuma barua kwa mkono sio posta sasani jumala nne sijapata jibu. Mimi mwenyewe binafsi na familia yangu hatujashiriki na haitatokea.

Wahusika Viongozi kulikoni? kwa nini kupuuza maoni?

Tumsifu Yesu Kristu

Mkristu

Dar es Salaam