Kauli ya Maaskofu imekuja wakati muafaka, izingatiwe

MWISHONI mwa wiki Baraza la Maaskofu Katoliki nchini lilitoa taarifa yake ya tahadhari na kuelezea wasiwasi wake kuhusu hali na mwenendo wa kisiasa na kijamii nchini.

Taarifa hiyo ya Maaskofu iligawanyika katika vipengele muhimu vinne: Kile wanachoona na wanachosikia, Mwenendo wa Demokrasia nchini, Wito wao wa kichungaji kwa viongozi na Watanzania wote na mwisho Katiba na Kampeni za Uchaguzi.

Juu ya wanachoona na kusikia, kiujumla maaskofu walisema sehemu kubwa ya jamii imekata au inaelekea kukata tamaa kwa kukosa huduma na mahitaji muhimu ya kijamii.

Watoto wengi wanakosa ada na uwezo wa kulipa michango ya shule, wanajamii hususan wanawake na watoto wanakosa huduma muhimu za jamii, wakulima wamesahauliwa na wameachwa peke yao wakabiliane na soko huria bila ushauri ufaao na ukosefu mkubwa wa ajira

kwa vijana ni miongoni mwa matatizo yaliyotajwa na Maaskofu.

Juu ya Demokrasia Maaskofu wamesema ilitarajiwa kwamba mfumo wa vyama vingi ungepanua demokrasia, lakini hali ilivyo hivi sasa inatia wasiwasi na kuzusha maswali mengi.

Mabadiliko ya Katiba yanayofanyika hayaonyeshi kwamba yanajali maslahi ya wengi bali vikundi.

Sisi tungependa kuzungumzia zaidi suala la Demokrasia na maamuzi yanayolenga katika kuwakomboa wanyonge badala ya kuwaongezea nguvu wenye nguvu na kuwafurahisha kwa gharama ya mateso ya wengi.

Tunajua wazi kwamba kama uamuzi wa tuwe na vyama vingi vya siasa au tusiwe nao ungekuwa suala linaloweza kuamuliwa na CCM au Serikali pekee, leo hii tusingekuwa na huu mfumo wa vyama vingi.

Awali wakati madai ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa, viongozi kadhaa wa juu wa CCM na Serikali kwa mtindo uliozoeleka wa kutetea chama waliibuka na kusema mfumo huo haufai kabisa nchini. Madai ya mfumo huo yalitokana na shinikizo la kimataifa ambalo halizuiliki, hatimaye ilikubaliwa mfumo huo uanze. Pamoja na hayo kukubalika kwa mfumo huo kunaonyesha kuwa hapakuwa na hoja ya kuishindanisha na ile ya umuhimu wa kuwepo mfumo huo ikashinda. Kwa hiyo kuanzishwa kwa mfumo huo kulimaanisha kuwepo nguvu ya hoja na mantiki ya ubora na umuhimu wa kuwepo mfumo wa vyama vingi katika maendeleo ya jamii.

Baada ya hapo wananchi tuliamini kuwa viongozi wetu baada ya kutafakari hayo kwa kina wameona mfumo huo unatufaa zaidi ya ule wa ukiritimba wa chama kimoja uliokuwepo.

Lakini kama walivyosema Maaskofu kinachoonekana hivi sasa kinakwenda kinyume na dhamira ya kupanua demokrasia, jambo ambalo linasababisha kujiuliza je, ni kweli Watawala waliukubali mfumo huu kwa dhati au kuwahadaa tu wafadhili wa nje na wananchi?

Nafasi haitoshi kutaja mambo yote yanayolalamikiwa kuwa yananyonga uwigo wa demokrasia, lakini kwa anayefuatilia mambo yakiwemo mabadiliko ya 13 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano hivi karibuni na makusudi ya mabadiliko ya Katiba Visiwani inatosheleza kusema kuwa tofauti na miiko ya demokrasia ya kweli inayoweka mamlaka kwa watawaliwa kuamua watawaliweje, sasa mamlaka ya watawaliwa watawaliweje inaporwa na watawala.

Mwelekeo wa sasa hautoi kipaumbele kwa maslahi ya wengi ambao ni wanyonge, bali vikundi vidogo vya watu wenye nafasi za kushinikiza wapate upendeleo ama kwa kujitajirisha au kudumu madarakani au kuwadumisha madarakani wanaowataka.

Tahadhari iliyotolewa na Maaskofu imekuwa wakati muafaka kwa vile tunaelekea katika Uchaguzi Mkuu na tunatarajia wanasiasa wetu, hususan watawala watazingatia maonyo hayo. Tunarudia kipengele hiki katika taarifa ya Maaskofu: Kiongozi mzuri hashughulikii mambo madogo madogo na kuyafukia yaliyo ya msingi.

Viundwe vyama vya siasa vya ki-sekta

Ndugu Mhariri,

Ni miaka kumi sasa tangu Tanzania iingie katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Je tumejifunza nini? Je, tumenufaika vipi na mfumo huo? kama yapo manufaa tulivyoyapata ni kidogo sana.

Kwa muda mfupi huu tumeona mambo mengi. Tumeshuhudia malumbano ya kisiasa miongoni mwa vyama lakini mtindo unaotumika si wa kunadi sera bali lugha za kashfa na kejeli kuashiria chuki binafsi baina ya viongozi wa vyama.

Tumeshuhudia migongano na migawanyiko miongoni mwa vyama, viongozi kuhama kutoka chama kimoja cha siasa kwenda kingine kwa nia ya kupata madaraka na kugombea fedha za ruzuku na kwa hiyo pia kuyumbisha wanachama na wananchi kwa ujumla.

Jambo la kujivunia Watanzania ni kwamba pamoja na uchochezi na fitina zinazopandikizwa na maadui zetu wa ndani na nje ya nchi bado tumeweza kudumisha umoja wa kitaifa amani na utulivu.

Hapa sina budi kuipongeza serikali kwa kazi nzuri ya kusimamia misingi hiyo.

sasa je ni masahihisho yapi yafanyike? Ni dhahiri vyama hivi vikiendelea na mtindo wa kashfa na malumbano pekee hatimaye vitakufa vyote na kuacha Chama cha Mapinduzi kikijigamba na viongozi wake kujiona machifu wateule wa Mungu.

Kwa kuwa nchi hii ni ya wakulima na wafanyakazi nadhani sasa wakati umefikawa kuunda vyama vya siasa vinavyotokana na wananchi.

Wakulima wawe na chama chao cha siasa na wafanyakazi pia wawe na chama chao cha siasa.

Katika hali hii ya ubinafsishaji na soko huria serikali licha ya mbolea na pembejeo zingine haina tena ubavu wa kupanga bei ya mazao na hivyo kutoa mwanya kwa makampuni yanayonunua mazao kuwanyonya wakulima kwa kutoa bei ndogo kadiri watakavyo.

Kwa wafanyakazi pia serikali baada ya kuvunja Scopo haina tena ubavu na kuwatetea wafanyakazi juu ya viwango vya mishahara na maslahi yao ndio maana waajiri wengi ni jeuri hawataki yaundwe matawi ya wafanyakazi mahali pa kazi na hata pale ambapo matawi yapo hayana nguvu yoyote. Mabaraza ya kazi hayasaidii wafanyakazi kwa vile hawashirikishwi kuyaunda wala katika maamuzi yanayohusu tija, maslahi yao na kugawana kwa haki matunda ya wanachozalisha.

Kwa miaka mitano hii ijayo ni vema tukawa na vyama vya siasa vichache vyenye nguvu vinavyoweza kukosoana kwa kunadi sera na malengo yaliyo wazi kwa wananchi.

Na hapo ndipo angalau tutakuwa tumepata mwanzo mzuri wa mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa maendeleo yetu. Tahadhari ni kwamba vyama hivyo visiundwe kwa misingi ya udini, ukabila au ubaguzi wa aina yoyote ile.

Vituo vya kujazia mafuta magari viongezwe

Mhariri Kiongozi,

Naomba nafasi kidogo katika Gazeti lako tukufu ili niweze kuelezea haya machache niliyo nayo kuhusu tamko la Serikali kuwataka madereva wawashushe abiria wakati wanapokwenda kujaza mafuta katika vituo vya kujazia mafuta.

Bila shaka kauli hii ni kweli ililenga kuwasaidia wananchi ama abiria kuepukana na ajali wanapokuwa katika vituo hivyo vya mafuta lakini kama haikuangaliwa vizuri huenda ikawa ndio hasa kichocheo cha ajali.

Lingekuwa jambo la busara kama serikali ingetoa changamoto kwa wananchi wake wajenge vingi zaidi vituo vya mafuta kwenye maeneo yenye idadi kubwa ya magari ili kuondoa adha na kero wanayoipata abiria pale wanapolazimishwa kuteremka njiani ili gari likaongeze mafuta,jambo ambalo huwafanya abiria wasubiri muda mrefu na wakati mwingine kuchelewa maofisini kwao.

Ikumbukwe kuwa amri nyingi zinazotolewa na serikali zisipoandaliwa mazingira mazuri ya utekelezaji huwaumiza wananchi wasio na hatia.

Inawezekana kweli madereva wametii amri ya kufika katika vituo vya mafuta bila kuwa na abiria lakini je, wanatumia utaratibu upi wanapotaka kuegesha magari yao na kuwashusha abiria? hili ni swali jingine.

Kuna adha kubwa wanayoipata abiria kutokana na ufinyu wa barabara ambao unaweza kusababisha mikwaruzano kwa magari mengine yanayopita, hivyo kuifanya ajali iwe kubwa pengine zaidi ya ile itakayotokea katika kituo cha mafuta.

Mpenda haki ,

Wiliblod Bandihai

Dar es Salaam.