Make your own free website on Tripod.com

Tunawashukuru Viongozi wa dini za Kikristo

WIKI iliyopita Viongozi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Viongozi wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania walitoa Tamko kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Wakiwa ni Viongozi wa Makanisa, walimu na walezi na manabii katika Taifa la Mungu,matamko waliyoyatoa yanadhihirisha umakini, kujali na upendo kwa jamii ya watanzania kama ndugu zao katika Bwana.

Katika Matamko hayo kuhusu Uchaguzi, Viongozi hao wamezungumzia wajibu wa kila raia kushiriki katika Uchaguzi huo Mkuu kwa hali na mali.

Wamezungumzia elimu ya uraia ambayo kwayo inamsukuma kila raia kutambua wajibu wake kuushiriki uchaguzi ili kuwapata viongozi bora.

Wametoa rai kuwaelimisha raia ili watambue wajibu huo wa kuwachagua viongozi wanaofaa, walio waadilifu, wenye uchungu wa nchi, na wenye kujitoa mhanga kwa ajili ya maendeleo ya taifa.

Kwa raia hasa Wakristo, kutokushiriki uchaguzi, ni kukwepa kutimiza wajibu na kila mmoja hana budi kujua kuwa yamekuwapo malalamiko mengi dhidi ya baadhi ya viongozi wa awali kutokana na jukumu ambalo jamii ya Watanzania ilikuwa imewakabidhikatika utendaji kazi wao.

Hata hivyo kinachosikitisha sana , ni pale inapojidhihirisha kimatendo kuwa wanaokuwa wa kwanza na kuongoza kuwalalamikia viongozi hao waliochaguliwa kwa kura, ni wale ambao wao wenyewe, hawakushiriki kikamilifu katika chaguzi zilizowaweka madarakani.

Ni jambo la kusikitisha sana kuona raia wengi hawataki kutumia haki yao ya kuwachagua viongozi walio bora ili waliongoze jahazi la kuelekea mandeleo ya kweli yenye kuwafa zaidi wananchi wote; yenye kutoa kipaumbele kwa watu, badala ya vitu.

Viongozi walio bora, ni wale wanaochaguliwa siyo kwa njia ya rushwa na hongo, ama upendeleo fulani, bali hasa kutokana na uwezo walio nao ikiwa ni pamoja na tabia zao za uadilifu na wenye kupenda kuwatumikia watu kwa upendo bila lengo la kujinufaisha wala agenda za siri.

Sisi tunaamini kuwa matamko hayo ya viongozi wa Kikristo, yamekuja wakati muafaka ambapo wananchi hawana budi kueleweshwa na kutumia uelewa wao ili kushiriki kikamilifu kuwachagua viongozi watakaosimamia sawia mipango yetu ya maendeleo katika karne na milenia hizi mpya.

Tunaamini kweli kuwa tutahitaji kuwa na viongozi watakaotuonesha dira itakayotuelekeza kwenye maendeleo ya kweli.

Viongozi wetu wa kidini wamewaonya wapiga kura kuwa ni mwiko kuwachagua viongozi kutokana na rushwa au hongo kama ilivyokuwa ikifanyika katika chaguzi za nyuma.

Wananchi hawana budi kukumbuka kuwa kizuri chajiuza na kibaya, chajitembeza.

Hivyo, wanaotafuta kura kwa njia ya rushwa au zawadi mbalimbali ni dhahiri kwamba hawafai na kwamba wanajitembeza tu.

Sisi Watanzania tunasema ,tusingependa tena kuwa na kesi za uchaguzi kama Uchaguzi Mkuu Uliopita ulivyokuwa na wingi wa utitiri wa kesi.

Ambazo nyingine zililazimisha taifa kufanya chaguzi ndogo za marudio.

Tunakataa hali hiyo kwa kuwa inalitia taifa hasara kubwa kwani uchaguzi kama chaguzi zinagharimu pesa nyingi.

Viongozi hao wametutaka tukatae kila aina ya rushwa katika chaguzi zetu zote zijazo.

Viongozi wa Makanisa wanataka wananchi wawachague viongozi wanaoyafahamu matatizo ya watu kimaendeleo, kiuchumi, kijamii, kimaisha na hata kimazingira.

Jamii yetu inapenda kuwa na viongozi walio karibu na watu waliowachagua.

Natumaini sisi Watanzania tumepata mang’amuzi ya kutosha kuhusu viongozi ambao tumekuwa tukiwachagua kila baada ya miaka mitano.

Chaguzi zilizopita ziwe ni kioo cha kujiona kurekebisha makosa na kuendeleza mazuri tuliyoyaona na yale makosa, tuyasahihishe katika uchaguzi huu kwaniviongozi wengi wamekuwa hawaonekani majimboni mwao hadi yanapotokea maafa, au basi kipindi kama hiki cha kuanza kuomba kura ndipo huonekana na juhudi zakufanya maendeleo ambazo ni "danganya toto" kwa maneno laini na lugha tamu.

Sisi tunasema wakati umefika wa kutokuwaonea haya viongozi kama hao wasiotekeleza wajibu wao wa kuwahudumia waliowachagua na wanaoishia kurubuni wapiga kura ili wawachague kimakosa.

Tunawataka viongozi watendaji na siyo wasemaji au wadanganyifu. Tumechoshwa mno na hali au tabia hizo za viongozi wasio waadilifu baada ya kuchaguliwa kwao katika nafasi walizoziomba.

Lingine lililotiliwa mkazo na viongozi hao wa kiroho, ni kuona Uchaguzi Mkuu ujao unakuwa wa huru, haki na amani.

Tanzania tumepata dosari kubwa kutokana na Uchaguzi wa mwaka 1995, na hivyo wanatoa mwito kwamba makosa hayo yasifanyike tena, yaani kusiweko kabisa ukosefu wa haki wala udanganyifu wa namna yoyote ile.

Kila raia na kila mwombaji wa kura anapaswa kulizingatia jambo hilo. Tunapenda kuona uchaguzi wa mwaka huu umesafisha kabisa uchafu ule uliokuwa umeleta dosari katika taifa letu.

Raia wapewe nafasi ya kuwachagua viongozi kwa hiari na siyo kwa kudanganywa au kupewa vizawadi na wahusika. Tunapenda kuona kuwa haki inatendeka chini ya Demokrasia ya kweli na siyo namna nyingine. Wagombea wanapaswa watuambie nini watakachotufanyia tukishawachagua na siyo vingine.

Ni dhahiri kuwa kwa wenye nia mbaya, viongozi hao wanapotoa tamko au neno linalogusa ukweli, wanaupinda na kuuchafua kwa madai kuwa wanajiingiza kwenye siasa, la hasha, hiyo sio siasa ni ukweli na uhali wa kazi wanayopaswa kufanya ili kuiokoa jamii isiangamie kimwili na kiroho.

Wanaifanya kazi hiyo kama walezi wa taifa kwa kuwa taifa letu halina dini. Kila mlezi hutamani kumpatia mtoto wake chakula na malezi yanayomfaa, ndivyo wafanyavyo.

Ni walimu wetu, na kwa kawaida kila mwalimu hufanya kazi ya kumfundisha mwanae mambo yale ya kumfaa katika maisha yake. Hivyo, wanao wajibu wa kuwaelimisha raia hasa waamini wao kuhusu jukumu hilo la Uchaguzi Mkuu kwa manufaa ya taifa.

Vilevile Viongozi wetu wa kidini wanayo ile sauti ya kinabii ambayo hutoa maangalisho kwa kuona mambo yajayo. Ni nani asiyependa kupata maangalisho kuhusu mambo ya baadaye?

Mwenyekiti wa TLP Augustine Lyatonga Mrema fafanua hao makafiri ni akina nani?

Ndugu Mhariri,

MARA kwa mara Serikali na chama tawala huwa kinatukumbusha kauli za marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, juu ya kukumbatia Udini,Ukabila Ujimbo kuwa ni hatari kwa Taifa letu. na pia hata Rais Benjamini Mkapa huko Dodoma alikemea jambo hili katika kipindi hiki tunachokaribia uchaguzi mkuu tayari sisi wananchi tunashuhudia baadhi ya vyama vya upinzani dhahiri vinaotesha mizizi ya Udini jambo ambalo linatuchanganya sisi wananchi wapenda amani.

Mnamo tarehe 14/06/2000 katika viwanja vya Jangwani katika hotuba zako ambazo zimenukuliwa na gazeti la Majira Toleo No 2354. Vol 11326 la tarehe 15/6/2000 ulisikika ukisema nanukuu: kuhusu swala la Waislamu kuwa na kadhi hakuna Uislamu nchini bila kuwa na Kadhi mkuu "Kesi nyingi za Waislamu na migogoro yao zinaamuliwa na MAKAFIRI tu. Lazima tuwe na kadhi kwani bila yeye hakuna uislamu nchini mwisho wa kunukuu.

Ndugu Mhariri kauli hii ya Mrema ina vipengele vingi sana vya kutafakari bila kufanya hivyo tutajikuta sisi wanananchi tunakumbatia vyama vya ajabu ajabu.

1. Nianze na hakuna Uislamu nchini bila kadhi. Je ni lini ulisikia kuwa Uislamu ni kadhi? Ninachojua mimi kwamba Waislamu wanaongozwa na Korani yao ya Alah.. na hadithi za Muhamand ndiyo mwongozo wa waislamu na kutekeleza maagizo ya allah na Mohamed ndiyo Uislamu. Kama wewe unaufahamu Uislamu basi tufafanulie sisi wananchi tujue kuwa kumbe Uislamu ni Kadhi.

2. Kesi nyingi za Waislamu na migogoro yao zinaamuliwa na MAKAFIRI tu. Kauli hii unawafundisha nini watu waliokuja Jangwani na sisi ambao tumesoma kwenye magazeti ninaomba ufafanuzi ili tuwaelewe Makafiri ni akina nani katika nchi hii na wewe kura zako unawaomba akina nani? Na je kama utapata Urais hawa makafiri unaowajua wewe utawapeleka wapi ambao hawafai kuwahukumu waislamu wenzako na hali nchi yetu haina ubaguzi wa DINI. Kwa maana hiyo kauli zako mara kwa mara unajiweka mbele kuwatetea Waislamu hali Wakristo, Wapagani, Budha Wahindu, hatujakusikia ukiwatetea. Moja kwa moja tumekugundua una ubaguzi wa udini unapendelea upande mmoja na pia unachochea udini.

3. LAZIMA TUWE NA KADHI. Hii ni kauli uliyoitamka ambayo Majira wameinukuu Uk.3. Inaashiria na wewe u mmoja wao wanaotaka kadhi ili uhukumiwe na kadhi basi usiwe na agenda ya siri bora tujue moja kuwa wewe ni Muislamu.

Marejeo katika kauli za Waislamu katika gazeti la Tafakari toleo No. 0095 la Machi 24-26:1999 lasomeka. Mrema sasa atakiwa kusilimu yadaiwa ndipo atashinda Urais 2000 yaelezwa waislamu walimsimika Temeke hizi ni kauli za waislamu wenzako kama sivyo vipi uing'ang'anie kadhi je umeshatekeleza sharti lao la kusilimu?Katika gazeti la Tafakari toleo No.00106 Mei 1-4 1999. Kulisomeka waislamu wampa Mrema masharti walisisitiza akitaka IKULU lazima asilimu. Je ulishatekeleza hili.

Ndugu Mhariri kwa ushahidi huu inatosha kuwaelewa viongozi ambao wanataka kutuga wa wananchi kwa msingi ya udini ndiyo hao na vyama vyao vina agenda ya siri juu ya nchi tuwe makini kwa kauli mbalimbali na ushahidi huu wa matamko ya Waislamu kumbe wanatueleza kuwa kwenda Ikulu ni lazima wawe waislamu tu hii ni hatari ya udini ushahidi wamazingira tayari unaonyesha vipo vyama vyenye mtazamo huu. Wananchi tuwe makini na hilo.

Makanisa ya Wakristo yanachomwa moto hapa nchini lakini hatujawahi kusikia ukitutetea ina maana wewe utetezi wako ni Waislamu tu au wananchi wote.

Ndugu Mhariri naomba ndugu Mrema afafanue Makafiri ni akina nani katika nchi hii.

Mwisho nakuomba Mheshimiwa Mrema asome Msemakweli juu ya hoja ya Kadhi kila Jumapili.

Mimi Mwinjilisti

 

C.Simbaulanga

MKURUGENZI WA HUDUMA YA BIBLIA NI JIBU

P.O. BOX 45290

DAR ES SALAAM