Kila la heri Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC)

HAPO jana Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), limemaliza Mkutano wake Mkuu wa Mwaka. Baraza HILO, hujumlisha Majimbo 29 yenye Idara, Vitengo na Taasisi mbalimbali.

Wapo wenyeviti wa idara mbalimbali zenye ofisi zake katika Kituo cha Baraza hilo Kurasini, Dar-Es-Salaam. Mkutano huo uliochukua takribani wiki mbili, kwanza ulikuwa na Kikao cha Kamati Tendaji ambayo ilishughulikia hasa mambo ya bajeti na mengine kwa ujumla.

Baada ya Kikao hicho, zilikuwapo siku mbili za kupokea ripoti toka Idara mbalimbali, vitengo na taasisi za Baraza.

Kisha, kumekuwa na Kikao Kikuu cha Maaskofu kilichojadili mambo mengi kuhusu Utendaji wa Baraza katika miaka mitatu inayokuja. Kulitolewa mapendekezo na maamuzi yatakiwayo kutekelezwa katika kipindi kingine kijacho cha miaka mitatu.

Baraza la Maaskofu linashughulikia maendeleo ya binadamu ya kiroho na maendeleo ya kimwili au ya kidunia pia. Kwa maneno mengine ni kwamba Kanisa Katoliki la Tanzania linamhudumia binadamu kimwili na kiroho.

Katika nafasi hii, tunapenda kulipongeza TEC kwa juhudi zake mbalimbali katika kuliendeleza Taifa la Mungu. Ufanisi wa shughuli zake, unatokana hasa na mshikamano na ushirikiano katika Baraza hilo.

Nidhahiri kwamba umoja ni nguvu, na utengano ni udhaifu. Hivyo, tunaweza kusema kuwa TEC, ni lenye nguvu kutokana na ushirikiano na umoja uliopo ndani yake.

Utendaji bora wa TEC unajionesha kuanzia hata katika kituo chake cha Kurasini chenye hostel itoayo huduma muafaka kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.

Baraza hilo pia limefanikiwa sehemu mbalimbali ukianzia hapa Kurasini penyewe. Kituo cha Mikutano cha Baraza la Maaskofu Katoliki kina Hostel nzuri sana inayotoa huduma nzuri kwa wageni mbalimbali ni chenye ufanisi mkubwa sana. Kutokana na mshikamano ulioko pamoja na ushirikiano Baraza la Maaskofu Katoliki limeweza kuanzisha Chuo chake Kikuu cha Mt.Augustino kule Mwanza, licha ya kuwa na Seminari Kuu tano zinazowaandaa Vijana kwa ajili ya Upadre. Pia kwa upande wa Idara, kuna Idara ya Caritas, Idara ya Elimu, Idara ya Mawasiliano, Idara ya Afya, Idara ya Kichungaji, Idara ya Liturujia, Idara ya Katekesi na ile Idara mama ya Fedha na Mipango. Idara zote hizo zina Wenyeviti na chini yao kuna Watendaji wakuu wa Idara pamoja na Watendaji wa Vitengo na taasisi. Baraza la Maaskofu lina ushirikiano wa karibu sana na Mashirika ya Kitawa katika utendaji wa kazi mbalimbali za kitume.

Ni jambo la kufurahisha sana kuona jinsi kila Idara inavyojishughulisha katika utendaji wake wa siku kwa siku. Kumekuwa na mafanikio mengi sana hapa na pale katika utoaji wa huduma katika Baraza la Maaskofu. Huduma za maendeleo zinazidi kuwa za mafanikio sana katika taifa letu. Tunalipongeza Baraza kwa huduma hizo zote katika Taifa la Mungu.

Kwa kuwa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linafanya shughuli mbalimbali kwa ajili hasa ya kuwahudumia wananchi wote bila ubaguzi, tungetaraji kwamba lingepewa misaada ya hali na mali kutoka upande wa serikali kila linapohitaji.Mara nyingi kumekuwa na hali ya kukwama katika utendaji wa Baraza la Maaskofu Katoliki kwa sababu ya kutopewa msaada unaotakiwa na kwa wakati unaofaa. Kwa mfano Kanisa linakwama katika kutoka huduma kwa vile kuna vikwazo vya mambo ya kodi na vitu vingine vya aina hiyo. Siyo maana yake kwamba Kanisa lisilipe kodi, lakini wao utaratibu wake uwe ni wa kueleweka kirahisi ili kuwezesha mambo yaende vizuri. Mara kwa mara kumekuwa na kukwama katika shughuli za huduma kwa upande wa Baraza kutokana na ule urasimu unaotumika.

Tunapenda kumalizia Kauli Yetu kwa kulitakia Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania mafanikio zaidi katika kipindi hiki kinachoanza katika karne mpya na hasa katika milenia mpya. Tunataraji kuwa utendaji katika kipindi hiki cha miaka mitatu utakuwa ni wenye ufanisi wa namna ya pekee kabisa tukijua kuwa ni karne ya sayansi na tekinolojia. Kwa hiyo ni wazi kwamba watendaji katika Baraza la Maaskofu watakuwa wabunifu zaidi na hivyo kuleta mafanikio zaidi na zaidi katika Taifa la Mungu. Tunapenda kutoa mwito kwa kila mtendaji katika Baraza la Maaskofu kuzidi kujitoa mhanga zaidi kwa ajili ya ufanisi wa shughuli hizo za Baraza la Maaskofu na hasa Kanisa Katoliki la Tanzania. Tunapenda kuona kuwa kila mtendaji katika Baraza anajisikia kuwa ni sifa yake kuliletea Baraza hili mafanikio kwa njia ya huduma zake.

Kwa upande wa waumini wengine, tunatumaini kuwa mwaka huu utakuwa ni mwaka wa uelewano na ushirikiano na Baraza letu la Maaskofu Katoliki Tanzania. Tusingependa kuona kunakuwa na mifarakano kati ya waumini wakatoliki na Baraza letu la Maaskofu. Waumini wote Wakatoliki wanapasawa kujiona kuwa wako chini Baraza la Maaskofu na hivyo kushika ile miongozo mbalimbali inayotolewa na Baraza hilo. Tusingependa kuona tena kuna mifarakano kati ya Baraza letu tukufu na waumini binafsi kwa sababu zao za binafsi.

Tunazidi kuliombea Baraza letu katika kipindi hiki cha miaka mitatu liwe na mafanikio zaidi ya kiroho na kimwili. Tungependa pia kuona Baraza letu linazidi kutoa mwanga kwa Mabaraza mengine ya Afrika ya Mashariki na mahali pengine. Mpaka sasa limefanya hivyo, lakini tunataka lieneze mwanga huo zaidi na zaidi. Lidumu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Kristu, Jana, leo na daima.