Kulikoni hata wanafunzi kusafirishwa kwa gari la takataka ?

Kwa miaka ya hivi karibuni, jamii ya Watanzania imekuwa ikishuhudia vifo vinavyotokana na ajali mbalimbali zilizo lifanya taifa kupoteza watu ambao ni tegemeo lake.

Miongoni mwa vifo vinavyokumbukwa katika historia ya nchi hii, ni vile vilivyotokea katika ajali ya meli ya MV . Bukoba iliyotokea katika Ziwa Viktoria Mei 21, mwaka 1996 ambapo zaidi ya Watanzania 600 walipoteza maisha.

Sababu kubwa na ya jumla iliyopelekea ajali hiyo ni uzembe na kutokujali kanuni za usalama katika njia hiyo muhimu ya usafiri.

Pia, ajali za barabarani zimekuwa zikisikika kila kukicha nchi ambazo nazo, zimepelekea vifo na vilema kadhaa kwa Watanzania.

Hata hivyo, tunapenda kulipongeza Jeshi la Polisi hasa Kikosi cha Usalama Barabarani kwa juhudi kadhaa linazozifanya kuona kwamba kama sio kuzikomesha kabisa, basi ajali hizo zinapunguzwa kwa kiasi kikubwa.

Tunasema hivyo kwa kuwa Kikosi hicho tayari kilishafanya tafiti mbalimbali na kubaini kuwa vyanzo na sababu za ajali nyingi, ni pamoja na mwendo mkali wa magari, pikipiki na baiskeli, uchakavu wa magari, uzembe wa watumiaji wengi wa barabara, ukosefu wa alama za barabarani, ulevi, ujenzi holela kando kando ya barabara na ongezeko la watu na magari hasa katika maeneo ya miji mikubwa ukiwamo Dar-Es-Salaam ambao unaongoza kwa ajali nchini kwa kipindi kirefu ukifuatiwa na Morogoro, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Mbeya na Iringa.

Tunasema tunakipongeza kikosi hicho cha usalama barabarani kwa kuwa kinachukua hatua za dhati kudhibiti hali ya kukithiri kwa vitendo vya ukiukwaji wa sheria na kanuni za utumiaji wa barabara.

Hii ni pamoja nakufanya doria na kuwakamata madereva wanaokiuka taratibu na kanuni hizo, kuyafanyia ukaguzi wa mara kwa mara, kuwafikisha mahakamani kwa kosa la kutumia magari mabovu, na kuwashauri wayatengeneze na kubwa zaidi, kutoa elimu ya usalama barabarani kwa wanafunzi wa vyuo, sekondari na shule za msingi ambapo somo hilo, limeingizwa kwenye mtaala hivi karibuni.

Hata hivyo zipo sababu nyingine ambazo bado hazijafichuliwa na endapo Kikosi hicho hakitalivalia njuga, ipo hatari ya jahazi hilo lililosheheni juhudi za kudhibiti ajali likawa na tundu linalozivujisha, na moja wapo ikiwa ni tamaa na ubadhilifu wa watendaji kadhaa wa serikali.

Tunasema hivyo kwa kuwa hivi karibuni katika ajali iliyotokea mjini Dodoma Mei 28, mwaka huu, iliyowahusisha baadhi ya wanafunzi wa shule za msingi, waliokuwa wakitokea Kondoa kwenda Dodoma imeshangaza na kuwapa maswali mengi watu kadhaa wakiwemo wazazi wa wanafunzi walihusika na ajali hiyo.

Wanafunzi walipinduka na gari walilokuwa wakisafiria kwenye makutano ya barabara ya Arusha yaliyopo mjini hapo karibu na uwanja wa ndege baada ya dereva kushindwa kukata kona.

Wazazi hao, wamekilalamikia kitendo cha kuwasafirisha wanafunzi kwa kutumia gari la kuzolea takataka mali ya Manispaa ya Dodoma lenye namba za usajili SM 1303.

Hivi kwa mtu yeyote wa kawaida, ni nani hatakubaliana au haitamuingia akilini kuwa kitendo cha kuwasafirisha wanafunzi kwa kutumia gari la takataka ni cha kinyama, kinacho hatarisha afya zao na pia kukiuka moja kwa moja sheria na kanuni za usalama barabarani?

Hivi ukiachilia mbali kutokea kwa ajali hiyo iliyowapelekea watu 87 kufikishwa hospitali ya mkoa wa Dodoma wakiwa majeruhi na wengine wawili kufariki hadi Mei 30, haiingii akilini kwa mtu yeyote mwenye upeo wa kawaida wa kuelewa kuwa kuwasafirisha wanafunzi kwa gari la kuzolea takataka kunaonesha dhahiri kuwa katika Manispaa ya Dodoma sambamba na uongozi wake wote uliohusika kuwapakia wanafunzi katika gari hilo, kuna uzembe, ubadhilifu na ukiukwaji wa wazi wa kanuni za usalama barabarani?

Hivi kulikoni hata wanafunzi wasafirishwe kwa kutumia gari la aina hiyo?

Hivi wahusika hawakuona kuwa ni hasara kuhatarisha maisha ya vijana wanaotegemewa na taifa ili kubana matumizi ya pesa ambayo matunda yake pengine wangeyafaidi wao wenyewe tena kwa kificho?

Hivi michango mbalimbali inayotolewa mashuleni ikiwa ni pamoja na ule unaohusu mambo ya michezo ya shule za msingi Tanzania (UMITASHUMTA), inafanya nini hadi watoto wasafirishwe kwenye malori ya kubebea takataka hata wapatwe na ajali badala ya kupewa usafiri unaothamini maisha yao kama raia wanaotegemewa kujenga Tanzania imara la kesho? Kulikoni?

Kamanda Luther Mbuthu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, viongozi wengine na Watanzania wote, tujue kuwa baadhi ya viongozi katika nafasi zao, wana mchango mkubwa wa kukaribisha ajali na hawana budi kukodolewa jicho la ukali bila kicheko wala tabasamu.