Uzazi wa mpango na Kondomu, ukweli utumike

Kila mwaka , Desemba 1, dunia hutambua na kuadhimisha siku ya janga la UKIMWI.

Ripoti ya hivi karibuni ya Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS), ilitoa takwimu za kusikitisha kuliko miaka iliyotangulia juu ya balaa hilo barani Afrika.

Kulingana na takwimu hizo, hadi mwishoni mwa karne ya 20, watu milioni 26 walikuwa wamekwisha kufa kwa ukimwi. Hiki ni kiwango cha juu mno kuliko balaa hili lilivyokuwa miaka ya nyuma.

Licha ya kupatikana dawa ya kupunguza makali ya gonjwa hili kwa muathirika katika nchi tajiri, wagonjwa wapya milioni 5.6 wamekwisha ripotiwa duniani kote.

Watu wazima milioni 32.4, na watoto milioni 1.2 wameambukizwa UKIMWI hadi sasa. 95% ya hao, wanaishi katika nchi masikini ikiwamo Tanzania. Hizi ni takwimu zinazotisha sana hasa tunapoelewa kuwa UKIMWI unaathiri sana nchi za Afrika.

Mkutano wa Lusaka uliofanyika Septemba 12-16, 1999, ulitahadharisha juu ya hali ilivyo mbaya. Kati ya 70% ya watu wenye uambukizo, watu milioni 23.3 huishi Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara, ingawaje idadi ya watu wake ni 10% tu ya watu wote duniani.

Inakisiwa kuwa wengi wao watakufa katika kipindi cha miaka 10 ijayo. Asilimia 8% ya watu wazima wana uambukizo, hali Ulaya ya Magharibi ni 0.25%, 0.13% Afrika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati.

Tangu mwanzo wa balaa hili watu milioni 34 Kusini mwa Sahara wameambukizwa virusi. Kati yao, milioni 15 wamekwishakufa ambao ni 83% ya watu waliokufa duniani tangu kuzuka kwake.

Mwaka 1998 watu milioni 2.2 walikufa kwa UKIMWI, katika Afrika na Kusini mwa Sahara ukilinganisha na watu 200,000 waliokufa kwa vita. Wastani wa maisha ulioongezeka kutoka miaka 44, katika miaka ya 1950 hadi miaka ya 59 katika miaka ya 1990 utapungua na kuwa miaka 45 ifikapo 2005 na 2010. Vifo hivi vitawahusu vijana,wenye elimu, wenye ujuzi wa taaluma mbali mbali wakiwamo Watanzania.

Hawa ndio walikuwa tegemeo. Wengi walikuwa wazazi wenye watoto wadogo na ndio maana wamekuwa chanzo cha tatizo laidadi kubwa ya yatima watokanao na UKIMWI. 95% ya yatima milioni 11.2 ni Waafrika.

Iwapo watu 7 katika kila 10 ya wanaoambukizwa UKIMWI wanaishi Afrika kusini mwa Sahara, kila uwiano wa watoto huongezeka kwa 9 katika kila 10.

Watoto 570,000 chini ya umri wa miaka 14 wameabukizwa mwaka huu, na 90% walizaliwa na wamama wenye virusi.

Takwimu hizi zinaeleza kuwa; UKIMWI "NI JANGA LINALOIMALIZA Afrika na kuharibu maendeleo ya kiuchumi na kisisasa.

Januari 10, mwaka huu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,lilikutana kujadili kwa kina tatizo hili na kutamka kuwa "UKIMWI ni janga kubwa linaloathiri uchumi na hata usalama barani Afrika.

Kanisa Katoliki halijajitenga na hali hii. Tangu janga lianze, limekuwa likitoa huduma kupitia hospitali zake, vituo vya matibabu, maparokia, huduma zitolewazo na watawa wa kiume na wa kike, mashirika ya misaada kwa wagonjwa na huduma mbalimbali kwa matatizo hayo.

Barani Afrika Kanisa, limekuwa mstari wa mbele katika kupigana na UKIMWI na vitendo viovu vya utoaji mimba kwa umri wowote tangu inapotungwa.

Kwa sababu hiyo Halmashauri ya Familia ya Kipapa, inayoshirikiana na Mabaraza ya Maaskofu imekuwa ikishughulikia mafunzo ya familia na maadili, ikifanya mikutano na madaktari na wauguzi wanaoshughulika na vita dhidi ya UKIMWI.

Lazima tukumbuke kuwa ushiriki wa Kanisa Katoliki umekuwa wa wazi na imara ambao hauna budi kuigwa na makanisa mengine na taasisi zenye mapenzi mema.

Tutambue mifano mizuri ya kujitoa na ukarimu wa watu wengi tuliowaona huko Uganda, Kenya, Tanzania, Ghana, Cote d' Avoire, Benin, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Bukina Faso kwa kuwatembelea wagonjwa majumbani mwao.

Wakati Kanisa na jamii nzima wanalia na janga hili ambalo linatishia, kasi ya taasisi kadhaa zinazohamasisha uzazi wa mpango wa matumizi ya madawa na utoaji mimba imekuwa ikiongezeka.

Sisi, hatukatai hoja ya kuwapo kwa uwiano mzuri wa idadi ya watu na uwezekano wa kuwapatia huduma wanazostahili kijamii ili kuishi maisha yenye unafuu pasipo kubeba mzigo tusio uweza.

Tunachokipinga, ni njia chafu na zisizo sahihi ambazo mara kwa mara taasisi hizo na hata baadhi ya viongozi wa serikali wamediriki kusimama kidete kuihamasisha jamii bila kujua kuwa njia hizo ni sawa na kukata matawi ya mti badala ya kung’oa shina ili kuangamiza mti huo.

Baadhi ya njia zinazohimizwa kutumika kama njia ya kupanga uzazi, ni matumizi ya vidonge vya majira, vitanzi na matumizi ya kondomu ambayo yanahimizwa kwa gharama kubwa bila hata kuzingatia athari zake mbaya ama, kwa kutokuzijua, au kwa kuzificha.

Ni dhahiri kuwa njia hizi za kupanga uzazi zina madhara yake kwa jamii husika hususani wanawake.

Kwa wanaoamini kuwa uhai wa binadamu huanza katika muunganiko wa yai la mama na mbegu ya baba, njia yoyote ya uzazi wa mpango inayoharibu ukuaji wa mtoto (mimba)haiwezi kukubalika wala viua mimba vyovyote vinavyotumika kama njia ya kudhibiti idadi ya watu.

Tafiti nyingi zimeonesha kuwa wanawake wengi wanaotumia vidonge(OC’s), wamo katika hatari kubwa ya kupata mimba nje ya tumbo la uzazi ikilinganishwa na wasiotumia kwani vinaongeza uwezekano huo unaohatarisha uhai wa mama.

Kibaya zaidi, tunacholaani, ni pale hata matumizi ya kondomu yanapohimizwa katika jamii hadi kufikia watoto wa shule za msingi kuomba watengenezewe za saizi yao.

Na hii inahimizwa kama njia ya kuepuka ukimwi na mimba zisizokusudiwa.

Hivi ni nani anayeweza kutoa ushahidi wa uhakika wa kisayansi na wa moja kwa moja kuwa kondomu huzuia ukimwi?

Sisi tunasema, namna yoyote ya kuzuia uhai au kusababisha uhai kuuawa, haikubaliki ndani ya jamii adilifu na yenye kumcha Mungu bila kujali itikadi, imani, msimamo au mtazamo wa mtu.

Taarifa za kweli juu ya kazi, mwenendo na athari zitokanazo na matumizi ya vidonge na vyote vitumikavyo kupanga uzazi ni lazima ziwekwe wazi kwa watu ili wenyewe waamue kutumia ama kutokutumia ili mradi wanajua faida na hasara zake.

Endapo jamii itazidi kuambiwa juujuu kwa propaganda tupu, bila ukweli wa njia za kupanga uzazi na kuepuka ukimwi, ipo hatari jamii yetu ikawa inapigwa na maadui wawili kwa wakati mmoja, yaani ukimwi na 'abosheni' za kimya kimya zinazofanyika kwa kisingizio cha kudhibiti idadi ya watu.

Hivi ni nani asiyejua kuwa njia sahihi inayostahili kufundishwa ili kupanga uzazi ni ile ya asili yenye kuzingatia mambile na njia pekee ya kujiepusha na ukimwi, ni kukana zinaa na wala kutohimiza matumizi ya kondomu.

Katika kudhibiti ongezeko hili la watu,na kuepuka ukimwi, ukweli utumike.

Nakupongeza Happiness kwa kuwatahadharisha Wakatoliki

Ndugu Mhariri,

Ninaomba nafasi kidogo katika gazeti lako la Kiongozi hasa kwa kuelimisha Umma wa Watanzania.

Katika toleo la tarehe 22-28 Aprili, 2000, Ukurasa wa Nne, niliyasoma maoni ya Mkristu mmoja kwa jina la HAPPINES ALOYES wa Babati Arusha. Yeye katika Maoni yake, alisema kuwa anakerwa sana na mienendo ya madhehebu ya Kipentekoste.

Hii ilikuwa hasa kwa kuwa baadhi yao hutoa mahubiri ya kujisifu na pia kulikashifu Kanisa Katoliki.

Mimi binafsi ninampongeza sana kwa msimamo alio kuwa na o kwa kuwa amekuwa msikivu wa Neno la Mungu.

Akajaliwa kutambua makwazo haya,.Kwa hakika huu ndio mwanzo wa mafedhehesho kwa Mkristuomwenye imani thabiti kwa Mungu na kanisa lake. Kutokana na hayo aliyoshuhudia, namshauri asome Injili ya Mathayo Mtakatifu 24:3-28, ili azidi kuitambua imani ya kweli na kuwafahamu manabii wa uongo. Mpendwa Happines, katika Kristu kumbuka kuwa Injili sasa inahubiriwa ulimwenguni kote ili kuwa shuhuda kwa mataifa yote wanao mwamini Yesu ili utumie Neno la Yesu.

Kwa sura hiyo niliyokuonesha uisome, utatambua kwa ufupi tu kuwa Imani yoyote inayompinga Baba Mtakatifu, haikuanzishwa na Yesu, Kristu maana Baba Mtakatifu sasa ni wa 264 tangu Mtume Petro.

Mtume Petro alipokufa alizikwa kule kule, na hata kaburi lake laonekana hadi leo, baada ya hapo Mtakatifu Lino alifuatia kushika wadhifa huo.

Hivi hivi, kila anayekuwa Askofu wa Roma kwa haki ni Halifa wa Mtume Petro na Mkuu wa Kanisa zima la Yesu Kristu duniani kote.

Ushauri kwa Wakatoliki wenzangu ni kuwa mikutano yoyote isiyokuwa na Baraka za Kanisa ni batili na wala wasiishiriki au kushindana na washiriki wala waandalizi wake kiimani isipokuwa, kwa ruhusa ya paroko wa eneo hilo au askofu Mahalia.

Wakristo Wakatoliki tukiwasikiliza kweli viongozi wetu wa kiroho Makwazo haya tutayashinda maana tuwasikilizapo wao tunamsikiliza Yesu Kristu mwenyewe aliyewaweka hao.

Lakini, tujihadhari tusije hukumiwa kwa kutambua kuwa sisi ndio hatukuwajibika katika kuishuhudia imani yetu kwa ujasiri na kwa upole bila woga wowote ule kwani imani yetu haipingani na Neno la Mungu hata kidogo. Jumuiya ndogo ndogo za Kikristu ni mfano mzuri wa kumtangaza Kristu Yesu kwa kuishi maisha Matakatifu yanayompendeza Mungu kwa kuungama dhambi na kukusudia kuziacha kabisa.

Kwa kumpokea Yesu wa Ekaristi mara kwa mara, tutayaelewa mapenzi yake.

Ingawaje imani nyingine haitambui Yesu wa Ekaristi, ni wajibu wetu kuwafundisha wote ingawa kweli ni vigumu kwa asiye Mkatoliki kuweza kujijua na kukiri Imani Katoliki ila kwa nguvu ya Yesu wa Ekaristi kila tumpokeapo na kutembea naye na kukutana na hao wanaoipinga Imani Katoliki ndipo watakapo wezesha kuifahamu.

Tumsifu Yesu Kristu

Pascal V. Lyatuu

Moshi