Watoto wasiajiriwe kucheza ngoma katika kampeni

Ajira kwa watoto wadogo ambao hawajatimiza umri wa utu uzima, ni jambo linalopigwa vita kama kampeini ya dunia nzima kwa kuwa inawaathiri watoto kiafya na kisaikolojia na pia, haitoi kipaumbele kwa maendeleo ya watoto hao kwa siku za usoni.

Waajiri hao haramu wanajidai kuwa wanawasaidia watoto hao kwa njia ya ajira ili waweze kujikimu katika mahitaji yao hasa baada ya kuonekana, ama wazazi wao hawajiwezi, au basi kwa hila zao za kilaghai, waajiri wameweza kuwarubuni na kuwapeleka katika ajira za kazi mbalimbali zikiwamo zile za mashambani, na zile mbaya za utumishi wa nyumbani maarufu kwa jina la House Girl.

Kwa kweli ajira hizo ni haramu kwa kuwa si tu kwamba zinawaumiza watoto kwa kuwafanyisha kazi kwa masaa zaidi ya 14, ukiachilia mbali yale 8 ya kawaida kwa wafanyakazi wa kawaida kwa siku.

Licha ya hali hiyo bado kipato kitokanacho na ajira za watoto wadodo sio tu kuwa ni cha kuhurumia, bali pia ni cha kusikitikia sana kwa sababu licha ya hali ngumu ya maisha hivi sasa, lakini eti mwenye kima cha juu cha mshahara, ni yule anayepata mshahara wa shilingi 8000/= hadi 10,000/=, kwa mwezi.

Ni mfanyakazi gani katika nchi yake, anayefanya kazi zaidi ya masaa 14, halafu analipwa mshahara wa shilingi 8000/= kama malipo yake halali kwa mwezi?

Hivi serikali, taasisi navyama husika vikiwamo vya siasa, hamuoni hali hii ili mshirikiane na jamii nzima kuikemea? Au basi kama hamjui kwamba ipo, tamkeni waziwazi ili jamii iwajue kuwa bado mmelala fofofo.

Na kama mnaijua kuwa ipo, kwanini msiitamkie jamii ijue wazi kuwa mpo ili kujinufaisha wenyewe na familia zenu zisizokumbwa na masaibu hayo huku mkiwaacha wanyonge hao tunaoita taifa la kesho, wakiteseka huku nyie mnazidi kuota vitambi ambavyo vinakaribia kutoboa shati?

Tunasikitika kuwaambia kuwa kiwango tulichokitaja hapo juu, ni cha mshahara wa house girl aliyesoma na mwenye uzoefu wa kutosha na kazi nzuri. Bado hatujamsemea yule house girl au mtoto aliyeajiriwa kwa kazi nyingi ngumu na akipata mshahara wa shilingi 2500/=

Hivi watoto hao ndio jamii ya Watanzania kila leo inaimba kuwa ni taifa la kesho wakati wengine wanatumikishwa kwa matusi hata ya nguoni na vipigo juu, ndio hao wanaoambulia mshahara wa KULA na KULALA kwa mwezi.

Je, inaingia akilini unapomwambia mtu kuwa malipo hayo ya kula na kulala pekee, au shilingi 2500/= hadi 10,000/=, yana mlengo wa kumjenga mtoto ambaye ni tegemeo la taifa letu la kesho wakati hawapewi nafasi ya kwenda walau shule za chekechea wala kufundishwa namna ya kusuka mkeka wenyewe?

Kinachotusikitisha zaidi, ni pale tunaposhuhudia baadhi ya watoto hao, badala ya kuhamasisha kushiriki katika masuala ya maendeleo kwa kadri ya maelekezo na uwezo wa jamii wakiwamo wazazi wao, sasa karibu kila mkutano wa wanasiasa utawakuta watoto wamehamasishwa kuwahamasisha wananchi kukusanyika pale ili kucheza ngoma mbalimbali zikiwamo za mdundiko, sarakasi na maagizo na ngonjera.

Hivi vyama vya siasa vinavyofanya hivyo, hata wagombea wake hawaoni aibu wanapowatazama mbele ya jukwaa wakicheza ngoma na miaka yao 9, 10, kisha wakapanda na kusema wanakemea ajira za watoto?

Hivi kwanini wanasiasa wanawaonesha Watanzania nyumba, kisha wanawadanganya kuwa hiyo ni gari?

Hivi wanasiasa wanaweza kutudanganya kuwa watoto wale wanaofanya michezo kwenye mikutano ya siasa huwa ni wakereketwa au wanachama wa vyama ijulikane bayana kwamba wanawashirikisha watoto katika siasa au wamerubuniwa na kupotezewa muda wa kufanya hata marudio ya masomo au kazi nyingine ambazo zingewasaidia?

Ni nani anayeweza kuudanganya umma wa Watanzania kuwa watoto wale wanapokuwa wanasafirishwa hata nje ya mikoa kufanya mazoezi na hata kuhamasisha mikutano hiyo ya viongozi na pengine kwenye kampeini kama ilivyo kuwa katika Uchaguzi Mkuu wa 1995, kuwa huwa wanalipwa allowance za safari, kama sio kuwapeleka kula ubwabwa na kucheza ngoma bila malengo wala matumaini ya kesho na kesho kutwa na kisha kuwaachia shilingi 2000/=?

Tunadhani umefika wakati wa viongozi na vyama vya siasa kuanza kujisafisha makosa toka katika vyama na majukwaa yao kwanza kabla ya kumwaga sera zinazokwenda kinyume na matendo ya vyama wanavyoongoza.

Kutoa ajira kwa watoto ambazo hata baada ya malipo waliyosotea kwa wiki nzima au mwezi, hayawatoshi kula chakula cha mchana na kujizuia kwenda kuvizia kwa jirani au kujirahisisha kwa kuuza utu wao hasa hawa watoto wa kike, kunaashiria kuwa kiongozi wa chama hicho atakaposhika madaraka, suala la kuwajali watoto, kurekebisha ajira na hali za wananchi kwa ujumla, itakuwa mbaya mithili ya kuruka maji na kukanyaga tope.

Tunasema umefika wakati muafaka ambao badala ya jamii hususan vyama vya siasa kuwatumia watoto wenye maisha mabaya kwa kuwatumikisha ili kujipatia umaarufu huku wakiwapa ajira ambazo ni sawa na maiti anayetembea ili wawakusanyie watu katika mikutano yao, wajue ajira hizo kwa watoto, ni unyama usiomithilika wanaotendewa watoto wetu na viongozi tunaowategemea.

Urasimu wa Benki za Posta unatuathiri wateja

Ndugu Mhariri,

PINDI tukiwa duniani adha na misukosuko lazima viwepo. Lakini, mambo mengine huwepo kutokana na kusababishwa na watu wengine kutokana na harakati au utendaji wao mbovu.

Maudhi yafanywayo na Benki ya Posta, ni kutokana na kujiamini mno na hivyo, kutojali muda, maslahi wala kutaka kuepusha adha kwa wateja.

Usumbufu upo kote katika kuweka; kuchukua kadhalika kubadilisha hela za kigeni. Unapotaka kuchukua hela katika benki ya akiba ambazo umeziweka wewe na unavithibitisho vyote, inabidi upitie madirisha matatu.

Dirisha la kwanza, utachukua fomu na ukishajaza, unaipeleka dirisha la pili ambapo utachukua nusu saa au zaidi.

Hapo, karani atapekua kitabu toka mwanzo hata kama umechukua hapo hapo mara nyingi nyingi tu, bila tatizo.

Kisha unangoja kwenye benchi kwa muda mwingine wa nusu saa au zaidi huku ukisota kungojea kuitwa.

Mimi mwenyewe kwa mara mbili nimekuwa nikibadilisha Paundi za Kiingereza.

Niliambiwa na ndivyo ilivyokuwa kuwa makumi yasiyotimia mia hayalipwi. Maana kwamba hesabu inapoangukia chini ya mia huandikwa lakini haulipwi hata kama unazo za kuchenji. Iwapo hazilipwi kwa nini zinaandikwa?.

Benki Kuu ya Posta mambo ni kama yalivyo kwenye hizi nyingine.

Nilikatwa hela za akiba yangu ya zamani katika kitabu changu na hivyo hawala ilijazwa baada ya siku tisa toka kukatwa hela zangu, bila hata maelezo. Je, kufanyiwa hivyo mteja, ni sawa?

Ushauri wangu ni kwamba, inafaa Benki ya Posta mfikirie adha nilizozitaja mimi na wateja wengine wa aina yangu ili mtututolee ufafanuzi juu ya hayo niliyoyataja kwa manufaa ya wateja, benki yenyewe na umma kwa ujumla.

 

 

Mzee Severin S.M. Ngunga

Merry Water Ltd,

P.O.Box 7472

Dar es Salaam

Majibu kwa Samsoni Mushy wa Fire Gospel International Church

Ndugu Mhariri,

Nakusalimu kwa Jina la Bwana Yesu.

Rejea maswali yako uliyoyauliza kupitia gazeti la Kiongozi la tarehe 8/7/2000.

Kwa upande wangu, nitakujibu swali la kwanza kwa sababu maswali mengine ni ya binafsi, maana mtu akijitangazia kuwa ameokoka halafu hatendi matendo ya wokovu, hakubaliki mbele za Mungu isipokuwa kwa sababu alishajitangaza, basi itaonekana kuwa Walokole ndivyo matendo yao yalivyo lakini kumbe, sivyo.

Katika swali la kwanza uliuliza, ni kwanini Walokole hawatumii Sala ya Baba Yetu?

Jibu ni kuwa sio lazima kuikariri sala hiyo kama wanavyofanya watu wengine isipokuwa, Yesu aliwafundisha wanafunzi vitu muhimu wanavyopaswa kuvifanya katika maombi kupitia sala hiyo.

Vitu hivyo ni;

a) Baba Yetu Uliye Mbinguni, Jina Lako Litukuzwe Ufalme Wako Uje.

kifungu hicho kinalenga kumuinua Mungu na kulitukuza Jina lake na ufalme wake Mkuu.

Hivyo Walokole wanatekeleza kifungu hicho kwa mapana zaidi pale inapofikia kipindi cha kumsifu Mungu na kumpa utukufu (ndani ya ibada)Filipi 4:4-6.

b) Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama huko mbinguni.

Kifungu hicho nacho kinalenga kujishusha na kumpa Mungu nafasi ya kufanya atakalo juu yetu.

Walokole wanatekeleza kifungu hicho katika kipindi cha kujitakasa na kujishusha mbele za Mungu. Mathayo 21:21-22, Luka 18:9-14.

c) Utupatie riziki yetu ya kila siku utusamehe deni zetu. Kifungu hicho kinalenga kumuomba Mungu juu ya mahitaji yetu ya kila siku na kutusamehe dhambi zetu.

Kinatekelezwa na Walokole kifikapo kipindi cha mahitaji, ambacho kila mtu anapata nafasi ya kumuomba Mungu atakacho Marko 11:24-26.

d) Na usitutie majaribuni lakini utuokoe na yule muovu, kwa kuwa ufalme ni wako na nguvu na utukufu hata milele. Kifungu hicho kinatekelezwa ifikapo kipindi cha kushindana na nguvu za giza na kumkaribisha Mungu aweze kutuongoza na kutuokoa na vishawishi. Efeso 6:11-18.

Hivyo ndugu Nabii unapo uliza maswali, uwe unayaangalia kiundani kabla hujayafikisha kokote.

Yesu hakufundisha kukariri labda tazama utofauti Mathayo 6:9, Luka 11:1-4. Hivyo basi kama Yesu angehitaji watu kukariri basi usingeona tofauti hizi bali angejitahidi kuona haibadiliki ili watu wasipingane katika usomaji wa sala hiyo.

Hivyo kutokana na hilo Walokole huwa wanasali sala hiyo kwa mapana na si kwa kufanya mchezo bali usali na kuomba kwa mzigo na kwa kuipa uzito unaostahili sala hiyo.

Kama una maswali zaidi endelea kutuma na Yesu Kristo atakujibu.

Naomba uelewe tu sasa hivi si wakati wa kushambuliana kimadhehebu, bali ni wakati wa kuwaelimisha watu wengine ambao wako nje kabisa na Ukristo.

 

Bwana akutie nguvu

 

 

Dominic Pius Mapima

Injili kwa Wote

S.l.P 61584/1717

Dar es Salaam.

TIPC Isitusahau watu wa kawaida

Ndugu Mhariri,

TUME ya Taifa ya Uwekezaji yaani Tanzania Investiment Promotion Centre tangu iliyoteuliwa na Rais imekuwa ikifanya kazi kimya kimya.

Labda ni kwa kuwa ni tume ya kitaalam sana sijui. Lakini hata hivyo ni yetu. Inabidi Umma uelewe ni kazi gani mpaka sasa imekwishafanya.

Tunasikia tu vitu kama Soko la Hisa au Mamlaka ya Soko la Mitaji na Dhamana mambo ambayo yanaonekana kujulikana na kuwahusu watu wasomi na wenye uwezo wa juu kipesa peke yao.

Tungetazamia kuwa na chombo kinachojishughulisha na wawekezaji wadogo wadogo Mfano: "Smaall Enterprenius Promotion" ili watu wenye biashara ndogo ndogo; mmojammoja au kwa vikundi, wawekeze mitaji yao huko na ikiwezekana, wawe na benki yao hata kama itaitwa Benki ya Walala Hoi, potelea mbali.

Hii itawasaidia hata akinamama lishe na watu wengine kupata mikopo kuliko kwenda kwenye michezo ya upatu ambapo hatimaye, hujikuta wanazozana kwa kuibiwa fedha zao.

Tume pia kwa kupitia chombo hicho, itaweza kuweka utaratibu wa kuwaelimisha na kuwapa wataalamu wa kufuatilia miradi yao pale inapokuwa lazima kufanya hivyo.

Katika mabadiliko kama haya ya siasa, nchi yetu iliyotawaliwa na serikali ya chama kimoja kwa muda mrefu, dira ikiwa ni Ujamaa na Kujitegemea na sasa Serikali ya vyama vingi na uchumi huria, kama hatutakuwa waangalifu ni dhahiri na haraka, tutajenga tabaka mbili za watu.

Tabaka moja dogo la wafanyabiashara wasomi ambao watatajirika sana na kuacha nyuma tabaka kubwa la wananchi wakiwa maskini.

Hii ndio matokeo ya kujenga Ubepari katika nchi na hatimaye ni kuzoza watu wa kawaida hawataweza kuvumilia kuona wenzao wanaishi kifahari na wao wanahangaika huku na kule kutafuta riziki bila kusaidiwa.

Ni vema tuwe waangalifu ili mabadiliko haya ya Siasa na Utawala bora yaendane na mabadiliko ya uchumi na hali bora ya mashina kwa Watanzania wote.

E.G. Msuguru

S.L.P 45471

Dar-Es-Salaam