Moyo wa kujitolea ni muhimu kwa Watanzania

MARA baada ya nchi yetu kujipatia uhuru, viongozi na hasa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, walitujengea moyo wa kufanya kazi, hususani za kujitolea ili kulijenga taifa kwa nguvu zetu.

Kulikuwa na shughuli mbalimbali zilizofanyika kwa moyo huo kama vile, ujenzi wa madarasa, nyumba za walimu, zahanati, hospitali mabarabara na vingine vya namna hiyo.

Raia na hasa vijana walilelewa katika msingi wa kujitolea na hiyo ndiyo maana hata kukawapo na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).

Mipango mizuri sana ilifanyika na watu wakazifanya shughuli nyingi chini ya mpango huo wa kujitolea katika maeneo wanayoishi; kwa hali na mali.

Hiyo ilitokana hasa na Watanzania kuijua hali halisi ya nchi yetu kiuchumi. Kila raia alielimishwa na akafahamu ukweli kuwa nchi yetu ni maskini, na hivyo hatutafika popote kimaendeleo bila kuwa na moyo wa kujitolea. Moyo huo wa kujitolea ukajengeka pia katika shida za dharura hasa zile za maafa.

Ulipotokea uharibifu katika maeneo yetu hasa ya vijijini, wananchi walialikana chini ya uongozi wa kijiji na hivyo kuweza kurekebisha pale ambapo mambo hayakuwa sawasawa.

Uharibifu wowote uliojitokeza, ulishughulikiwa mara moja na hivyo mambo yakaenda kwa utaratibu kama kawaida.

Lakini siku ya leo mambo hayo yamerudi nyuma kabisa na karibu hakuna tena ule moyo wa kujitolea; sehemu nyingi na kwa watu wengi nchini.

Gazeti la NIPASHE, la Jumatano, Julai 12, mwaka huu, kuna habari isemayo kuwa Wanafunzi wakosa masomo miezi tisa, kisa, madarasa yao kuezuliwa mapaa. Kwanza tunawapa pole wanafunzi hao kwa maafa hayo ya kuharibikiwa shule.

Tunasema hiyo ni habari ya kusikitisha na ya kutisha kabisa. Tena, ni ya aibu, na kinyume cha utamaduni tuliojijengea kwa miaka mingi.

Tunasema kuwa ni jambo la kutisha kwani kwa wanafunzi wetu kukosa masomo kwa muda wa miezi tisa, ni jambo zito hasa ukitilia maanani kwamba kila saa ya mwanafunzi kuwemo darasani ni ya muhimu wa namna yake.

Inampasa mwanafunzi apate masomo katika mazingira mazuri. Lakini, ikiwa mwanafunzi atasomeshwa chini ya mwembe au katika darasa linalovuja kutokana na paa kuharibiwa na kimbunga, kweli mambo ni magumu.

Kwa ukubwa sana hatuwezi tukategemea wanafunzi waanaosoma katika mazingira kama hayo, wataweza kufanikiwa kimasomo ipasavyo.Kuhusu tukio hilo la Shule ya Msingi ya Mloda, kata ya Makang’wa, wilaya ya Dodoma Vijijini, tunajiulliza, ni kweli sehemu hiyo ina uongozi unaofaa au sivyo?

Inakuwaje kwa muda wa miezi tisa wanafunzi wakose masomo wakati mahali hapo pana Waratibu wa Elimu na maafisa mbalimbali wa elimu.

Tunatambua kuwa hali ya wananchi kule kiuchumi siyo nzuri, lakini, hata hivyo tunasikitika kusema kuwa uongozi wa kata, wa tarafa na hata ule wa wilaya umezembea kabisa suala hilo la kurekebisha hali ya shule hiyo.

Pia tunajiuliza huyo Mbunge wa sehemu hiyo anafanya kazi gani kuhusu maendeleo ya elimu katika jimbo lake? Je, wananchi watakuwa kweli na moyo wa kumpatia kura zao hapo Oktoba 29 baada ya kuonesha uzembe kama huo?

Tunarudia kusema kuwa jambo hilo ni la aibu sana kwani inaonekena kuwa viongozi wa sehemu hiyo hawatambua wajibu wao hasa katika shida kama hizo.

Huo ni mfano mmoja tu kati ya mingi inayotokea hapa na pale.

Kwa vile kama tulivyosema hapo mwanzoni hakuna moyo wa kuwajibika na kujitolea katika nchi yetu, kuna shule na majengo mengi ya umma ambayo pengine yangehitaji matengenezo ya haraka, lakini yanaendelea kuharibika kama vile hayana mwenyewe. Ni kweli sisi Watanzania kwa ujumla hali zetu kifedha siyo nzuri, lakini papo hapo tunao ule utajiri wa nguvu ya kufanya kazi. Tatizo kubwa hatupendi kujituma wala kujitolea na hivyo kufanya kazi kwa sifa ya taifa letu, labda kidogo kwa ajili ya faida yetu binafsi.

Kibaya zaidi, kwa wananchi wengi siku ya leo hakuna moyo wa kufanya kazi kwa ajili ya kujenga taifa, ingawaje tunahimizwa kwamba taifa letu litajengwa hasa na watu wenye moyo wa uzalendo na kujituma.

Tunapenda kutoa rai yetu kwa viongozi hasa wabunge, wakuu wa wilaya, tarafa na kata, wakuu wa mashina wawe karibu au katikati ya watu waweze kuona matatizo ya watu na watoe msaada wa hali na mali.

Viongozi hao wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuhimiza utendaji kati ya wananchi.

Kiongozi ni yule anayekwenda mbele na watu wanamfuata nyuma yake. Lakini kama kiongozi anafifia kabisa na hivyo kukaa mbali na wananchi, hataweza kamwe kuongoza ipasavyo.

Tunahitaji viongozi wanaoona shida za wananchi na wanakuwa nao bega kwa bega katika kuziondoa.

Tunatumaini tunapoelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, ni vema tunakalifikiria jambo hilo. Tuwapatie kura viongozi ambao kweli watakuwa na wananchi kwa ukaribu zaidi huku wakijua matatizo yetu na kutusaidia katika kuyatatua.

Kwa upande wa wananchi, tungependa sana kuona moyo wa kujitolea unafufuliwa na kuendelezwa tena katika taifa letu. Inatupasa kufanya kazi nyingi za kujitolea kwani bado hatuna pesa za kutosha.

Tuwe na uchungu na nchi yetu ambayo kweli ni maskini. Tusingojee kila kitu kutoka Serikali Kuu kwani nayo ina mambo mengi ya kufanya kitaifa. Kuna mambo mengi ambayo yako chini ya uwezo wetu na tunaweza kuyafanya na kuokoa pesa nyingi.

Sasa nii wakati mwafaka wa kufanya kazi mbalimbali siyo kwa ajili ya kupata malipo, bali hasa kujenga jina katika taifa letu kama wafanyavyo wenzetu walioendelea ambao wako tayari kutoa nguvu zao kwa ajili ya kujenga majina.

Nasi pia tuone ni sifa ikiwa tunaweza kufanya kitu fulani kwa ajili ya jumuiya na hivyo majina yetu yakaingia katika historia ya Tanzania.

Kibakwe: Chagueni Mchumba anayefaa

Ndugu Mhariri,

Naona aibu kukusumbua unitafutie nafasi katika gazeti lako ili niseme machache yanayonisumbua na kutukera sisi wakazi wa Jimbo la Uchaguzi Kibakwe.

Tunasikitika na kupenda kuuambia umma wa Watanzania muwe tayari kukabiliana na vitisho, kashfa, matusi, kero na kejeli za kila aina zinazotolewa na wana CCM na viongozi wao, kipindi hiki tunapoelekea katika Uchaguzi Mkuu.

Tunaomba mzivumilie popote mpakapofikwa nazo(hasa wapinzani), hizo ni kelele za chura tu. Mambo hayo yanayofanywa na wana CCM na viongozi wao tunashindwa kuyaelewa hatma yake huko mbele itakuwa nini.

Malumbano ni malumbano, lakini, inapofikia hivi tulivyo, wakazi wa Jimbo hili tunaanza kuwa na wasiwasi kuwa huenda hata jimbo letu likakumbwa na shetani aliyefika jimbo la Uchaguzi la Bahi, kati ya CUF, na CCM.

Ee Bwana. Tunakuomba utukinge na balaa hilo lisitutokee na sisi. Baadhi ya wanachama na viongozi wasioiva kisiasa wamechukulia upinzani kama visa na vita.

Tutaendelea kusema kweli daima ili tujenge nchi yetu inayodidimia kimaendeleo kila kukicha; hatutaogopa kusema ati kwa sababu ya uhusiano na mtu fulani.

Kipindi cha kuchagua, ‘mchumba anayefaa’ kwa wanajimbo wa Kibakwe, ni sasa.

Tunamtaka mchumba ambaye kwa kipindi kifupi cha maisha yetu hapa duniani ndiye atakayetusadia katika matatizo na si awe mzigo kwetu baada ya kumchagua. Muogope anayetafuta nafasi ya uongozi ili apate kiburi cha kukuonesha ugali kwa mguu ati kisa, "ndoa" inamlinda.

Hiyo, haitatufaa. Mtu wa namna hiyo, muogopeni kama NJAA. Kuchagua kiongozi kutokana na ITIKADI na wala si sera zinazotekelezwa.

Tofauti na hayo, ni sawa na kuisaliti familia yako utakayoizaa. Kwani ni hapo utakapoikuta nyumba iliyokosa matumaini kama lilivyo jimbo letu ambalo linateseka kwa shida na matatizo tele.

Kwa ujumla Kibakwe hatuna matumaini ya kupata maendeleo milele kama hatutaubadili uongozi wa Jimbo uliopo.

Hatuna madawati mashuleni pamoja na michango yote tuliyoitoa. Hakuna madawa hospitalini, majosho hakuna, barabara ni mbovu pamoja na propaganda za CCM kuwa zimetengenezwa asilimia 10.

Kodi na wafugaji zinazorudi vijijini hatujui zinafanya nini pamoja za taarifa nzuri kuwa yamekarabatiwa bila dawa? Ng’ombe utawaogesha maji?

Tulipoanza kuhoji yote hayo ambayo ni ya uongo, limelipuka la ugawaji wa mipira ya michezo vijijini ili kuinua sekta ya michezo.

Shida ya wananchi siyo burudani, ni kuondoa kero zinazowakabili, kero zitakazowapa unafuu wa maisha.

Wanajimbo tujiulize ‘kama mchumba anafaa’ anahofia nini mpaka aanze kugawa zawadi za aina hii tena wakati tukielekea katika uchaguzi ambao hata yeye anagombea?

Mtu au mchumba asiyekuamini mpaka akupe zawadi kabla ya kufanya kazi, hakufai. Hivi kwanini wanajaribu kutubembeleza na kununua kura zetu kwa ubwabwa, pombe, pesa, mipira n.k.

Hilo wanajimbo mmeliona, kataeni msiwape kura watawasaliti tena.

Tunashukuru wapinzani kuwa, "Mwenyezi Mungu" ametupa moyo wa kuvumulia matusi na kashfa zao na pia tunamshukuru ametukubali tuive kisiasa na kutuepusha kuwajibu kwa matusi.

Tumechoshwa na tuliyofanyiwa Kibakwe na tunaahidi tutasema ukweli yafahamike yote tunayotendewa huku tukiendelea kuienzi amani na utulivu aliyotuachia Marehemu Baba wa Taifa.

Kiongozi, kwa nini unadiriki kuwaambia watu wako mambo ambayo hujawafanyia? Siri ya uongozi ni kuwa mkweli Kiongozi ni yule anayewajali kipindi cha shibe na njaa. (asomaye akumbuke).

Kibakwe na Rudi Hospitali tunahitaji madawa kwa wingi na gari za kubeba wagonjwa ili yatusaidie mafukara na wakesha hoi kuokoa maisha ya ndugu zetu.

Jimbo letu ni la mwisho katika maendeleo pengine hata kitaifa, hakuna lolote la kujifunza ndiyo maana hata Rais alifika Kingiti tu, akashindwa kufikishwa jimboni ambapo ni umbali takribani Km 7 tu.

Jimbo limebaki na uongozi wa kubabaisha na linafanana na mtoto yatima, akiitiwa ugali kila nyumba anakula. Tutakuwa katika hali hii mpaka lini

Viongozi hao hao waliofanya Jimbo lifukarike kiasi hiki kimaendeleo wameanza kuja kuomba kura zetu kwa zawadi za pombe, mabati, pesa huku wakiwa wameweka na kutembea mikono nyuma kama ishara ya utii kumbe ni wasaliti wasioelezeka na lugha nyepesi.

Hatuwataki na hatuwahitaji tena viongozi waliotukimbia katika kipindi cha njaa 1999/2000.

Tukumbuke sifa kuu ya kiongozi bora na mwema ni yule mwenye kumjali na kumpenda kwa moyo wote, yule aliyemchagua na kumpa kura. Hilo litawauma sana linaowagusa lakini lazima tuseme ukweli tutafanyaje? "Mtajua ukweli nao ukweli utawapeni uhuru," (Yohana 8:32)

 

Damasus G. Mtalaze

Box 114, Kibakwe

MPWAPWA