Polisi katika vituo vya uchaguzi; wajua wajibu wao?

WAKATI taifa linaelekea Uchaguzi Mkuu wa Pili wa Vyama vingi vya Siasa Oktoba 29 mwaka huu, vyombo husika na jamii kwa jumla havina budi kufumbua macho na hata kutumia Uchaguzi wa mwaka 1995 na chaguzi ndogo zilizofuatia kama kioo na hivyo kurekebisha na kuondoa makosa yaliyojitokeza ili yasijirudie.

Moja ya matatizo yaliyojitokeza katika Uchaguzi wa 1995, ni upya wa dhana ya demokrasia ya vyama vingi kwa wananchi walio wengi.

Hii inatokana na ukweli kuwa, wananchi waliojishirikisha katika harakati za kudai uhuru kwa takribani miaka 30 ya nyuma, walikuwa wachache mno.

Licha ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukiri kuwa ililemewa katika maeneo kadhaa; kama kuchelewesha kwa masanduku na makaratasi ya kupigia kura vyama vyenyewe vya siasa kikiwamo Chama Tawala, havikuwa tayari vimetambua umuhimu na uzito wa kazi iliyowakabili hadi wanaingia ulingoni.

Katibu Mkuu wa CCM Bw. Philip Mangula, hivi karibuni alikiri hilo wakati akizungumza katika Mkutano wa Nane wa Kitaifa kuhusu hali ya kisiasa Tanzania ili kusawazisha uwanja wa ushindani wa siasa uliofanyika jijini Dar-Es-Salaam.

Tunaipongeza Serikali kwa kuhimili jazba kubwa la vyama vya siasa ambavyo vingi pamoja na wafuasi wake vilikuwa nje kabisa ya wigo na taratibu sahihi za kinyang’anyiro cha Uchaguzi.

Kwa kuzoea na hata kubweteka katika mfumo wa chama kimoja, bado umma haukuwa unajua umuhimu wa uchaguzi huo katika kusukuma gurudumu la maendeleo na ndiyo maana yeyote aliyechaguliwa, kwao alikuwa ni sawa; bora liende.

Kwa mujibu wa Taarifa ya Tume ya Uchaguzi kwa majuma mawili ya mwanzo Agosti hadi Septemba, ni asilimia 26.7 tu ya watu waliotarajiwa, walikuwa wamejiandikisha kupiga kura.

Hali hii ililazimu muda kuongezwa huku viongozi wa kata na vyombo vya habari kuongeza sauti kupigia kelele umuhimu wa kujiandikisha hata sasa wakafikia milioni 8.9.

Ni kweli uliojidhihirisha wazi kuwa wakati wa kampeni, ama vyama havikutumia; au vingi havikuwa na Ilani wala Programme za kunadi kwa wananchi ili wavichague.

Kilichojitokeza zaidi ni vyama kung’ang’ania dola na kwenda Ikulu. Hiyo ikageuza kampeni kuwa viwanja vya matusi na vitisho.

Mangula amesema hiyo ndiyo ilikuwa agenda ya kujikusanyia kura.

Tunalaani mtindo huo uliopelekea vyama vya upinzani karibia vyote, kukisakama kwa matusi Chama Cha Mapinduzi.

Pia tungependa safari hii kupitia wagombea wake, CCM isitishie wapiga kura wakati wa kampeni mbalimbali kuwa wapinzani wakichukua madaraka, Tanzania itageuka iwe Rwanda, Burundi, Kongo au Kosovo kwa kukosa amani.

Tunasema Uchaguzi bila Ilani inayokitambulisha chama na sera zake katika kuwaongoza Watanzania, ni vurugu tupu ambazo hatuna haja nazo.

Safari hii hatupendi kuambiwa fulani kafanya hivi,ameshindwa kufanya hivi hatutaki maana tumeona na tunaona tunachotaka wagombea watuambie watafanya nini na watatumia mbinu gani.

Tunasema hivyo kwa kuwa hatutaki Mtanzania yeyote apoteze haki yake kwa kumchagua kiongozi kapi eti kwa kuwa alisukumwa na uoga wa vitisho na jazba la ulaghai na hatimaye, akamchagua kiongozi kwa misingi batili ya ukabila, udini na mingine isiyojenga umoja wa kitaifa.

Kwa kuwa suala la amani na utulivu ni muhimu hasa katika kipindi cha uchaguzi, ni jukumu la serikali kudhibiti vurugu zote wakati wote wa shughuli za uchaguzi ili zifanyike kwa faida ya umma.

Viongozi wa vyama vyote hawana budi kuungana na kuwa mstari wa mbele kuzuia vurugu za wafuasi wao na kila Mtanzania ajue kuwa ulinzi wa Tanzania ni jukumu la kila Mtanzania na hasa mzalendo.

Licha ya elimu au uzoefu anaoweza kuwa nao, ni kiongozi asiyewafaa Watanzania, endapo atatumia ishara au kauli yoyote inayoelekea kuchochea vurugu na kupoteza amani nchini; huyo, haifai Tanzania.

Kwa mujibu wa Ibara ya 63 (2) (j) ya Sheria ya Uchaguzi No.1 ya mwaka 1981, kila kituo cha Uchaguzi hakina budi kuwa na mlinzi wa amani. Hiyo ni muafaka na haistahili kupingwa.

Kwa kuwa polisi hawatoshi, ipo haja ya kutumia walinzi wengine wa amani.

Hata hivyo suala la idadi ya polisi au Walinzi vituoni, sio hoja sana. Suala linalotia utatani kwamba, polisi (walinzi) hao wakati wanasimamia uchaguzi katika vituo vyao, wanajua wanayopaswa kufanya kwa mujibu wa sheria na taratibu?

Je, wanajua ni watu gani wanaruhusiwa kuingia kituoni kwa mujibu wa sheria? Na kwamba watu hao wanatakiwa kuwa katika hali gani?

Je, wanazijua kanuni zinazoelezea mambo muhimu ya kuzingatia katika kituo cha kupigia kura; ikiwa ni pamoja na utaratibu wa kujipanga mstarini?

Ni dhahiri kuwa wasimamizi wa vituo hupata semina kabla ya kwenda vituoni. Lakini, polisi hawapewi semina na elimu za namna hiyo za kutosha.

Wanafika kwa msimamizi na kuoneshwa Mkuu wa Kituo na Msaidizi wake; kisha wanafuatana hadi kituoni.

Je, Hiyo tu, inatosha wajue na kutimiza wajibu wao?

Tume ya Taifa ya Uchaguzi na vyombo vingine husika hawana budi kuzingatia ukweli kuwa wasimamizi wa vituo wana kazi nyingi na hivyo siyo rahisi wakamudu kuwafundisha polisi kila kitu siku ya uchaguzi pale vituoni zikiwemo kugundua fujo zinazoendelea katika mistari ya wapiga kura au eneo la mita 100-200 toka alipo.

Ni vyema polisi ‘wakanolewa’ vya kutosha kabla ya kupelekwa katika vituo vya kupigia kura wakiwa hawajui wanayopaswa kufanya.

 

Kupigana mbele ya marehemu ni kuzidhalilisha dini zetu

Ndugu Mhariri wa Kiongozi,

Naomba nitumie gazeti lako kuwaambia ndugu zangu wanaojidai wanausongo na wakereketwa feki wa dini zao wanasababisha vurugu na mapigano kwenye misiba badala ya kushirikiana katika majonzi tunapotokewa na misiba.

Hivi jamani; ndugu zangu, ni vipi mtu unayejiita "mwanadini" au mtumishi wa Mungu, uamue kuvunja Amri ya Mungu ya Upendo kwa wenzio na kuamua kupigana eti unamzuia mwenzio kuuhufadhi mwili wa NDUGU YENU MAREHEMU?

Ndugu zangu, tunakwenda wapi? Tunakwenda wapi Watanzania wenzangu? Yaani jikumbushe kama binadamu unayetembea na uliyekwisha kutana na watu mbalimbali duniani katika harakati za maisha; ni watu wangapi umekutana nao? Ni wangapi wamekusaidia bila wewe kujua ni wa dini gani? Mbona hukukataa au kuuliza kwanza

Kama sio unafiki?

Ni shetani gani anawavamia ndugu zangu hadi leo muamue kuwapiga wenzenu wanaotaka kumhifadhi huku mwili na roho yake (marehemu), ikishuhudia kwa uchungu namna unavyomkana mwanadamu mwenzako eti kwa kuwa amekufa?

Hivi, mbona wakati wa uhai wake hukukataa msaada wake kwa kuwa sio wa dini yako? Mbona hukukataa misaada ya ndugu zake ambao nao sio wa dini yako?

Mbona kama unajali ukale na upuuzi wa ubaguzi wa kidini, kwenye daladala hukujitenga upande lako na hata mashule na hospitali huenda za dini yako?

Mimi nina wasi wasi kuwa wale wanaokuwa msitari wa mbele kujionesha kuwa wanajua na ni wakereketwa, mara nyingi ndio mbumbumbu wasiojua kuandika hata kutamka au basi kuiwazia "A" ya imani yao.

Ninasema ni hao wanaokata tamaa za maisha na kutumia fani, majina na sehemu takatifu kama mwavuli wa kujikinga dhidi ya tabia zao mbovu zilizokithiri katika jamii; na hao ni wanafiki kwelikweli.

Ukichunguza sana, utakuta hao ni wale ambao wanatafuta umaarufu katika baadhi ya vikundi vya dini ili wapewe tenda na kuwa maarufu wa kuwa wanahudhuria misiba na wala sio kwa kuwa wana uchungu, bali ni hao wanaokuwa wanaigeuza misiba kama poneo na mahali pao pa kuhemea na kuzamia.

Ni hao ambao ni wataalamu wa kugombea pilau na ubwabwa misibani ambao hata ikitokea chakula kikapungua msibani, badala ya yeye kuongeza kwa kutoa mchango, yeye ndiye anakuwa kiongozi wa lawama eti hakushiba.

Naomba kuwambia ndugu zangu kuwa hakuna ugonjwa mbaya kama ule wa kukata tamaa au kujidhani unajua; kumbe miongoni mwa wasiojua, wewe ndiye hujui.

Sina zaidi lakini ninasema kupigana mbele ya maiti ni kizidharirisha dini zetu na ni heri wasiojua namna ya kufanya kazi za Mungu, waache wamuombe Maulana awasaidie kwa mapenzi yake, wakajifunze kwanza ndipo warudi.

Mwananchi Mpenda Amani

Mbagala Kizuiani

DAR-ES-SALAAM.

Wizara ya afya ichunguze dawa zinazouzwa mitaani

Ndugu Mhariri,

Naomba unipe walau nafasi kidogo katika gazeti lako hili la kidini, ili nieeleze na kuishauri serikali yetu kupitia Wizara yake ya Afya.

Naomba nafasi hii ili pengine kwa ushauri wangu, serikali inaweza kufanya utafiti wa kina kujua ni kwanini dawa nyingi zinazouzwa hapa nchini; tena zikiwa zimetengenezwa hapa hapa nchini kwetu, huwa hazisaidii na badala yake zinadhoofisha tu bila kuponya.

Ninapenda kuiarifu hivyo serikali kwa kuwa, mimi binafsi ninadhani upo udhaifu katika uzalishaji na hata ukaguzi mzima wa dawa zinazozalishwa kama zinastahili kutumiwa na watu.

Kama serikali haitatilia maanani kutafuta sababu ya wasiwasi wangu, ninahofu kuwa ipo hatari Watanzania tukazidi kuathirika kwa kutumia madawa ambayo huenda yana walakini.

Hivyo, ni matumaini yangu kuwa kama serikali iko makini na inajali afya za watu wake, basi itafanya uchunguzi wa kimya kimya katika viwanda vyote vya serikali na makampuni halali na hata kuyachunguza makampuni yasiyo halali yanayojihusisha na uzalishaji huu unaohatarisha afya za jamii.

Ninasema kweli, kama Watanzania hatutaoneana huruma, sijui tutakuwa na lipi la kujibu mbele za Mungu hasa wale wanaojua na wanaouza dawa batili huku wakikaa kimya, labda kwa tamaa ya pesa au basi chochote.

Hii haina tofauti na kuua kwa kukusudia na mimi hilo ninawaambia wazi wale wote wanaouza dawa huku wanajua kuwa labda hazifai na badala yake zinaweza kuangamiza.

Tumaini Kasika,

S.L.P.

Ukerewe.

Walokole nijibuni maswali yangu

Ndugu Mhariri,

MIMI ni mwanafunzi wa Yesu, nami ninamtumikia Mungu wangu.

Nina maswali yangu ninaomba kuwauliza Walokole pamoja na wachungaji wao wote.

Swali la kwanza:

Kwa nini tunasali Sala ya Baba Yetu ambayo wanafunzi wa Yesu waliuliza, "Tukitaka kusali tusalije?"

Akasema, salini hivi, akawafundisha sala hiyo ya Baba Yetu. Sasa mbona walokole hawasali sala hii? Na wao wanasema ni wanafunzi wa Yesu? Tena wanachachamaa kabisa!

Swali la pili:

Haya maagizo ya Bwana Yesu, alisema neno ulilonipa nami ndilo niwapalo jinsi mimi nilivyokuwa shirika moja mimi na wewe, basi na wao wawe na ushirika mmoja ili ulimwengu ujue kuwa hawa siyo wa ulimwengu huu.

Lakini cha ajabu ni kwamba, wanajiita Walokole na kusema, "Yesu ameniokoa," na kutangaza kila mahali lakini hawapendani wala hawashirikiani kabisa katika jamii inayowazunguka na hata baina yao wenyewe kwa wenyewe.

Swali la tatu.

Neno la Mungu lina sema Amri iliyo Kuu ni hii, Upendo kwa maana upendo upo juu ya mambo yote hakuna mtu anayeweza kumuua rafiki yake anayempenda au mtu anayeweza kumkata au kumpiga rafiki yake anaempenda, au anayeweza kumnyima chakula au akimwacha akaangamia.

Haiwezekani kabisa; sasa Walokole kusema kwamba wanapendana wakati hawasaidiani hata kama una matatizo makubwa kabisa. Tena kibaya zaidi, wanapokuuliza kama umeokoka na ukasema bado, ujue hata kama unaelekea kufa kwa kukosa sindano ya kushonea hawawezi kukupa hata kama wanazo na zinawaozea.

Hawana msaada wowote kwa wengie wakati wa matatizo wala hawajui eti Mungu amesema kwamba tulie nao hao waliao na tufurahi nao wanaofurahi (Warumi 12:15) Amina.

Vyombo vya habari naomba jambo hili mlifanyie kazi maana ni Roho wa Mungu anauliza watu wake hapa duniani wanao litamka Jina Lake kwa uongo.

Nao, naomba wayajibu maswali haya. Naomba wajibu ili ulimwengu utambue kwanini hawazifuati Kanuni za Mungu jinsi alivyo agiza watu wake kwa maana Neno la Mungu halipunguzwi wala haliongezwi, Amina.

 

Wako katika Bwana

Nabii Samson Kisarika Mushy,

Fire Gospel Interational Church,

Box 21168

Dar - Es Salaam