TUSICHEZE NA UKIMWI

RAIS Benyamin Mkapa ametangaza kuwa mwaka huu wa 2000 ni kwa ajili ya vita dhidi ya ugonjwa wa UKIMWI. Kwanza rais ameelezea kuhusu hasara kubwa sana zinazotokana na ugonjwa huu wa ukimwi. Ameonyesha masikitiko yake makubwa kwa jinsi wananchi wengi wanavyopoteza maisha kutokana na ugonjwa huu wa ukimwi. Kutokana na ugonjwa huo wa ukimwi, nguvu kazi inazidi kupungua hasa kwetu sisi Watanzania ambao uchumi wetu hutegemea sana kilimo.Kwa hiyo ni dhahiri kabisa tunalazimika kuchukua hatua za tahadhari na za thati kabisa ili kuepukana na janga hilo.

Mheshimiwa rais ametoa wito na mapendekezo mbalimbali likiwemo lile la kuwasihi viongozi na wakuu wa madhehebu mbalimbali ya kidini nchini kukaa pamoja na kujadiliana kwa kina na kutafuta mbinu zaidi ambazo watazitumia dhidi ya ugonjwa huo.Pia rais amevitaka vyombo vya habari nchini kulipa Uzito wa pekee suala hili katika habari zaoza kila siku na kusisitiza kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wanatimiza wajibuwao katika kuelemisha jamii, kuonya na kuitahadharisha ilikufanikish mapambano haya.

Kwanza tunapenda kumpongeza rais wetu kwa tamko hilo la vita dhidi ya ugonjwa huo.Kwa tamko hilo tunaamini kuwa rais wetu anao upendo na huruma kwetu sisi raia zake. Hivyo inatupasa nasi kuupokea mwito huo kwa mioyo mikunjufu kweli kweli. Kwa maneno mengine tungeweza kusema kwamba rais ametangaza hali ya hatari katika nchi yetu kupambana na huo ugonjwa wa ukimwi. Jambo linalosikitisha zaidi ni lile la kuona kuwa kuna baadhi ya wananchi na hasa vijana wanalichukulia jambo hilo kama mzaha tu. Maneno yale yasemayo kuwa mtu mwenye kupatwa na ugonjwa huu wa ukimwi ni kama ajali kazini ni usemi usio na ukomavu wala hekima. Inakuwaje mtu anashuhudia kabisa ndugu yake akiteseka na kisha kupoteza uhai wake na asichukue hatua za tahadhari?

Tunaamini kuwa sisi binadamu ni viumbe wenye akili na utashi. Tunatumia akili zetu katika kupima na kuhukumu mambo yaliyo mema na mabaya. Kwa kawaida matukio mbalimbali hutufundisha, hututahadharisha, hutuogopesha na kisha hutuonya na kutushauri. Lakini inapotokea kwamba kuna kila dalili mwenzetu kafa kwa ukimwi na chanzo cha ugonjwa huo kinaeleleweka, na papo hapo hatuchukua tahadhari basi hilo linakuwa ni jambo la kichekesho na la upuuzi. Binadamu sharti tupime na kuangalia matokeo ya matendo yetu hasa yale ya kiburudani na kianasa. Kwa nini tuangamize maisha yetu kwa kitendo kimoja kichafu tunachokiita sherehe? Wataalamu wa kirumi walikuwa na msemo usemao:cho chote ukifanyacho, kifanye kwa busara na kisha angalia mapato yake. Hivyo ndivyo inavyotakiwa tufanye sisi Watanzania hasa katika mambo ya mapenzi, mambo ya kujaminiana na hata yale yote ya burudani na michezo.

Kwa upande wa madhehebu ya kidini kuna mambo mengi sana yamefanyika kuhusu vita dhidi ya ukimwi. Kwa mfano katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania kuna kitendo cha Ukimwi kinachoendesha semina na mikutano mbalimbali ya ushauri wa mambo ya ukimwi. Kumeendesha semina za majimbo, za kanda na hata za kiparokia. Vijana wamekuwa wakielimishwa kuhusu ugonjwa huo wa ukimwi. Kutakuwa na mipango mingi zaidi siku za usoni kuhusu ugonjwa huo wa ukimwi. Hatuna shaka kuwa wito wa rais umepokelewa vema sana na madhehebu ya dini.

Neno kubwa ambalo madhehebu ya dini hulizingatia kuhusu mapambano hayo dhidi ya ukimwi na watu wanapaswa kubadilisha tabia zao. Tunaposema kuhusu kubadilisha tabia ni kwamba kila mmoja anatakiwa ajitawale binafsi. Ingawaje pengine huonekana kuwa ni jambo gumu kujitawala hasa katika mambo hayo ya kijinsia na kimapenzi, iweje hakuna njia nyingine isipokuwa kufanya hivyo.

Sote tunakubaliana na tunatambua kuwa uhai wetu ni kitu cha thamani kubwa sana na hivyo ni sharti kitunzwe kwa gharama kubwa sana.

Ni jambo la kusikitisha sana kama Watanzania tumepoteza ndugu, marafiki na jamaa wetu kutokana na ugonjwa huu mbaya. Kuna watoto wengi ambao ni yatima, kuna akina mama wengi ambao ni wajane, na hivyo kuna wazee wengi ambao hawana watoto wa kuwatunza kwa sababu watoto wao wamekufa kutokana na ugonjwa huo wa ukimwi.

Tunaambiwa kuwa kosa moja dogo sana laweza kusababisha janga kubwa sana. Sawa sawa na mtu mwenye kuacha mshumaa ukiwaka usiku na hivyo kuangukia kwenye godoro na kuunguza nyumba yote. Na hivyo ndivyo ilivyo katika jambo hili la ukimwi kwani ni tendo moja tu la kujaminiana huweza kuleta maafa makubwa sana.

Kubadilisha mienendo yetu au tabia zetu ni kama vile kufanya "about turn", yaani kugeuka kabisa.

Kubadilisha tabia ni kuachana kabisa na ile tabia mbovu, tabia ya uasherati, tabia ya kupenda kujamiana bila utaratibu na mpango wa kibinadamu ambapo akili na utashi hutumika Hapo tunayakumbuka yale maneno ya hekima ya wataalamu wa kirumi yaliyosema cho chote ukifanyacho kifanye kwa busara na kisha angalia matokeo yake. Binadamu anapaswa kubashiri matokeo ya matendo yake ayafanyayo. Kwa vile ana akili na utashi, haiwezekani kamwe akategemea bahati na hivyo yakitokea mambo mabaya akasema kuwa ni bahati mbaya.

Hatukatai kuwa kuna bahati mbaya katika maisha, lakini katika matendo haya ya kujamiana, bahati mbaya huwa ni kidogo sana, kwani mara nyingi mtu hufanya matendo hayo kwa matayarisho au kwa kutojiangalia mwenyewe.

Mafao ya wastaafu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki yanavuka mipaka ya utu

Ndugu Mhariri,

Ninasikitika kuomba nafasi katika gazeti lako nikiwa na huzuni moyoni mwangu ingawa sio makusudio yangu lakini hali halisi ya nchi yetu inanilazimisha kuwa hivyo.

Mhariri wa KIONGOZI, ninasema hivyo kwa kuwa tangu malipo ya mafao kwa ajili ya waliokuwa wastaafu wa iliyokuwa awali Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya kulitumikia taifa au jumuiya hiyo kwa muda kadhaa yanafedhehesha mno.

Kinachoshangaza na hata kunisikitisha ni pale nionapo baadhi ya hundi zinazozoushangaza Umma hasa kupitia vyombo vya habari ambavyo navyo huonesha kuduwazwa na malipo yanayofanywa na Serikali kwa watumishi hao kama mafao yao baada ya kustaafu.

Hivi kweli Serikali huwa inafanya uchunguzi wa kisayansi kabla ya maamuzi yake au inafanya maamuzi kwa jazba.

Kwa nini nisime hivyo hali sina shaka kuwa kila aliiyeona hundi ya sh 2000/=,170/= au hata sh 10/= tu, alipigwa na butwaa?

Hivi kweli kama serikali inao wataalamu wake wa masuala ya uchumi; waliogharimu mamilioni ya pesa za nchi kwa ajili ya masomo yao wanadiriki kukubali kuwa baadhi ya wastaafu hao wanastahili kulipwa kiasi hicho? sh 10/=? au ni kwa jazba tu, baada ya maandamano?.

Hivi hao tunaowaita wataalamu wa masuala ya uchumi wanaithaminishaje sh 10/= ya mwaka 1977 na sh 10/= ya mwaka 1999/2000? Wanaona elimu yao inaridhika kusema ni sawa na hivyo aliyestahili kulipwa sh 10/= mwaka 1977 alipwe sh 10/=hiyo hiyo mwaka 2000, bila kujali kupanda kwa gharama za maisha ukiwemo usafiri toka mikoani hadi DSM ambapo wengine kwa ruti moja hutumia zaidi ya sh, 45,000/=?

Hivi hata hao wachumi hawaoni gharama za kitabu cha hundi hizi (cheque) ni zaidi mno ya gharama za malipo yenyewe; hiyo inaitwaje?

Biashara ya ubuyu au ila ya..... Hivi hao ndio wachumi tulionao nchini au ni kwa makusudi t u wanaonesha kuwa hawako makini?! au ....

Hivi hata wale walionadi sera zao mwezi Oktoba 1995 wakati wa uchaguzi Mkuu uliopita waliomba uongozi hayo mambo hawayaoni au hawajui? au wanayafumba.

Hivi ndio hao watakao kuja tena na sera nzuri za maneno Oktoba mwaka huu. Jamani angalieni tutokako, msisahau tuendako.

Mpenda Haki,

Julius Chacha,

Magu.