Karne ya 21 iwe ni ya ukombozi kwa wanyonge

KWA ujumla sisi sote tunafurahi sana kuweza kuingia katika karne mpya ya 21, au katika milenium ya tatu. Hakuna mtu mwenye akili ambaye hatambui bahati hiyo. Sote tunapaswa kumshukuru Mungu aliyetuwezesha kuingia katika karne hii mpya. Tunajiuliza ni wangapi ambao wameshindwa kuingia katika karne hii na kuufikia mwaka huu wa 2000.

Kuna wengi wamepoteza maisha yao kwa magonjwa, kwa ajali na hata kwa vita na pia kwa ukatili wa aina mbalimbali. Lakini kumbe Mungu ametuepusha sisi tulio hai na majanga ya kila aina na kutuwezesha kuingia katika milenium ya tatu, karne ya 21.

Hapo tunapaswa kusema ahsante mbele ya Mwenyezi Mungu na pia kwa binadamu wenzetu waliotusaidia kwa namna moja au nyingine.

Licha ya kusema ahsante kwa Mwenyezi Mungu na kwa binadamu wenzetu, tunapaswa kuweka ahadi ya kubadilisha mienendo na tabia zetu katika jamii zetu. Tungependa kutoa mwito hasa kwa wale wote wanaowaajiri vijana, wasichana na wavulana kuwa katika karne ya 21 kuwe na haki za malipo.

Ni jambo la kusikitisha kuona jinsi wafanyakazi hasa wale wanaoajiriwa kufanya kazi za nyumbani, kwenye mahoteli, kwenye mabaa na hata katika mashamba ya matajiri. Wafanyakazi wengi wa aina hiyo hawalipwi mshahara wenye kulingana na kazi wanazozifanya.

Kwa mfano msichana wa nyumbani huamka asubuhi mapema na kuanza kushughulika hadi usiku. Mshahara anaoupata kwa mwezi hauzidi pengine Tsh.10,000/-. Tunasema hiyo ni kweli dhuluma.

Hivyo pia kwa wale wahudumu kwenye mabaa ambao hufanya kazi hiyo katika mazingira magumu sana. Lakini nao mshahara wanaoupata haulingani kamwe na huduma hiyo wanayoitoa.

Wahudumu wengi wa nyumbani na kwenye mabaa au hoteli wanadhulumiwa sana licha ya kufanya kazi mchana kutwa na hadi usiku. Ni jambo la kusikitisha sana kuona binadamu mwenye akili pamoja na kisomo na imani alivyo navyo anamdhulumu mwenzake.

Hivi karibuni kulikuwa na habari katika gazeti fulani la kila siku hapa nchini yenye kueleza kwamba mabinti wawili waliokuwa wakifanya kazi za nyumbani wametoroka, na haikujulikana wapi walikwenda.

Sisi hatuwezi kufikiri kama hao mabinti wametoroka tu, bali kuna sababu zilizowafanya waondoke bila kuwaaga waajiri wao.

Tunahisi kwamba ni kutokana na kutokulipwa mshahara wa kulingana na huduma walizokuwa wakizitoa. Mara nyingi sana wahudumu hasa wale wa nyumbani hunyanyaswa siyo tu na wazazi, bali hata na watoto wa hapo nyumbani. Hiyo tunasema ni tabia mbaya na inapaswa kukomeshwa kabisa katika karne hii ya 21.

Jambo la kukumbuka ni hili kwamba kila binadamu anastahili ujira wenye kulingana na jasho analolitoa.

Huwa ni jambo la kusikitisha wakati hao wahudumu na wafanyakazi wanapodai haki zao hutishwa na hata kufukuzwa.

Tunasema huo siyo uungwana wala ubinadamu kwani mtu anapokufanyia kazi au umeamua kumwajiri, ni sharti apewe haki yake kulingana na kazi aliyoifanya. Kwa nini sisi binadamu tunapenda sana kuwapunja wengine na kuwanyima haki zao?

Kuna ukosefu wa haki katika ajira ndani ya taasisi mbalimbali pia hivyo kuna manung’uniko mengi ya hapa na pale. Inakuwaje kwa mfano mhudumu katika ile hoteli kubwa ya kitalii inaingiza hela nyingi sana kwa siku, lakini hulipwa kiasi kidogo sana. Dhuluma hiyo huwaingiza hao wahudumu katika vishawishi vibaya na kuwaletea matatizo. Yote hayo husababishwa na ule ukosefu wa haki katika kuwalipa hao waajiriwa.

Ikiwa mtu aliyeajiriwa analipwa mshahara wa haki kulingana na kazi yake, hapo siyo rahisi akafanya uhalifu wa wizi.

Tunasema tuingie katika karne hii tukiwa na moyo wa haki kwa wanyonge na wale wote wenye hali ya chini. Tunapaswa kuondoa dhaluma katika jamii yetu, hasa katika karne hii mpya ya 21.

Kila mwenye mamlaka au madaraka hana budi kutoa haki kwa wale walio chini yake, na hivyo pia kwa kila mwenye kumwajiri mwenzake awe ni kijana awe ni mtu mzima hupaswa kulipwa mshahara wa haki. Katika mwaka huu wa 2000 inatupasa kila mmoja kuona anatoa haki kwa mwenzake hasa katika mambo ya ajira.

Hongera Makamba kwa msimamo wako

Ndugu Mhariri,

KUMEKUWA na mazoea mabaya waliyoyajenga madereva wa Daladala kuacha njia za magari na kukatiza kwenye njia za watu waendao kwa miguu na kusababisha ajali mbalimbali.

Sisi Wananchi tunampongeza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Luteni Yusufu Makamba kwa kuwakemea askari wa usalama Barabarani kwa uzembe wa kuwaona wenye daladala hizo zinazokatisha kwenye njia za waendao kwa miguu na kuwafumbia macho, hali ambayo inazidi kuleta maafa hususani kwa watoto na hata wapita njia wanaokuwa wanatumia njia hizo kwani daladala hizo zinakatisha hata kwenye nyumba za watu.

Hali halisi tunaifahamu sisi wananchi kuwa mapolisi wa usalama barabarani (Trafiki) wanafahamu fika kuwa daladala zinakiuka njia ya magari na kutumia njia za waendao kwa miguu. Na si daladala tu bali hata magari mengine ya watu binafsi hutumia njia za waendao kwa miguu na hali ambayo ni kukiuka taratibu zinazotakiwa na kusababisha ajali na trafiki.

Kwa kweli Watanzania wote tunapaswa kujenga utamaduni wa kuheshimu sheria za nchi kwani zimewekwa kwa manufaa ya wote, badala ya kujali tu maslahi yetu binafsi. Huo sio utu na wala binadamu mwenye akili timamu hapaswi kufanya hivyo., Tukumbuke kuwa hata Mwenyezi Mungu anatutaka tuheshimu sheria za nchi na ndipo tutaweza hata kuheshimu sheria za Mungu kwa uaminifu zaidi.

Iweje wewe dereva una barabara yako, lakini kakichochoro kadogo ka waendao kwa miguu unakaingilia? Acheni mchezo huo.

Kwa uzembe huo watu wengi ninaowafahamu wamegongwa na magari na polisi wa Usalama Barabarani wanawafumbia macho, hali ambayo inasababisha kuongezeka kwa watu wanaokufa kwa kugongwa na magari wakiwa wanatumia njia za miguu.

Tunamshukuru sana na kumpongeza Luteni Makamba kwa Uongozi wake mzuri wa kukemea maovu yote kwa mkoa wake wa Dar es salaam kwani hali hiyo itawafundisha madereva wale waliozoea kuvunja sheria hususan kusimamisha magari hovyohovyo (hasa wale wa daladala) bila kujali vituo muhimu na wale ambao walikuwa wanataka kuiga tabia za madereva hao.

Hatuwezi kuendelea kuvumilia wazermbe watuue kwa kisa cha kutamani utajiri wa harakaharaka. Tunashukuru kwamba ‘mkwara’ wa Luteni Makamba umesaidia Polisi wa Usalama barabarani wametilia mkazo kuwasaka madereva hao wanaotumia njia tofauti na zinazotakiwa na hatimaye kuwakamata wengi na kuwafikisha mahakamani ambapo wengi wao walilipishwa faini na wengine kufungwa, hali ambayo inatoa fundisho kwa wote wenye tabia hizo.

Kwa hali inavyoonekana ni dhahiri kuwa trafiki wanatakiwa kuwa makini katika kazi zao na kuwa wakweli wakati wawapo kazini ili kuhakikisha kuwa usalama unakuwapo kwa kila raia kwani uzembe unaofanywa na madereva wenye magari kwa kukiuka sheria unasababisha madereva wengine waaminifu nao waingizwe katika mkumbo wa wazembe bila sababu.

Ni kazi nzuri hiyo Luteni anayoifanya ya kuepusha ajali ambazo zilikuwa zimezidi na kwa juhudi ambazo amezifanya. Inaeleweka wazi kuwa hali hiyo ilipelekea kuwa na hali ya kutokuwepo na ajali nyingi kupita kiasi katika sikukuu za Krismasi na ni mategemeo ya wananchi wengi kuwa hali hiyo itaendelea hadi katika sikukuu za mwaka mpya na kuanza mwaka katika hali nzuri ya kiusalama, hasa wakati huu tunapoingia milenia mpya, karne ya 21 ya Sayansi na teknolojia..

Mwananchi mpenda amani,

Innocent Byagarama

S.L. P 1438

Dar es Salaam.