Tunahitaji masomo ya dini

YAPO manung’uniko mengi mengi sana katika taifa letu kuhusu utovu wa maadili. Pia kuna uhalifu mwingi unaotokana na ukosefu wa malezi ya kidini hasa kwa upande wa vijana wetu. Kila siku hatukosi kusikia juu ya vijana na hata watu wazima wanaofanya mambo yaliyo kinyume kabisa cha utu na ubinadamu. Mara kwa mara tunasikia juu ya vitendo vichafu kama vile vya ubakaji, ulawiti, madawa ya kulevya, umalaya, ulevi, unyang’anyi, ujambazi, na kila aina ya wizi. Pia kuna ile tabia ya uzembe na uvivu wa kutotaka kufanya kazi.Tunajiuliza, je, hayo yote hutokana na nini? Je, ni kwa njia gani tutaweza kuyamaliza matatizo hayo ama sivyo?

Katika kutafakari kwa kina, sisi tunaona kuwa mambo hayo yanasababishwa hasa na ukosefu wa mafunzo ya kidini katika familia zetu na hasa katika shule zetu nyingi. Ni dhahiri kuwa katika shule zetu nyingi somo la dini au halifundishwi kabisa na mahali pengine hatiliwi mkazo. Tuna mashaka makubwa sana kama kweli katika shule hizo zinazoitwa ni Shule za "kimataifa" au "International Schools" zenye kutumia Kiingereza kama ndio lugha yao, kuna vipindi vya dini kwa ajili ya watoto hao. Kwa hiyo hao watoto mwishowe watafahamu sana lugha ya kizungu, lakini watakuwa maskini kabisa katika elimu ya kidini.

Mapato yake tunazidi kuyashuhudia kila siku tunapoona jinsi hao vijana wanavyokosa heshima na adabu mbele ya wakubwa. Hatuwezi kamwe kujisifia katika hali ya namna hiyo. Kuna wazazi wengine wametambua jambo hilo na hivyo wanapenda sana kuwapeleka watoto wao kwenye shule zile ambazo zinatoa malezi licha ya elimu na maarifa. Vijana wengi wanapomaliza masomo ya Sekondari huwa wamefuzu kweli kweli katika masomo hayo ya kidunia, lakini kumbe wanakuwa chini sana katika mambo ya kiroho au kidini.

Taifa letu limetangaza kupiga vita maovu mbalimbali. Lakini jambo la msingi lingekuwa ni kwamba kujenga msingi wa kimaadili kwa njia ya kuhimiza malezi ya kidini katika mashule yetu yaani kutoka shule za awali hadi katika vyuo. Vijana wanapaswa kuelimishwa kuhusu urai mwema au maadili sahihi. Katika mashule na sehemu nyingine za malezi, watoto na vijana wetu wafundishwe nidhamu inayotakiwa na hivyo wache wawe ni raia wema.

Walimu wetu wanapaswa kufahamu kuwa wao ni walezi, yaani waundaji wa watoto na vijana wetu. Hivyo ndivyo ilivyokuwa hapo awali katika shule zile za zamani. Kila mwalimu alijiona kuwa ni mlezi wa watoto na hivyo licha ya kuwapa elimu na maarifu aliwafunza vile vile adabu njema na nidhamu iliyotakiwa. Pia kulikuwa na ushirikiano kati ya walimu na wazazi katika kuwalea watoto. Lakini siku ya leo kwa ujumla mambo ni tofauti sana, kwani walimu wanafanya kazi ya kutoa maarifa tu, na hapa pengine siyo kwa ukamilifu wakingoja wanafunzi waje kwenye ‘tuition’. Kwa vile walimu wengi wanakosa hata kutoa elimu na maarifa kikamilifu, hapo inakuwa ni vigumu sana kuweza kuwafundisha wanafunzi elimu na maarifa ya kidini.

Nimewahi kusikia kuwa kuna shule ambazo walimu wanakatazwa kabisa kuingilia utovu wa nidhamu ya wanafunzi. Jambo hilo liko hasa katika zile shughule za binafsi ambazo wamiliki wanatafuta hasa pesa na wala siyo malezi ya wanafunzi. Hao walimu wanaambiwa kuwa kazi yao ni kufundisha masomo na siyo kutoa malezi ya kitabia au kinidhamu. Sote tunafahamu nguvu aliyo nayo mwalimu katika darasa. Cho chote asemacho huwa kina nguvu kabisa, na kinyume chake cho chote asichokisema, basi huwa hakina nguvu. Mambo ndivyo yalivyokuwa hapo zamani, lakini kwa sasa hivi hayako katika mashule na vyuo vingi.

Sisi tungependa kuona kuwa Serikali na hasa Wizara ya Elimu inakazia kabisa somo la dini na malezi katika shule zetu. Somo la dini lisiwe la hiari, bali la lazima kabisa. Wanafunzi wanapaswa kufundishwa pia somo la uraia. Kwa kufanya hivyo tunatumaini kuwa tutaweza kuokoa huo mmomonyoko wa maadili katika taifa letu. Lingekuwa ni jambo jema kabisa kukawa na mtihani wa somo la dini au malezi. Mtihani huo uwe wa lazima, na tena wenye nguvu kwa wanafunzi. Kwa kulegeza somo la dini na malezi na kufanya liwe la hiari tunashuhudia mapato yake kila siku.

Tunapenda kupongeza uongozi wa shule zile ambazo hutilia mkazo masomo ya dini pamoja na malezi ya nidhamu. Kuna viongozi wengi hasa wale wa Majimbo na Makanisa mbalimbali wanaotilia mkazo somo hilo la kidini. Kwa hiyo serikali licha ya kunung’unika kuhusu uhalifu unaofanyika na vijana na hata watu wazima ingetilia mkazo mkubwa katika somo la malezi ya kidini.

Mara kwa mara serikali na hata mashirika mengine hupenda kushughulikia matatizo yakiwa katika hali mbaya, kwa mfano kuanza kupigana na wahalifu ambao wameshadumaa. Lakini lingekuwa ni jambo bora zaidi kama ingeshughulika na chanzo cha uhalifu huo. Tusipofanya hivyo tutazidi kuwaweka watu katika magereza na bado uhalifu utaendelea bila kupungua. Kwa hiyo tunalopaswa kulifanya sasa hivi ni kukazania hasa malezi ya kidini. Kutoka kwenye familia na jamii itaonekane kuwa ni wajibu wa kila mmoja kujenga tabia za watoto na hivyo huko mashuleni walimu wetu wajione kuwa ni walezi na siyo wagawaji wa maarifa tu.

Tuna hofu na bili za umeme za kukadiriwa

Ndugu Mhariri,

Ninaomba unitafutie walau ka-nafasi kidogo ili niweze kutolea dukuduku langu kupitia gazeti lako ambalo hivi sasa limetokea kuvuma , kupendwa na hata kuvutia wasomaji wengi.

Ipasipo kukuficha mapema, lengo la ombi la nafasi katika gazeti lako leo hii ni kuelekeza lawama zangu kwa Shirika letu la Umeme (TANESCO), hususan katika wilaya yetu ya Temeke.

Mimi ni miongoni mwa wakazi wachache wa wilaya hii waliobahatika kupatahuduma hii ya umeme, lakini wanasumbuka badala ya kufaidi kuwepo kwa nyaya hizo licha ya huduma iliyotarajiwa.

Ninasema hivyo kw kuwa katika eneo letu la Keko Machungwa, huduma hii imekuwa kama zawadi tu, unayopata pindi mtoaji anapokuwa amefurahi. Ni kama siku hizo tunapopata umeme kwa maana ya siku ambazo TANESCO wamefurahi.

Kinyume na hapo, kuna tofauti gani na maeneo ya vijijini ambako huduma hii ni msamiati mgumu?

Ninasema hivyo si kwa kuwa tu tatizo la katizo la umeme ovyo ovyo linazidi kukera jamii ikiwemo familia yangu, bali kwa kuwa licha ya katizo hilo hata wakati wa malipo bili inayodaiwa inashangaza ukilinganisha na matumizi halisi ya umeme.

Kinacho nikera zaidi ni kwamba TANESCO wanao watumishi mbalimbali wakiwemo wale wasoma mita kwa ajili ya kupanga bei muafaka ya umeme uliotumika. Lakini je, tatizo ni nini mpaka waanzishe utaratibu wa kumsubiri mteja amekwenda kulipa mwenyewe ndipo wamkadirie malipo yake na kumbebesha mzigo usio wake?

Kwanini wakisie hali mita zipo na zinafanya kazi sawia? Hivi ni mara ngapi wamekuja kusoma mita wakakuta aidha mbwa akawazuia, wakakuta nyumba imefungwa , au basi kikwazo chochote kilichowafanya mara kadhaa washindwe kusoma mita na badala yake kuamua "kuwauma" wateja wao namna hiyo?

Mimi naona shirika letu haliwezi kupinga tukidai kwamba limeamua kutuibia pesa kimachomacho kupitia ulipaji wa bili za umeme na ndiyo maana bila sababu yoyote wanaamua kukisia malipo, hali vipimo vipo.

Ninadhani umefika wakati kila mtu kwa nafasi yake akafanya kazi zake kwa nia nzuri isiyolenga mapato ya kificho wala kushawishi rushwa ya aina yoyote.

Kama ndivyo basi wito wangu kwa ndugu zetu wa TANESCO ni kuwa, TUMIENI MITA ZENU, MSIKISIE MALIPO ; MNATUUA.

Michael Samwel,

Keko Machungwa,

Dar es Salaam