Kidogo tulicho nacho ni vema tukakitunza

SISI Watanzania tunayo matatizo mengi na mbalimbali. Tunayo matatizo ambayo yako juu ya uwezo wetu, na tunayo matatizo ambayo yako chini ya uwezo wetu. Matatizo yale ambayo yako juu ya uwezo wetu ni hasa yale ambayo huhitaji pesa au utaalamu wa pekee. Lakini matatizo yale ambayo yako chini ya uwezo wetu, ni yale ambayo yanahitaji hasa jitihada zetu na nia ya kukabiliana nayo. Kwa mfano utunzaji wa vitu vile ambavyo viko tayari huhitaji tu nia ya kufanya hivyo kutokana na ustaarabu na uwajibikaji tulio nao.

Hivi sasa tunakabiliwa na shida kuu mbili hasa katika Jiji la Dar Es Salaam na hata katika miji mingine ya nchi yetu. Kuna shida kubwa sana ya maji na pia shida ya umeme kukatikati hapa na pale. Wataalam wetu wamejitahidi sana kuleta maji katika Jiji na katika miji mbalimbali. Ni jambo la kweli kuwa huduma ya maji haitoshi bado kulinganisha na idadi ya wakazi inavyozidi kuongezeka siku kwa siku. Lakini tatizo hilo la maji huzidi kuongezeka kutokana pia uzembe wa wananchi wengine. Kwa mfano kuna wale ambao hukata mabomba ovyo ovyo kwa ajili ya manufaa yao binafsi. Tunasema vitendo hivyo ni vya uzembe na si vya kistaarabu. Pengine hutokea kwamba kwa bahati mbaya bomba zinatoa maji na hivyo wahusika hawashughulikia tatizo hilo kwa haraka na mapato yake ni kwamba maji mengi hupotea bure. Mara ngapi tunashuhudia jinsi maji yanayobubujika mabarabarani na huko vichochoroni bila matumizi.

Kuna swali la kujiuliza, ni kwa nini wakati wa shida kubwa sana ya maji, kama vile siku hizi kunakuwa na bomba ambazo hutoa maji bila wasiwasi? Je, kuna upendeleo wa namna fulani ama sivyo. Tunashuhudia jinsi watu na maplastiki wanavyomiminika sehemu fulani kuteka maji kutoka ya bombani na sehemu nyingine ni bomba kavu sana. Tungewaomba wahusika wangetupa maelezo na hivyo tukaelewa sababu za baadhi ya watu kutohangaika na shida hiyo ya maji, na papo hapo wengine wakiwa katika matatizo makubwa sana ya maji.

Tatizo la pili tumesema ni lile la umeme. Kwa kadiri ya habari zinazopatikana mara kwa mara ni kweli kuwa kuna uharibifu mkubwa sana wa njia za umeme. Mara kwa mara tumesikia kuwa nyaya za umeme zimekamatwa huko Mkoani Tanga. Kuna wahalifu na waharibifu ambao hukata nyaya za umeme na kwenda kuziuza nchi jirani. Vitendo hivyo kusema kweli ni vya uharibifu na pia ni ukosefu wa ustaarabu. Je, wenzetu waliostaarabika wanaposikia kuhusu vitendo hivyo wanatuelewaje sisi Watanzania?

Hivi karibuni kiongozi mmoja wa Shirika la Umeme (TANESCO) alileza kwamba kuna waharibifu wanadiriki hata kuiba mafuta ya transforma na hivyo kusababisha matatizo makubwa ya umeme. Hilo tena ni jambo la aibu sana tena la kukosa ustaarabu na lenye kuturudisha nyuma kabisa kimaendeleo. Wengine husema hayo yote husababishwa na hali duni tuliyo nayo sisi Watanzania. Kuna wengine ambao wanataka kuchukua njia za mkato katika kumaliza matatizo yao. Hao wanona ni heri watu wengi wapate taabu ya kukosa umeme, wakati wao wakikata hizo nyaya na kwenda kuziuza ili wapate fedha ya kuishi. Hivyo pia wanaona ni vizuri zaidi transforma zikakaa bila mafuta na wao wachota hayo mafuta na kwenda kuyauza kwa faida yao. Tunazidi kusema kuwa vitendo hivyo si vya ustaarabu na kamwe haviwezi kutufikisha kwenye maendeleo tunayoyatarajia.

Wakazi wa Jiji wanadai kuwe na taa za barabarani, lakini ebu angalia hizo taa zilivyo. Kumekuwa na uharibifu mkubwa sana na hata wizi wa hizo taa. Inashangaza sana kuona ni kwa jinsi gani wahalifu hao wamefanikiwa kukweli zile nguzo ndefu na kuweza kunyofoa taa hizo. Na siyo tu barabarani, bali pia katika sehemu mbalimbali hasa zile zilizo mahali pale ambapo watu wengi hukusanyika. Jambo la kushangaza pengine hao wahalifu hafanya vitendo hivyo hata mbele ya watu wengine. Lakini la kushangaza ni kwamba hakuna mtu wa kuwakemea katika vitendo hivyo.

Tunapaswa kutambua kuwa ni wajibu wetu sisi sote kutunza na kulinda mali ya umma kwa sababu ni kwa ajili ya faida yetu sisi sote. Uharibifu huo umeenea sasa katika kila sehemu. Kwa mfano ile barabara ya Kawawa imeanza kupendeza, lakini wengi tuna mashaka kama kweli itadumu hivyo ilivyo sasa hivi. Kwanza kabisa tunashuhudia jinsi watu wanavyopitapita kila sehemu, licha ya kuwekwa vibarabara maalumu vya kupita wale waendao kwa miguu. Hivyo tunashuhudia ile Barabara ya Morogoro kwa jinsi watu wanavyozidi kuharibu nyasi zilizopandwa kwani hakuna ustaarabu kabisa.

Uharibifu mkubwa sana hutokea hata kubomoa vile vibanda ambavyo vimetengenezwa kwa ajili ya kungojea basi. Kuna wahalifu wanaezua mabati na kwenda kuyatumia kwa shughuli zao binafsi. Mapato yake ni kwamba wasafiri wengi hupata shida hasa nyakati za mvua na jua kali. Na kuna wale wendawazimu ambao wanapitapita kuandikaandika katika kuta za vibanda na sehemu nyingine. Kwa nini watu wanawaachia waendelee kuchafua sehemu ambazo ni kwa ajili ya umma? Hao vichaa ni lazima wathibitiwe ili wasiwe waharibifu .

Watanzania tunapaswa kushikilia ule msemo usemao, ‘kitunze, kidumu’. Tunapaswa kujifunza kutunza vitu kwanza vyetu binafsi na pia vile vya umma. Yule ambaye hutunza mali yake binafsi, atakuwa tayari pia kutunza mali ya umma. Tunapaswa kutumia vizuri mali tuliyo nayo, hasa ile ya umma, kwani ufadhili unazidi kupungua siku hata siku. Tu maskini, lakini tunaweza kufanya jambo hilo la kiistaarabu la utunzaji wa mali tuliyo nayo.

Akina mama Wakatoliki Kibakwe pongezi kwa kukemea mavazi

Ndugu Mhariri,

Tafadhali naomba nitafutie nafasi kidogo japo pembeni kabisa mwa gazeti lako, ili nami niseme japo machache yaliyo katika utima wangu.

Napenda kutoa pongezi zangu za dhati kabisa tena kwa moyo mkunjufu kwa akina mama wa Kanisa Katholiki Kibakwe kwa kujitoa hadharani bila woga kukemea maovu yanayoenea hapa nchini na hasa parokiani petu.

Yale mliyoyasema mama zetu tarehe 16/1/2000 (kuhusu mavazi) hayawezi kupita bila kuungwa mkono na mtu yeyote mpenda utu.

Akina mama mmeunga mkono ujumbe kama huo ambao ulitolewa na VIWAWA hapa Parokiani katika sikukuu ya kutimiza miaka 25 ya Baraza la Walei.

Kumbukumbu la Torati 22:1-5, Nani Musa anatoa tahadhari juu ya mavazi naye anasema "Mwanamke asivae mavazi yampasayo mwanaume na wala mwanaume asivae mavazi yampasayo mwanamke, kwa maana kula afanyae mambo haya ni machukizo kwa bwana Mungu wako" (Sijui kwa ufahamu wangu mdogo wa Biblia kama torati hii imebadilika au inaendelea ilivyo hadi utimilifu wa dahiri. Kama haujabadilika mbona viongozi wa Kanisa hamyakemei haya? Kemeo la maovu na himizo la mema ndilo hasa chimbuko aina ya Biblia yote mojawapo la maovu hayo ni pamoja na mavazi yasiyo na heshima.

Nguo zilizopasuliwa mgongoni, suruali, pensi nyanya kwa wasichana kwa bwana hili chukizo wamekwisha liona na walichukia sana.

Nawapongeza mno moto ukikuunguza hata kama kwa kiwango kidogo kujikung’uta ni lazima.

Yakemeeni maovu siku zote na Bwana hatawaacha siku zote. Kanga, kitenge, kitambaa kichwani, sketi, gauni na blauzi juu mmeziona zina udhia gani mpaka mvae nguo zinazostahili wanaume? Kuhusu kujichubua nako, rangi nyeusi aliyokuumba nayo Mungu ina sifa yake na Mungu alikuumba hivyo kwa malengo yake kwa nini mmefikia kukosoa uumbaji? Kumbuka ulivyoumbwa hivyo Mungu hakukosema ila alikuwa na sababu maalum juu yako. Mtufahamishe mtendayo hayo mnayatenda kidini au kiserikali au kipagani? Busara ya mtu ni pamoja na yale ayatendayo kwa busara mbele za watu.

Uiheshimu Biblia na Qurani hapo utakuwa mtu mbele za watu. Je, unawezaje kusema namheshimu Mungu wakati watu wa Mungu walioko hapo duniani kuwaheshimu? Siku za mwisho ndizo hizi Wakristo na ndugu zetu Waislamu siyo lazima kila kitu tukumbushane, soma Biblia kila siku uitafakari na vile vile kwa ndugu zetu Waislamu Qur’ani tutayaelewa haya na tutayaishi.

Kwenu wazazi wa Kiume (yaani Baba) umwopoe Binti yako amevaa mavazi haya tena yanayombana viungo unajisikiaje? Au binti yake amevaa gauni lililopasuliwa mgongoni na kukuonyesha nguo za ndani unajisikiaje? Kwa mtu au watu wenye akili timamu swali aliloulizwa Adamu na bwana linatujia (mko wapi?) tuko naye au tumegeukia njia zetu? Kama tupo naye mbona hatukemei maovu au hatuyaoni? (Torati 22:1-3) "lichukieni lililo ovu, mkiambataana na lililo jema Rumi 12:10-21 ushauri kwa viongozi wa kanisa Katoliki "Watengeni watendao maovu kwa makusudi na wakiona uchungu kwa kutengwa na kanisa Waongoke.

Ushauri huu pia na kwa makanisa mengine yampendayo Kristo.

Someni kwa makini sana barua ya Yuda inavyotuonya wote tuliopotea

"Chukieni hata mavazi yao ambayo yamechafuliwa na tamaa zao mbaya"

Damasus G. Mtalaze

Kanisa Katoliki Kibakwe

S.L. P 114, Kibakwe

Dodoma.