Wavivu ni wabaya kuliko ombaomba

KWA ujumla inaonekana Watanzania wengi ni wavivu, na hawapendi kabisa kufanya kazi kwa hiari, licha ya nchi yetu kuwa maskini. Siyo jambo la ajabu kabisa kuona watu wazima, pamoja na vijana ambao wana nguvu na afya nzuri wakishinda bila kufanya kazi. Kwa vile nchi yetu inazidi kuelemewa na umaskini, tunajiuliza tutafika wapi na hali hiyo duni. Ni kweli kuwa hakuna ajira za kutosha, lakini kuna wananchi wengi wangeweza kujiajiri na hivyo wakafanya kazi za kujiletea maendeleo wao binafsi na pia kwa jamii kwa ujumla.

Tunaweza kutofautisha kati ya zile kazi ambazo mtu huzifanya kwanza kwa ajili ya kuboresha maisha yake. Binadamu anapaswa kuwa na chakula cha kutosha , anapaswa kuwa na mahali pazuri pa kulala, na pia awe na nguo nzuri za kujisitiri na hivyo kuonekana amependeza mbele ya wenzake. Lakini inapotokea kuwa binadamu anakula chakula cha kubabaisha, analala mahali pa wasiwasi na anavaa nguo, mradi tu ni nguo, basi hapo tunamshangaa.

Tokea mwanzoni mwa Uhuru wa nchi yetu, tumekuwa tukihimizwa kuwa na bidii katika kazi ili kujipatia riziki zetu mbalimbali. Lakini yaonekana kuwa maneno hayo yanatua kwenye masikio yaliyozbwa kwa kuwa kuna wananchi wengi ambao hawataki kabisa kufanya kazi. Mtu yuko radhi kabisa kuishi katika kibanda ambacho kimeanguka upande moja, au kimeharibika. Lakini utamkuta ameketi toka asubuhi hadi jioni, wala hajishughulishi na kukitengeneza kibanda hicho. Wengi wa wananchi wanaishi katika mazingira machafu sana kutokana na uvivu ulioshamira sana katika vijiji vyetu. Mtu akipita huko vijijini atashangaa sana na kujiuliza hao watu wanajisaidia wapi, kwani nyumba nyingi hazina vyoo kabisa. Tunasema hilo ni jambo la aibu, hakuna ustaarabu, ni uvivu tu uliojaa. Wengi wa wananchi hawana kabisa ile hamu ya maendeleo na hivyo wanaridhika tu na hali duni waliyo nayo.

Tunasema kuwa nchi yetu ni ya wakulima na wafanyakazi. Sehemu nyingi katika nchi yetu ni ardhi nzuri ya kufaa kwa kilimo. Lakini wananchi wengi hawataki kufanya kazi hiyo ya kilimo, licha ya uwezo walio nao. Wataalamu husema kuwa uhuru bila kuwajibika ni utumwa. Na hivyo ndivyo ilivyo kwetu sisi Watanzania. Tunasema kuwa tu huru, lakini kusema kweli tuko kama watumwa wa umaskini kutokana na uvivu ulioshamiri katika taifa letu. Viongozi wetu na wale wote wenye kututakia mema wamejitahidi sana kutuelewesha kuhusu umuhimu wa kufanya kazi, lakini kwa wengi ni jambo ambalo wanalidharau kabisa. Tunazidi kunyemelewa na umaskini ambao tungeweza kuushinda kama wananchi wangekuwa tayari kila mmoja kufanya kazi kwa kadiri ya uwezo na nguvu alizo nazo.

Tokea mwanzoni Mungu alipomwumba binadamu aliagiza kuwa ni lazima afanye kazi ya kuutawala na kuutisha ulimwengu huu. Mtume Paulo akiwaandika Watesalonike anasema wazi kuwa mtu yule asiyefanya kazi hastahili kula chakula. Lakini kuna watu wengi wanataka kula bila kufanya kazi, wanataka kuvaa bila kufanya kazi, na mbaya zaidi wanataka kupata starehe mbalimbali bila kufanya kazi bali kuwa wategemezi. Tunasema kuwa hii ni tabia iliyo kinyume cha maumbile ya binadamu.

Wakati umefika kwa Watanzania kuuonea aibu uvivu na kutowaonea aibu wavivu. Inatupasa tuanze kuwapongeza wale wote wanaofanya kazi na kubadilisha mazingira wanamoshi. Tungeshauri kuwa sheria ya nguvu kazi itumike sasa ipasavyo kuwasukuma wananchi kufanya kazi kwani uhuru uliopo sasa unatuletea umaskini na kuwadunisha wananchi wengi. Tunapohangaika na vibaka au wevi na majambazi, sisi tungependa kwanza kuona sheria ya kila mtu afanye kazi ikitiliwa mkazo. Mkoa wa Dar Es Salaam umefanikiwa kuwaondoa ombaomba, sasa tunapenda kuona kuwa kunakuweko sheria za kuwafanya wawaliosalia wanafanya kazi na kusiwe watu wanaokaa siku nzima wakipiga porojo au kunywa pombe kwani hao ni wabaya zaidi ya omba omba.

Tunamalizia Kauli Yetu kwa kuwakumbusha viongozi wetu kuwa wahimizaji wa kufanya kazi kimatendo. Tungependa kuona kuwa kila kaya, kila jamii inakuwa na mipango ya utendaji katika sehemu zao. Viongozi wetu wabadilishe mielekeo na kuona kuwa kazi yao kubwa ni kuhimiza na hata kulazimisha kwa namna yoyote watu wafanye kazi zenye kuwaletea maendeleo.

 

Ujamaa na Ubepari havikai nyumba moja

Ndugu Mhariri,

Katika kukusanya maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya katiba kupitia waraka wa Serikali imedhihirika kuwa wengi wametetea maneno ya ujamaa na kujitegemea yaendelee kuwemo katika katiba ya Tanzania.

Maana yake ni kwamba wananchi bado wanaipenda siasa ya ujamaa yaani kuishi kwa kuheshimiana kupendana na kutendeana haki hata katika kugawana mapato yatokanayo na kazi zetu kila mmoja kwa kadiri ya jasho lake.

Mimi nina wasiwasi kama hali hiyo inawezekana katika Tanzania ya sasa ambayo imeamua kuliacha azimio la Arusha na kuanza kuelekea kwenye ubepari kupitia ubinafsishaji wa mali asili na njia kuu zote za uchumi.

Ubepari ukishamiri utajenga tabaka mbili za watu.

Tabaka moja dogo la watu matajiri sana na tabaka kubwa la watu masikini sana.

Katika siasa ya kibepari wananchi wa kawaida hawawezi kutendewa haki.

Tukifika mahali msuguano utaanza kati ya wanyonge na hao matajiri jeuri na hatimae wanyonge kushika hatamu za siasa na hapo ndipo tutakaporejea tena kwenye falsafa ya Baba wa Taifa hayati Mwalimu Nyerere na kuunda siasa ya ujamaa na kujitegemea katika mazingira yatakayokuwepo wakati huo. Tuna bahati kwamba tunapo mahali pa kuanzia.

E.G.Msuguru

S.L.P 45471,

Dar es Salaam

 

Je, unasumbuliwa na ulevi wa Pombe?

Pombe ni moja ya tatizo kubwa sana katika ulimwengu wa leo.

Inadhuru mtu kimwili, kiakili na kiroho. Pombe inampotezea mtu kila kitu mathalani , mke, watoto mali, heshima, kazi na mwisho ni kumpoteza yeye mwenyewe, maana yake ni kifo kwa lugha ya uwazi.

Hapo zamani ulevi ulijulikana kama suala la tabia mbaya, lakini siku hizi watu waliokuwa walevi na wameacha, na baada ya kutathimini maisha yao ya ulevi imekuja kugundulika kuwa ama 'ULEVI NI UGONJWA' kama magonjwa mengine yoyote yale , kama vile mgonjwa wa Malaria anavyoweza kukubali kuwa anaumwa na anahitaji tiba, vivyo hivyo na mgonjwa wa ulevi wa pombe sharti la kwanza ni kujikubali kuwa yeye ni mlevi ana tatizo na anahitaji matibabu.

Lakini bahati mbaya kitu kimoja kwa mlevi hawezi kukubali kirahisi kwamba pombe imemshinda. "Aaha itanishindaje pombe? Chunguza jinsi unavyobugia pombe, mambo unayoyatenda baada ya kunywa pombe Matibabu ya pombe hayapatikani hospitalini kwa daktari, bali yanapatikana katika hospitali ya A.A (Alcoholic Anonymous). Kwa vile dawa ya ulevi wa pombe ipo huko Ulaya na Amerika. Vikundi vya A.A viko vingi sana na vinasaidia sana walevi wa pombe.

Bahati mbaya hapa Afrika bado havijafika kwa wingi. kwa neema ya Mungu chama hiki cha Alcoholic Anonymous kimeanzishwa hapa Mwanza, huko Nyakato Parokia ya Katoliki chini ya usimamizi wa Fr. Mapunda Baptiste ambaye ana mang'amuzi ya pombe na madhara yake na pia anao ujuzi wa kuwasaidia wanaosumbuliwa na pombe.

Wale waliojiunga na Chama cha A.A wameanza kujipatia maisha mapya na familia zao zimeanza kuwa na furaha tena. Lakini ili kupona mpango wa A.A unatoa hatua 12 na hatua ya kwanza ni muhimu sana kwa mlevi kupona, kwa sababu inamfanya mtu mlevi ajikubali kuwa ni mgonjwa bila kuona haya, Nayo inasema "Tulikubali kuwa hatukuwa na nguvu yoyote ya kuitawala pombe au kushinda ulevi, kwamba hatukuweza kutawala maisha yetu. 'Bila kukubali kwamba una tatizo basi mlevi ni mtu gani? Ni mtu ambaye hawezi kuitawala pombe ya aina yoyote ile nabaalayake pombe humtawala yeye Je wewe umetawaliwa na pombe? Basi njoo jiunge na A.A na huo ndio usalama wako wa pombe unasababisha mateso, vurugu, ugomvi, hasara kwako na familia? Basi kama jibu ni ndiyo, ujue una tatizo la pombe, na usione aibu njoo ujipatie maisha ili mradi weka nia ya kuacha pombe kabisa.

Alcoholic Anonymous ni nini?

A.A ni ushirika wa wanaume na wanawake ambao hushirikiana pamoja kupeana maarifa, nguvu na matumaini ili waweze kutatatua matatizo yao ya ulevi na kuwasaidia wengine kuacha pombe. Kinachotakiwa katika kujiunga na A.A ni nia ya kuacha pombe. Hakuna malipo wala ada kwa uanachama wa A.A Pia ijulikane kwamba A.A haihusiani kabisa na chama chochote, madhehebu ya dini yeyote, wala siasa yoyote haina nia ya kujiingiza katika mabishano yoyote haipendelei wala kupinga mambo yoyote yale.Nia yetu ni kuacha pombe na kuwasaidia wengine kutotumia pombe ili maisha yao yawe bora na ya raha.

Basi iwapo unaonekana kuwa una tatizo na unywaji wako au kunywa kwako kumefikia kiwango cha kukutia wasiwasi ya kutosha au watu wamekuambia una tatizo basi inakufaa ujue habari za A.A na mapango wa A.A wa kuacha ulevi. Hakuna aibu katika mambo hayo, kumbuka "Mficha ficha magonjwa, kifo humuumbua"

A.A haiwezi kumwambia yeyote eti wewe ni mlevi inasaidia mtu kujielewa jinsi anavyokunywa na madhara yake. Ni juu ya kila mmoja wetu kujipima lakini kwa kawaida hakuna mlevi anayetaka kukubali kuwa ana tatizo .

Neno kubwa ni kukiri udhaifu na kupambana nao. Hivi chunguza unywaji wako kwa uangalifu, halafu jikatie shauri mwenyewe kama pombe ni tatizo kwako au hapana, sisi tuko tayari kukusaidia kwa moyo mkunjufu kabisa.

Sisi katika A.A wanaume kwa wanawake ambao hatuwezi kutawaliwa na pombe tumetambua kuwa tukiwa tunataka kuishi salama sisi wenyewe bila maafa kwa jirani na ndugu zetu, inatubidi kuacha pombe. Pombe haina cheo hakuna maskini wala tajiri sote tunaweza kudhurika lakini sote tunaunganishwa na tatizo letu moja yaani 'pombe'. Kwa kukutana pamoja kuzungumza na kuwasaidia walevi pamoja tunafanikiwa kuishi bila pombe na kusahau mvuto wake, ambao zamani ulitawala maisha yetu.

Ukweli ni kwamba tumejua mengi kuhusu ulevi na vile vile mengi kuhusu sisi wenyewe kwa njia ya A.A. hivi sasa tunajaribu kila wakati kukumbuka mambo hayo katika fikara zetu kwa sababu ni kwma ufunguo wa usalama wetu. Kwetu kutotumia pombe linapaswa kuwa daima jambo la muhimu.

Kuishi bila pombe inawezekana? Jibu ni kwamba baada ya kupata mazoea ya kutokunywa kupitia utaratibu wa A.A tunajaribu kutunza hali hii kwa kufuatia njia na ujzi wa wale waliotangulia katika A.A. Ujuzi wao unatupatia silaha za kutumia ili kupambana na vishawishi vya pombe.

Kwa hiyo basi kama unajiona una tatizo na pombe unakaribishwa kwetu Nyakato Catholic Church. Kila Jumamosi saa 9:00 tuna mikutano yetu, pia kama upo katika maeneo ya mjini nenda pale Kanisa Katoliki Nyakahoja katika mikutano ya kila Jumamosi saa 10:00 jioni. au ukitaka maelezo zaidi na kama una maswali tuletee kwa anuani hii:-

Fr. Baptiste Mapunda (M. Afr),

Ofisi ya A.A,

Nyakato Parish,

S.L.P 3032,

Mwanza.