Twaipongeza Tume ya Jiji

KWA wakazi wa Jiji la Dar Es Salaam kama kuna jambo lenye kuwafurahisha sana ni zile juhudi za Tume la Jiji katika utendaji wake mbalimbali, licha ya kushughulikia mambo ya usafi na utaratibu.

Tunaweza kusema kuwa mwenye macho haambiwa tazama, bali akifungua macho yake atashuhudia jinsi Jiji hili linavyopendeza. Hapo hakuna ubishi wala mashaka kuhusu jambo hilo. Kazi iliyofanyika na Tume ya Jiji kwa kipindi kifupi sana imefanikiwa mno. Tunapenda kuipongeza hiyo Tume ya Jiji kwa kazi hiyo nzuri.

Sote tunatambua kuwa Jiji la Dar Es Salaam ni kama vile kioo cha nchi yetu ya Tanzania. Ye yote anayefika hapa Tanzania kutoka huko Ng’ambo kwa kawaida hufikia Dar Es Salaam.

Hivyo mambo anayoyaona hapo humpa picha ya miji mingine ya Tanzania. Wageni wetu wengi walipouona Mji wetu Mkuu, ukiwa katika hali mbaya sana ya usafi, walisema wapi kuwa sisi Watanzania tu wachafu na hatupendi kuiweka miji yetu na mazingira katika hali ya usafi.

Kwa vikubwa kabisa Tume ya Jiji imetuondolea aibu hiyo kwa kuusafisha na kuendelea kuusafisha Mji wetu. Mpaka hivi sasa wageni wetu walio wengi hawaachi kulisifia Jiji letu hili kwa hali nzuri lilivyo.

Twafahamu pia kwamba Tume imekuwa na mipango mingi sana na tena yenye maana kwa Jiji. Ingawaje labda muda wake wa kufanya kazi kama Tume unakaribia kwisha, sisi tungeona wazidi kuongezewa muda ili Jiji letu lizidi kuwa sura nzuri. Kwa mfano wanatuambia kwamba watatayarisha dampo la kisasa lenye kugharimu mabilioni ya pesa.

Sidhani kama hizo Halmashauri za Miji zitaweza kufanikiwa katika jambo kama hilo. Tunachokifahamu mpaka sasa ni kwamba utendaji wa Halmashauri hauna ufanisi mkubwa kwa sababu ya vikao vingi ambavyo hula zaidi pesa za wananchi kuliko kuzalisha.

Ni kweli kuwa mambo yanapaswa kuendeshwa kwa njia ya kidemokrasia, lakini ikitokea kwamba hiyo demokrasia huturudisha nyuma kimaendeleo, basi afadhali kutumia njia nyingine ambayo itatuletea mafanikio.

Sisi tungependa kufananisha huduma za Tume ya Jiji na yale mashirika yaliyobinafsishwa. Mashirika hayo yamekuwa na uzalishaji mkubwa sana na pia watendaji wake wamekuwa katika hali ya juu kabisa ya nidhamu. Hivyo ndivyo ilivyo hata kwa watendaji wa Tume ya Jiji kwani nao wanafanya kazi kwa nidhamu kabisa.

Mapato ya kufanya kazi kwa nidhamu na kujituma ndiko kunakotuletea maendeleo. Angalia ni kwa jinsi gani wale wanaofanya kazi ya usafi hapa na pale wanavyojishughulisha bila ya kuwa na mnyapara au msimamizi. Hivyo pia ilivyo katika sekta mbalimbali za huduma yao.

Kwa wale ambao walizoea kuona makao makuu ya Halmashauri ya Jiji, wakifika hapo siku leo watashangaa sana kuona jinsi Tume ya Jiji ilivyoyakarabati yale majengo kwa ufundi wa hali ya juu kabisa. Majengo hayo huwa kivutio kikubwa sana kwa wapita njia na wageni mbalimbali wanaoitembelea nchi yetu. Pia bustani nyingi za miti na maua zinazidi kulipamba Jiji letu. Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayovutia yakiwa ni matunda ya juhudi za Tume.

Je, ni nani kati ya wakazi wa Jiji asiyefurahia ile stendi mpya ya basi kule Ubungo? Ingawaje mambo hayakukamilika kabisa, tunatumaini yatazidi kuwa mazuri. Wasafiri wengi siku hizi kujisikia raha kusafiri kwani kuna ulinzi mkali na hivyo hakuna bugudha yo yote kutokana na vibaka au wapiga debe. Pia tunaona ni kwa jinsi gani Tume ilivyo makini katika kukusanya kodi na mapato yake na hivyo kutumia kwa ajili ya maendeleo ya Jiji.

Tume ya Jiji imeletea ajira kubwa sana kwa wakazi wa Jiji hili. Tunashuhudia katika utendaji huo kwamba hakuna ubaguzi, kwani akina mama na akina baba wanafanya kazi za usafi na nyinginezo kwa pamoja na kwa bidii kabisa.

Hapo tunaona kwamba hakuna ile kasumba ya kuchagua kazi, eti kwa sababu huyu ni mwanamke hawezi akafanya kazi ya kufukua mifereji ya maji machafu.

Kumbe sasa hakuna tofauti hiyo kwani wote hufanya kazi sawasawa kwa ushirikiano.

Kama walivyotamka viongozi wetu mbalimbali kwamba Tume iendelee na kazi yake hiyo njema, nasi katika Kauli Yetu hii tunazidi kuunga mkono.

Tunawasihi wahusika wasiivunje Tume hiyo hata kama walikuwa wameipangia muda fulani.

Litakuwa ni jambo lisilo sawa sawa kuvunja Tume kwa sasa hivi, wakati ambapo kila mwananchi mwenye busara angependa iendelee katika kufanya kazi yake hiyo. Kwa kadiri ya mang’amuzi kurudisha shughuli za Tume kwenye Halmashauri za Wilaya ni kuongeza ulaji na siyo utendaji. Kama walivyodokeza wasemaji na waandishi wenzetu kwamba ingetakiwa kabisa Halmashauri mbalimbali za Miji yetu nazo ziige kabisa mtindo huu wa Tume ili kuharakisha maendeleo katika Miji yetu.

Tunapenda kumalizia Kauli Yetu kwa kuzidi kumpongeza Mwenyekiti wa Tume ya Jiji, Mheshimiwa Charles Kaenja pamoja na washauri na watendaji wote kwa kazi nzuri waliyoifanya, wanayoendelea kuifanya na ile ambayo wataifanya hapo baadaye.

Tunaomba wasikatishwe tamaa na shida za hapa na pale zinazowakabili katika kuliendeleza Jiji letu hili. Twasema hongera na pongezi nyingi kwa Tume ya Jiji.

Mwaka huu tuzae matunda mema

KAA pembeni kidogo. Acha kelele. Fikiria sana sana maisha yako mwaka uliopita. Unaweza kuwa na furaha? Unaweza kusema umezaa matunda gani mema? au kusema kweli, umezaa matunda mabaya. Ikiwa umezaa matunda mabaya kwa mwaka huu, utaendelea kufanya hivyo?

Labda unafikiri unaweza kukaa hivi hivi, yaani ingawa huzai matunda mema, hutazaa matunda mabaya. haiwezekani kuishi hivi. Unakaa kati ya mwanadamu. Lazima kuwa msumbufu yaani, mtu asiyefaa, au mtu ambaye anafaa. Huwezi kukaa hivi hivi tu.

Sikiliza mawazo ya Mungu juu ya watu kama hawa: Nayajuua mambo yako yote! Najua kwamba wewe si baridi wa la si moto. Afadhali ungekuwa kumojawapo: baridi au moto. Basi kwa kuwa hali yako ni vuguvugu, si baridi wala si moto, nitakutapika! (Ufunuo 3:15-16).

Hujui Mungu alikupa karama zako? Anangoja, Utatumia karama zako? utazaa matunda mema?

Sasa Mwenzanagu, ingawa hujazaa matunda mema mwaka huu, utaendelea hivi hivi tena mwaka ujao? Usifanye hivi Tengeneza tabia yako, ujirekebishe ili uzae matunda mema mwaka ujao; sivyo, Mungu atakungoja mpaka lini? Uchukue mafundisho yake Yesu Kristo.

'Mtu mmoja alikuwa na mtini katika shamba lake. huyo mtu akaenda akitaka kuchuma matunda ya mtini huo, lakini akaukutaa haujazaa hata tunda moja.

Basi akamwambia mtunza shamba: "Angalia! kwa miaka mitatu nimekuwa nikija ili nichume matunda ya mtini huu, nami nisiambulie chochote. Ukate! kwa nini uinyonye ardhi bure? lakini huyo mkulima akajibu: Bwana, tuuache tena mwaka huu; nitauzungushia mtaro na kuutilia mbolea kama ukizaa matunda mwaka ujao, sawa; la sivyo basi utaweza kuukata.' (Luka 13:6-9)

Padre Karoli Giambrone

Washairi Wetu

KARNE HII YA WASOMI

1. Watanzania twalaki KARNE mpya duniani,

KARNE Wasomi hakiki, Uduwanzi siyo ndani;

Wasomi kuwa mikiki, KARNE ya Wanamakini

KARNE hii Wasomi Watanzania tujue

2. Serikali ipanie, ufundi ndiyo malengo,

Isishike MAGOBOLE, nguvu zipelekwe SIDO,

Mafundi jadi belele, usiwaweke Lupango.

KARNE hii ya Wasomi, Watanzania tujue.

3. Tumekaribisha soko, Twaita soko huria,

Twauza miradi ovyo, Katu na kufikiria,

Nchini tupate michumo, mikataba kuridhia,

KARNE hii ya Wasomi, Watanzania tujue.

4. Ndugu Buruno Mpangala, salamu zako zatua,

Wafanyakazi mahala, Wajibu wetu twajua,

Waajiri wa Maghala, Karne hii waijua,

KARNE hii ya Wasomi, Watanzania tujue.

5. Chombo chetu SHIRIKISHO, Kiimarishwe kwa sasa,

Waajiri waja mbogo, ajira huria sasa,

Sheria zawekwa kando, Wakili yeye na pesa.

KARNE hii ya Wasomi, Wafanyakazi tujue.

6. Makatibu wa vyamani, imarisheni T.F.T.U

Wafanyakazi Kazini, elimisho mara dafu,

Sheria tujue makini, Tetea yako Lufufu,

KARNE hii ya Wasomi, Wafanyakazi tujue.

7. Serikali na uchumi, ndiyo yetu hasa dira,

Imeruhusu Wachumi, hawaongezi Rupia,

Wafanyakazi tuduni, Wawekezaji holela,

KARNE hii ya Wasomi, Wafanyakazi tujue.

8. Ndugu yetu P.KIMITI, Shokoa zako twaona,

Ofisi umedhibiti, rufaa zetu twaona,

Mtu pesa ilikidhiri, Ushindi tumeuona,

KARNE hii ya Wasomi, Wafanyakazi tujue.

9. Muheshimiwa Waziri, Kamilisha kazi yako

Sheria Chama kazini, Wafanyakazi ni ngao,

Twababaishwa kazini, Sheria Chama haiko,

KARNE hii ya Wasomi, Wafanyakazi tujue.

10. Ajira binafsi ilindwe, Wageni wasitumeze,

Wamachinga Wangaliwe, wasibughuziwe kamwe,

Serikali imarishe, Kazi isiwe ya kiwewe,

KARNE hii ya Wasomi, Wafanyakazi tujue.

11. Sayansi hii ya ufundi; vijijini na ituwe,

Ukuzwe ufundi JADI, Mabunduki yaboreshwe,

Wayalipie na kodi, Sayansi yake marishwe,

KARNE hii ya Wasomi, Watanzania tujue.

12. Na hapa nahitimisha, Wafanyakazi zatiti,

Wakati wa elimisha, Wajiri wengi miluki,

Watamaki kwa mashaka, hawana sifa lukuki,

KARNE hii ya Wasomi, Wafanyakazi tujue.

 

Ignas A. Charaji

(Kufa siyo mwiko)

TUICO (MKOA)

BOX 14402

DSM