Heri ya Pasaka

WAUMINI Wakristo ulimwenguni kote hivi sasa wanasherehekea Sikukuu ya Pasaka. Katika Sikukuu hii Wakristo na wale wasio Wakristo wanakumbuka mateso, kifo na Kufufuka kwa Bwana Yesu Kristo.

Sikukuu ya Pasaka hutanguliwa na maandalizi kabambe ya majuma sita ya Kwaresma.

Katika kipindi hicho cha Kwaresma Waumini wamekuwa wakihimizwa kufanya toba kwa kusali zaidi, kufanya malipizi na kitubio kwa kukiri na kutubu madhambi yao. Pia wamekuwa wakihimizwa kufanya matendo mema mbalimbali na hasa kuwasaidia maskini na wale wote wasiojiweza. Kwa kifupi kumekuwa na maandalizi makubwa sana kabala ya Sikukuu hii ya Pasaka.

Kwa kadiri ya mafundisho ya imani ya kikristo, Pasaka ,yaani ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo ni kiini na msingi hasa wa Ukristo. Ni kama asemavyo Mtume Paulo anapowaandikia ndugu Wakorinto.

Anasema hivi: "Kama Kristo hakufufuka, imani yenu ni bure; mngalimo katika dhambi zenu." (1Wakorinto 15:17). Au pia anasema kuwa kama Kristo hakufufuka, basi kuhubiri kwetu ni bure; na imani yenu ni bure (1Wakorinto 15:14).

Hayo ndiyo mafundisho ya imani ya kikristo na ndio msingi wa ukristo. Kwa sababu hiyo siku ile ambapo Kristo alifufuka ni siku kubwa sana, yaani siku ya Jumapili.

Tunasimuliwa kuwa baada ya kufufuka kwake Kristo aliwatokea Mitume na wafuasi mbalimbali. Katika nafasi hiyo Bwana Yesu aliwasalimu kwa kuwatakia Amani ndani ya mioyo yao na katika jumuiya zao.

Anawaambia wafuasi wake: ‘Amani iwe kwenu.’ Kufufuka kwa Yesu kulileta tena amani na utulivu ndani ya mioyo ya wafuasi wake na pia katika mazingira yote ambamo hao wafuasi wake walikuwa wakiishi.

Tunaambiwa baada ya kumkuta huyo Kristo Mfufuka, wafuasi walijazwa nguvu ya upendo na wakawa wanaishi maisha ya amani na utulivu, wakiwa tayari kusaidiana katika shida na mahangaiko yao ya kila siku.

Kipaji cha amani ambacho wafuasi na mitume walikipewa kutoka kwa Bwana Mfufuka ndicho ambacho hata sisi siku ya leo tunakihitaji sana.

Ulimwengu wa leo unazidi kupungukiwa amani siku kwa siku na hivyo kumejaaa machafuko, vita na maasi mbalimbali. Kuna mapigano kati ya mataifa na makabila na hivyo amani imetoweka.

Kuna nchi ambazo tokea zimepata uhuru hazijafurahia amani yo yote kama vile wale wenzetu wa Angola. Tunashuhudia wakimbizi kutoka huko Congo, Burundi, Rwanda na mahali pengine kutokana na ukosefu wa amani. Licha ya vita na machafuko katika nchi mbalimbali, pia katika nchi yetu hii kuna hali ya wasiwasi kwamba kuna kweli amani ambayo itadumu siku zote. Kuna vitendo ambavyo vinaashiria kuvunjika kwa amani pia katika nchi yetu.

Tunapaswa kuzuia hali hiyo isitupeleke kwenye ukosefu wa amani.

Tutaweza kudumisha amani katika jumuia na taifa letu ikiwa tu sisi binadamu tutakuwa tayari kuchukuliana hali na tabia zetu zilizo tofauti. Lakini ikiwa kila mmoja atataka daima kujilipizia kisasi pamoja na ubinafsi hapo hatutaweza kamwe kuwa na amani ya kweli.

Daima binadamu anapoamuwa kurudisha jino kwa jino na jicho kwa jicho, amani haitaweza kudumu. Tunaambiwa kwamba baada ya kufufuka kwake Bwana Yesu hakuchukua hatua ya kulipiza kisasi kwa wale waliomtesa, waliompiga, waliomwua kwa kumwamba pale msalabani na hata wafuasi wake ambao walimtoroka. Lakini alilolifanya ni kuwatakia kuwasamehe na kuwatakia amani wote.

Tunapenda kuchukua nafasi hii kwanza kabisa kuwatakia heri nyingi sana waumini wote wakristo wanaosherehekea Sikukuu ya Ufufuko wa Bwana wao.

Lakini hasa tunawaomba sana hao waumini wanaosherehekea Sikukuu ya kufufuka kwa Bwana wao wawe ni vyombo vya amani katika kila jamii, katika taifa letu, katika familia zao na popote pale wanapoishi na kushughulika. Tunapenda kuona kuwa Kristo Mfufuka anawaunganisha wakristo wote wanaomwamini.

Utengano ambao pengine tunaushuhudia kati ya wakristo na waumini wengine kwa ujumla ni vitu ambavyo ni kinyume kabisa cha habari njema ya ufufuko. Pale ambapo Kristo Mfufuka anatawala, basi kuna amani na utulivu, lakini mahali pale ambapo kuna fujo, hapo shetani hutawala.

Kwa hiyo tunazidi kuomba amani ya kweli itawale ndani ya mioyo ya waumini wote na wale wote wenye mapenzi mema. Tunaomba pia amani ya kweli itawale ndani ya viongozi wetu wa serikali na siasa ili waweze kutuongoza kwenye mafanikio na maendeleo ya kweli.

Tunaambiwa na wataalam wale wa kirumi kuwa katika vita na fujo, ile miungu ya maendeleo haifanyi kazi. Maana yake ni kwamba katika hali ya kukosa amani, basi hapo hakuna mtu anayeweza kushughulikia maendeleo na hata kuweza kuwa na watafiti wafanyao kazi hizo katika utulivu wa moyo na mazingira.Heri nyingi sana kwa Sikukuu ya Pasaka na Kristu mleta amani azidi kuwa pamoja nanyi siku zote.

Mmomonyoko wa maadili katika jamii

Ndugu Mhariri,

Naomba nafasi hii katika gazeti lako ili niseme machache niliyonayo kuhusu maadili katika jamii.

Maadili katika jamii ni mada inayohusu mambo mengi yanayohusu tabia au nidhamu. mimi nitaongelea tabia inavyoharibiwa katika vipengele vifuatavyo ambayo ndio vielelezo vya utamaduni wa jamii yoyote.

Vipengele hivyo ni, Lugha, mavazi na chakula. Lugha yetu Tanzania, kiswahili kimekuwa kikiharibiwa kila kunapokuacha maneno mengi ya kiswahili yanachanganywa nayale ya lugha za kigeni bila msingi wowote katika mtindo huu tunapata lugha ambayo baadhi ya watu wanaita KISWANGILISHI. Inasikitisha zaidi tunapoona maovu hayo wazi wazi hata katika baadhi ya vyombo vya habari kama redio na magazeti kwa wakati huu wa biashara kama redio na magazeti. Kwa wakati huu wa biashara huria baadhi ya vyombo hivyo vinatumia lugha isiyosanifu ili kuvutia wateja kusema kweli wanawaharibu wateja wao kwa kuwauzia taarifa hizo zisizo na ubora wa lugha.

Ukiachilia mbali suala la usanifu wa lugha kumekuwa na matumizi ya maneno (ikijumuisha lugha katika picha) ya matusi hadharani, kwa mfano utasikia matusi ya nguoni hata kwenye vyombo vya usafiri (mabasi) yakitamkwa na watu wazima bila aibu wala kujali utu wa watu wengine.

Ukiangalia mavazi, tabia za vijana wengi sio za kuridhisha hata kidogo. hapa nitagusa zaidi jinsia yangu kama msichana. Wasichana wanashangaza na kusikitisha utawaona katika mavazi yasiyo ya heshima, wanavaa nguo fupi zinazofika futi moja juu ya goti (miniskirt). Pia wanavaa nguo zinazobana, kiasi kwamba maungo yake ya mwili yanakuwa wazi vilevile wengine huvaa nguo zinazoonyesha nini kinachosetiriwa ndani ya (transparents). Mitindo ya uvaaji huu huamusha ashiki kwa wanaume na ndio chanzo cha ubakaji. Inasikitisha inapofikia wakati badala ya wao kuona aibu kwa kile wanachokifanya watazamaji wanaona aibuu kwa kile wanachokiona. Kielelezo cha tatu cha mmomonyoko wa maadili katika jamii zetu ni katika vyakula. Kumekuwa na utumiaji wa vileo katika unywaji wa pombe kali na madawa ya kulevya. Gongo, Cocaine, Heroni na bangi yamekuwa sehemu ya maisha kwa baadhi ya watu katika jamii. Utumiaji wa vileo hivyo humfanya mtu asiwe na uwezo wa kufanya kazi wala kupanga mambo ya maendeleo zaidi ya hapo huwa mharibifu daima wa utaratibu wa mfumo wa maisha katika jamii wanakuwa wagomvi, wabakaji, wafujaji mali na wavivu.

Kwa ujumla kumomonyoka kwa maadili hayo kumetokana na mambo mengi. Baadhi yao mimi niyaonayo kuwa yanahusika zaidi ni kwanza taifa au jamii zetu kutokuwa na taratibu zinazostahili kufuatwa au kuzingatiwa katika jamii. Ingawa huko nyuma taratibu hizo zilikuwawepo na kufuatiwa hivi sasa tamaduni za kigeni zinaigwa mno na zinaonekana kuwa bora kumbe sio.

Pili wazazi hawajali wajibu wao katika kulea na kuelekeza familia zao katika misingi bora ya maisha, Watoto wanakuwa bila muongozo wanapofikia umri wa ujana hawaelewi lipi jema au lipi baya. Lolote watakalofanywa kwao ni sawa tu, kitu kibaya zaidi wazazi wanawaachia walimu (mashuleni) kulea watoto wao kusema kweli wazazi na walimu wana nafasi tofauti zinazojitegemea katika malezi ya vijana.

Mwisho taifa halionyeshi kuwa na msimamo wa malezi ya vijana . Hivi sasa taifa halina utaratibu unaoeleweka kwa vijana. Vijana wameachwa waamue wenyewe mambo yao.

Mimi binafsi napendekeza vyombo vifuatavyo visaidie kurudisha hali ya maadili katika mfumo unaostahili.

Madhehebu ya dini yachukue mzigo kuwaelekeza na kuwandaa vijana kuwa na tabia njema katika jamii. kwa mfano kila kanisa kuna idara ya vijana idara hii ibuni mbinu mbalimbali za kuwawezesha vijana wanakuwa na tabia njema katika lugha, mavazi na vyakula.

Vile vile Serikali kwa kutumia sheria iandae utaratibu utakaoulazimisha kila mzazi anawajibika kulea familia yake kwa mfano mtoto anapomaliza darasa la saba mzazi atoe maelezo jinsi anavyomuandaa kijana wake kukabiliana na maisha baada ya shule kinyume na hapo sheria ichukulie mkondo wake kumuadibisha mzazi anayehusika.

Kuhusu mavazi na madawa ya kulevya, Serikali itangaze vita dhidi ya watuhumiwa. Jeshi la polisi ikiwezekana jeshi la wananchi litumike kukomesha na kusafisha tabia hizo mbaya katika jamii.

Kama kiongozi mtarajiwa katika karne hii ya ishirini na moja naahidi kutokuona haya kwa kuwaonea haya wasio na haya nitapambana kamwe sitalalama.

Luiza E. Kawonga,

Sekondari ya Wasichana Songea

S .L.P 268,

Songea

Kristu asihubiriwe kama kampeni za siasa

Ndugu Mhariri,

Naomba nafasi katika gazeti lako linaloongoza, nimekerwa na mwenendo wa mahubiri ya dhehebu la Pentekoste (walokole) kwa kile kinachoitwa kujisifu nafsi zao.

Tabia ya kashfa juu ya Kanisa Katoliki ni ya kawaida kwao. Sasa wamegeukia jina la Baba Mtakatifu wetu Yohane Paulo II. (Msema Kweli toleo la 109 la tarehe 2-4 -2000 Uk.8). Ushuhuda wa Kristo hauhitaji majina ya watu au kanisa fulani. kufanya hivyo ni kuonyesha kutokujiamini katika mahubiri yako.

Amini usiamini, kubali ukatae kanisa Katoliki limejengwa juu ya mwamba thabiti, halitingishiki wala haliyumbi kwa kuwa Kristu mwenyewe ndiye aliyeiweka linaongozwa na Roho Mtakatifu. Pia linayo wakili ambaye ni Baba Mtakafifu kuanzia kwa Petro mtume alipokabidhiwa na Bwana wetu Yesu Kristu mwenyewe . Mathayo 16:18-19.

Wanasiasa hutumia mbinu za kujisifu na kujikweza ili kuwachanganya akili watu ili mradi wafaulu Yesu Kristo hakututuma tukamtangaze kwa njia hizo ili mtambue mnayoyatenda ni kinyume naye Kristo alishatutabiria hayo basi soma Mathayo 6:5-na 7:15 na 21-23. Kisha Mathayo 12:34-37, mtaona jinsi gani mwahubiri Kristo? au mwahubiri uwezo wenu kwa kutafuta utukufu wenu wala usiwe wa Mungu.

Tumsifu Yesu Kristu

Happiness Aloice,

S. L.P 212,

BABATI