Wanafunzi vyuo vikuu komaeni

KUNA methali ya Kiswahili isemayo kuwa hasira ni hasara. Maana yake mambo yanayofanyika katika hasira mara nyingi huleta hasara. Hivyo ndivyo mambo yanavyotokea katika ulimwengu huu.

Hivi karibuni vijana wetu wanaosoma katika Chuo chetu Kikuu cha Dar es Salaam wameamua kutumia hasira na hivyo kusababisha hasara kubwa sana ya mali.

Imeriptiwa na vyombo vya habari kuwa wanafunzi wa Kitivo cha Sheria wamekuwa na ugomvi mkubwa na wale wa Kitivo cha Uhandisi.

Sababu iliyopelekea hao vijana wetu waingie katika ugomvi mkubwa huo ni kutokana na vyumba vya madarasa. Tunasema kuwa hilo ni jambo la kusikitisha sana kuona vijana wetu wanagombana na kuleta uharibifu wa kuvunja vioo vya madirisha, kuvunja meza na hata viti kwa sababu tu eti hawataki wenzao wafanyie mitihani katika darasa lao.

Kwanza kabisa tunatambua kuwa hakuna uzalendo kabisa katika vijana wetu hao kwa vitendo hivyo ni kinyume kabisa cha ustaarabu.

Sisi tunaamini kwamba vijana wetu wanaosoma Chuo Kikuu ni ndugu, na hivyo daima watakuwa wanasaidiana katika mambo mbalimbali na hasa yale yanayohusu elimu yao. Na tendo la kutumia darasa la wengine kwa mitihani, sisi tungeona ni la kawaida kabisa na lisingeleta matatizo yo yote yale. Lakini tunaposikia kwamba limesababisha fujo kubwa tunashangaa na kusikitika mno.

Jambo la pili lenye kuleta masikitiko ni uamuzi wa hao vijana kuvunja na kuharibu vifaa mbalimbali vya shule. Hakuna asiyetambua kuwa nchi yetu ni maskini, na hivyo hutupasa kutunza cho chote kile tulicho nacho.

Lakini inapofikia mwanafunzi anafanya uamuzi wa kuharibu kwa makusudi mali ya shule ambayo ni mali ya umma tunatiwa hofu kubwa sana. Je,hao vijana ambao watakuwa ni viongozi wetu wa hapo kesho wataweza kweli kutunza mali ya umma? Jibu lake ni kwamba siyo rahisi kabisa! Wenzetu ambao wamestaarabika wanapenda kujivunia vitu vya zamani na hasa vile ambavyo watu maarufu walivitumia.

Mtu ukienda kule Oxford au Cambridge utashangaa kuziona zile meza na hata viti vilivyotumika na wale wasomi wa zamani. Hiyo ni fahari kubwa sana kwa Chuo na pia kwa Taifa. Kinyume chake sisi Watanzania - vijana wetu wanafanya uharibifu mkubwa sana.

Licha ya hayo ni kwamba hao vijana wetu wamesimamishwa masomo yao kwa sababu ya fujo hizo. Hilo tena ni jambo la kusikitisha mno. Tunataraji kwamba vijana wetu wasome vizuri, na hivyo waweze kufaulu mitihani yao.

Lakini siyo kufaulu mitihani tu, bali pia wajengeke kitabia, na hivyo tuweze kuwa na viongozi wanaoamini. Taifa liwe na viongozi wanaovumiliana katika magumu na matatizo mbalimbali. Hatutaki viongozi waliojaa hasira na jazba, kwani hawataweza kamwe kuwa viongozi hodari wakiwa wamejaa jazba.

Vijana wetu wanapaswa kujifunza namna ya kumaliza matatizo kwa njia ya mazungumzo na wala siyo kwa kutumia fujo.

Kwa upande mwingine ni vizuri pia hata uongozi wa Chuo nao ukaketi chini na kuona ni wapi chanzo cha matatizo hayo. Wataalam hutuambia kwamba ikiwa kunatokea tatizo lo lote lile ni lazima kuangalia pande zote mbili zenye kuhusika na tatizo hilo.

Kwa hiyo sisi tunapenda kushauri kuwa matatatizo hayo ya Chuo chetu Kikuu sharti yaangaliwe kwa kina sana kwani yawezekana kuwa hata kwa upande wa uongozi kuna shida pia. Kwa mfano tendo la kuongeza idadi ya wanafunzi bila kufikiria mahali pa kusomea, yaani kuongeza madarasa nalo pia laweza likaleta fujo.

Serikali au uongozi wa Chuo unapoamua kuongeza idadi ya wanafunzi, ni lazima pia ifikirie juu ya idadi ya madarasa, mahali pa kulala, vitabu na mambo mengine.

Ni jambo la aibu kabisa kuona vijana wetu wanaosoma katika Chuo Kikuu wanachangiana madarasa, labda iwe ni kwa bahati mbaya. Kwa hiyo tunaomba jambo hilo liangliwe vizuri ili fujo hizo zisitokee tena.

Kwa kifupi sisi tunalaani kabisa vitendo vya vijana wetu kule Mlima kufanya fujo na kuharibu mali ya umma.

Tunawasihi wasifanye tena vitendo hivyo kwani havijengi bali kubomoa tu. Wakumbuke kuwa kufanya mambo katika hasira ni kuleta hasara kwa mtu binafsi na pia kwa umma.

Wafadhili wetu watatucheka sana wakiona kuwa licha ya umaskini tulio nao, hatuko tayari kutunza kile tulicho nacho. Na kwa upande wa uongozi inafaa kuwa na busara katika kuwaongoza vijana na hasa katika kuviendesha Vyuo vyetu.

Jambo kubwa linalosisitizwa katika uongozi ni kwamba inatupasa kuwa na mazungumzo katika maamuzi mbalimbali. Hivyo pia ilitakiwa hata kwa vijana wetu kabla ya kuchukua hatua ya kuleta fujo. Ni kwa njia ya mazungumzo tu tunaweza kumaliza mambo kiungwana, na siyo kwa njia ya kuleta fujo.

Kulikoni Sekondari za Serikali?

Ndugu Mhariri,

Nikiwa kati ya wakereketwa wa swala muhimu la elimu ambayo ni ufunguo wa maisha ya kila mwanadamu, naomba unipe nafasi katika gazeti lako hili la KIONGOZI ili niweze kusema kuuliza na hata kutoa dukuduku langu juu ya suala hili.

Kama ilivyotangazwa katika vyombo mbalimbali vya habari nchini, hivi karibuni serikali imetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne.

Kilichonishangaza zaidi ni kuona kuwa shule za sekondari za serikali zimethibitisha ukweli kwamba, labda kuna udhaifu katika kuziendesha ndiyo maana zimefanya vibaya kiasi cha kuogofya namna hiyo.

Ndugu Mhariri, kinachonishangaza hadi kuomba kuzungumza kupitia gazeti lako ambalo ndiyo njia yetu ya kusema ni kwamba, katika shule za serikali ambayo ndiyo inaongoza kwa ujumla, kuna udhaifu gani hadi zishindwe namna hiyo tofauti na matokeo mazuri ya shule za seminari?

Labda nitolee mfano kwa shule za mkoa wa Dar Es Salaam ambao ni kituo kikubwa cha maendeleo kinachojulikana Tanzania nzima.

Shule ya Mzizima inayoongoza katika mkoa huu, ndiyo imekuwa eti ya 30, kuna kasoro gani katika uongozi mzima au hata kwa wanafunzi wa shule hizo?

Yaani mkoa mzima wenye shule nyingi namna hiyo hakuna shule hata moja katika 20 bora? What is wrong?

Jambo muhimu la kutafakari na kujiuliza kwa makini ni kwamba, kuna dosari gani inayozifanya shule za sekondari za sekarili zifanye vibaya namna hiyo hata kuzidiwa kwa kiasi cha kutisha namna hiyo na shule za seminari?

Mimi nadhani ipo haja ya serikali hasa katika mkoa wa Dar Es Salaam kukubali kuwa imezembea katika ufuatiliaji kuona kwamba elimu inayotolewa shuleni, inatolewa kwa kiasi cha kutosha na kwa muda muafaka.

Maana yangu hapa ni kuwa, upo uwezekano mkubwa kuwa uongozi na walimu hawakuwajibika ipasavyo pale wanafunzi ambao wanaweza kuwa chanzo cha tatizo hili walipozembea, aidha, kwa kutoroka masomo na kuendekeza anasa au basi sababu nyingine yoyote inayoweza kuwa.

Pia upo uwezekano mkubwa kuwa walimu walikuwa wanatoa elimu duni darasani kwa makusudi ili kuwashinikiza wanafunzi hata wasio na uwezo, waende kufundishwa tuisheni.

Ni ukweli usiofichika kuwa ingawa tuisheni nyingine zimekuwa zikiendeshwa aidha kwa usiri au uwazi, lakini kwa nia nzuri na pia, ni ukweli usiofichika kuwa wapo "fisi" ambao wanaendesha tuisheni kwa lengo la kujipatia pesa na hata kama mtego kwa ajili ya kufanyia vitendo vyao vya unyama ambavyo badala ya kuambulia elimu bora kwa watoto wetu, vimezaaa matunda machungu ya "kujaza watoto kwenye mitaro wakiwa katika mifuko ya rambo" , waliozaliwa kabla ya miezi 9, nadhani hata kama serikali haitakubali moja kwa moja, hili wanalifahamu na ninawashauri wakubali kuwa wameshindwa kulikemea na kulidhibiti.

Ipo haja ya kufanya uchunguzi wa kutosha juu ya tatizo hili ili tuandae Tanzania imara kwa siku za usoni.

Kwa nafasi hii, naomba kuzipongeza shule zote za seminari zilizofanya vizuri kiasi hicho na hata uongozi wa taasisi zinazo ziongoza na kusema SHULE ZA SEMINARI, PONGEZI SANA NA ONGEZENI BIDII ILA, MUWE MAKINI MAANA AJIDHANIAYE AMESIMAMA, AANGALIE ASIANGUKE.

Nyageye C. Kinani,

Chuo Kikuu cha

Dar Es Salaam,

Mwenge- Dar Es Salaam.

Pongezi Bunge kuwajali viongozi wastaafu

Kwanza napenda kukupongeza kwa kazi nzuri unayoifanya ya kuwaelimisha, kuonya, na kuwa burudisha wananchi kupitia gazeti lako la KIONGOZI.

Baada ya pongezi zangu hizo, naomba pia kutoa pongezi za dhati kwa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kuongeza marupurupu kwa viongozi wetu wakuu watakaostaafu kuanzia baadaye mwaka huu.

Nasema Bunge letu linastahili kupongezwa kwa uamuzi wake huo, kwa kuwa utawatia moyo hata viongozi wengine waliopo chini na watafanya kazi kwa bidii wakitarajia kufika juu na kupata marupurupu hayo.

Kimsingi uaminifu wa binadamu yeyote yule unaweza kuishia iwapo atakuwa katika mazingira ya kupigania kuishi.

Ninaposema kupigania kuishi nina maana kuwa iwapo mfanyakazi atalipwa mshahara ambao hata chakula na nauli havitoshi, basi ni lazima kwamba hatakuwa mwaminifu kwa mali za umma ambazo atakuwa wakizitumia katika utendaji wake wa kazi wa kila siku.

Hivyo mimi binafsi ninaona ni hatua na uamuzi wa busara uliofikiwa na Bunge kuwafikiria wastaafu. Hata hivyo Bunge na serikali kwa ujumla havina budi kuona vina jadili mambo mengi muhimu yanayo husu jamii nzima bila kujali matabaka.

John Changoni,

S.L.P

DODOMA

Watanzania wote tuzingatie usafi

Napenda kutumia nafasi hii kuwashauri watanzania wenzangu kuepuka magonjwa mbalimbali ya mlipuko ukiwemo huu wa kipindupindu na kuhara kwa kuweka mazingira yetu katika hali ya usafi.

Sina maana kuwa hayo ni magonjwa pekee yatokanayo na kutokuwa wasafi sisi wenyewe na mazingira yanayotuzunguka, bali pia ya magonjwa mengine yanayotokana na uchafu kama vile malaria ambayo huonesha kuwa mazingira haywekwi katika hali ya usafi na hivyo kuwaruhusu mbu kuzaliana ovyo.

Yapo magonjwa mengine ambayo ni aibu kuyaugua hasa haya yatokanayo na kukosa usafi wa mwili na mazingirakikiwamo chakula.

Nitoe mfano kwa mtu na heshima zake anapougua ugonjwa wa kuharisha, lazima ieleweke kuwa huwa kwa vyovyote amekutana na mazingira machafu hasa katika kinywaji au chakula alichokula.

Tuzingatie kuchemsha maji na kula vyakula vikiwa katika hali ya joto la kutosha kuuua wadudu wa maradhi na pia ni muhimu kunawa kabla na baada yakula na hata baada ya kutoka chooni.

Mhariri nashukuru endapo utanipa nafasi hii ili niwashauri Watanzania wenzangu kuepukana na mambo haya yanayochelewesha maendeleo yetu.

Chacha Muniko,

S.L.P. 10,

MUSOMA